Anga la washenzi na Joana anaona kitu usiku

ANGA LA WASHENZI -- 001



Simulizi_za_series










Mvua ilikuwa inanyesha sana. Hali ya hewa ilikuwa baridi ikiambatana na upepo wa wastani. Watu wengi hawakwenda kazini, na hata wanafunzi pia wakitega shule kwa kisingizio cha barabara kufurika maji.
.
.
.
Pengine watu hawa walikuwa na hoja kutokana na miundombinu dhaifu ya jiji la Dar es Salaam ambayo haiwezi kurandana na mikikimikiki ya mvua. Ila kwa mwanaume Jonathan Mchau, hilo halikuwa na mashiko kamili kwani yeye alikuwa ofisini akiendelea na kazi zake kama ilivyo ada.
.
.
.
Ni ndani ya chumba kidogo kinachopatikana maeneo ya mwenge. Kwenye kuta za chumba hicho kulikuwa kumetundikwa picha kadhaa za kuchorwa kwa mikono. Picha hizi zilikuwa zimeundwa kimafumbo lakini pia zikibeba utajiri wa tamaduni za Afrika kwa ujumla.
.
.
.
Kama ungelipata nafasi ya kutembelea hapo basi ungepatwa na kamshangao kidogo kutazama picha hizo zilizofumwa na rangi mbalimbali za kuvutia kiasi kwamba ukasahau kuwa eneo hilo limepakana na barabara yenye makelele lukuki ya magari. Na hata kuta za jengo hilo zina nyufa kadhaa.
.
.
.
Mwanaume huyu ajulikanaye kwa jina la Jonathan, joh, ama Jona kama wamuitavyo watu wa karibu, alikuwa ni mwanaume mweusi mtulivu mwenye mwili wa kujaa, macho makubwa mabovu yasaidiwayo na vioo vya miwani, nywele ndefu kichwani na ndevu alizozichonga umbo la 'o'.
.
.
.
Hakuwa mtanashati sana, pengine kwasababu alikuwa kazini na kazi yake aihitaji unadhifu wa hali juu ilhali unacheza na rangi. Ila alikuwa mtulivu sana, na macho yake yaliganda kwenye karatasi aichorayo kwa umakini wa hali ya juu.
.
.
.
Alikuwa ndani ya ulimwengu wa peke yake asijali kabisa yanayoendelea nje ya karatasi. Unaweza kudhani mwanaume huyu hakuwa anajua kama kuna mvua ilikuwa inanyesha. Umaanani huu kupita kiasi ukamfanya asifahamu kama kuna mgeni ameingia eneo lake na kusimama kwa sekunde kadhaa.
.
.
.
Akashtuliwa, "Hello!"
.
.
.
Akatazama na kumkuta mwanamke fulani mrembo, mrefu mwenye rangi maji ya kunde. Alikuwa amevalia sweta rangi ya kijivu iliyofunika blauzi yake nyeupe, pamoja na suruali ya jeans iliyobana vema umbo lake la figa. Miguuni alivalia raba nyekundu.
.
.
.
Nywele na masikio yake alikuwa ameyaziba kwa kofia kubwa jeusi la soksi. Mgongoni alikuwa amebebelea begi kubwa jeusi, haya ya kuhifadhia tarakilishi mpakato. Uso wake ulikuwa mfupi na mpole. Macho yake yalikuwa ya wastani ila makali. Mdomo wake mdogo alioupaka rangi ya kahawia ulichanua kwa tabasamu.
.
.
.
"Samahani kwa kukutoa kazini," akasema mwanamke kwa sauti ya kumlaghai nyoka.
.
.
"Usijali," akadakia Jonathan, "karibu sana." Akaacha kazi akasimama kumlaki mgeni.
"Ahsante. Hapa ndiyo kwa Joh?"
"Yes, ndiyo hapa."
"Na wewe ndiye Joh mwenyewe?"
"Ndio, ni mimi."
"Ook, nimeagizwa na Beatrice Shauri kuulizia mzigo wake."
