Wazee wa miaka ya 60 na 70 ndio mmetufikisha hapa
Pichani ni Mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Tinde, Josephine Otieno (AMO) ambaye ameshurutishwa kupiga magoti na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, ili kumuomba msamaha Mbunge wa jimbo la Solwa, Ahmed Salim kwa niaba ya watumishi wa kituo chake ambao wanatuhumiwa kutoa lugha chafu za kashfa na matusi kwa wagonjwa.
KWA NINI NASEMA HUU NI UDHALILISHAJI?
DHAMBI moja haihalalilishi DHAMBI nyingine na wala kosa moja halihalalishi kosa lingine. Binafsi napinga na kulaani vitendo vya baadhi ya Watumishi wa afya kuwakashifu, kuwatukana na kuwadhalilisha wagonjwa. Vitendo hivi vinafaa kushughulikiwa na mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria.
Watumishi wa afya wana mwajiri na mamlaka ya kinidhamu ya kuwashughulikia. Alichofanya huyu Mwenyekiti wa CCM ni udhalilishaji. Ameidhalilisha taaluma ya udaktari, amewadhalilisha Watumishi wa idara ya Afya, amemdhalilisha huyu mwanamke. Hii sio sawa hata kidogo.
Wanasiasa wa nchi hii wamejawa na kasumba ya ulimbukeni, kibri na dharau dhidi ya Watumishi wa umma. Hii si mara ya kwanza udhalilishaji kama huu kufanyika hadharani.
Nani hakumbuki tukio la Mkuu wa Wilaya kuamuru Walimu wacharazwe viboko hadharani na kweli Walimu kwa HOFU na UOGA wakasalimu amri na kucharazwa bakora tena mbele ya wanafunzi. Yule DC alifanywa nini? Hakuna!
Nani hakumbuki kitendo cha yule Diwani kule Tanga alivyomdhalilisha Mwalimu. Mwalimu kasaini kitabu cha mahudhurio saa 6.45 A.M. Diwani anamuuliza Mwalimu umeripoti kazini saa ngapi, Mwalimu kamjibu saa moja kasorobo. Diwani anamwambia Mwalimu wewe nakuona una kiburi na jeuri kwa nini unanidanganya wakati kwenye kitabu umesaini saa kumi na mbili na dakika arobaini na tano. Anaanza kumtisha Mwalimu na kumuambia atatoa amri aondolewe kwenye halmashauri yake.
Nani hakumbuki sakata la udhalilishaji Ali Hapi aliomfanyia yule mama wa idara ya Ardhi, akimtisha tena mbele ya umma kwamba yeye ni mtu hatari sana. Hivi unategemea nini mfanyakazi anapotishwa na Mkuu wa mkoa?
Nani hakumbuki Bashite akiwatisha Walimu kuwa kama wangedhubutu kunyanyua mabango ya kudai nyongeza ya mshahara, kupandishwa madaraja na malimbikizo ya madeni yao angewacharaza viboko Walimu hadharani pale pale uwanjani. Yani mtu mwenye tuhuma za kufoji vyeti anapata ujasiri wa kuwatisha na kuwanyamazisha Walimu kwa sababu tu yeye ni mwana CCM mwenye madaraka ya uongozi. Kwake anaona taaluma za watu si chochote wala lolote.
Mambo mengi ya kitaaluma kwa sasa yanakabiliwa na shinikizo la wanasiasa wa CCM wanaotaka kumfurahisha mwenyekiti wao wa CCM.
Wafanyakazi wamebaki kama mayatima hakuna wa kuwasemea. Wamejawa HOFU na UOGA, kila mwanasiasa anayezuru eneo lao la kazi anakuja na vitisho na maagizo ya kipuuzi. Udhalilishwaji umekuwa sehemu ya maisha ya Wafanyakazi.
Hata kama tuhuma zilizotolewa ni za kweli. Tujiulize je Mwenyekiti wa CCM ndizo mamlaka za kinidhamu za kuwawajibisha Watumishi wa idara ya Afya?
Je adhabu ile ndio iliyoainisha kwenye kanuni za utumishi wa umma? Kwamba washurutishwe kupiga magoti kwenye mkutano wa hadhara wa CCM na kuomba msamaha?
Hivi Wafanyakazi wa nchi hii wameikosea nini serikali hii ya CCM? Kuwapandisha mishahara na madaraja imeshindikana wamekaa kimya wameamua kufa kwa njaa kimya kimya kama wafuasi wa Kibwetere. Hiyo haitoshi bado mnaamua kuwadhalilisha kwa nini?
Maeneo mengine Walimu wanashurutishwa kufundisha hadi weekend, hakuna likizo. Naibu Waziri anasema amesitisha uhamisho mwalimu asijisumbue kuomba uhamisho. Hii maana yake nini?
NANI WA KULAUMIWA?
Wa kwanza anayestahili kidole cha lawama ni hivi vyama vya Wafanyakazi. Tuna vyama vya Wafanyakazi vya hovyo haijawahi kutokea Duniani. Madaktari na wauguzi wanadhalilishwa chama cha Madaktari na kile cha Watumishi wa afya kipo kipo tu. Walimu wanacharazwa bakora hadharani, chama cha Walimu (CWT) kipo tu kinakula asilimia za mishahara ya Walimu kila mwezi.
Pili ni serikali ya CCM. Wanasiasa wa CCM Mpya wanadharau na kupuuza taaluma za watu. Yani Diwani au Mwenyekiti wa CCM ambaye anajua tu kusoma na kuandika kwa tabu ana ujasiri, dharau na kiburi cha kudhubutu kumdhalilisha Mwalimu, Daktari, Muuguzi, Injinia au Muhasibu mwenye vyeti vyake. Huu ni upuuzi ambao ukifumbiwa macho siasa itazidi kuangamiza elimu, idara ya afya n.k. Tujifunze kuheshimu taaluma za watu. Penye makosa watu wawajibishwe na mamlaka husika kwa mujibu wa Sheria, taratibu na kanuni. Acheni mizuka, nchi hii mnaipeleka korongoni kwa sababu mnaendesha nchi kwa mizuka. Lazima kuwe na clear line inayotenganisha mpaka wa siasa na taaluma.
Mwisho nimnyooshee kidole cha lawama huyu Daktari na Watumishi wengine wengi wanaokubali kuweka kando taaluma zao na kudhalilishwa na wanasiasa hawa uchwara. Wafanyakazi mna haki zenu, zipo Sheria za kuwalinda acheni kujidhalilisha, kataeni kudhalilishwa. Hivi kwani huyu Daktari angedinda kupiga magoti hapo huyo Mwenyekiti wa CCM angemfanya nini? Ana jeuri ya kumfuta kazi kwa Sheria ipi na kwa mamlaka gani?
Aidha nanyi ndugu zetu baadhi ya Madaktari, wauguzi n.k. Chonde chonde kazi hii ni wito tunapokuja hospitalini hebu kuweni na UTU, hekima, adabu na busara. Wapo Watumishi wa afya wanaofanya kazi hii kwa weledi, wito, hekima na upendo mkubwa. Lakini baadhi yenu hata mgonjwa usipokuwa na uvumilivu unaweza ukamchapa nesi makofi, mnakuwa na kiburi na dharau utadhani mmelazimishiwa kazi. Badilikeni hii kazi ni zaidi ya utume.
Nanyi wanasiasa kama mwanataaluma anatuhumiwa, mpelekeni kwenye mamlaka za kinidhamu kwa kuzingatia taratibu, Sheria na kanuni akawajibishwe kwa mujibu wa Sheria pasipo kudhalilishwa.