BAK
JF-Expert Member
- Feb 11, 2007
- 124,825
- 287,849
Bei ya umeme Z'bar yafikishwa kwa Lowassa
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima
SAKATA la kupanda kwa bei ya umeme Zanzibar limezidi kupata sura mpya baada ya viongozi kuamua kulifikisha suala hilo kwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na Waziri Kiongozi wa SMZ, Shamsi Vuai Nahodha.
Katika maamuzi yaliyofanywa hivi karibuni, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Mafuta (EWURA), iliruhusu Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 21.7 kwa Tanzania Bara na asilimia 168 kwa Zanzibar, kwa maelezo kuwa kwa muda mrefu bei ya umeme Zanzibar ilikuwa ya chini mno.
Suala hilo limefikishwa katika ngazi hizo za juu baada ya kukosekana kwa muafaka kutokana na majadiliano yaliyokuwa yakiendelea tangu kutangazwa kwa bei hizo mpya.
Hayo yalielezwa na Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Salum Hassan, alipozungumza na Tanzania Daima kuhusiana na kikao kilichowahusisha viongozi kutoka Zanzibar na Tanzania Bara, kujadili suala la ongezeko la bei ya umeme.
"Baada ya kikao, uamuzi uliofikiwa ni kwamba suala hilo ajenda yake itapelekwa kwa viongozi wa juu, Waziri Mkuu Lowassa na Waziri Kiongozi, Shamsi Vuai Nahodha kutafutiwa ufumbuzi," alisema.
Hassan alisema katika kikao hicho, menejimenti ya Tanesco ilibainisha kuwa katika mapendekezo yake, ilitaka bei ya Zanzibar ipandishwe kwa asilimia 39 tu, lakini jambo la kushangaza, EWURA imepandisha kwa asilimia 168.
Alieleza kwamba katika kikao hicho, menejimenti ya EWURA ilijitetea kuwa haikufahamu mapendekezo ya Tanesco na ndiyo maana ikapandisha kwa kiwango hicho.
Alisema kwa kuwa viwango hivyo vya bei vinapangwa na Bodi ya EWURA kupitia chombo maalumu cha udhibiti wa huduma za nishati na maji, menejimenti ya EWURA haina uwezo wa kutengua maamuzi yake.
"Wenzetu wa EWURA wamesema hawana uwezo wa kutengua maamuzi yaliyofikiwa na bodi ndiyo maana tumeamua suala hili tulipeleke ngazi za juu za uongozi litafutiwe ufumbuzi," alisema Salum.
Alieleza hadi sasa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), linaendelea kutumia bei ya zamani hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi.
Salum alisema iwapo bei mpya zilizopendekezwa na EWURA zitatumika, wananchi wa Zanzibar wataathirika kwa kiasi kikubwa kwa vile kima hicho hakilingani na kipato cha wananchi.
Alisema hivi sasa Zanzibar inatumia megawatt 40 za umeme na kutumia kati ya sh milioni 800 hadi 900 kwa mwezi kwa ajili ya kununua umeme huo.
Ofisa huyo alisema kulingana na viwango vipya vilivyotangazwa na EWURA Zanzibar, hivi sasa italazimika kutumia sh bilioni 2.1 kwa mwezi kununua umeme, kiwango ambacho ni kikubwa mno.
"Tutaendelea kutumia viwango vya zamani hadi hapo vikao vya ngazi ya juu vya viongozi watakapolipatia ufumbuzi tatizo hilo," alisema.
Aliwataka wateja wao kuondoa wasiwasi kwa vile serikali inaendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo, ili kuepusha athari iwapo viwango vipya vitaanza kutumika.
Wiki iliyopita ujumbe kutoka Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) na baadhi ya maofisa wa Wizara ya Maji, Nishati na Ardhi Zanzibar, ukiongozwa na Meneja wa ZECO, Juma Ishaq, walikwenda Dar es Salaam katika mchakato wa kulizungumzia suala hilo.