Unapozungumzia suala la nchi unapaswa uzungumzie pia mfumo wa maisha ya binadamu. Binadamu anaweza kuishi bila kuwepo kwa dhahabu...dhahabu inapewa thamani baada ya uwepo wa binadamu. Thamani ya dhahabu itaonekana pale tu binadamu anapopewa hadhi, heshima na thamani yake. Kwa mtazamo wangu, utakuwa ni upuuzi wa kiwango cha juu kuiweka thamani ya dhahabu mbele kuliko thamani ya binadamu. Suala la dhahabu kuibiwa halijaanza leo na mwasisi ni mfumo ule ule.
Uzalendo ni utamaduni unaotengenezwa, unaojengwa na kuimarishwa na mamlaka iliyopo. Utamaduni hautengenezwi na kujengwa majukwaani kwa hotuba na risala au ziara za kushtukiza. Uzalendo hutengenezwa kwa matendo yanayoonekana na kupimika. Tuliona uzalendo kipindi cha kudai uhuru wa Tanganyika, tuliona uzalendo wakati wa vita ya Kagera. Watanzania waliungana kwa sababu mfumo ulikuwa sehemu yao, mamlaka ilikuwa sehemu yao. Watanzania hawakuunganishwa kwa hotuba ndefu na nyingi zenye kuamabtana na vitisho. Jinsi uwatishavyo watu ndivyo uwasambalitishavyo.
Nchi haijengwi na mtu mmoja, inajengwa na mfumo. Mfumo ukiwa imara, ukazingatia utawala wa sheria na demokrasia, mfumo ukawa tayari kupokea nushauri na kukosolewa nchi inaweza kusonga mbele kwa haraka kwa sababu kila mwananchi atajiona ana mchango katika kuendeleza nchi yake, atajiona anathaminiwa na kuheshimiwa mawazo na maoni yake, ataona hata kero zake zinasikilizwa. Huwezi kujenga nchi kwa kutegemea hotuba za upande mmoja tu.