Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

*ANGA LA WASHENZI --- 03*


*simulizi za series inc*



Jona alifika kazini akiwa tayari amechoka. Amechoshwa na mawazo. Hakushika kazi yoyote akitafakari kwa dakika kadhaa. Alitoa kiti ndani akakiweka nje alipoketi kutazama mazingira.



Hii ndiyo ilikuwa desturi yake. Kila anapokumbana na jambo analohitaji kulifikiria vema, basi hutafuta mahala tofauti atakapopata hewa safi na kumtoa kwenye mazingira ya mazoea.



Bado mazingira yalikuwa ya giza, giza la asubuhi. Magari yalikuwa yanakatiza barabarani mara kwa mara watu wakienda makazini. Fremu za maduka zilikuwa zinafunguliwa, sauti za milango ya bati zikasikika huku na kule.



Lakini yote hayo hayakutosha kumuondoa Jona fikirani. Alijikuta anasonya kisha akachomoa simu mfukoni, ile aliyokabidhiwa na mwanamke aliyenadi kuagizwa na bwana Eliakimu Mtaja.



Akaifungua na kuzama mtandaoni. Akaperuzi vichwa vya habari vya magazeti apate kujua kinachoendelea nchini na duniani kwa ujumla.



Kwa muda mrefu sana hakufanya hilo zoezi. Alijiweka mbali na ulimwengu kabisa, si kwasababu ya kutokuwa na simu bali kwasababu ya kutotaka bughdha za ulimwengu. Aliuchoka, akataka mapumziko.



Ila kwa sasa, kwa namna mambo yalivyokuwa yanatukia, aliona kuna haja ya kupitia na kufahamu mambo kadhaa. Pengine anaweza pata jambo muhimu la kumpa mwongozo.



Alipitia vichwa vya magazeti nane. Miongoni mwao kichwa kimoja kikamgonga kichwa na kumpa hamu ya kutaka kujua zaidi. Kichwa hiki kilijirudia kwenye magazeti matano. Kilikuwa kinahusu mauaji ya mfanyabiashara ndani ya jiji la Dar es salaam.



“Mfanyabiashara auawa na majambazi.”
“Mfanyabiashara, almaarufu Bite wa China, auawa kwa risasi na watu wasiojulikana.”
“Majambazi wamvamia na kumuua Bite!”



Kusaka undani zaidi wa taarifa hiyo, Jona akazama tena mtandaoni. Akaperuzi blogu kadhaa zilizojaribu kuelezea tukio hilo, hatimaye akakata kiu yake ya habari.



Kwa msaada wa picha za mlengwa na taarifaze, aligundua kumbe aliyeuawa ni Beatrice Shauri! Hili likamshtua.



Si muda mrefu sana nyuma mwanamke huyo alionana na Jona akamkabidhi kazi ya kufanya aliyoahidi kumlipa pesa nzuri. Bado Jona alikuwa anamkumbuka vizuri mwanamke huyo kwa tabasamu na sauti tamu.



Alikumbuka hadi nguo alizokuja nazo siku hiyo alipoingia naye kwenye mahusiano ya kibiashara. Alikuwa amevalia suruali ya jinsi ya kubana na topu ya pinki. Nywele zake zilikuwa fupi, amezikata na kuzirepea vema.



Ameuawa!?



Jona aliacha shughuli zake akaufuata ule mzigo wa Beatrice Shauri, akautazama kwa kina. Ni kana kwamba kuna kitu alikuwa anatafuta. Japokuwa kazi hiyo aliifanya yeye mwenyewe kwa mikono yake, ila hakuwa amepata wasaa wa kuiperuzi.



Mzigo huo ulikuwa mkubwa. Picha kubwa ya kuchorwa kwa mkono ambayo kama ungeitazama vibaya, basi ungesema imechukuliwa na kamera, tena yenye uwezo wa hali ya juu.



Ilikuwa ni picha ya kisiwa kilichozingirwa na maji ya bahari. Kisiwa hicho kilikuwa cha kijani. Kilivutia machoni. Ukitazama vizuri pia hapo hapo pichani utaona ndege wekundu na weupe, upande wa kusini mwa kisiwa, wakiwa wanaruka pamoja.



Kulikuwa kuna vialama na viashiria vingi pichani. Jona alishindwa kuving’amua. Kwa mara ya kwanza, wakati anavichora, hakuvijali ila kwa sasa anapata mushkeli na kuumiza kichwa.



“Kwanini hii picha inatafutwa?” alijiuliza. Alitafakari kwa sekunde tano kabla hajaamua jambo kichwani:
“Ni lazima itakuwa na mahusiano na kifo cha Bite.”



