Bashungwa Ashiriki Misa ya Kutabaruku Kanisa la RC Visiga, Aipongeza WAWATA

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,897
941
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameupongeza Umoja wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele kujitoa katika maendeleo ya kanisa na kutegemeza kazi za Kanisa Katoliki Tanzania.

Bashungwa ameeleza hayo leo Feburuari 10, 2024 katika Misa Takatifu ya kutabaruku Kanisa la Seminari ndogo ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Visiga, Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es Salaam iliyoongozwa na Mhashamu Askofu Mkuu, Jude Thaddaeus Ruwa’ichi.

“Pamoja na michango yetu waumini katika ujenzi wa Kanisa hili la Visiga, niwapongeze WAWATA kwa michango na kazi kubwa mnayofanya katika kuhudumia na kujenga Kanisa, hakika WAWATA ni jeshi imara la Kanisa letu”, amesema Bashungwa.

Katika Misa hiyo, Waziri Bashungwa amepokea ombi la ujenzi wa barabara kutoka njia panda ya barabara kuu ya Morogoro - Dar es salaam inayoelekea katika Seminari hiyo, ambapo ameeleza kuwa Serikali inaenda kujipanga kuhakikisha kipande cha barabara hiyo cha kilometa 1.2 kinatengenezwa.

“Mheshimiwa Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi, kwa niaba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, naomba niahidi kuwa Serikali tunaenda kujipanga kutengeneza barabara kutoka barabara kuu hadi hapa Seminari ili ipitike vizuri”, amesema Bashungwa.

Aidha, Waziri Bashugwa ametoa wito kwa waumini wa Kanisa Katoliki kuendelea kijitoa katika kazi za Kanisa na akaahidi kuendelea kushirikana na uongozi katika upatikanaji wa fedha za kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.

“Tumeelezwa pamoja na mafanikio ya kujenga kanisa zuri, bado tunalo jukumu la kukamilisha, mimi naomba nichukue jukumu la kuchangisha milioni 10 na kuileta ndani ya mwezi mmoja” amesema Bashungwa.

Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo kuu la Dar es salaam, Mhashamu Jude Thaddaeus Ruwa’ichi amepongeza Waumini na Viongozi wote walioshiriki katika ujenzi wa Kanisa la Seminari ya Visiga ambalo lipo chini ya usimamizi wa Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA).

“Niwashukuru WAWATA ambao mmeshiriki kwa kiwango kikubwa kufanikisha kazi ya ujenzi wa Kanisa na nimpongeze Waziri Bashungwa kwa kuwa mkeleketwa wa kanisa lake, naomba uendelee kuwa kiungo kizuri na kuitangaza Injili huko Bungeni na Serikalini”, amesema Askofu Mkuu Ruwa’ichi.

WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.08.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.09.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.10.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.12.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.13.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.14.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.14(1).jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.15.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.38.jpeg
WhatsApp Image 2024-02-10 at 16.50.39.jpeg
 
Back
Top Bottom