Buriani mtandao, Uenyekiti wa Magufuli CCM utaondoa mitandao

kalulukalunde

JF-Expert Member
May 27, 2016
1,056
1,083
WAKATI Rais John Magufuli alipoketi kwenye kiti cha Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ndani ya ukumbi wa Dodoma Convention Julai 23 mwaka huu; chama hicho kilikuwa kimeingia kwenye zama mpya.

Uenyekiti wa Magufuli umehitimisha takribani miaka 20 ya kundi la wanasiasa ndani ya CCM waliojulikana kwa jina la mtandao. Hili ni kundi ambalo limehusishwa na kila aina ya fitina, majungu, ukiukwaji wa taratibu, ufisadi na uozo mwingine ambao haukuwa sehemu ya chama hicho hapo kabla.

Kuna wakati, hasa katika miaka miwili ya kwanza ya utawala wa Rais Jakaya Kikwete, mtandao ulikuwa na nguvu kuliko hata CCM yenyewe.

Majina yote mazito katika siasa za Tanzania katika miaka 20 iliyopita yalihusishwa na kundi hili. Jakaya Kikwete, Edward Lowassa, Samuel Sita, Emmanuel Nchimbi, Rostam Aziz, Nazir Karamagi, Andrew Chenge, Yusuf Makamba, Didas Masaburi na wengine wengi walikuwa ndani ya kundi hili.

Tofauti ya mtandao na makundi mengine yaliyowahi kujitokeza huko nyuma ni kwamba lenyewe lilihusisha wanasiasa na wasio wanasiasa.

CCM imewahi kukumbwa na migogoro huko nyuma. Kwa mfano, wakati wa kutafuta mbadala wa Abood Jumbe na mbadala wa Mwalimu Nyerere mwaka 1985; kulikuwa na makundi mawili; Vijana na Wakombozi.

Vijana hawa walikuwa ni kizazi kipya cha wakati huo ambacho kimsingi kilikuwa kimelelewa na wakombozi ambao ni wanasiasa walioshiriki katika kutafuta Uhuru wa Tanganyika na Mapinduzi ya Zanzibar.

Lakini, makundi haya yote yalikuwa ya wanasiasa.
Lakini kwenye mtandao hali ilikuwa tofauti. Kulikuwa na wafanyabiashara maarufu waliokuwa wakifahamika kuuchangia. Kulikuwa na maofisa wa mabenki, makachero na wawekezaji.
Nilikuwa mwandishi wa habari mchanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005, wakati hasa niliposhuhudia ushawishi na ubabe wa kundi hili.

Nilishuhudia kurasa za magazeti zikibadilishwa wakati magazeti yakiwa yamepelekwa mitamboni. Nilishuhudia waandishi wasio wafuasi wa kundi hili wakihenyeshwa na kuonekana si kitu.
Nilishuhudia mwanadiplomasia mbobezi na mtu muungwana. Dk. Salim Ahmed Salim, akidhalilishwa kwa kutupiwa kashfa; na nyingine kuzushiwa kwa sababu ya kutoungwa mkono na mtandao huo wa ndani ya CCM.

Kwa macho yangu, niliona namna aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM (sasa Makamu Mwenyekiti), Philip Mangula, alivyoachwa bila usafiri kutoka ukumbi wa mkutano, baada ya mzee Makamba kuteuliwa kushika wadhifa wake.

Mangula hakuwa mwana mtandao na hakupendwa kwa sababu yeye ndiye aliyetoa taarifa za kimaadili zilizoonyesha namna vinara wa kundi hilo walivyosigina na kuvuruga taratibu zote kwenye mchakato wa kutafuta mgombea urais wa CCM mwaka 2005.

Mzee Mangula kwa unyenyekevu na fadhaa; na huku akitupiwa maneno ya dharau, alirejea kijijini kwake mkoani Iringa kufanya shughuli za kilimo. Mtandao ulidhamilia “kumshikisha adabu” kwa kufuata kwake maadili !

Wakati mtandao ukiwa katika kilele chake cha hatamu, Marekani ilikuwa inaongozwa na Rais George W, Bush. Baada ya tukio la ugaidi la Septemba 11, mbabe huyo wa vita alikuwa na kauli moja; “You are either with us or with enemy”.

Hiyo pia ndiyo ilikuwa kauli mbiu ya mtandao. Wale wote ambao hawakuwa upande wao; walikuwa ni watu wa kupatilizwa.

Baada ya Kikwete kuukwaa Urais na Uenyekiti wa CCM; mchezo ulibadilika. Zamani wazee wa busara walikuwa ni akina Pius Msekwa, Jaji Joseph Warioba, Joseph Butiku. Ndani ya mtandao; wazee wa busara wakaibuka kuwa wawili- Kingunge Ngombale Mwiru na Peter Kisumo.

Ni baada ya nguvu za mtandao kuanza kupungua, hususani katika ngwe ya pili ya utawala wa Kikwete, ndipo tulipoanza kusikia akina Warioba wakianza kuonekana “wapo”.
Nini kimeua mtandao?

Hili ni swali ambalo pengine litahitaji kufanyiwa utafiti zaidi na, inshallah, ninaweza kuja kulifanyia kazi huko mbeleni; lakini kwa sasa naweza kusema kwamba kazi kubwa sana imefanyika.

Nadhani kazi kubwa imefanywa na vyombo vyetu vya usalama hususani vile vya kikachero. Niliwahi kuambiwa na mmoja wa makachero waandamizi hapa nchini kwamba kwenye tasnia yao, kazi yao kubwa ni kumlinda Rais.

Hivyo, Kikwete alipoingia madarakani, kazi kubwa ya vyombo hivyo ilikuwa ni kuhakikisha kwamba hakuna mtu au kundi lenye nguvu kumzidi Kikwete. Hii ndiyo namna ambayo nchi zote zinaendeshwa.

Wakati Kikwete akiingia madarakani, kulikuwa na utatu mtakatifu kati yake na Lowassa pamoja na Rostam. Edward, ambaye sasa amehamia Chadema alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kampeni iliyomwingiza madarakani na Rostam ndiye alikuwa mmoja wa wana mkakati na wachangiaji wakubwa kifedha wa kundi hilo.

Rostam Aziz alikuwa na nguvu za ajabu wakati huo. Nakumbuka siku moja mwaka 2006, niliwahi kwenda ofisini kwake katikati ya jiji la Dar es Salaam na kukuta foleni.

Ndani, alikuwa akizungumza na mmoja wa mawaziri waandamizi wa serikali na mbele yangu kulikuwa na naibu waziri na aliyekuwa kigogo wa Idara ya Usalama wa Taifa wakati huo.
Alikuwa na mamlaka ya kuwapanga foleni mawaziri na mashushushu !

Ili kumlinda Kikwete, ilikuwa muhimu kwa vyombo vyetu kuhakikisha utatu huu mtakatifu unavunjika. Na hili si jambo la ajabu kufanyika.

Baada ya Fidel Castro kuingia madarakani Cuba, kulikuwa na utatu mwingine kati yake na Ernesto che Guevarra na Camilo Cienfuegos Gorriaran. Utatu huu ulivunjika kwa vifo vya wawili hao.

Ili Mao ze Dong atawale vema, ilibidi swahiba wake; Deng Xiao Ping aumie kule China. Deng alishushwa hadhi kiasi cha kutoka kuwa mtu wa pili kwa mamlaka baada ya Mao (kama ilivyokuwa kwa Edward na Jakaya) hadi kuwa mwangalizi wa matrekta ya kijiji !

Ili Jomo Kenyatta atawale vema Kenya; ilitakiwa Jaramogi Oginga Odinga aumie kidogo. Jaramogi angeweza kuwa Rais kabla ya Kenyatta lakini alikataa kwa masharti kwamba ni lazima kwanza swahiba wake huyo atolewe gerezani. Swahiba alipoingia madarakani, wa kwanza kuumia akawa Odinga !

Watu wanaweza kuwa na mawazo tofauti na yangu lakini nadhani kashfa ya Richmond ilikuwa ni sababu ya kumtoa Lowassa madarakani. Hii ilikuwa ni kashfa iliyomhusisha Lowassa na Rostam kwa wakati mmoja.
Hadithi ya kuua ndege wawili kwa jiwe moja !

