SoC02 Barua kwa Mtoza ushuru!

Stories of Change - 2022 Competition

Tyler Durden

Member
Aug 5, 2021
73
114
Katika pitapita zangu mtandaoni wiki hii. nilikutana na habari moja ambayo haikuvuma sana, labda kwa sababu ya mambo chungu nzima ya umbea na vituko yavumao kila uchwao katika mitandao ya kijamii nchini.

Habari hiyo ni ile inayohusu uchumi na sarafu ya nchi ya Zambia kupaa maradufu. Ni wazi sasa Zambia iliyo chini ya mfanyabishara na mchumi nguli Bwana Haikande Hichilema. inakuwa nchi nyengine tunayoishuhudia ikipiga hatua kubwa kiuchumi huku sisi tukiwa palepale, baada ya Rwanda na Kenya kufanya hivo miaka ya hivi karibuni!

Mwanamuziki nguli wa miondoko ya kufoka foka na Mbunge mstaafu Bwana Joseph haule a.k.a Profesa Jay aliwahi kusema tunapiga hatua tatu mbele kisha hatua mbili nyuma halafu tunajipongeza. Nadhani mwendo huu wa mlevi ndio umetufanya tumekuwa tukiwaangalia tu hawa majirani zetu wakipaa kila uchwao.

Lakini, Zambia wenyewe wamewezaje kufanikisha haya bila TOZO? Tena baada ya janga la korona na vita vya urusi na ukraine ambayo sisi tumefanya sababu za kuleta tozo?

Kenya , Rwanda, Zambia wote hawa walikuwa na karantini zisoisha, miezi mingi walikaa tu ndani bila kufanya lolote, lakini bado wanapandisha mishahara, uchumi unakua , demokrasia inaongezeka maradufu, na bila kusahau hawana kodi mlundikano kama huku kwetu iliyobatizwa jina la Tozo.
Niweke mambo sawa ,KODI ni muhimu sana na ni msingi wa taifa lolote linalotaka kupiga hatua kimaendeleo.

lakini KWAMWE kodi haiwezi kuwa suluhisho la kila tatizo kama tunavyoaminishwa sasa, zaidi sana inamuumiza tu mwananchi wa Hali ya chini (kama tunavyoshuhudia sasa).

Iko hivi ngoja nikuibie siri kidogo, nimefanya sana biashara, katika watu wajanja nimewahi kukutana nao ni wafanyabishara, hawa watu wanatumia akili nyingi sana, kila TOZO au kodi utakayomlundikia atahakikisha haibebi yeye, bali mwananchi wa kawaida au kwa jina lingine mlaji wa mwisho. Anafanya haya kwa kupandisha tu bei....hapo tunapata mfumuko mkali sana wa bei kama tunaoushuhudia kwa sasa.

waziri husika umeshika nyundo, kila mwanya unaopata unaponda tu...wanaoweza kuzuia ambao ni wawakilishi wetu nao nguvu hawana, sababu mamlaka yao walipewa na wenye mamlaka na sio wenyenchi. Wananchi na hasa wa Hali ya chini wamebaki mayatima hakuna kudeka tena kama zamani. Tunaimba wimbo mmoja sasa.

Hizi TOZO ni kama vile mti wa mchongoma ambayo umekomaa sasa na umeanza kuchoma watu .Tunapiga kelele baada ya miiba kukomaa huku tukisahau sisi ndio tuliutunza mti huu, tukaumwagilia maji, ukatoa maua na hatimaye miiba.

Tumefikia haya ya TOZO kwa sababu ya mambo makuu matatu.

1. Demokrasia mfu....hakuna kitu kibaya kama kuongozwa na mwanasiasa ambaye anajua hata avurunde vipi wewe mwananchi huna uwezo wa kumuengua, uhakika atakutenda atakavyo. Tumeshuhudia chaguzi ya juzi ya majirani zetu kenya! Unadhani wawakilishi wao wataenda kuwa upande wa Nani wakifika mjengoni? hasa baada ya kuenyeshwa kweli kweli kwenye maboksi ya Kura zilizokuwa na uwazi mkubwa ni mfaidika wa mfumo tu ndio hatakubalina na Mimi nikisema tunahitaji tume ya uchaguzi yenye uwazi kama ilivyo kwa majirani zetu.

2. Miswada na sheria zinazopitishwa bungeni, miswada iliyopitishwa na kusainiwa na raisi kuwa sheria ikiwamo hizi za tozo zililetwa na hawahawa wawakilishi wanaotuwakilisha! Ifike mahali mambo nyeti kama haya tusiishie kuwaamini hawa wawakilishi wetu ambao wengine tunasikia wanavuta majani kabla ya kuingia mule.