"Bite?"
"Ndio!"
.
.
.
Jonathan akatabasamu. Akafuata mfuko mmoja mkubwa mweupe wa rambo, ndani yake ulikuwa na kitu cha umbo la mstatili, akaunyanyua na kumkabidhi mgeni.
.
.
.
"Unaweza ukatazama."
.
.
.
Mgeni akatazama mzigo huo kisha akaurudisha ndani ya mfuko.
.
.
.
"Ahsante sana. Unamdai?"
"Hapana."
"So naweza nikaondoka nao?"
"Hapana." Jonathan akatikisa kichwa. "Siwezi nikakupatia maana sijapata ridhaa ya mmiliki."
"Bite ni dada yangu."
"Taarifa hiyo haijitoshelezi kukupa mzigo wake, dada. Hakunipa agizo hilo."
.
.
.
Mwanamke yule akaguna na kubinua mdomo. Akapandisha mabega na kuzungusha macho.
.
.
.
"Ok," akasema kwa kupitia puani kisha akaenda zake. Ila punde anarejea tena.
"Kaka mbona unakuwa si mwelewa lakini?" Alilalama. Macho yake yalikuwa yamelegea, mdomo wake ukitepeta.
"Nimekwambia Bite ni dada yangu, ameniagiza. Simu yangu imezima chaji unajua umeme unavyosumbua siku hizi, ningempigia uongee naye!"
.
.
.
Joh alipigwa na bumbuwazi. Kuna kitu alikikokotoa kichwani.
.
.
.
"Dada," akaita. "Siwezi nikakupa kazi ya mtu. Na hii ni kwasababu sikupewa agizo hilo. Ni swala la uaminifu tu. Sikufahamu, siwezi kukuamini namna hiyo."
.
.
.
"Basi ntakuongezea pesa mara mbili ya aliyokulipa Bite," akasema mwanamke huyo kwa kujiamini. Hapo sasa ndiyo Jonathan akapata wasiwasi zaidi. Kwanini mwanamke huyu anataka mzigo huu kiasi hiki?
.
.
.
Aliona haja kubwa ya mwanamke huyo ndani ya macho yake. Alikuwa anataka ule mzigo kwa hali na mali.
"Sema basi," mwanamke akasisitiza. Uso wake ulikuwa umekunjana. Alitazama majira ya saa yake kana kwamba mwanafunzi aliyechelewa zamu ya mwalimu mnoko.
"Unataka shilingi ngapi?" Akauliza.
"Sitaki pesa yako," Jonathan akajibu na kuongezea: "Naomba uende, dada."
.
.
.
Mwanamke akashusha pumzi ndefu. Akavua begi lake na kuzamisha mkono wake wa kuume ndani. Jonathan akapata shaka. Alitazama mkono huo vema. Alidhani huenda ukatoa silaha.
.
.
.
Kabla mkono huo haujatoka ndani ya begi, sauti ya wanaume ikasikika. Jonathan na mgeni wake wakatazama sauti hiyo inapotokea. Mlangoni wakawaona wanaume wawili waliovalia makoti marefu meusi ya kuwakinga na mvua.
.
.
.
Wanaume hawa walikuwa warefu na weusi. Mmoja alikuwa na mustachi mnene, mwingine kidevu na mashavu yake yakiwa hayana harara za ndevu. Miili yao ilikuwa imejaa wakitembea kikakamavu.
.
.
.
Haikuchukua muda mrefu Jonathan akagundua wanaume hao walikuwa ni wana usalama. Kwa namna walivyokuwa wanaongea, kutembea na muonekano wao pia ulisadifu hiyo dhana.
.
.
.
Alirudisha macho yake kwa yule mwanamke, akaona mwanamke huyo akifunga begi lake na huku mkononi akiwa mtupu. Mwanamke akamtazama Jonathan kwa jicho baya kisha akaondoka zake akisonya.
.
.
.
Jonathan alimsindikiza mwanamke huyo mpaka alipotoka mlangoni, kisha akahamishia macho yake kwa wageni wapya.
.
.
.
