Nyie @tcra_tanzania kwanini mnazuia media zisiripoti press ya Askofu Gwajima? Na zile zilizoripoti kwanini mnalazimisha zifute? Kama maudhui ya Gwajima yana shida, si aitwe polisi kuhojiwa?
Pamoja na mambo mengine, Gwajima ameongelea issue ya watu kutekwa/kupotea. Hivi nyie hamuoni hilo ni tatizo? Hamuoni taarifa mitandaoni watu kudaiwa kutekwa na kupotea? Yuko wapi Mdude? Yuko wapi kijana aliyechoma picha ya Rais? Yuko wapi Erick Msyaliha? Yuko wapi Daniel Chonchorio?
Gwajima amesema ana orodha ya watu zaidi ya 80 waliotekwa/kupotea mwaka huu. Hivi nyie hamshtuki? Watu 80+ kwa miezi minne? Kumbuka hao ni walioripotiwa. Je, ni wangapi hawajaripotiwa au hawana umaarufu?
Taarifa hii ilitakiwa iwashtue na mtoe ushirikiano ili watu hao wajulikane walipo. Mtoe mawasiliano yao ya mwisho ambayo yangeonesha waliwasiliana na nani kabla ya kupotea.
Lakini badala ya kufanya hivyo, nyie mnazuia maudhui ya Gwajima yasichapwe. Hivi kati ya hao waliopotea, wangekuwepo wafanyakazi wa TCRA, mngezuia maudhui yasichapwe? Ndio maana Gwajima akauliza, hivi mnadhani nyie ndio binadamu peke yenu, wengine ni mbuzi? Mpaka apotee mtoto wa nani ndio muone hili ni tatizo?
Cha ajabu, Gwajima amekemea utekaji, nyie mnazuia habari zake zisiandikwe, lakini wale wanaomjibu wakisema utekaji umekuwepo tangu enzi za Nyerere, mnaruhusu habari zao zichapishwe. Hivi mnataka tuwaeleweje? Kwamba mnaunga mkono utekaji au?
Halafu mnadhani mkizuia "mainstreams" ndo mmedhibiti habari isisambae? Hayo ni mawazo mgando. Imeshaenea nchi nzima, kwa sababu inahusu maisha ya watu. Kwa hiyo, nakupeni pole. Mmechelewa sana.
Bibi yangu kule Tarakea (95) aliposikia roho za watu 80 hazijulikani zilipo, ameumia sana. Ameanza Novena ya Mtakatifu Rita wa Kashia kukemea watekaji. Nimemuomba aunganishe na watumishi wa TCRA wanaozuia habari za utekaji zisichapwe. Kwa hiyo, subirini matokeo.
Na nyie waandishi mnaozuiwa kuripoti, msifikiri mko salama. Kumbukeni alitekwa Azory Gwanda, mwandishi mwenzenu, na hadi leo hata mfupa wake haujaonekana. Kufyata mkia ni kuungana na watesi. Siku mkitekwa, hakutakuwa na wa kuwapazia sauti. Chagueni leo kusimama na umma. Kuweni sauti ya wasio na sauti. Kila mtu ana haki ya kuishi!