muhosni
JF-Expert Member
- Feb 12, 2011
- 1,108
- 152
Augustino Lyatonga MREMA, Nakuvulia kofia
Muda wote ameheshimika, ni mpambanaji wa kikweli kweli dhidi ya udhalimu
Ni jasiri, mjanja, mvumilivu, mstaarabu
Lakini anapenda sana kuwa kiongozi wa juu kwenye taasisi yoyote atakayokuwemo.
Aliwahi kuwa waziri wa mambo ya ndani, alifanya maajabu ya kupambana na ujambazi, kudhibiti wanaume wanaupiga wake zao, kuanzisha polisi jamii iliyofanikiwa sana. Alipambana na mafisadi kwa staili ya kuwapa siku saba watekeleze maagizo yake. Alisimamia maagizo na amri zake. Alifanikiwa kukusanya silaha za wizi na baadhi ya majambazi walitubu na kusamehewa. Wakati wa uongozi wake jeshi la polisi halikuwa lelemama.
Aliwahi kuwa waziri wa kazi. Utoro ulikoma, uchelewaji kazini ulikoma, na magari ya serikali yalipunguza safari za baada ya muda wa kazi. Alipatia vijana ajira na alitatua kero nyingi zilizokuwa zimeshindikana katika wizara hiyo.
Utendaji wake huu mzuri ulimfanya achukiwe na wanasiasa mafisadi. Walimuundia zengwe, na ilimlazimu kutoka serikalini na pia katika CCM mwaka 1995.
Alijiunga na NCCR ambayo ilikuwa haina umaarufu wowote, kwa masharti awe mwenyekiti wa taifa. Ndani ya muda mfupi NCCR ikawa na nguvu na ikawa tishio kwa serikali. Alipigwa mabomu ya machozi na polisi kuliko mwanasiasa yeyote aliye hai Tz, alinyanyaswa kwa namna nyingi. Lakini aliwezesha NCCR kupata wabunge kadhaa pamoja na kuonekana kuwa chama kikuu cha upinzani Tz kwa wakati ule.
Kwa kuwa NCCR nako kulikuwepo na mazagazaga ya mafisadi, alishindwa kuendelea kuwepo na akakimbilia TLP, pia kwa masharti kwamba yeye lazima awe mwenyekiti. Ghafula TLP ikafufuka na kuwa na heshima katika vyama vya upinzani. Kikajulikana, mrema akagombea ubunge Temeke akashinda.
Pamoja na umri kusogea, akachuja kwa muda kutokana na misuko suko ndani ya chama chake. Ameendelea kupambana na sasa amerudi kwenye chati. Alipotangaza kwamba anakwenda kugombea ubunge kule Vunjo kila mtu alidhani kuwa anazeeka vibaya. Ameshinda ubunge, na amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati ya hesabu za serikali za mitaa. Sasa ana uhakika wa maisha ya heshima zaidi.
Amerudi kwenye chati, anangara, na sasa anaheshimika tena
Na mimi, namvulia kofia na kutamani angeweza kuunganisha nguvu na Dr. Slaa (The Prezidaa)