"Karibuni."
"Ahsante," aliitikia mwanamume mmoja kisha kwa pamoja wakamsalimu Jonathan.
"We ni Jonathan Mchau?" Aliuliza mwanaume mwenye mustachi. Sauti yake ilikuwa ya madaraka. Walikuwa wanamtazama Jonathan kana kwamba wanamfananisha na mtu waliyemuona kitambo.
"Ndiye mimi," Jonathan akajibu.
.
.
.
Leo ilikuwa ni siku ya tofauti sana kwa Jonathan. Ugeni wa pili sasa huu unamtembelea. Kazi iliyomfanya asijali hali ya hewa akaja ofisini, ilikuwa imesimama. 'Karoho' kalikuwa kanamuuma. Aliona anapoteza muda.
.
.
.
"Tuna maongezi kidogo na wewe," akasema mwanaume mwenye mustachi. Yeye ndiye alikuwa muongeaji mkubwa mwenzake akiwa kimya.
"Karibuni," Jonathan akasema akinyooshea mikono yake ndani.
"Tunaweza tukafanyia hayo maongezi kwenye gari?"
"Kwenye gari!" Jonathan alistaajabu. "Ni maongezi gani hayo? Na nyie ni wakina nani? - hamjajitambulisha."
"Sisi ni polisi." Wanaume wale wageni wakaonyeshea vitambulisho vyao. "Hivyo usijali."
"Sijali, ila ningependekeza tufanyie hayo maongezi hapa hapa ofisini kwangu," Jonathan alisema akiketi kitako.
Wanaume wale wawili wakatazamana kisha muongeaji akasema:
"Sawa."
.
.
.
Wakavuta viti vilivyoko kando, walionyeshewa na Jonathan, wakaketi.
.
.
.
"Jonathan, sisi sio wakaaji sana. Kwa majina naitwa inspekta Norbet Mlanje na huyu mwenzangu ni inspekta Nombo tumetokea kituo kikuu, central."
"Karibuni inspekta."
"Ahsante kwa mara nyingine. Nadhani mpaka hapo utakuwa ushajua tumekuja kufanya nini."
"Sijajua," Jona akasema akitikisa kichwa.
"Sawa, si mbaya tukaliweka wazi," akasema Inspekta Norbet akikuna ndevu. "Kama tulivyosema hapo awali, tumetoka central, na tumeagizwa kuja hapa kwa ajili ya kukuomba kurejea kundini. Mkuu anakuhitaji sana."
.
.
.
Jona akatabasamu.
.
.
.
"Siwezi kurudi," akajibu kwa ufupi na kisha akasimama. "Nina kazi nyingi zinaningoja. Mnaweza mkanipa nafasi?"
.
.
.
Inspekta wakatazamana alafu wakanyanyuka kishingo upande.
.
.
.
"Jona," inspekta Norbet aliita. "Taifa lako linakuhitaji kwa sasa. Nadhani ni wakati wa wewe kuacha ukaidi na kusikiza wito huu."
"Inspekta Norbet," Jona akaita. "Sihitaji kazi yenu, naomba umwambie mkuu hilo. Tena umsisitizie. Sihitaji kazi yenu hata kidogo."
.
.
.
Inspekta wakatazamana kwa macho ya paka.
.
.
.
"Sawa, ila utakapobadili mawazo yako usisite kututaarifu."
.
.
.
Jonathan hakujibu, inspekta wakaondoka. Walifika mlangoni Norbet akamtazama tena Joh kana kwamba mama aliyekata tamaa juu ya mwanaye. Kisha wakatokomea.
.
.
.
Jonathan alitafakari kwa dakika mbili, akaketi kuendelea na kazi yake aliyokuwa anaifanya hapo awali. Ila kwa sasa akili yake haikuwa imetulia. Mawazo yalimpoka atensheni. Alimfikiria yule mwanamke, alafu pia na wale inspekta. Alijikuta anakosea kutenda kazi kila mara.
.
.
.
Mwishowe aliacha, akasimama na kwenda nje kutazama madhari, pengine angechangamsha akiliye. Alitazama namna mvua inavyokita ardhi, barabara ilivyolowana. Alitazama jinsi matairi ya magari yanavyotapanya maji barabarani.
.
.
.
Alitazama anga lilivyojibana na kuwa jeusi. Namna palivyokuwa tulivu usidhanie kama hapo ni Dar, tena majira hayo.
.
.
.
Akiwa anarandisha macho yake mithili ya mtalii mbugani Serengeti, kuna kitu alikiona kikamvutia. Mara ya kwanza alikipuuzia, na hata ya pili pia. Mara hii ya tatu akaamua kukitilia maanani. Ilikuwa ni gari kubwa, Range Rover Sport nyeusi, lililosimama hatua ishirini na tano za mtu mzima toka kwenye banda lake.
.
.
.
Taa za nyuma za gari hilo zilikuwa zinawaka. Gari lilikuwa linachemka, ungeliona hilo kwa wepesi kwa kutazama bomba lake la kutolea moshi. Pleti namba ya Kenya. Vioo vyake vilikuwa vyeusi, hivyo hata kama ungekuwa karibu usingeona walio ndani.
.
.
.
Jona alilitazama gari hilo akijiuliza maswali mepesi kichwani. Lipo hapo tangu muda gani? Linafanya nini hapo? Mbona haliondoki? Linamsubiri nani ama nini ilhali mabanda yamefungwa? Mara gari hilo linatiwa moto na kuondoka. Jona analisindikiza likiyoyoma kisha anarudi zake ndani kuendelea na kazi. Angalau akili yake ilikuwa freshi.
.
.
.
Alidumu kazini mpaka majira ya jioni akiwa ameisogeza sana kazi yake. Alifunga banda kwenye majira ya saa kumi na mbili, akapanda bodaboda mpaka kwenye baa moja isiyo na jina, maeneo ya karibu na makazi yake, Mbezi beach GOIG. Hapo akatulia akiwa ameagizia Alvaro baridi.
.
.
.
Watu walikuwa wachache, bila shaka sababu ya hali ya hewa. Jona alijitenga mbali na watu, akiketi kwenye meza pweke. Macho yake yalikuwa yanachambua mazingira huku mdomo wake ukipiga mafundo kadhaa ya kinywaji.
.
.
.
Taratibu akiwa hapo, anamezwa na tafakuri na taswira mithili ya ndoto. Haikuchukua muda mwingi kuhamishwa toka kwenye fahamu zake mpaka ulimwengu huo mwingine.
.
.
.
Hii ndiyo sababu mwanaume Jona hapendi kuketi pasipo shughuli. Kila anapokuwa huru, akili yake humkumbusha yaliyopita. Na yaliyopita si mema. Humuumiza. Humtonesha kidonda sugu kisichotaka kupona.
.
.
.
Anajiona kwenye nyumba kubwa inayoungua moto. Anavuja jasho jingi akitoa macho huku na kule. Anaita jina lisilosikika. Anazunguka huku na kule. Mbao za paa zinaanguka. Hewa inakuwa nzito ndani ya nyumba anashindwa kuhema. Macho yake yanamwaga machozi. Anajikuta anaishiwa nguvu akikohoa kwa pupa.
.
.
.
Haraka anatoka ndani. Anatembea hatua kadhaa kuacha kibaraza, mara anaanguka chini. Anajitahidi sana kuhema. Jasho bado linaendelea kummiminika. Punde fahamu zinaacha mwili wake, anazirai.
.
.
.
“Kaka!” kwa mbali sauti ya kike ilipenya kwenye ngoma ya masikio ya Jona.
“Kakaa!” sauti hiyo ikajirudia, mara hii kwanguvu ikiambatana na kupigwa kwa meza. Jona akashtuka. Mbele yake alikuwa amesimama mhudumu, mwanamke mtu mzima mwenye uweupe mwekundu wa kujichubua.
.
.
.

