Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,783
- 14,975
UCHAMBUZI WA BAJETI YA OFISI YA WAZIRI MKUU KUHUSU MAPITIO NA MWELEKEO WA KAZI ZA SERIKALI 2025/26
“Serikali inaogopa uchaguzi huru na haki”
Utangulizi
Tarehe 09 Aprili 2025 Waziri Mkuu aliwasilisha Bungeni mapitio na mwelekeo wa kazi za Serikali na makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2025/2026 jijini Dodoma. Katika kuendeleza wajibu wetu wa kuisimamia Serikali, nikiwa Msemaji Mkuu wa Kamati ya ACT Wazalendo ya Kuisimamia Serikali (Waziri Mkuu Kivuli), tumepitia na kuchambua hotuba hiyo ya Waziri Mkuu na tumebaini mambo yafuatayo:
Ni matarajio yetu kwamba hotuba ya Waziri Mkuu ingeweza kuzungumza na kutoa majawabu katika changamoto mbali mbali zinazoikabili jamii na nchi yetu. Ni matarajio yetu kwamba Waziri Mkuu, ambaye kwa mujibu wa Ibara ya 52 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ndiye mwenye madaraka ya juu kusimamia na kutekeleza shughuli za kila siku za serikali, angeweza kuzungumza na kutoa majawabu kuhusu ukosefu mkubwa wa ajira, hali ngumu ya maisha, matukio ya kutekwa, kuuawa na kutekwa kwa raia, ufisadi mkubwa bila uwajibikaji na sintofahamu ya wananchi kuelekea uchaguzi mkuu 2025.
Uchambuzi wetu wa hotuba ya Waziri Mkuu unaonesha kwamba, serikali ya CCM imeamua kujiongoza na kujihusisha na siasa za uongo, ulaghai na zisizo shughulika na matatizo ya wananchi; huku masuala makuu ya wananchi na kitaifa yakiwa hayajapewa kipaumbele. Miongoni mwa mambo ambayo yalipaswa kutolewa kutolewa muelekeo, lakini serikali haijafanya hivyo ni kama yafuatayo:
Ofisi ya Waziri Mkuu inahusika moja kwa moja na masuala ya ajira na uwezeshaji kupitia Wizara ya Vijana, kazi na ajira. Mwenendo na hali ya ukosefu wa ajira nchini inazidi kuwa mbaya, kuna ongezeko kubwa la nguvukazi ambayo haina ajira na iliyo kwenye sekta isiyo rasmi nchini. Hata vijana waliohitimu katika fani mbalimbali nchini wameendelea kusota bila ajira. uwezo wa serikali kuajiri na kuzalisha ajira ni mdogo mno. Mathalan Mwaka huu 2025 serikali ilitangaza ajira 12,000 za ualimu lakini walioomba walikua watu 201,707, Mamlaka ya Mapato Tanzania ilitangaza ajira 1,596 Lakini waliojitokeza kuomba ni watu 135,027 Hii ni ishara kuwa Maelfu ya watazanzia wasomi wanakosa ajira kutokana na uwezo mdogo wa serikali katika kuzalisha ajira.
Athari za janga hili ni kubwa sana katika jamii yetu kwa sasa, ikiwemo kuongezeka kwa wimbi la umasikini na utegemezi, kuongezeka kwa mmomonyoko wa maadili na uhalifu nchini ikiwemo vitendo vya wizi, ukahaba, unyang’anyi, uporaji. Kuongezeka kwa upendeleo, kujuana, rushwa katika utolewaji wa kazi, kuongezeka kwa utumikishaji wa watoto kwa ujira mdogo au bila malipo hususani; Mashuleni, viwandani, majumbani, migodini nk kwa kigezo cha kupatiwa ajira.
Waziri Mkuu hajaliambia bunge ni hatua gani watakabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini badalayake ameeleza tu kwa jumlajumla kuwa Kwa miaka mitano ya serikali wamezalisha ajira Milioni 8.084. Katika hotuba za Waziri Mkuu kwa miaka mitano mfululizo inaonyesha jumla ya ajira zilizozalishwa katika sekta ya umma na binafsi ni Milioni 2 [2,196,619]. Kwa takwimu hizi, tunakila sababu ya kuhoji taarifa ya Waziri Mkuu iliyotolewa siku ya jana; hawa watu Milioni 6 wameongezeka kutokea wapi?
Takwimu zinaonesha kuwa ajira rasmi nchini (sekta ya umma na binafsi) kwa ujumla ni watu Milioni 3.717, katika mchanganuo huu Sekta Binafsi inatoa ajira Milioni 2.577. licha ya sekta binafsi kuajiri watu wengi zaidi hali ya malipo kwa wafanyakazi ni mbaya na haiendani na mahitaji ya sasa, mathalan 37% ya wafanyakazi sekta binafsi wanalipwa chini ya Lakitatu. Na asilimia 13.4% tu wanalipwa zaidi ya laki saba.
Kwa upande mwengine zaidi ya watu Milioni 25 wako kwenye shughuli zisizorasmi kama kilimo, uvuvi, umachinga, ufundipikipiki, uyaya, udalali,upishi, udereva bodaboda nakadhalika. Kazi hizi hazitambuliki na hazina hifadhi ya jamii. Hii ina maana kuwa mtu huyu akipata changemoto kidogo anatumbukia kwenye lindi la umasikini. CCM kwa zaidi ya miaka 63 imeshindwa hata kuchochea shughuli zinazozalisha kazi na ajira zakutosha.
ACT Wazalendo tunaitaka serikali kuacha mzaha na suala la ajira na maslahi ya wafanyakazi nchini, mapendekezo yetu katika kuongeza upatikanaji wa ajira ni kama ifuatavyo:
- Mosi, tunataka Serikali kuwekeza vyakutosha kwenye Sekta ya Kilimo, sekta ya kilimo inaajiri zaidi ya 65% ya watanzania, kuwekeza kwenye kilimo kwa kuhakikisha upatikanaji wa uhakika wa mbolea, viwanda vidogovidogo na vikubwa vya kuongeza thamani ya mazao.
- Pili, tunaitaka Serikali itekeleze miradi mikubwa kama kiwanda cha gesi asilia (LNG) ya Lindi itakayozalisha mamilioni ya Ajira kwa vijana kuanzia uzalishaji wa Gesi, usambazaji na matumizi. Pamoja na mradi wa Chuma na makaa ya mawe wa Mchuchuma na Liganga. Kuharakishwa kwa ujenzi wa miradi hii kutasaidia kuzalisha ajira nyingi nchini.
- Tatu, Serikali itoe ajira za kutosha kwa waalimu, watumishi wa afya na wataalamu wengine kulingana na mahitaji ili kupunguza uhitaji uliopo.
- Mabadiliko ya kisiasa kuelekea Uchaguzi mkuu 2025
Katika hotuba yake Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (Mb) ameliambia Bunge kuwa “hali ya demokrasia nchini imeimarika” Hata hivyo Waziri Mkuu anaeleza tu suala la kubadilishwa jina kwa iliyokua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) lakini haelezi chochote juu ya mwenendo wa kisheria wa tume hiyo. Kauli hiyo ni kauli ya serikali kiziwi isiyosikiliza na kujali maoni ya wananchi.
Vilevile, Waziri Mkuu ameeleza kuwa tume imeshakamilisha utungwaji wa Kanuni za uchaguzi 2025. Hata hivyo, katika kanuni hizo yapo maeneo mengi yaliyolalamikiwa sana na wadau na vyama vya siasa, uchambuzi wetu unaonesha kuwa kanuni hizi zinalenga kuendeleza hila katika uchaguzi. Miongoni mwa masuala yanayolalamikiwa ni kama vile kiapo cha kutunza siri, uteuzi wa waangalizi wa uchaguzi (haki, wajibu, makatazo kupotezasifa) Mawakala wa upigajikura, Matokeo katika kituo cha kupigia kura, Ratiba ya kampeni na maeneo mengine mengi.
Mfano, Kanuni za sasa mgombea hana haki ya kuingia vituo vya kura kushuhudia zoezi la upigwaji kura kama ilivyokua huko nyuma, huu ni mtego wa wazi unaoashiria mipango michafu inayolindwa na kanuni hizi. Ni wazi kanuni hizi zinapaswa kupitiwa na kuandikwa upya.
Takribani Chaguzi tatu zilizopita tumeshuhudia wagombea wa vyama vya Upinzani wakienguliwa, tumeshuhudia kura feki zikizunguka mitaani na kusambazwa kwenye vituo vya kupigia kura, mawakala kuzuiwa vituoni, vyombo vya ulinzi na usalama na watumishi wa umma wakishiriki kuisaidia CCM kuzitumbukiza kwenye masanduku.
Hali hii inafanya sisi kama chama makini cha kisiasa kuingia kwenye mapambano, mapambano ya kuihami Demokrasia. ACT Wazalendo tumeamua kutoa uongozi katika kudai mabadiliko mahususi ya mifumo ya uchaguzi, tumeamua kupigania kurejesha heshima ya Kura kupitia kampeni ya #OperesheniLindaDemokrasia. Katika oeresheni hii pamoja na mambo mengine tunataka utekelezaji wa sheria Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 1 ya Mwaka 2024 na tunataka mambo yafuatayo yarekebishwe ili kurejesha Imani ya wananchi katika uchaguzi na kuwapa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowataka, madai hayo sita ni;
- Makamishna wa Tumehuru ya taifa ya Uchaguzi wapatikane kwa ushindane
- Wakurugenzi wa halmashauri wasiwe wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo
- Mawakala wa vyama vya siasa wafanyekazi zao bila bughudha na wasizuiwe
- Wagombea wasienguliwe
- Pasiwe na kura feki
- Vyombo vya ulinzi na usalama visiingilie mchakato wa uchaguzi
Nchi hii kila chama kina haki sawa kisheria, tumeshuhudia CCM wakifanya ziara zao bila bughudha, huu ni mwaka wa uchaguzi, vyama vyote viachwe vifanye kazi kwa usawa.
Usalama wa Raia
Hali ya usalama wa raia nchini imeendelea kuzorota kwa kiwango cha kutisha katika mwaka 2024/25, ambapo matukio ya utekaji, kupotea kwa watu na mauaji ya kikatili yameripotiwa waziwazi bila hatua madhubuti kuchukuliwa. Tanzania imeingia katika orodha ya nchi ambazo usalama wa binadamu unazidi kuwa wa mashaka, huku raia wakitekwa mchana kweupe, wakiuawa kwa mazingira ya kutatanisha au wakipotea bila maelezo ya Serikali. Matukio haya si ya bahati mbaya; yanaakisi udhaifu wa vyombo vya usalama na ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
Mwaka 2024 Taarifa rasmi za Tanganyika Law Society ilionesha watu 89 walitekwa, kuteswa au kuuawa katika mazingira ya kutatanisha. Miongoni mwa matukio haya ni pamoja na kupotea kwa Deusdedit Soka, kutekwa kwa Manase Daniel na Method Damian Machi, Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana Taifa wa ACT Wazalendo Ndg.Abdul Nondo, Edger Mwakalebela, kuuawa kwa mwanachama wa CHADEMA Ndg. Ali Kibao na matukio mengi yaliyokithiri tangu kuingia madarakani serikali hii. Vyombo vya dola vimehusishwa na baadhi ya matukio haya, lakini hakuna uwazi kuhusu uchunguzi wala hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.
Mtakumbuka mwaka 2023 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya Usalama wa Taifa, katika sheria hiyo kifungu 4 (3) kinatoa haki ya Idara ya usalama wa Taifa kukamata na kuhoji watuhumiwa, lakini haifahamiki mahojiano hayo yanafanyikia wapi. Hivyo wanaweza kukuchukua na kukupeleka kusikojulikana, Uchambuzi wetu tunaiona sheria na kifungu hicho kama sheria inayoruhusu utekaji (Kidnaping act) na inapasa kuondolewa.
Katika hali ya kusikitisha, Serikali kupitia hotuba ya Waziri Mkuu imeyanyamazia au kupuuzia matukio haya, ikidai kuwa hali ya usalama inaimarika. Kauli kama hii si tu kwamba ni kinyume na ukweli wa mambo, bali ni dhihaka kwa waathirika, familia za waathirika na taifa kwa ujumla. Wananchi wanapoteza imani kwa vyombo vya ulinzi na usalama
ACT Wazalendo tunaitaka Serikali kuchukua hatua zifuatazo;
Mosi, Rais arejesha tena Bungeni Muswada wa sheria ya usalama wa Taifa na kuondosha kabisa kifungu kinachoruhusu maafisa wa idara ya usalama wa Taifa kukamata raia.
Pili, Maka Rais aunde tume ya kijaji ili kuchunguza matukio yote ya utekaji, mauaji na ukiukwaji wa haki za binadamu dhidi ya wananchi.
Tatu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aweke wazi ripoti ya tume ya haki jinai na kufanyia kutekeleza mapendekezo yote yaliyotolewa na Tume hiyo kuhusu mfumo wetu wa haki jinai.
Masuala ya Uwajibikaji
Tumeshuhudia watu wachache wakiendelea kutafuna fedha za umma bila kuchukuliwa hatua, Ripoti ya CAG kwa mwaka 2022/23 imebaini ubadhirifu wa zaidi ya Shilingi trilioni 3.2. fedha nyingi namna hii zingeweza kutumika katiak kuboresha hali ya maisha ya wananchi masikini.
Licha ya upotevu wa fedha za umma, hatujasikia mahala popote, kiongozi yoyote amechukuliwa hatua kwa ubadhirifu huu. Waziri mkuu kama mtendaji mkuu wa serikali hakusema lolote kuhusu jambo hili, ni dhahiri kuwa jambo hili lina Baraka ya serikali na kwamba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania halijatoa uelekeo madhubuti wa kuisimamia serikali.
Ripoti za mashirika ya kimataifa kama Global Financial Integrity zinaonesha kuwa Tanzania inapoteza zaidi ya dola za Marekani bilioni 1.5 kila mwaka kupitia utoroshaji wa fedha haramu nje ya nchi. Hii ni zaidi ya Shilingi trilioni 3.9.
Kuendelea kwa matukio ya ubadhirifu wa rasilimali za umma kumesababisha kuongezeka sana kwa matabaka ya watu wenye ukwasi na mali nyingi na masikini wa kutupwa nchini, utumishi wa Umma sasahivi si wito bali ni bahati ya utajiri. Watumishi wasio na hofu wanalindwa na Dola wanaendelea kuchukua haki za mamilioni ya watanzania wanaokufa kwa kukosa dawa, maji safi na barabara mbovu. Ubadhirifu sasa hivi si jambo la kuogofya, imezoeleka kuwa sasa ubadhirifu unafichwa kwa utaalamu wa kihasibu na kusafisha vitabu huku mafisadi wakichota fedha za umma.
ACT Wazalendo tunaitaka kutengeneza mfumo thabiti wa kudhibiti uvujaji wa fedha za umma na kunufaisha watu wachache. Tunaitaka serikali kuwachukulia hatua kali za kisheria ma afisa massuli wote waliohusika na Wizi, Ufisadi, uzembe na upotevu wa fedha za umma. Kukalia kimya masuala haya ni kiashiria kwamba wizi, ubadhirifu na utoroshaji fedha una mkono wa Serikali. Tutaendelea kuibua masuala mbalimbali yaliyofanyiwa ukaguzi na CAG na kuueleza Umma namna ambavyo serikali ya CCM inashiriki wizi wa fedha za Umma na kuwacheleweshea maendeleo.
Mwisho, Mwaka huu ni mwaka wa Uchaguzi mkuu, mwaka huu ni mwaka wa watanzania kuamua kuhusu nchi yao, tunafahamu wananchi wana majeraha makubwa, tunafahamu wananchi mmekata tamaa. Mmekata tamaa si kwasababu mliowachagua hawafanyi mnayoyataka bali mliowachagua waliondolewa kwa hila na woga na walioteuliwa wamezigeuza ofisi za umma kama maduka binafsi. Wito wetu ni mmoja tu, wito wa mapambano, mapambano ya kulinda Demokrasia. Hatuna wakumsusia nchi hii, hakuna wakumlaumu, ni wakati wetu sote kuungana pamoja katika kudai mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi.
Ahsanteni sana.
Imetolewa na:
Isihaka R. Mchinjita.
Waziri Mkuu Kivuli
ACT Wazalendo
10 Aprili 2025