Leo Lowassa yuko Chadema na Rostam anatumia muda mwingi kuishi Dubai.
Mtandao wakati wa Magufuli

Magufuli ni mmoja wa waathirika wa mtandao. Ile tu kwamba alidumu katika Baraza la Mawaziri la Kikwete kwa muda wote wa miaka kumi; hususani ile mitano ya kwanza, ni mojawapo ya maajabu ya kisiasa.

Magufuli hatakuwa na huruma wala hofu na mtandao. Watu wawili walibaki kuwa walezi wa mtandao ndani ya CCM; Lowassa na Emmanuel Nchimbi. Lowassa yuko Chadema na Nchimbi ni kama vile alijimaliza kisiasa kwa kupinga kukatwa kwa jina la Edward mwaka jana.

Mangula, bosi namba mbili wa CCM chini ya Magufuli anazifahamu na ameziishi vurugu za mtandao. Mwenyezi Mungu hawezi kumpa nafasi nzuri zaidi ya kulizika kundi hili.

Mtandao sasa utazikwa. Utazikwa kwa sababu hauna nguvu tena. Utazikwa kwa sababu pumzi yake muhimu; fedha, sasa haitakuwa na nafasi tena chini ya Uenyekiti na Umakamu wa Magufuli na Mangula.

Labda wakati umefika sasa wa kutoa mkono wa kwaheri. Buriani mtandao.

Raia Mwema

 
1469869447153.jpg
 
mtandao umeuawa na wenye chama tayari waliona namna chama kinatoka mikononi mwa wanachama na kuwa mikononi mwa watu ila panga kamili litakuja pale wakati chaguzi kuu za chama zinafanyika kwani yale masalia yote yataondolewa kama watabaki ni wachache lakini hawatakuwa na ushawishi wowote kwa upande wa serikali wakurugenzi,makatibu tawala,wakuu wa mikoa na wilaya wameshaondolewa
 
Lowassa bado anaota wafuasi wake ndani ya ccm wamuunge mkono
Ccm kwenyewe kwa moto unataka bado watu wakuunge mkono
 
mtandao umeuawa na wenye chama tayari waliona namna chama kinatoka mikononi mwa wanachama na kuwa mikononi mwa watu ila panga kamili litakuja pale wakati chaguzi kuu za chama zinafanyika kwani yale masalia yote yataondolewa kama watabaki ni wachache lakini hawatakuwa na ushawishi wowote kwa upande wa serikali wakurugenzi,makatibu tawala,wakuu wa mikoa na wilaya wameshaondolewa
Muwe na akiba ya maneno
 
Asante sana mkuu kalulukalunde sasa ninaelewa kwanini Jakaya alimtoa Othman kutoka ubalozini Uingereza kuja kuwa Mkurugenzi wa TISS. Pili kwanini Lowassa alikuwa na mategemeo makubwa ya kuwa mgombania wa CCM na tatu umemsahau mama Sophia Simba katika vinara wa mtandao, baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa UWT taifa limpigia vijembe mama Janeth Kahama kuwa "asishindane na watoto wa mjini".
 
Teh teh teeeh mwandishi wa hii makala kapiga mulemule yani...nikiwaza kitu ambacho sijawahi kiona wala kusikia popote zaidi ya kutumia mtazamo wangu na baadae nikaja kukisikia au kukisoma tena kutoka kwa mtu makini kama mwandishi wa makala hii ndipo napojikubali zaidi na kuamini hapa nilipofika hapatoshi, nijiongeze zaidi huenda nilizaliwa Nije kuwa mtu mwenye nguvu flani ndani ya jamii yangu...Genius Me!
 
Hii article imeandikwa vizuri saana. Lakini inaacha maswali kadhaa;
1. Ni nani aliyevunja mtandao kama ndio huo uliyemuweka madarakani Mh Kikwete?
2. Kwanini Kikwete hakuendeleza mtandao huo kama na yeye alikuwa mnufaika?
3. Kama neno ni mtandao, hivi mtandao maana yake ni majina ya hao wachache wanaofahamika?
4. Huu mtandao ambao unasemekana upo mpaka mwisho wa Kikwete, kwa Mkapa ulinusurika vipi, kwanini hakuuvunja na yeye yupo upande upi?
 
Back
Top Bottom