***
***
***
 
*JOANA ANAONA KITU USIKU!*

*Simulizi za series inc.*







Jua linapozama, Joana hukosa raha. Si kwasababu anaishi Brussels, Ubelgiji, kipindi hiki cha baridi, la hasha! Bali kwasababu usiku huwa mzito sana kwake.


Punde giza linapoingia, anapoteza amani na mwili wake unaanza kutetemeka kwa hofu. Na zaidi pale ambapo kila mtu akishalala, machozi huanza kumbubujika na hujifunika shuka gubigubi.


Si kwamba Joana ni mwoga kukithiri. Hapana. Joana huona watu usiku. Watu waliokufa, watu wanaotisha na kuogofya!


Habari hii ilianzia miaka kumi na mitano huko nyuma kwenye jiji la Berlin, Ujerumani. Joana alikuwa anasoma huko chuo kikuu akichukua fani ya sheria.


Alikuwa ni msichana mrembo na mwenye kuvutia kwa namna alivyokuwa anajipangilia nguo, maneno na hata hoja.


Alikuwa na marafiki lukuki, lakini zaidi mpenzi wake mwenye asili ya Brazil, akiitwa Moa Santos. Aliyekuwa anampenda na kumheshimu sana.


Mara kadhaa Joana alikuwa anaonekana na mpenzi wake huyo wakirandaranda maeneo ya chuo wakishikana mikono.


Kama ingelikuwa si vipindi kutofautiana, Moa alikuwa anasomea mambo ya ugavi, basi wangelikuwa wanaonekana pamoja muda wote, kuanzia asubuhi mpaka jioni kabla hawajaenda hostel.


Moa hakuwa mbahili wa tabasamu wala cheko. Hakuwa na sababu yoyote ya kununa wala kuyaona maisha machungu.


Baba yake alikuwa mfanyakazi wa kampuni kubwa ya simu ya Samsung, huko Korea. Na mama yake alikuwa mwanasiasa nguli huko Ubelgiji.


Kabla hajalia shida, babaye alikuwa tayari ashamfikia na kumkabidhi pesa, ama basi mamaye.


Ila leo hii Joana ni mpweke, macho yamemvimba muda wote. Uso wake umekuwa mweusi na mhaba wa furaha. Amekuwa mtumwa wa kujificha, kukwepa wengine na kujiona mtupu.


Maisha yalibadilikia wapi?


Punde baada ya kumaliza muhula wake kwanza wa masomo chuoni, Joana alisafiri kwenda Rio de Jenairo pamoja na mpenzi wake, Moa.


Lengo la safari hii ilikuwa ni kwenda kutambulishwa kwa kina Moa kama mchumba mtarajiwa. Mwanamke ambaye Moa anampenda zaidi.


Walipofika Rio, Joana akatembezwa kwanza jiji lote la Rio. Akafurahia sana kwani alipenda sana kutembea na kujifunza mambo mapya.


Alikutana na wazazi na ndugu wa Moa, akatambulishwa kama mchumba. Alikaribishwa kwa tafrija waliyokula na kunywa kwa kusaza wakifurahia haswa.


Familia ya Moa ilikuwa ni ya watu wa kati. Hawakuwa na uwezo wa juu wala hawakuwa duni. Baba yake Moa, mzee Santos alikuwa mkulima mfanyabiashara.


Mama alikuwa mwanamke tu wa nyumbani akilea familia. Umri wao ulikuwa umeenda sana, Moa akiwa ndiye mtoto wao wa mwisho.


