Anayemcheka Chidi Benz hana tofauti na muuza unga

mcubic

JF-Expert Member
Mar 3, 2011
10,307
6,514
Naupenda wimbo Ten Crack Commandments wa Christopher Wallace ‘Notorious BIG’. Kwa Kiswahili chepesi, wimbo huo unaweza kuuita Amri 10 za Biashara ya Dawa za Kulevya.

Sababu ya kuupenda wimbo huo ni kuwa amri zote 10 kama ambavyo BIG a.k.a Big Small aliziorodhesha katika shairi lake kisha kuchana kwenye mdundo mzuri wa Hip Hop, zinajenga picha wauza unga ni watu wa namna gani.

BIG kwa kutambua kuwa wangeweza kutokea watu wakambishia katika hizo amri zake 10, anaanza kwa kutamba kuwa hakuna mtu wa kumwambia kitu kwenye biashara ya dawa za kulevya. Anasema aliifanya biashara hiyo kwa miaka kadhaa na ilimfanya awe mnyama.

Chukua mstari huo; biashara ya dawa za kulevya ilimfanya BIG awe mnyama. Maana yake ukiwa muuza dawa za kulevya unakuwa mnyama. Yaani unapoteza roho ya utu.

Amri zote nazikubali, lakini huvutiwa zaidi na amri ya nne; Never get high on your own supply.

Kiswahili: Kamwe usitumie unachouza.

Kwamba unapokuwa muuza unga unajua kuwa hicho ni kilevi cha maangamizi, kwa hiyo BIG anakufahamisha kuwa usijaribu kutumia, maana utaangamia.

Amri ya tano ni muhimu; never sell no crack where you rest at. I don’t care if they want a ounce, tell ’em “bounce!”

Kiswahili: Usiuze dawa kwenye maeneo yako ya kujidai. Sijali kama watataka japo cha ukucha, waambie imegonga mwamba.

Ufafanuzi ni kuwa unga ni maangamizi, kwa hiyo unatakiwa kuuza mbali, siyo kwenye maeneo unayoishi, maana utawaangamiza watu wanaokuzunguka.

Ipo amri ya saba ambayo BIG anasema “tenganisha biashara na familia yako”, kwamba haitakiwi hata kidogo watu wa familia yako wahusike na uharamia wako ili ukipata msala ujikute matatizoni peke yako.

Amri ya nane pia anaelekeza “usijibebeshe mzigo mwenyewe”, kwamba ukiwa muuza unga unafahamu kuwa ni kimeo, kwahiyo wabebeshe wengine ili wakikamatwa uwe msala wao.

Sera ya wauza unga

Afghanistan wakati wa utawala wa Taliban chini ya Mullah Omar, walikuwa wastawishaji wakubwa wa cocaine. Hata hivyo, sera yao ilikuwa na kanuni mbili.

Kanuni ya kwanza; cocaine yote iliyokuwa inastawishwa kutouzwa nchini humo. Yaani ni lazima isafirishwe yote kwenda nje. Hawakutaka ibaki Afghanistan kisha raia wa nchi hiyo watumie na kuangamia.

Kanuni ya pili; wasafirishaji lazima wathibitishe kuwa cocaine yote wataipeleka Marekani na Ulaya. Shabaha yao ilikuwa kuhakikisha vijana wengi wa Marekani na Ulaya hasa Uingereza, wanatumia dawa za kulevya ili kudhoofisha kizazi cha mataifa hasimu.

Ukichukua sera hiyo kuwa hakuna kuuza unga nyumbani na sharti ni kuwauzia maadui, unaungana na amri ya tano ya Big Small kuwa ‘ngada’ haiuzwi maeneo ya kujidai. Kuuza nyumbani ni uharibifu wa kizazi.

Muuza unga akimkuta mwanaye anatumia atalia kisha atamtafuta mtu ambaye anamuuzia na akimkamata vita yake haitakuwa ndogo. Maana anajua kazi ambayo anaifanya kwa watoto wa wenzake.

Ni kwamba muuza unga hutaka utajiri kupitia kuharibu watoto wa wenzake lakini huwalinda wa kwake na matumizi ya ‘madubwasha’ hayo.

Kicheko cha muuza unga

Unapomuona teja ameharibikiwa na matumizi ya dawa za kulevya, maana yake muuza unga anakenua vizuri kabisa, kwani anakuwa ameshafanya biashara na kuingiza fedha nyingi.

