Biashara holela shubiri kwa usalama Morogoro

Biashara holela shubiri kwa usalama Morogoro

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
30
Reaction score
25
Machi mwaka 2019, maisha ya Bi. Mwajuma Rajabu mkazi wa Tubuyu, Kata ya Tungi, Manispaa ya Morogoro yalibadilika ghafla. Akiwa anauza samaki pamoja na wafanyabiashara wenzake pembeni ya barabara ya Boma, gari lililokuwa likipita lilipoteza mwelekeo na kuwavamia.

Ajali hiyo ilimjeruhi vibaya mguu, na baada ya kufikishwa hospitalini madaktari walilazimika kuukata ili kuokoa maisha yake. “Ilikuwa siku ya kawaida tu kazini. Ghafla gari lilituvamia. Nilipata majeraha makubwa sana mguuni, na baadaye ukakatwa. Tangu hapo nimebaki mlemavu,” anasema Mwajuma kwa huzuni.

Kwa Bi. Mwajuma, ajali hiyo haikumgharimu tu kiungo cha mwili, bali pia uhuru wa kujitegemea. Leo hii anaishi kwa kutegemea msaada wa watoto wake, tofauti na zamani alipokuwa akijitafutia kipato mwenyewe.
WhatsApp Image 2026-05-19 at 11.25.51.jpeg

Mkuu wa Idara ya Viwanda na Biashara Manispaa ya Morogoro John Kulunge

Kisa chake ni mfano halisi wa hatari inayowakabili maelfu ya wafanyabiashara wadogo wanaofanya biashara kando ya barabara katika Manispaa ya Morogoro, jambo ambalo licha ya hatari zake, limegeuka kuwa jambo la kawaida.

Katika mitaa kadhaa ya Manispaa ya Morogoro, hasa eneo la Msamvu katika Kata ya Mafisa hadi barabara ya Mazimbu katika Kata ya Kihonda, pamoja na maeneo ya katikati ya mji ya kata za Mji Mkuu, Kingo, Sabasaba na Boma, biashara kando ya barabara imekuwa zikifanyika hasa nyakati za usiku.

Vibanda vya muda, meza za mbao na bidhaa zilizotandazwa ardhini hutawala hifadhi za barabara, huku wafanyabiashara wakijipanga umbali mdogo (kwa kukadiria chini ya meta moja) kutoka barabarani vinakopita vyombo vya moto.
WhatsApp Image 2026-05-19 at 11.25.50.jpeg
Kwa macho ya kawaida, hali hii inaonekana kama juhudi za wananchi kujipatia kipato katika mazingira magumu ya kiuchumi. Hata hivyo, nyuma ya juhudi hizo kuna swali kubwa: je, mamlaka husika zinachukua hatua ipasavyo kusimamia sheria za mipango miji, matumizi ya barabara na usalama barabarani?

Sheria zinavyopuuzwa
Kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, kifungu cha 23 (1) na (2), ni kosa kwa mtu yeyote kufanya biashara ndani ya hifadhi ya barabara bila kibali rasmi cha maandishi.

Hata hivyo, wachuuzi wengi wanaendelea kufanya biashara katika maeneo hayo bila vibali. Rashidi Mohamed, dereva wa bajaji katika eneo la soko la Chifu Kingalu, anasema hali hiyo imekuwa chanzo cha msongamano na ajali.

“Barabara zinapungua upana kwa sababu meza na vibanda vinajengwa karibu sana na barabara. Magari, pikipiki na watu wanajikuta wanatumia njia moja. Ajali zinatokea mara kwa mara,” anasema Rashid na kuongeza:

“Watu wanaopita kwa miguu wanashindwa kutumia njia zao kwa sababu zimechukuliwa na wafanyabiashara. Mwisho wa siku wanapita barabarani pamoja na magari, hali inayoongeza hatari ya ajali.”

Kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 ya mwaka 1973, kifungu cha 49 (a) na (b) kama kilivyorekebishwa mwaka 2023, Jeshi la Polisi lina wajibu wa kuondoa vizuizi vyote vinavyovamia barabara na kuhatarisha usalama wa watumiaji. Lakini hali halisi ya Morogoro inaonyesha sheria hiyo haitekelezwi kikamilifu.

Hatari kwa walemavu
Mbali na madereva na watembea kwa miguu, kundi jingine lililoathirika zaidi ni watu wenye ulemavu. Shomari Mhando, ambaye ni mlemavu wa viungo anayetumia baiskeli ya magurudumu matatu, anasema uvamizi wa njia za watembea kwa miguu umepunguza uhuru wao wa kutembea.

“Njia za watembea kwa miguu zimegeuzwa sehemu za biashara. Sisi wenye ulemavu tunalazimika kupita barabarani pamoja na magari, jambo ambalo ni hatari sana,” anasema.

Hali hii inapingana na Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, kifungu cha 4 (1) kinachotaka mamlaka za miji kuhakikisha matumizi ya ardhi yanafanyika kwa usawa na kwa kuzingatia usalama wa wananchi wote.

Takwimu za jali
Takwimu za Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro zinaonyesha ukubwa wa tatizo. Katika kipindi cha miaka saba kuanzia 2019 hadi 2025, zaidi ya watu 100 waliuawa katika ajali zilizowahusisha wafanyabiashara na wateja waliokuwa pembeni ya barabara.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, anataja tukio la Septemba 28, 2024 kuwa miongoni mwa ajali mbaya. “Gari la kubeba taka lenye namba T 882 DQJ lilitoka barabarani na kuwagonga watu waliokuwa kando ya barabara eneo la Kihonda maghorofani. Watu wawili walifariki papo hapo,” anasema. Waliopoteza maisha katika tukio hilo ni Lisa Zakaria Josia (20) na Habibu Shabani Nassoro (63), huku wengine wawili wakijeruhiwa.

Kadhalika mkoa wa Morogoro una kumbukumbi ya tukio la Alhamisi, Agosti 15, 2019 wakati watu zaidi ya 70 waliporipotiwa kupoteza maisha na maakumi wengine kujeruhiwa, katika ajali ya lori la mafuta eneo la Msamvu. Miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo ni mama kina mama lishe kadhaa ambao walikuwa wakifanya biashara ya chakula pembezoni mwa barabara.

Kwa mujibu wa wataalamu wa usalama barabarani, ajali nyingi katika maeneo ya mijini hutokea kutokana na uvamizi wa hifadhi za barabara pamoja na shughuli zisizo rasmi karibu na barabara, hali inayoongeza hatari kwa watumiaji wote wa barabara.

Simulizi ya mtoto anayejulikana kwa jina la kubuni Bakari Hassan inaakisi athari za majanga hayo ni yatima aliyempoteza mama yake mzazi katika ajali ya gari lililowaka moto. Baada ya tukio hilo aliachwa bila mzazi, na kwa sasa anaishi chini ya malezi ya wasamaria wema wanaojitolea kulea watoto yatima.

Athari za kiafya
Mbali na ajali, wataalamu wa afya wanasema biashara kando ya barabara pia zina madhara kiafya. Mtaalamu wa afya ya jamii katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro anasema wafanyabiashara hawa hukaa muda mrefu wakivuta moshi wa magari.

“Moshi wa magari una kemikali hatari zinazoweza kusababisha pumu, kifua sugu na magonjwa mengine ya mfumo wa hewa,” anasema na kusisitiza kuwa hali hiyo ni hatari zaidi kwa watoto na wajawazito.

Chembechembe za metali nzito kama risasi zinazotoka kwenye moshi wa magari zinaweza kusababisha shinikizo la damu kwa wajawazito, kuharibika kwa mimba au mtoto kuzaliwa akiwa na uzito mdogo.

Kwa watoto wadogo, kemikali hizi zinaweza kuathiri ukuaji wa ubongo na kupunguza uwezo wa akili.

Uharibifu wa mazingira
Uchunguzi pia unaonyesha biashara hizo zinaathiri mazingira ya mji. Sophia Kalinga, Mkurugenzi wa Shirika la Unganisha Environmental Conservation, anasema taka zinazotokana na biashara hizo mara nyingi hutupwa kwenye mitaro.

“Taka za plastiki, mabaki ya vyakula na maji machafu huziba mitaro na kusababisha mafuriko wakati wa mvua. Hali hii pia huongeza hatari ya magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu,” anasema.

Kwa mujibu wa Kanuni za Usimamizi wa Mipango Miji za mwaka 2018 (Sehemu ya 17–19), halmashauri zina jukumu la kutenga maeneo maalum ya biashara ili kulinda mpangilio wa miji na kuzuia mwingiliano hatari kati ya watu na vyombo vya usafiri.

Uchumi na Usalama
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoa wa Morogoro, Bw. Emmanuel Ndyamukama, na Afisa Mwandamizi Mkaguzi wa barabara wa Wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Morogoro, Bw. Benjamin Mwendapole wanakiri wachuuzi kuendesha biashara kando ya barabara ni hatari kwa wafanyabiashara na pia huathiri barabara.

Hata hivyo, ukweli unaobaki ni kwamba wafanyabiashara wengi wanategemea maeneo hayo kupata wateja kwa urahisi. Hali hii inaonyesha mgongano kati ya mahitaji ya wananchi kujipatia kipato na wajibu wa serikali kulinda usalama na mpangilio wa miji.

ANDIKO LA: Farida Mangube, Morogoro
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Back
Top Bottom