TUTARAJIE MABADILIKO ZAIDI CHINI YA MASTERCLASS ARTETA
Arsenal inahitaji mabadiliko makubwa, sio kukimbia hovyo kama kuku wasiokuwa na kichwa, sio suala la kujituma, ama kukaba kitimu, mabadiliko lazima yaanzie katika vitu vya msingi kama kupokea mpira, kutoa pasi na kujua wapi alipo kila mchezaji aliyepo uwanjani.
Moja ya vitu vipya nilivyoviona ni kwamba hataki wachezaji wakipata mpira wazunguke kabla ya kupiga pasi, hilo lilikuwa ni tatizo kubwa la Arsenal, nenda angalia mechi yeyote ya Arsenal chini ya Unai, utakuwa mabeki wa Arsenal hasa Sokratis, Chambers na Maitland-Niles wamepokea mpira wanazunguka duara (nyuzi 360) au nusu duara ili kupata nafasi ya kupiga pasi, wanapofanya hivyo iwapo pasi haitamfikia mlengwa timu inaingia katika wakati mgumu sana.
Pia tatizo jingine ni kwamba wachezaji wa Arsenal wakipata mpira hasa mabeki hawajui nani wa kumpasia, mfano mzuri ni ule mchezo dhidi ya Watford, Sokratis kapasiwa mpira na Leno hajui aupeleke wapi, kabla hajaamua watu wanakuja kukaba, akapaniki, akabutua mpira kufamfikia Tom Cleverly, akapiga shuti langoni mwa Arsenal, waya.
Hayo ni makosa ambayo nimeona Mikel Arteta akijaribu kuyarekebisha, anataka kila mchezaji ajue mchezaji mwingine alipo kabla hajapata mpira, ili akipata mpira asitumie muda mwingi kuwaza na kusababisha magoli ya kizembe kama lile la Watford.
Mikel Arteta anachojaribu kukifanya Arsenal, aliwahi kukifanya aliyekuwa kocha mkuu wa Manchester United mholanzi Louis Van Gaal, kwa wale waliokuwa wanaangalia gemu ya Man Utd kipindi hicho watakumbuka jinsi Van Gaal alivyokuwa akiwafanyisha mazoezi kulingana na nafasi zao wanazocheza na kufanya mazoezi ya pasi nusu saa kabla ya mchezo, naamini ndiyo sababu kubwa ya Arteta kumleta, Albert Stuivenberg kama msaidizi wake, ikumbukwe ya kwamba Stuivenberg alikuwa msaidizi wa Van Gaal alipokuwa Man United.
Mabadiliko hayo yalianza kuonekana katika mchezo dhidi ya Bournemouth na kama Lacazette asingekosa magoli ya wazi siku hiyo Arsenal ingeibuka na ushindi mnono.
Najua Arteta hawezi kuibadilisha Arsenal ndani ya wiki moja, atahitaji muda na kusajili baadhi ya wachezaji watakaofuata mfumo wake, lakini nina imani iwapo ataungwa mkono na mashabiki, bodi na wamiliki wa Arsenal ataibadilisha hii timu ya kuanza kucheza soka la kuvutia na la kishindani.
Tumpe muda Mikel Arteta, mambo mazuri yanakuja, #COYG