Muuza unga hana tofauti na mtu ambaye anamtoa kafara mtu mwingine ili apate utajiri. Muuza unga ni sawa na mchawi anayemiliki misukule.

Kijana na nguvu zake anaanza kutumia unga kisha anakuwa mtumwa wa kilevi hicho cha maangamizi. Jinsi anavyoendelea kutumia ndivyo anavyoteketea.

Muuza unga hawezi kumhurumia teja anayeangamia na unga kwa sababu kadiri teja anavyoangamia ndivyo inavyomaanisha yeye kuzidi kuingiza fedha na kutajirika.

Ukiona kijana alikuwa na mwili mzuri, afya bora kabisa, ghafla anaanza kudhoofika na kupukutika. Hapo piga mahesabu kwamba kuna wauza unga wamejenga majumba, kununua magari na kufanya kufuru nyingi za starehe kupitia afya ya kijana huyo na fedha zake.

Hivyo, kwa kila mtu mwenye moyo wa kibinadamu, anayeumizwa na vijana wengi kutopea kwenye mihadarati, anapaswa kila akimuona teja anateseka, aanze kusikitika.

Tofauti yako na muuza unga lazima ionekane pale nyote mnapomtazama mtumia dawa za kulevya. Muuza unga achekelee kwa sababu ananufaika kwa kuingiza fedha kupitia mabadiliko ya kiafya ya teja. Wewe unapaswa kuumia maana nguvu kazi inapotea.

Inapotokea wewe unamcheka teja kama ilivyo kwa muuza unga, maana yake hapo tofauti yenu haionekani. Nyote mpo sawa! Je, wewe unakuwa umeingiza nini kwa mabadiliko ya kiafya ya teja zaidi ya kushuhudia nguvu kazi inapotea?

Vijana wengi ambao walikuwa na nguvu zao, walikuwa wakifanya kazi na kuingiza vipato halali, mara wakajikuta kwenye vishawishi na kuanza kutumia. Walipoanza wakashindwa kutoka, mwisho wameteketea.

Je, huoni kama taifa tunakuwa tunapoteza mzunguko wa wachapakazi? Na hiyo ni hasara kubwa mno katika nchi.

Tumzungumzie Chidi Beenz

Rejea amri ya tano ya Big Small kuwa muuza unga hatakiwi kuuza kwenye maeneo yake, kisha chukua sera ya Taliban kuwa cocaine haiuzwi ndani ya Afghanistan isipokuwa inasafirishwa tu hasa kwenda Marekani na Ulaya palipo na maadui zao.

Hapo unapata jawabu kuwa wanaouza unga hapa nchini ni adui wa taifa zima. Maana wameona mahali pekee pa kupatia fedha kupitia kuwapa watu vilevi vyao vya maangamizi ni hapa nchini kwetu.

Kwa kutumia tafsiri hiyohiyo ni kwamba unapomuona Chidi Beenz anaangamia, maana yake ni mafanikio makubwa kwa maadui wa nchi ambao waliweza kuingiza biashara yao nchini kisha Chidi na vijana wengine kushawishika na kutumia.

Hivyo basi, unapomuona Chidi alivyoangamia, hutakiwi kukenua, badala yake sikitika. Maana ni matokeo makubwa ya kushindwa kwa nchi dhidi ya biashara ya dawa za kulevya.

Chidi Beenz a.k.a Chuma, mwite kwa jina lake la kwenye hati ya kusafiria, Rashid Abdallah Makwilo, unadhani alipokuwa anaanza kuonja alijua angefika alipo leo? Hakujua, alidhani ni kilevi tu cha kujiburudisha lakini mwisho amekuwa alivyo leo.

Ungetakiwa kumfikiria Chidi Beenz yule mwenye mwili wake mzuri aliyejiita King Kong au Busta Rhymes wa Bongo. Umtazame wa leo, kisha ikutie hasira.

Chidi Beenz alikuwa anatengeneza muziki wake na anafanya biashara kisha kuendesha maisha yake. Leo hii amegeuka tegemezi, tena anahitaji msaada mkubwa. Hilo halifai kukuchekesha, linatakiwa kukutia hasira.

Tuwe na vita ya pamoja

Uingizwaji wa dawa za kulevya nchini husababishwa na matokeo ya aina mbili, kwanza ni mafanikio ya wauza unga wasiokipenda kizazi cha Watanzania, pili ni udhaifu wa watu ambao wamekabidhiwa kuongoza dola.

