Mwili wa Wakili Maira kurejeshwa Aprili 30
Wednesday, 22 April 2009 16:07
Na Makumba Mwemezi
MWILI wa aliyekuwa wakili katika kesi ya Abdallah Zombe, marehemu Moses Maira (66) aliyefariki dunia juzi nchini Marekani alikokuwa kwa matibabu unatarajiwa kuwasili nchini Aprili 30 kwa ajili ya mazishi.
Akizungumza nyumbani kwa marehemu Dar es Salaam jana, Msemaji wa familia Bw. Semba Wilson alisema awali walitarajia kusafirisha mwili wa marehemu kesho ambapo ungefika Jumapili lakini kutokana na ndege kujaa wamepangiwa Aprili 28 ambapo ndege itafika nchini Aprili 30.
Alisema taratibu za mazishi zinaendelea vizuri na kuwa Marehemu anatarajiwa kuzikwa Dar es Salaam mara baada ya mwili kuwasili.
Marehemu Maira ndiye aliyekuwa wakili katika kesi inayomkabili aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam ambapo anatuhumiwa kuwaua wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge, Morogoro pamoja na dereva teksi wa Dar es Salaam.
Kifo cha wakili wa Zombe kimekuja siku chache baada ya kifo cha aliyekuwa mshitakiwa na shahidi muhimu katika kesi hiyo ya mauaji marehemu Koplo Rashid Lema aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa saratani.
Akimzungumzia wakili Maira, mkwe wa marehemu ambaye pia ni Wakili katika kampuni ya Membar Law Attorneys, Bw. Yassin Membar alisema alikuwa mchapakazi mwenye upendo na moyo wa kusaidia.
Source:Gazeti la Majira.