Aidan Eyakuze: Ripoti ya TWAWEZA iliyoonesha kupungua kwa Umaarufu wa Rais ilifanya nipokonywe Hati ya kusafiria

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,989
Waraghbishi ni wananchi wanaofanya kazi ya kuichokoza jamii iweze kujitambua na kuona wao ni watendaji wakuu katika maendeleo ya maisha yao.

Zaidi ya waraghibishi 170 kutoka Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Maswa, Mbogwe, Kigoma-Ujiji, Kishapu na Pangani wanakutana Dar es Salaam kufahamiana, kubadilishana mawazo na kujifunza kutokana na uzoefu wao katika kuchochea ushiriki wa wananchi kujiletea maendeleo.

FeXWIfEWQAAhjgG.jpg

AIDAN EYAKUZE - Mkurugenzi Mtendaji, TWAWEZA
Mara nyingi viongozi wengi hawapendi kukosolewa, mfano Serikali ya Awamu ya 5 ilikuwa na maono yake lakini ilikuwa ngumu kufanya nayo kazi

Wanasiasa walidhibitiwa na hakukuwa na mikutano ya kisiasa, AZAKI pia zilipitia changamoto nyingi

Hata leo bado kuna wasiwasi kama wameruhusiwa mikutano ya kisiasa au la, Bunge ‘live’ lilizuiliwa, Tundu Lissu alinusurika kuuawa.

Wapinzani walirubuniwa kuhamia upande wa pili, wengine wakatoweka kabisa, ilikuwa hali ya msukosuko na hofu.

TWAWEZA tulipambana kulinda haki za msingi, ilikuwa kazi ngumu sana.

Tulipofanya utafiti wapo Wananchi waliosema wanapenda demokrasia, na wapo waliosema wanaunga mkono usitishwaji wa mikutano ya kisiasa.

Mwaka 2019, tukishirikiana na LHRC tulialikwa Dodoma kutoa maoni yetu na ya wengine, kuelimisha Wabunge kuhusu mapunguvu ya Sheria zinazowekwa

Siku chache baadaye habari ikatoka Gazetini kuwa ‘Wabunge 11 wamehongwa na Twaweza’, ilikuwa ni uongo.

Dodoma Hotel tulipofanya mkutano wetu napo wakahojiwa kiasi wakatuambia tukiwa na tukio tutafute hoteli nyingine.

Sisi pia tukaitwa TAKUKURU kuhojiwa, nilihojiwa kwa saa tatu, nikawaambia hatukuhonga bali tuliwapa chai Wabunge labda hiyo ndio hongo.

Wakati wa Awamu ya 5, Vyombo vya habari vilipitia changamoto, mfano wanahabari kulazimishwa kuwa na vyeti na wasajiliwe.

Mnamkumbuka Azory alitoweka mpaka leo hatujui yuko wapi, magazeti yakafungiwa, faini zikawa nyingi, hofu ilikuwa kubwa.

Mwaka 2019, Serikali ilibadilisha Sheria kadhaa ili ipate uwezo wa kuzifuta AZAKI bila kuwa na uwezo wa kwenda Mahakamani.

Masharti yamekuwa mengi, wengine walitishiwa, uhuru wa Wananchi kukusanyika kupitia mwamvuli wa taasisi yoyote ulikuwa mgumu.

(Awamu ya 5) Masharti ya kuwa na AZAKI yakawa magumu, kuna ambazo zimefutwa, wengine wakatishiwa akaunti zao kufungiwa, urasimu ulikuwa mwingi.

Serikali ilisema inataka maendeleo, Mkurugenzi wa Uchaguzi alisema watu wanataka maendeleo hawataki Demokrasia. Tulisisitiza vitu hivyo vinaendana na ni lazima maendeleo yapatikane katika misingi imara, hata wasanii nao walipata vitisho kadhaa.

Julai 2018, Twaweza tulitoa matokeo ya utafiti yaliyoonesha umaarufu wa Rais, Madiwani na Wabunge umeporomoka. Uhamiaji wakachukua pasi yangu ya kusafiria, wakakaa nayo kwa miaka 2 na miezi 7 wakidai kuwa na shaka na uraia wangu.

Kuna watu waliniambia nikaombe msamaha, nilipowauliza kosa langu hawakuwa na majibu. Wakataka Twaweza tuwe tunatoa mambo mazuri mazuri, nikasema nikifanya hivyo tumekwisha na heshima yetu yote ingeishia hapo.

Binafsi Polisi walienda kuangalia makaburi ya babu yangu na babu mzaa babu, wakanisaidia kuithibitishia uraia wangu kuwa mimi ni Mtanzania. Niwaambie ukidai haki hata katika mazingira magumu unaweza kuipata, tetea haki zako, usinyamaze.

Tulikaa kimya kwa miaka minne, hadi mwaka huu (2022) ndio tukatoa ripoti ya utafiti.

Tukatengeneza utafiti wa Tozo, siku tunataka kutoa ripoti, polisi walikuja hadi RPC alikuwepo, tukawaambia tuna haki ya kutoa takwimu na tumefuata mchakato wote.

Tukawaambia ndani ya ukumbi kuna waandishi na mtakapoingilia mtawapa nafasi ya kuwapiga picha na hiyo ndio itakuwa stori.

Tukatoa takwimu za Tozo, mjadala ukawa mkubwa, hatimaye wiki iliyopita wakapunguza tozo. Sauti za wananchi zikasikilizwa.
 
Back
Top Bottom