Ila kuna jambo lilitokea kumtatiza Joana na akataka kulipatia ufumbuzi. Jambo hilo lilikuwa linamhusu mama yake Moa, bi Lusia.


Mwanamke huyo alikuwa na macho yote mabovu, yenye viini vilivyomezwa na ute kama maziwa. Upande wake wa kushoto wa uso ulikuwa una alama ya kushonwa kana kwamba alipigwa panga.


Lakini mbali na hayo, alikuwa mchangamfu, tena asiyeonyesha kasoro yoyote kwenye kuona. Alishika alichokitaka, na kutenda alichokitaka.


Hili likamshangaza sana Joana. Aliwezaje kufanya haya?


Alimuuliza Moa, Moa akaonyeshwa kutofurahishwa na hilo swali. Joana naye akahisi vibaya kwani hakutaka kumkwaza Moa.


Kwa namna moja ama nyingine, Joana akahisi huenda Moa amehisi amemdharau mamaye, kitu ambacho hawezi kufanya kabisa.


Hivyo basi akaamua kupotezea mada hiyo.


Baada ya juma moja aliaga kuondoka Brazil aende kwao Ujerumani kabla ya kurudi tena chuo. Basi kama zawadi, mama Moa akamkabidhi Joana bangili.


Ilikuwa bangili ya bati inayometameta. Bangili hii ilikuwa ina maandishi madogomadogo ambayo Joana hakuyaona.


Pasipo kujua, siku hiyo Joana akawa ameingia agano asilolijua.


Alifurahia sana zawadi hiyo na akaitumia kuwaonyesha wenzake huko chuoni akijitapa kwa namna gani alivyopendwa na kutunukiwa na mama mkwe wake mtarajiwa.


Aliipenda sana bangili yake, si tu ilikuwa nzuri bali ilikuwa inamkumbusha upendo wake kwa Moa.


Lakini kuna jambo lilikuwamo ndani bangili. Na jambo hili lilikuwa linatukia usiku tu. Bangili hii ilikuwa inawaka pindi inapofika saa nane usiku.


Zaidi, ilikuwa inamwamsha Joana pasipo kujua na kumfanyisha mauaji ya kutisha!


Punde Joana aliporudi chuoni, ndani ya mwezi mmoja, wanachuo nane wakauawa kwa mtindo mmoja wa kifo.


Wote waliuawa kwa kuchomwa kisu kifuani. Mauaji haya yakaamsha taharuki kubwa chuoni. Hata ikapelekea kuundwa kwa ulinzi shirikishi kumng'amua muuaji.


Siku moja Joana aliamka, hana hili wala lile, akaandaa kifungua kinywa chake kabla hajaenda darasani.


Alikuwa amevalia gauni jeupe la kulalia miguuni akiwa amejivesha viatu vyepesi vya chuichui.


Akiwa anapika, mara mwenzake anayelala naye chumba kimoja, kwa jina aitwa Lisa Moan kutoka Uingereza, anafunika mdomo wake kwa kiganja akitoa macho.


Aliona kitu mgongoni mwa Joana. Alipiga kelele akimshtua Joana akisema:
"Joana nini hiko mgongoni mwako?"


Joana akakurupuka na kuruka. Alidhani buibui. Alijikuta anavua nguo yake kwa upesi mno na kuitazama.


Loh! Ilikuwa imelowa damu!


Alishangaa damu ile imetoka wapi na ilhali hakuwa na jeraha. Iliwatia hofu mno. Lakini wakamezea hilo jambo na wakakubaliana litakuwa siri.


Siku hiyo baadae wakiwa darasani, wakapokea taarifa zingine za msiba. Alikuwa amekufa mwanafunzi mwingine. Tena chumba kinachofuatia na cha wakina Joana!



****




MPO?
 
Back
Top Bottom