Akaketi kitini akiendelea kutafakari na picha ipo mkononi. Akili yake ilimwambia kabisa wale watu aliowaona jana usiku nyumbani kwake watakuwa wanahusika na kifo cha Bite kwa namna moja ama nyingine.



Lakini je sababu itakuwa ni hii picha? akaitazama tena.



Maswali hayo yalikuwa magumu na majibu yake yalihitaji jitihada. Kama kuna siku mwanaume huyu alitamani kurudia kazi yake ya upelelezi basi ni hii. Alitamani kujua zaidi kuhusu Beatrice na ile picha.



Alikuja kuondolewa kwenye lindi hilo la mawazo na mlio mkali wa simu. Alikuwa ni Mh. Eliakimu Mtaja. Pasipo kufikiria mara mbili, Jona akapokea na kuitweka sikioni.



“Naongea na Johnathan Mchau?” Sauti kavu iliuliza.
“Ndiye mimi.”
“Kijana, naomba tukutane, nina shida nawe. Nimekutafuta kwa muda mrefu sana.”



Jona hakuona tabu, akakubali wakapanga miadi. Bwana Eliakimu alimsisitizia na kumwomba sana asije akakosa.



“Nakutegemea sana,” alisema kisha akakata simu.



Ilikuwa ni saa moja sasa ya asubuhi. Mwanga wa jua ulishatawala na kuangaza. Haikupita muda mrefu, akaja mwanaume mmoja mfupi rangi maji ya kunde. Macho yake makubwa, ndevu lukuki kwenye taya.



Mwanaume huyu anaitwa Jumanne. Ni mfanyakazi mshirika na Jona ndani ya banda moja. Ni maarufu sana kwa uchoraji, haswa michoro ya tingatinga.



“Afadhali umekuja,” Jona akasema baada ya salamu. “Kuna mahali nataka kwenda mara moja!”



Akaaga na kuondoka na mzigo wa Bite alioupitishia kwenye makazi yake. Baada ya nusu saa akawa ndani ya nyumba kubwa ya kuvutia. Mlinzi alimkaribisha na kumuelekeza mahali pa kukaa punde alipojitambulisha. Ilikuwa ni eneo dogo lililopo kwenye bustani, lina viti na paa dogo la kigae.



Muda si mrefu akatoka mwanaume mnene, mfupi, mweusi mwenye panki. Alikuwa amevalia tisheti nyeupe iliyobinuliwa na kitambi chake kikubwa, bukta na viatu vyepesi.



Akatazama kushoto na kulia kabla hajaenda kukutana na Jona bustanini. Walisalimiana na kujuliana hali kisha wakaelekea kwenye kiini cha mkutano.



“Jona, nina shida kubwa, na nimeambiwa wewe ndiye unayeweza kun’saidia. Ni muda mrefu sasa nimeliripoti polisi, lakini naona hamna kitu. Kama bahati tu, afisa mmoja akanambia nikutafute japokuwa alikuwa hana namna yoyote ya kukupata. Alichokuwa anakijua kuhusu wewe ni makazi yako tu, napo hakuwa na uhakika sana.”



Eliakimu akaweka kituo. Jona alikuwa anamsikiliza kwa umakini mkubwa.



“Ila naamini yote yatakuwa historia sasa maana nimeshakupata,” Eliakimu akaendelea kunena.
“Ni takribani mwezi mmoja sasa tangu mke wangu apotee. Nimemtafuta maeneo yote ninayoyajua, sijampata. Kwao na kwa marafiki zake! Napata mashaka sana juu ya hili. Nahofia usalama na uzima wake.



Jona, naomba unisaidie kumpata mke wangu. Nipo radhi kwa gharama yoyote ile ilimradi tu apatikane. Hata kama ameuawa, basi nijue na nani amehusika.”
“Mzee,” Jona akaita. “Sidhani kama ninafaa kufanya hiyo kazi. Sipo tayari kwa sasa.”



Uzuri bwana Eliakimu alishataarifiwa mapema juu ya ukaidi wa Jona. Mwanaume huyu alikuwa mgumu na mwenye msimamo mkali. Ilikuwa inahitaji roho ya nanga kumbadili fikra na mwenendo.



“Jona, nimekuomba hili kama mume anayemhitaji mke wake, baba anayemtafuta mama wa watoto wake. Si kwamba nakupa kazi, la hasha! Tafadhali naomba unisaidie.



Nipo radhi kukusaidia kwa namna yoyote ile. Nina mtandao mpana, ninafahamiana na watu lukuki wakubwa. Bila shaka itaweza kukurahisishia kazi.”



Uso wa bwana Eliakimu ulikuwa umenyong’onyea. Usingeweza kuamini kama mtu huyu, waziri wa Habari na michezo, angewahi kuja kuomba kitu kwa mtu wa kawaida kiasi hiki.



Watu hawa walikuwa wamezoa kutoa amri na maagizo na kisha jambo hutendeka. Ila kwa leo ilikuwa kinyume, alikuwa anaomba, tena kwa unyenyekevu.



“Mheshimiwa,” Jona akaita. “Hili jambo si la kukurupukia kabisa, linanihitaji niwe mtulivu.



Ningeomba unipatie usiku huu nilitafakari, nitakupa majibu.”



Bwana Eliakimu hakupendezwa sana na hilo jibu. Aliona kama vile Jona ametumia njia ya kistaarabu kukataa ombi lake. Ila hakuwa na namna, alipiga konde, akaamini.



“Sawa,” akasema kishingo upande. Jona akanyanyuka na kumpatia mkono wa kwaheri, akahepa zake.



Baada ya robo saa akawa ameshafika kazini. Alimkuta Jumanne akiwa ameketi anabofya kioo cha simu yake kubwa isiyo na jina.



“Vipi, kila kitu kipo sawa?” aliuliza.
“Shwari tu,” Jumanne akajibu na kuongezea: “Kuna mgeni alikuja kukuulizia. Yani ile we umetoka tu, akaingia.”
“Nani?” akauliza Jona akiwa anaketi.



Kwa mujibu wa maelezo ya Jumanne, Jona alipata picha halisi. Mgeni huyo alikuwa ni yule dada aliyekuwa anataka mzigo wa Bite.



“Bonge la ndinga mwanangu alikuja nalo, nikasema yees leo si ndo’ leo!” alisema Jumanne akitabasamu meno yote nje.
“Ulivyomwambia sipo akasemaje?” Jona alipeleleza.
“Akaniuliza vipi nyumbani kwako, nikamjibu haupo home.”



Jona akawa kimya akitafakari. Tabasamu la Jumanne lilififia akiuliza:
“Vipi mzee, kuna usalama?”



Jona hakutaka kumpa mashaka Jumanne. Alilazimisha tabasamu usoni akapachika kiganja begani mwa mwenzake.



“Kila kitu kipo sawa, J. Huna haja ya kuhofia.”
“Haya bana, ila huyo manzi ni mkali! Nifanyiefanyie basi na mie mwenzako ning’aze.”
“Sina hata namba yake. Hatujuani.”
“We si ndo’ zako hizo. Wazungu wewe, hadi na wabongo wewe. Sijui mie hawanioni?”



Kidogo Jona akapumzisha akili yake alipokuwa ananena na Jumanne. Walitabasamu na kucheka. Na siku ilikuwa hivyo mpaka jioni walipofunga wakiwa wameingiza USD 900 toka kwa watalii fulani wa kiamerika.



Kama kawaida Jona akapitia bar aliipoketi kwa masaa mawili akinywa Alvaro baridi. Hapa ni mahala pake mahususi pa kupunguzia muda wa kwenda kuwa mpweke nyumbani.



Alipomaliza akajikusanya na kuelekea nyumbani akitembea ado ado. Kichwani alikuwa na fikra mbalimbali zilizokuwa zinakatiza kwa awamu.



Alifika nyumbani, akashika geti. Ajabu likafunguka pasipo kungoja funguo. Moyo wa Jona ukakita, akili yake ilimkimbiza haraka kwenye usalama wa mzigo wa Bite.



Milango yote ilikuwa wazi. Kulikuwa kuna chapa za viatu sakafuni, na mazingira yalikuwa shaghalabaghala kuonyesha upekuzi ulitendeka.




***
***






Sent from my SM-J110F using JamiiForums mobile app
 
Nimeamua kuweka zote.

Sent from my SM-J110F using JamiiForums mobile app
Tatizo sio kuamua tu! bali ni kuamua vyema.
sidhani kama ni vyema hivyo ulivyofanya,kwanza kutakuwa na mkanganyiko kwa wale tunaotaka story moja na inaleta usumbufu kuview maana mtu unakuwa unatafuta wee.. pia inaweza katisha mtu tamaa ya kusoma hivyo kukatisha!
vyema kitu kimoja chenye mtiririko mmoja itapendeza zaidi.
 
Tatizo sio kuamua tu! bali ni kuamua vyema.
sidhani kama ni vyema hivyo ulivyofanya,kwanza kutakuwa na mkanganyiko kwa wale tunaotaka story moja na inaleta usumbufu kuview maana mtu unakuwa unatafuta wee.. pia inaweza katisha mtu tamaa ya kusoma hivyo kukatisha!
vyema kitu kimoja chenye mtiririko mmoja itapendeza zaidi.
Hivyo ndivyo ulitakiwa uongee, kistaarabu tu na mtu anakuelewa. Nashukuru, niliona usumbufu kufungua threads mbili kwa wakti mmoja.
 
Back
Top Bottom