Wauza unga hawawezi kufanikiwa kama dola inakuwa imara, vilevile kuwa na nia ya dhati kabisa ya kutokomeza dawa nchini ili kulinda kizazi na nguvu kazi.

Namwangalia Chidi Beenz, namfikiria Ray C, Nando wa Big Brother Africa na mastaa wengine, kisha nakwenda mtaani na kutazama vijana wengi wanavyoteketea. Baada ya hapo jicho langu ni kwa dola.

Wauza unga hatuwajui labda mateja ndiyo wanaowafahamu. Na kwa kawaida mateja huwajua wauzaji wadogo ambao hufahamika kama pusher. Hao pushers wakikamatwa watasema mzigo wanasambaziwa na akina nani.

Sasa basi, kwa vile wauzaji hatuwajui, basi hasira zetu zielekee kwa Serikali, ni kwa nini jeshi la polisi linashindwa kudhibiti unga usiingie nchini? Maana Tanzania hatustawishi dawa hizo.

Unga ukidhibitiwa kuingia nchini maana yake akina Chidi Beenz hawawezi kuupata. Ikiwa hivyo itakuwa rahisi kuwaponya. Tena na vijana wengine ambao labda wangeshawishika wanakuwa wamepata kinga.

Chidi Beenz wakati wa ukuu wake kwenye Hip Hop Tanzania, Waziri wa Mambo ya Ndani alikuwa Lawrence Marsha, akapita Shamsi Vuai Nahodha, Emmanuel Nchimbi kisha Mathias Chikawe. Wote hawa wanajisikiaje kushindwa kudhibiti unga na ukawa unaingia nchini mpaka kuharibu vijana wetu?

Marsha na Nchimbi ni vijana lakini hawakufanya kazi yenye kutukuka kutokomeza biashara hiyo ili kuwaokoa vijana ambao ni wadogo zao. Wanaweza kusema walijitahidi, swali ni moja tu, walishindwa nini kutokomeza kabisa?

Kama hali bado ni mbaya mtaani na kasi ya vijana kuingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya inaongezeka, aliyekuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema, kipindi hiki amestaafu, anavunia nini? Je, IGP wa sasa, Ernest Mangu, hali hii iliyopo haimtii hasira?

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba, hivi karibuni alikwenda kumtembelea mama yake Chidi Beenz baada ya kuona hali ya msanii huyo kama ambavyo picha zake zilisambazwa mitandaoni.

Kwangu mimi, pamoja na Mwigulu kumtembelea mama yake Chidi Beenz, kwa nafasi yake, anatakiwa kufanya kazi ya heshima kuhakikisha dawa za kulevya zinatoweka nchini.

Ni kama ambavyo Rais Jakaya Kikwete kwa wakati wake, alifanya kazi nzuri ya kumtibu Ray C mpaka alipona kabisa, kabla ya mwenyewe kujichanganya na kurudi tena.

Hata hivyo, JK angefanya tukio lenye thamani kubwa kama angehakikisha wakati wa utawala wake dawa za kulevya zinapotea kabisa.

Huu ni ujumbe kwa Rais John Magufuli, kwamba vita ya wauza unga haitaki hatua legelege. Inahitaji mapambano yenye dhamira ya kufa au kupona.

Ikae kichwani kuwa unapopewa mamlaka ya ukuu wa nchi, unakabidhiwa kila kitu, ushindwe wewe tu. Marais waliopita walishindwa wao tu kutokomeza dawa za kulevya, maana walikuwa na kila kitu. Rais Magufuli naye ana kila kitu, ashindwe yeye tu.

Ukiwa Rais unakuwa ndiye Amiri Jeshi Mkuu, kwa hiyo majeshi yote ya nchi hii yapo chini yake. Mtu wa namna hiyo anaposhindwa vita dhidi ya dawa za kulevya na nyinginezo, maana yake anakuwa ameshindwa yeye tu.

Usimcheke Chidi Beenz

Chidi na wengine hawanunui unga nje ya nchi, wanaupata hapahapa. Hii nchi ina hatari sana. Februari 21, 2011 walikamatwa Wapakistan na Watanzania wakiwa na mzigo wa dawa za kulevya zenye thamani ya Sh6.2 bilioni.

Sheria za nchi zinaelekeza kuwa mtu akikamatwa na mzigo wa dawa za kulevya zenye thamani kuanzia Sh10 milioni kwenda juu haruhusiwi kupewa dhamana.

Basi, sheria zikiwa hivyo, na watu walikamatwa wakiwa na mzigo Mbezi Beach, Dar es Salaam. Kituko ni kuwa walipewa dhamana kisha wakatoroka zao na mpaka leo hawajakamatwa.

