ACT Wazalendo: Mashauri ya ukatili wa Watoto na Wanawake yaendeshwe ndani ya miezi miwili

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Katika kuadhimisha ya Siku ya Mtoto wa Kike Duniani ambayo inaadhimishwa Oktoba 11 kila Mwaka, Chama cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kusimamia kupunguzwa kwa muda wa kuendesha mashauri ya ukatili dhidi ya Watoto na Wanawake.

Chama hicho kupitia taarifa yao iliyotolewa na Janeth Joel Rithe (Waziri Kivuli wa Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Watoto) kimependekeza usikilizwaji wa mashauri hayo usizidi muda wa miezi miwili.

"Tunapendekeza Serikali isimamie kupunguza muda wa uendeshaji wa kesi za ukatili dhidi ya Watoto na Wanawake. Tunataka zipunguzwe hadi kufikia miezi isiozidi miwili kumalizika kwa kesi."

ACT imetoa pendekezo hilo baada ya kudai kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na changamoto kubwa pamoja na matukio mengi ya ukatili dhidi ya Watoto wa kike, ambapo wametoa mfano wa matukio hayo kuwa ni pamoja na udhalilishaji wa Watoto mitandaoni.

"Changamoto kubwa zinazowakabili Watoto wa kike ni kukithiri kwa matukio ya ukatili dhidi yao, kama vile Ubakaji, Ulawiti na udhalilishaji wa mitandaoni. Vilevile wanakabiliwa na changamoto ya ndoa za utotoni pamoja na mimba za Utotoni."

Aidha, taarifa hiyo, imedai kumekuwepo kwa changamoto ya mazingira salama shuleni kwa mtoto wa kike kama vile kukosa vifaa vya kujisitiri (taulo za hedhi) na Sheria zinazozuia waathirika wa mimba kuendelea na masomo.

"Kuendelea kuwepo kwa changamoto hizi kunazuia fursa kwa watoto wa kike kupata haki zao na kutimiza malengo yao katika jamii," imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, katika mapendekezo yao ambao wamesema yanaweza kuleta utatuzi, wameshauri Serikali pamoja na Wadau kuunganisha nguvu katika kupiga vita ndoa za utotoni, mila za ukeketaji na mimba za utotoni.

Pia wameshauri "Serikali iongeze usalama na stadi za maisha kwa Watoto shuleni kwa kupanua na kuanzisha Mabaraza ya Watoto, klabu za watoto na kwa upekee kabisa kutoa bure vifaa vya kujistiri na hedhi kwa wasichana."

Wametoa wito kwa Serikali kuboresha madawati ya Watoto ili kukomesha ukatili dhidi ya Watoto.

Hata hivyo, wameeleza wazi athari ambazo zimekuwa zikitokana na ukatili dhidi ya Watoto wa kike katika jamii, ambapo wamedai ni pamoja na athari za kijamii, kiuchumi na hata kiafya.

Pia wameweka bayana kuwa ukatili unapalilia kukosekana kwa usawa katika upatikanaji wa huduma muhimu za kijamii baina ya mtoto wa kike na wa kiume.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom