na hii ni nukuu kutoka mwandishi Mohamed Said....
[SIZE=+2]Kuvunjwa kwa jumuia ya EAMWS[/SIZE] HII ni sehemu ya nane ya mfululizo wa makala ambazo ni sehemu ya muswada wa kitabu "Mwalimu Julius K. Nyerere, Kanisa Katoliki na Uislamu: Dola na tatizo la Udini Tanzania" kitakachotoka hivi karibuni. Kitabu hicho kimeandikwa na mwandishi maarufu wa masuala ya historia hasa ya Tanganyika BWANA MOHAMMED SAID.
MKUTANO wa Iringa ulipitisha katiba ya jumuiya mpya ya Waislam, katiba ambayo ilikuwa sawasawa na katiba ya TANU. Hivi ndivyo BAKWATA ilivyoundwa.
BAKWATA ikamchagua Saleh Masasi, Muislam tajiri na ambae alikuwa kama mwenyekiti wa mkutano ule kuwa Mwenyekiti wa Taifa na Adam Nasibu akawa Katibu Msaidizi. Nafasi zote za juu katika BAKWATA kama ilivyotegemewa zilichukuliwa na kundi la Adam Nasibu, kundi ambalo toka mwanzo lilikuwa likidai kuvunjwa kwa EAMWS.
Uongozi wa BAKWATA uliomba serikali itambue jumuiya hiyo mara moja na ipige marufuku EAMWS kama jumuiya isiyo halali na mali zake zizuiwe. BAKWATA ilitoa maazimio kadha lakini azimio namba nne ndilo hasa linafaa kuelezwa. Azimio hilo liliomba serikali, TANU na ASP kuwatazama na kufanya uchunguzi wa kina kwa viongozi wote wa EAMWS, hasa Rais, Makamo wa Rais, Katibu wao na baadhi ya viongozi wa mikoa na wilaya ambao wana chuki na hii jumuiya mpya.[SUP]70[/SUP] Uongozi wa BAKWATA katika ushindi wao hawakutaka salama na mawaelewano na Waislam wenzao katika EAMWS wala kuwaonea huruma kama Uislam unavyofundisha, bali ulitaka chama na serikali uwaandame, hasa wale waliokuwa viongozi.
Baada ya kuundwa BAKWATA, ili kuondoa wasiwasi na kuwarudishia imani Waislam, Katibu wa Tume ya Waislam, Mussa Kwikima alitoa taarifa iliyosema:
Hakuna anaeweza kutishia kuwepo kwa EAMWS isipokuwa wanachama wake, sheria na serikali, lakini si watu binafsihata ikiwa mikoa yote kumi na saba ikijitoa haitamaananisha kuwa jumiya imekufa kwa kuwa kuwepo kwake hakutokani na kuwepo kwa mikoa hiyo kama wanachama isipokuwa kuwepo kwa wanachama wake, Waislam.[SUP]71[/SUP]
Wakati ilipotoka taarifa hii BAKWATA ilikuwa bado haijaandikishwa rasmi na Msajili wa Vyama. Kisheria ilikuwa haiwezekani kwa kundi la Adam Nasibu kuunda jumiya mpya iliyokuwa na malengo sawa na jumuiya ambayo tayari ishaandikishwa. Kwa muda wa siku tatu BAKWATA na EAMWS zikawepo kwa wakati mmoja. Ilionekana kama kwamba EAMWS itashinda vitimbi vya serikali na vya kundi la Adam Nasibu.
Tarehe 19 Desemba, 1968 serikali kama vile imegutushwa na taarifa ya Kwikima, iliipa BAKWATA Cerificate of Exemption na kuifungia EAMWS.[SUP]72[/SUP] Waziri wa Mambo ya Ndani Said Ali Maswanya kwa niaba ya serikali alitoa taarifa fupi:
Waziri wa Mambo ya Ndani kwa kuamriwa na Rais anatangaza kuwa tawi la Tanzania la East African Muslim Welfare Society na Baraza la Tanzania la la East African Muslim Welfare Society ni jumuiya zisizotambulika kisheria chini ya kifungu 6 (i) cha Sheria ya Vyama.[SUP]73[/SUP]
Kwa tangazo hilo la Rais wa Tanzania, Julus Nyerere, Waislam walinyimwa nafasi ya kukutana na kuzungumza kuhusu tatizo ambalo kwa kweli liliwahisu Waislam peke yao. Kwa ajili hii basi Waislam walinyimwa nafasi ya kujadili na kulitolea uamuzi tatizo hilo.
Viongozi wa EAMWS waliitwa mbele ya Kabidhi Wasii ambae ndiye alikuwa amekabidhiwa na serikali jukumu la kusimamia shughuli za kufunga rasmi shughuli za EAMWS. Viongozi walifahamishwa kuwa chini ya sheria ya vyama mali zote za EAMWS zitauzwa na madeni yatalipwa kutokana na fedha hizo na fedha zitakazobaki watapewa wanachama. Serikali ilikuwa haiwezi kufanya kama sheria ilivyokuwa imeelekeza. Ilikuwa jambo zito sana kwa serikali ya Nyerere kuonekana anasimamia kuuzwa kwa mali za Waislam. Viongozi wa EAMWS walipoitwa kwa Kabidhi Wasii mara ya pili walifahamishwa kuwa serikali imebadilisha mawazo yake kutekeleza amri kama sheria inavyosema kwa ajili hiyo basi imefanya mabadiliko ya sheria ya vyama ambayo yanaiwezesha sasa kutoa mali ya EAMWS na kukabidhi BAKWATA. Hivi ndivyo mali za EAMWS zilivyochukuliwa na kupewa BAKWATA bila ya ridhaa ya Waislam wenyewe. Hivi ndivyo shule zote zilizojengwa na EAMWS pamoja na mradi wa Chuo Kikuu cha Kiislam kilipoanguka katika mikono ya kundi la Adam Nasibu. BAKWATA haikuwa na uwezo wa kuendesha mipango yoyote na taratibu shule na miradi yote ya elimu ikafifia na mwishowe kufa kabisa. Hivi ndivyo halikadhalika moto wa Waislam uliowashwa kwa kupatikana kwa uhuru waliopigania hadi ukapatikana ulivyokufa. Moto huu ulikuja ukawaka tena, lakini hiki ni kisa kingine. Insha Allah Mwenyezi Mungu akipenda tutakuja kukieleza.
Huu ndiyo ukawa mwisho wa kile kilichokuwa kikijulikana kama mgogoro wa Waislam ulivyomalizika. Mgogoro ambao ulianza pale mwalimu wa shule ya msingi asiyefahamika na yeyote alipofanya maandamano katika mitaa ya Bukoba akimuunga mkono Julius Nyerere na Azimio lake la Arusha na ukaishia kwa mwalimu huyu akiwa na nafasi juu katika jumuiya ya Kiislam ambayo ilikuwa ikichukiza machoni mwa Waislam. Mwalimu huyu ambae sasa amekuwa Makamu Katibu Mkuu wa BAKWATA alianza kazi yake kwa kuwashutua Waislam. Katika mkutano wa waandishi wa habari Adam Nasibu aliiomba TANU na ASP kujikinga na watu wanaohujumu umoja wa nchi kupitia dini. Akaendelea na kusema kuwa BAKWATA ni sawa na Baraza la Kikristo la Tanzania. [SUP]74[/SUP] Kwa kuwa Waislam walinyimwa fursa ya kujadili "mgogoro' hivi sasa kilichobaki na dhana tu, kuwa nini kingelitokea endapo wangeliruhusiwa kufanya mkutano ule ulioitishwa na EAMWS. Waislam wa Bukoba ambao ilitaarifiwa kuwa walifanya maandamano kuunga mkono Azimio la Arusha hawakutayarisha maandamano ya kuunga mkono BAKWATA. Dar es Salaam na katika miji mingi ya Tanzania, neno BAKWATA halina tofauti na tusi. Kumuita Muislam kuwa yeye ni mwanachama wa BAKWATA ni sawa na kumuita Mkristo mfuasi wa Yuda Iscariot, aliyemsaliti Yesu kwa vipande thelathini vya fedha.
Mjumbe mmoja wa Tume ya Waislam inastahili kuelezwa habari zake - Mussa Kwikima. Mussa Kwikima mwaka 1968 alikuwa ameteuliwa kuwa jaji na Rais Nyerere. Yeye ndiye hasa alikuwa nguvu kuu katika tume ya Waislam. Wakati alipojitolea kuisaidia tume katika kupambana na kundi la Adam Nasibu, Waikela alimuonya kuhusu hatari ambayo itamkabili yeye mwenyewe binafsi na kazi yake. Kwikima alijibu kuwa umoja wa Waislam ni muhimu kuliko maslahi yake binafsi. Ilipoundwa BAKWATA na hapo kuwa ndiyo mwisho wa 'mgogoro', Kwikima alihamishwa kutoka Dar es Salaam na kupelekwa Mwanza kama Hakimu Mkazi na Rais Nyerere akamvua madaraka ya ujaji wake. [SUP]75[/SUP]
Kilichobakia baada ya kuvunjika kwa EAMWS ilikuwa ni kujaribu kuiweka BAKWATA katika mikoa kama jumuiya inayowakilisha Waislam wote wa Tanzania Bara. Mwaka mzima wa 1969 Adam Nasibu na kamati ya watu wanne walitembea katika mikoa wakiahidi msaada wa fedha kwa katibu yeyote wa zamani wa EAMWS ambae atashirikiana na BAKWATA makao makuu kuisaidia kufungua ofisi katika mkoa wake. Waislam waliipuuza BAKWATA.
Tabora ambayo haikujitoa katika EAMWS, serikali iliwaruhusu Adam Nasibu na kikundi chake kufanya mkutano wa hadhara. Kabla Adam Nasibu hajahutubia Waislam, Maulid Kivuruga mmoja wa wakongwe wa African Association na muasisi wa TANU Tabora, alipanda jukwaani kwa niaba ya Waislam wa Tabora na kuweka sharti kuwa Waislam watakuwa tayari kumsikiliza Adam Nasibu endapo Waikela mjumbe wa Tume ya Waislam iliyokuwa ikitafuta sulhu na yeye ataruhusiwa na serikali kuwahutubia Waislam ili aeleze upande wa pili wa kisa kile. Kivuruga alisema kuwa Waislam wanaomba sharti hili likubaliwe kwa sababu katika Uislam panapotokea mgogoro basi mpatanishi ni lazima asikilize pande zote mbili. Sharti hili lilikataliwa na BAKWATA na serikali. Palepale mbele ya waheshimiwa wa serikali na viongozi wa BAKWATA, Waislam wakaanza kuzomea huku wakitawanyika wakipiga takbir na wengine wakiitikia Allahu Akbar.
Siku chache baada ya tukio hili Waikela aliitwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai kusailiwa kwa nini anaipinga BAKWATA. Wakiwa ndani ya chumba cha Tabora Hotel, Geoffrey Sawaya, Mkrugenzi wa C.I.D, alimpiga maswali Waikela na kutaka kujua kwa nini yeye hayuko tayari kushirikiana na serikali kuipa nguvu na kuieneza BAKWATA. Sawaya akatoa hongo ya shilingi elfu arobaini kwa Waikela ili asaidie kuimarisha BAKWATA. Waikela kama istizai alimuuliza Sawaya kama fedha zile zilikuwa zimetoka bait mal. Waikela alikataa kupokea hongo ile. Sawaya akamtisha lakini Waikela hakutishika. Waikela aliwekwa ndani ya chumba kile akiulizwa maswali kwa kiasi cha saa nne na kisha akaamrishwa kuweka sahihi yake katika makaratasi fulani. Hili alilifanya. Waikela hakufuatwa tena na serikali. Ingawa kulikuwepo na juhudi za chinichini za kuipinga BAKWATA, juhudi hizi hazikushinda kwa kuwa BAKWATA iliweza kufungua matawi yake nchi nzima pamoja na Tabora. Wapo baadhi ya viongozi ambao hawakuweza kuhimili vishawishi vya kupokea ile hongo ya serikali na kwa ajili hii walishirikiana na serikali hivyo kuwezesha ofisi za BAKWATA kufunguliwa, hata kama zipo pale kwa jina tu. Kuangushwa kwa EAMWS kulisababishwa na watu watatu ambao wao ndiyo walikuwa mstari wa mbele kabisa - Adam Nasibu, Sheikh Kassim Juma na Abdallah Chaurembo[SUP]76[/SUP] - na njama hii ikaungwa mkono na Rashid Kawawa na Abeid Amani Karume. Mkono wa Julius Nyerere na Kanisa Katoliki katika njama hii haukuonekana kabisa kama ilivyo kawaida katika njama zote za kupiga vita Uislam na Waislam Tanzania