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa ambaye aliwakamata watu hao, alishangaa kupewa taarifa kuwa watuhumiwa wake walipewa dhamana na kutoroka.

Hii ndiyo nchi yetu. Kwa hiyo kabla hujakimbilia kumcheka Chidi Beenz, jiulize anapata wapi dawa? Kwa nini tusiwanunie kwanza tuliowapa kazi ya kuhakikisha dawa hazipo nchini ambao wanashindwa kutimiza wajibu wao sawasawa? Wakitimiza wajibu, dawa zitaondoka.

Chanzo: Maandishi Genius
 
Watu walimuonea huruma mara ya Kwanza wakamsaidia kumpeleka kwenye matibabu wengine wakawa wanamwombea kwa Mungu arudie hali yake ya kawaida lakini juhudi zote za wasamalia wema kazikataa watu wafanyeje sasa kumsikitikia mtu asie jisikitikia haisaidii kitu hawacheki kama mazuri
 
Watu walimuonea huruma mara ya Kwanza wakamsaidia kumpeleka kwenye matibabu wengine wakawa wanamwombea kwa Mungu arudie hali yake ya kawaida lakini juhudi zote za wasamalia wema kazikataa watu wafanyeje sasa kumsikitikia mtu asie jisikitikia haisaidii kitu hawacheki kama mazuri
Soma tena uzi....kisha tathmini jawabu lako.
 
Watu walimuonea huruma mara ya Kwanza wakamsaidia kumpeleka kwenye matibabu wengine wakawa wanamwombea kwa Mungu arudie hali yake ya kawaida lakini juhudi zote za wasamalia wema kazikataa watu wafanyeje sasa kumsikitikia mtu asie jisikitikia haisaidii kitu hawacheki kama mazuri
Deod 360.hujaelewa hoja iliyopo hapa.chid katumika Kama sample tu kuwakilisha kundi kubwa la vijana wanaopotea.hasara ya haya madawa haishii Kwa chid tu au mateja wa hapo magomeni au jwngwani Bali ni taifa lote Kwa ujumla.tufanye kitu kukomesha HII kitu.
 
Well said bro! Hili ni tatizo kubwa. Na unapomcheka Chidi Benz kumbuka kuna mwanao, mdogo wako etc ambaye naye yupo vulnerable na tatizo hili la unga. Shida hao wafanyaboashara za unga wana pesa nyingi na jamaa wa vyombo vya dola ndio wanakopatia pesa huko wakisahau kuwa huo unga utakuja kudhuru ndugu na jamaa zao... Hii inatakiea iwe vita kubwa
 
Unakuta mtu anamcheka teja wakati hata yeye wakati anaanza kuvuta sigara au kunywa pombe alianza kwa ushawishi wa kijinga !!
 
Watu walimuonea huruma mara ya Kwanza wakamsaidia kumpeleka kwenye matibabu wengine wakawa wanamwombea kwa Mungu arudie hali yake ya kawaida lakini juhudi zote za wasamalia wema kazikataa watu wafanyeje sasa kumsikitikia mtu asie jisikitikia haisaidii kitu hawacheki kama mazuri

Mkuu,unazungumzia madawa ya kulevya au soda fanta???
 
Mkataa pema pabaya panamwita, umenena vyema sana....lakini kumbuka chid sifa za kijinga ndo zinamwaribu kumsikitikia haitasaidia hata chembe.....anapaswa kubadili mwenendo basi, kama ushauri ashapata vya kutosha lakini hataki kusikia na kujiona yeye ndio mtoto wa mjini then guess what next....watu watamwacha na at the end tutampoteza japo wote tutakufa lakini, jamaa hataki msaada kabisaa kasaidiwa na kina babu tale lakini wapi, mama yake kila siku analia mtoto hataki kusikia wacha ulimwengu umfunze sasa....na hapa vijana tujifunze ukikosea kidogo tu katika maisha mambo yataharibika sana.
 
Mi najiuliza haya madawa yana ladha gani ambayo huwezi acha??
 
Umetoa analysis nzuri saana..hii imekua tatizo sugu hapa nchini nadhan ifikie kipindi bangi isiingizwe kwenye madawa ya kulevya kama mbunge msukuma alivyo weza kutoa faida zake..
Ilachonde chonde unga ni angamizi kwa kizazi jijacho ukipita stand utaona tena amelala humu AME simama
 
Back
Top Bottom