Hivi Ulishawahi kumuhoji mbunge wako kwanini alipitisha hizi tozo? ilihali akijua madhara yake? Hivi huwa wanapimwa afya ya akili? Maana mambo mengine hayafikiriki. Ifike mahali wananchi tujue kuwa hawa wawakilishi tunawapa makucha ambayo muda mwengine huweza kuturarua sisi wenyewe hadi kutumaliza. Tusikubali kuchaguliwa watu wa kutuwakilisha...tusikubali wapite bila kupigwa, tunajichimbia makaburi yetu wenyewe bila kujua.

3. Uelewa mdogo wa maswala ya kiuchumi. Mwanafalsafa mmoja aliwahi kunukuliwa akisema umahiri katika fani yeyote hupimwa na uwezo wako wa kutatua matatizo....kwanini sisi tunatatua matatizo kwa kuongeza matatizo...tayari tuna watu walio tayari kulipa kodi bila shuruti kwa nini tunazidi kuwalundikia (kiingreza wanaita double taxation) ni kama vile unaadhibiwa kwa kufanya vizuri. Naamini wapo na tupo wenye uweo wa kufanya au kushauri na nchi inapiga hatua bila hatua bila Tozo. Tujiulize Thailand wamepiga hatua sababu ya tozo? Singapore je? Vipi China? Malaysia? Hizi ni nchi ambazo kwa nyakati Fulani tulilingana uchumi! Wakifika hapo walipo wa TOZO ? Tubadilike.

NIni kifanyike sasa

1.Tuongeze fedha za kigeni!
Fedha za kigeni huja kwa utalii, kuuza raslimani, au bidhaa mbalimbali. Naona sisi ni kama tumeweka kambi kwenye utalii pekee...tunakosea sana...tunamwezeshaje mwanachi anayezalisha bidhaa bora mfano kandambili za ngozi halisi, kuuza nje ya nchi? Bado kuna danadana nyingi ukitaka kutoa bidhaa ndani kuipeleka nje! ukilinganisha na majirani zetu Kenya. Kwanini tunaruhusu hili? Tukija kwenye utalii kwanini tunan'gan'gania utalii wa wanyama pekee? Hivi tunafahamu kwamba dubai inapokea watalii mamilioni kila mwaka ilihali hawana wanyama?

Watu huenda tu kuchezea mchanga wa jangwa na kuogelea na pongwe? Tanzania tuna kimondo mbeya, maporomoko ya maji kila kona! Fukwe nzuri kuliko za giriki zinazowazuzua mabwanyeye huko ulaya, chakula kizuri, n.k...kwanini tusitangaze fukwe zetu kama tunavyoutangaza mlima? Tuna maelfu ya viutio vya utalii je vinafikika kiurahisi? Tuamke , huku kuna fedha nyingi kuliko tunazopata kwenye tozo kama tukichanga karata zetu vizuri!

2. Vijana ,vijana, vijana,
Miaka 20 ijayo taifa litakuwa linaongozwa na vijana. Vijana hawa hawa tunaoonekana si lolote si chochote kwa sasa. Ifike mahali vijana tuanze kushirikishwa kwenye masuala nyeti kama haya ya tozo. Ili uzee wenu muishi kwenye nchi salama. Mnaweza mkawa mmetuzidi uzoefu, umri busara n.k. lakini haibadilishi ukweli kwamba vijana wa sasa wana utandawazi zaidi, ujanja zaidi na maarifa pia, tuwe warahisi kuingiza damu mpya na mawazo mapya. Ni kama kwenye timu za mpira wa miguu huwezi kuta wachezaji wote ni wakongwe, lazima uingize chipukizi pia , huwa wanaokoa jahazi kunchi. muda mwengine!

3.Mtandao wa intaneti
Tukitaja orodha ya matajiri kumi wakubwa duniani lazima sita kati yao wanajishughulisha na biashara za mtandao wa intaneti, mfano wamiliki wa mitandao ya Google, Facebook, Amazon, Netflix, n.k.
Kwanini sisi tunaiona mitandao kama dubwana baya linalotisha, ilihali tulitakiwa kuikumbatia kwa mikono yetu miwili?

Dada yangu ni mahiri sana wa kusuka! Leo hii anaweza kuonyesha umahiri wake kwenye mtandao wa YouTube na kuingiza hadi fedha za kigeni! Lakini eti analipishwa ! sababu kuna John wa sinza anautumia huo huo mtandao kumtusi kiongozi. Ama kweli Kiroja cha mwaka.

Hivi Kuna kiwanda chochote kinaweza kuzalisha ajira ambazo mtandao unaweza kutupatia? Nawauliza nyie viongozi! La hasha ! Hasa kwanini mnaipinga? Ni kwa maslahi yenu sio? Au tumerogwa? Mi sijui.

4. Uzalishaji, uzalishaji, uzalishaji,? Tanzania tuna Gesi, Mafuta, Tanzanite, dhahabu, almasi, Rubi, chuma, miti asili, mafundi, kahawa, asali, mpunga, ufuta, korosho, pamba, mkonge, maua, mtama, mihogo, matunda kila aina, siwezi kutaja malighafi zote hatutamaliza.

Hivi tunawezaje kuwa na haya yote na zaidi tuna ardhi kubwa yenye rutuba, halafu unaendesha nchi kwa Tozo? Kwanini tusiende nchini Misri kuwauliza wamewezaje kuwa wazalishaji wakubwa wa juisi na matunda duniani ilihali wana mto mmoja pekee..(Nile) ambao chanzo chake ni Tanzania, (hapo kwanza ncheke).....mi naamini tunaweza.

5. Tuongeze usimamizi wa fedha za miradi ya ndani.....Tozo zinaibuka kila uchwao sababu pesa zinazotengwa kwa ajili ya kuleta maendelea zinapigwa na wachache, sote tumeona kibanda cha mlinzi cha mamilioni, bila kusahau ripoti za kila mwaka za mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali zilizojaa madudu...swali ni, kwanini wafujaji wa hizi fedha bado tunakunywa nao kahawa huku mitaani? ilhali kuna vijana wapo magerezani kwa kesi za kuiba kuku? Tulianzisha mahakama ya ufisadi kwa ajili ya kina Nani sasa? Kungekuwa na uwajibishwaji kwa wabadhilifu hawa ikiwapo kufilisiwa kabisa kungepunguza mzigo kwa serikali kama sio kuondoa kabisa izi Tozo.

6. Tozo zilipwe na makampuni ya simu na mabank kwa kushirikiana na wananchi.....ukifanya miamala utaona kuna kiasi kinakatwa kwa ajili ya tozo! Na kuna kiasi makampuni huchukua kama faida....lakini ukichunguza utaona makampuni yanachukua mara mbili ya fedha inayochukliwa na serikali, nadhani serikali zinaweza kuja na mbinu ya kuichukua kiasi cha tozo kutoka kwenye faida inayokatwa na mitandao ili kumpunguzia makali mwananchi wa kawaida.

7. Tozo na kodi mbalimbali zingeingizwa kwenye mfumo kwa awamu. Kuzileta zote kwa pamoja ni kumuumiza mwananchi ambaye kipao chake hakijaongezeka kama sio kupungua. ....mfano Tozo za miamala zingeletwa mwaka wa fedha 20/21, Tozo za jengo zinazokatwa kwenye luku zingeletwa mwaka wa fedha 22/23 n.k hii ingesaidia mwananchi kuzikubali kiurahisi.

8. Elimu ya kodi ifundishwe kuanzia shule za msingi, leo hii Mtanzania anafanya manunuzi bila kudai risiti kwa sababu hana elimu ya umuhimu wa kodi.. Hakuna mwananchi anaelewa umuhimu wa hizi tozo. Inahitajika elimu kubwa itolewe kuhusu umuhimu wa kodi kwa mstakabali wa maendeleo ya nchi na pia matumizi ya kodi na tozo hizi yawe wazi kwenye magazeti ya serikali na mbao za matangazo katika kila halmashauri. Ni fedha za wananchi na ili wakubali kuendelea kutoa lazima waoneshwe na zinavyotumika.

9. Nafasi nyeti kama uchumi wa nchi tunaweza kuitengalisha na siasa na kuangalia zaidi uwezo na elimu ya mtu..kumekuwa na historia ya mawaziri wengi wa fedha kutodumu nchini, labda sababu wengi hawana uwezo sahihi wa kusukuma hili gurudumu.

Kama tunao wataaalamu wa uchumi manguli kabisa (naamini tunao) tusisite kuwatumia na kigezo cha kuwa sio wanasiasa tusizingatie.

10. majadiliano ya miswada bungeni ambayo baadaye huwa sheria mfano hii ya tozo isihusishe wawakilishi (wabunge) pekee.

Wawakilishi wengi wapo kwa ajili ya matumbo yao. Tunaweza kuichukua maoni kutoka kwenye mabaraza ya vijana, vikundi vya wanawake, vyuo vikuu (mwalimu vyerere alipenda sana kuwatumia hawa) vyama vya upinzani, dayaspora. Maoni mbalimbali katika mitandao ya kijamii .n.k hii itatusidia kupata mawazo mpya kutoka kwa wahusika haswa wa sheria hizo bila kusahau mijadala na upitishwaji wa sheria hizo uwe wa wazi.

Naamini bado kama nchi tunaweza kujirekebisha na sio kila siku tunatatua matatizo tuliyoyaanzisha wenyewe huku tukijipigia makofi.
Wako mwananchi.
Mwenye nchi.
Mwisho.
 
Back
Top Bottom