green rajab
JF-Expert Member
- Oct 16, 2015
- 11,305
- 35,852
Unamuita mfungwa afande au ni mhalifu mwenzioJaribio la pili la aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), Christopher Bageni kujinasua na adhabu ya kunyongwa, baada ya kutiwa hatiani kwa kuwaua wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi, limekwama katika Mahakama ya Rufani juzi.
Mahakama hiyo ya juu kabisa nchini, imeyaondoa mahakamani maombi aliyofungua Bageni, akitaka hukumu iliyomtia hatiani irejewe upya.
Ilieleza kuwa sababu zake za kuiomba ibadilishe hukumu hiyo hazikuwa na mashiko ya kisheria, kwani Bageni alifungua maombi mengine ya marejeo akiomba jambo lilelile.
Majaji Gerald Ndika, Mwanaisha Kwariko na Barke Sehel, waliosikiliza maombi hayo waliridhika na hoja ya Jamhuri kuwa maombi hayo yalifunguliwa nje ya muda.
Bageni na askari wenzake 12, akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Abdallah Zombe walishitakiwa mwaka 2006 kwa mauaji ya wachimba madini watatu kutoka Mahenge, Morogoro.
Hili ni jaribio la pili la kachero huyo la kutaka uhuru, baada ya maombi yake ya kwanza kutupwa na mahakama hiyo Septemba 2019 kwa kutokuwa na mashiko kisheria.
Katika kuishawishi mahakama, Bageni, katika maombi yake ya pili aliambatanisha uamuzi wa kesi iliyowahi kuamriwa na mahakama hiyo inayoonesha kuwa mahakama inaweza kusikiliza maombi ya marejeo juu ya maombi mengine ya marejeo.
Hata hivyo, jitihada zake ziligonga mwamba juzi baada ya Mahakama ya Rufani kuibua hoja juu ya usahihi wa maombi hayo na hivyo kulazimika kuyaondoa mahakamani.
Wakili wa Serikali Mkuu, Monica Mbogo alileta pingamizi akieleza kuwa mwombaji huyo tayari alikwishafungua maombi kama hayo yaliyokwishaamriwa, hivyo hakuwa na haki ya kisheria kufungua maombi mengine kama hayo.
Bageni, ambaye hakuwakilishwa na wakili, alipingana wa wakili huyo wa Serikali akidai Serikali haikuwa na sababu za msingi.
“Maombi haya yameletwa tangu mwaka 2019 na tayari yalikuwa yasikilizwe juzi. Sasa Serikali kuja leo na pingamizi hili ni mbinu tu ya kutaka kuchelewesha usikilizwaji wa maombi haya. Hivyo naomba muone kwamba Serikali haina sababu ya msingi na myakatae,” alisema Bageni.
Hata hivyo, baada ya ufafanuzi wa mahakama kuhusu umuhimu wa kusikiliza pingamizi hilo, Bageni aliridhia na kuamua kuondoa pingamizi lake na mahakama ikalipokea pingamizi hilo la Serikali.
Kiongozi wa jopo la majaji, Jaji Ndika alieleza kuwa mbali na pingamizi hilo la Serikali, mahakama nayo ilikuwa na hoja yake ya msingi, ikitaka kwanza kujua iwapo maombi ya Bageni yaliwasilishwa ndani ya muda wa siku 60 baada ya hukumu ya kwanza kama sheria inavyotaka.Katika marejeo ya pili, Bageni alikuwa akiiomba mahakama irejee uamuzi wake wa rufaa aliyokata Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) na kuamriwa Septemba 16, 2016 na maombi yake hayo ya marejeo ya pili aliyawasilisha Oktoba 10, 2019, miaka mitatu na mwezi mmoja baadaye.
Baada ya maelezo hayo, Bageni alikiri kuwa maombi yake yaliwasilishwa nje ya muda na akaridhia yaondolewe ili akajipange upya.
“Baada ya majadiliano na mahakama, mleta maombi (SP Bageni) amekubali kuyaondoa mahakamani chini ya kanuni ya 58(1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani. Mjibu maombi hakuwa na pingamizi,” alisema Jaji Sehel, aliyesoma amri ya mahakama na kongeza:
“Nasi tumekubaliana na maombi ya mleta maombi. Hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 58(1) ya Kanuni za Mahakama za Mahakama ya Rufani, tunayaondoa maombi haya.”
Haikuweza kufahamika mara moja kama Bageni alimaanisha kuwa atafungua maombi mengine au la, pale alipoomba muda wa kwenda kujipanga upya.
Kama bado anataka kuendelea na kesi hiyo, Bageni atapaswa kwanza kuwasilisha mahakamani maombi ya kibali cha kufungua maombi ya marejeo nje ya muda na kutoa sababu zitakazoishawishi mahakama kwa nini alichelewa kufungua maombi yake hayo ndani ya muda.
Juzi mahakama ilidokeza kuwa hata akifanikiwa kuishawishi ikubali afungue maombi ya marejeo nje ya muda, askari huyo atakabiliwa na kiunzi kingine cha kuishawishi mahakama kuwa ana weza kufungua maombi ya marejeo juu ya maombi mengine ya marejeo.
Mwananchi