Bwawa la umeme la Julius Nyerere liwe kichocheo cha matumizi ya nishati ya umeme katika kupikia

Uchumi wa Mifugo

JF-Expert Member
May 20, 2021
345
575
Mradi wa bwawa la kufua umeme wa maji la Julius Nyerere ulioko katika mto Rufiji unategemewa kukamilika juni 2022.Bwawa hilo linatarajiwa kuzalisha megawati 2115 ambazo zikichanganywa na megawati zilizopo zitaifanya Tanzania kuwa na umeme mwingi utakaotosheleza mahitaji ya ndani na ziada kuuzwa nje ya nchi.

Aprili 10,2021 Waziri mkuu mh.Kasim Majaliwa alitembelea mradi huo na kusema"lengo la kuanzisha mradi huu ni moja ya juhudi za serikali za kupunguza gharama za umeme kwa wananchi kwa sababu uzalishaji wake ni wa gharama nafuu ukilinganisha na vyanzo vingine,uniti moja ya umeme unaozalishwa kwa kutumia maji inagharimu shilingi 36 hadi 50 huku umeme unaotumia vyanzo vya mafuta uniti moja inazalishwa kwa gharama ya shilingi 440 hadi 600".

Mradi huo mkubwa ambao umechukua asilimia tatu ya hifadhi ya Selous umeleta uharibifu mkubwa wa mazingira lakini uharibifu mkubwa na wa kutisha ni ule unaotokea kila siku nchini kwa kukata miti kwa ajili ya kuni na kutengeneza mkaa ili kupata nishati ya kupikia.Taarifa mbalimbali za wataalam wa mazingira zinasema hekta 469,871 za misitu ya miti ya asili zinateketea kila mwaka nchini kwa ajili ya shughuli za kibinadamu kama kukata miti kwa ajili ya kuni na kutengeneza mkaa.Uharibifu huu wa mazingira unaleta athari nyingi kama mmomonyoko wa ardhi na upotevu wa rutuba kwenye udongo pamoja na kuleta jangwa.

Nishati za mkaa na kuni zimechangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira nchini kwa sababu ni rahisi kupatikana na pia gharama yake ni nafuu na Wananchi wanaweza kumudu gharama zake tofauti na nishati nyingine kama umeme na gesi,lakini pia nishati hizo zinaleta athari nyingi kama moto,moshi na vumbi ambazo ni hatari kwa mpishi.Pamoja na kuwepo nishati nyingine kama mkaa mbadala lakini umekuwa hausaidii kwani Wananchi wengi hawautumii mkaa huo bado wanaendelea kutumia mkaa wa kawaida kwa sababu mkaa mbadala bado haujasambaa mitaani.

Taarifa ya wakala wa umeme vijijini na ile ya ofisi ya taifa ya takwimu iliyotolewa mwaka 2020 inaonyesha asilimia 63.5 za kaya zote nchini zinatumia kuni na ndiyo nishati kuu,asilimia 26.2 zinatumia mkaa, asilimia 5.1 zinatumia gesi na asilimia 3.0 hupika na umeme.Hii taarifa haileti tumaini kwa mazingira yetu bado kaya zinazotumia umeme kwa ajili ya kupikia ni chache sana ingawa uzalishaji wa umeme umewafikia Watanzania kwa asilimia 78.4 lakini wanautumia zaidi kwa ajili ya kupata mwanga,kuchaji simu, redio na kuangalia luninga.Haya ni matumizi madogo sana ya umeme na kama hii hali itaendelea hata bwawa la umeme la Julius Nyerere litakapokamilika litakuwa halina maana yoyote kwa mazingira ya Tanzania.

Juni 5,2021 wakati wa siku ya mazingira Duniani Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango alisema "wakati mradi wa bwawa la umeme la mwalimu Julius Nyerere utaongeza uzalishaji nishati ya umeme kwa megawati 2115,ukikamilika tunatarajia kaya zinazotumia kuni na mkaa zitatumia umeme" .

Lakini kaya zinazotumia kuni na umeme hazitaweza kutumia umeme kama gharama za umeme zitaendelea kuwa hizi hizi hata kama zitaongezeka megawati 2115,kwani tatizo si uchache wa megawati tatizo ni gharama za umeme . Serikali inatakiwa ishushe gharama za bei za uniti kwa umeme wa majumbani, inatakiwa isitoze kodi kwenye majiko ya umeme na vifaa sanifu vya kupikia,kinyume cha hapo Wananchi wataendelea kutumia kuni na mkaa hata Kama kutakuwa na megawati 2115.

Kwahiyo megawati 2115 ziwe kichocheo cha kutumia nishati ya umeme katika kupikia kwa sababu bwawa na miundombinu ni ya Serikali na gharama ya kuzalisha umeme wa maji ni nafuu kulinganisha na vyanzo vingine basi ni wakati mwafaka wa kushusha gharama za umeme ili Tuache kuharibu misitu ya Tanzania.

Tuitunze nchi yetu yenye miti ya kila aina.
 
inabidi serikali ishushe gharama wote tuwe ile gharama ya chini ilo tupikie
 
Bwawa hili litaathiriwa na uhaba wa mvua na ukame sawa na mabwawa yote. Ujenzi ulikuwa azimio la kisiasa la kupuuza wataalamu wengi, bila ushirikiano wa umma. Tutaona.
 
Back
Top Bottom