SoC02 Baada ya Sensa ya 23, Agosti 2022, Tuhamie kwenye Sensa Endelevu. Teknolojia imekua

Stories of Change - 2022 Competition

Vitamin K

Senior Member
Dec 2, 2017
158
168
UTANGULIZI:
Sensa ya watu na makazi ni nini?
Ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua, kutathimini na kuchapisha na kusambaza takwimu za kidemographia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na watu wote na makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum. Kwa maana nyingine, sensa ni zoezi maalum lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsia, mahali wanapoishi na hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi.(Chanzo Tovuti ya NBS)

Sensa ya mwaka huu(2022) ni sensa ya 6 tangu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo nyuma ziliwahi kufanyika sensa mwaka 1967, 1978, 1988, 2002 na 2012.(Chanzo Tovuti ya NBS).
chart.png

Graph: Chanzo Tovuti NBS

Sensa zote hizo zilifanyika baada ya miaka kadhaa, kwasasa utaratibu wa kufanyika sensa ni baada ya miaka kumi.

Kwa sasa tuko kwenye Dunia ya Utandawazi iliyojaa teknolojia inayofanya mambo mengi kuwa rahisi ambapo kipindi cha nyuma yalikuwa sio rahisi, hatuna budi kwenda na teknolojia katika kutekeleza mambo ikiwemo hili la Sensa, hivyo basi baada ya hii ya tarehe 23, Agosti 2022 tuhamie kwenye Sensa ya kila siku(Endelevu) sio kila baada ya kipindi fulani kama sasa.

Sensa Endelevu itatekelezwaje?

1. Tuwe na mfumo wa Takwimu ya Sensa(Census Statistics Management Information System), Mfumo huu utabeba taarifa zote za watu wanaohesabiwa na kutunzwa humo kama ilivyo mifumo mbalimbali ya Taasisi mbalimbali nchini.

2. Suala la kuhesabu lianzie ngazi ya Kijiji/mtaa na Mahospitalini(Vituo vya Afya)

a)Kijiji/Mtaa
Mfumo wa Uongozi wa Taifa letu unaanzia ngazi ya chini kabisa Kijiji/Mtaa ambapo humo humo kuna uongozi wa nyumba kumi(Balozi). M/kiti wa Kijiji/Mtaa kwa kushirikiana na Balozi anapaswa kukusanya taarifa za vizazi katika eneo lake na kuziwasilisha ngazi ya Kata, Ngazi ya Kata wataziwasilisha ngazi ya Halmashauri na kwenda kuingizwa kwenye mfumo wa Sensa(nilioutaja hapo juu namba 1)
IMG_20220803_181908_049~2.jpg

IMG_20220803_180952_129~2.jpg

Picha: Chanzo Mtandaoni

b) Vituo vya kutolea huduma za Afya(hasa kujifungua)
Mtoto pindi anapozaliwa kituo kinapaswa kuchukua taarifa zake kwa kushirikiana na mzazi na kuzihifadhi kwenye mfumo wa Sensa.

Kuhusu wanaoingia na kutoka Nchini:

Hapa Idara ya Uhamiaji itahusika.
Kila mtu anayeingia nchini ambaye sio raia wa Tanzania, uhamiaji wanapaswa kufahamu kaja kwa lengo la kutalii/kutafuta hifadhi(mkimbizi)/kuhamia.
Wale wanaohamia na kuandikishwa kuwa raia, Idara ya uhamiaji ichukue taarifa zao na kuziingiza kwenye mfumo wa Sensa, pia wale wanaohama nchi Idara ya uhamiaji ichukue taarifa zao na kuzitoa kwenye mfumo wa Sensa.

Tuwe na Sheria itakayochochea utekelezaji wa Sensa Endelevu:
Sensa ya sasa ipo chini ya Sheria ya Sensa sura 351, Serikali kupitia Idara ya Takwimu(NBS) itunge sheria mpya/ifanye marekebisho pamoja na kuweka kanuni zake ili kila mzazi aweze kuwajibika kutoa taarifa za kizazi kipya(mtoto aliyezaliwa) kwa uongozi wa shina(Balozi) na Balozi aweze kuzikusanya na kuziwasilisha ngazi inayofuata( kwa M/Kiti) na yeye ataziwasilisha ngazi inayofuata(Kata) halafu Halmashauri kwa ajili ya kwenda kuingizwa kwenye Mfumo wa Sensa. Hiyo sheria pia impe mamlaka M/kiti wa Kijiji/Mtaa kuhoji taarifa za mtoto aliyezaliwa katika eneo lake.

FAIDA YA SENSA ENDELEVU:
1. Njia rahisi na sahihi ya kupata idadi ya watu kwa muda wowote tofauti na Sensa ya sasa ambapo ikipita miaka 2 mbele huwezi kupata idadi angalau inayokaribia usahihi wa idadi ya watu waliopo kwa muda huo, utaishia kuambiwa kulingana na Sensa ya mwaka 2022 idadi ya watu wa mji fulani ilikuwa inakadiriwa kuwa ni watu kadhaa. Sensa Endelevu tutaweza kupata idadi ya watu ama kwa mwaka au nusu mwaka.

2. Itawezesha kupanga bajeti sahihi kulingana na idadi sahihi ya watu waliopo kwa kipindi hicho, kipindi cha bajeti idadi sahihi ya watu inaweza kutolewa na NBS na ikatumika kupanga bajeti, tofauti na sasa inapofanyika kwa makadirio tu.

3. Itarahisisha kutoa huduma za kijamii hasa huduma za Afya(chanjo) kwa watoto kwani idadi halisi inakuwa inajulikana katika eneo husika.

4. Itaokoa gharama nyingi zinazotumika katika kuandaa Sensa kama hii ya sasa tunayoitarajia ambapo maandalizi yalianza tangu mwaka 2018.(Chanzo Tovuti ya NBS)

5. Itasaidia kubaini kwa haraka maeneo muhimu yanayohitaji huduma za maendeleo kwa haraka kulingana na idadi ya watu inayoongezeka

Kila lenye faida lazima liwe na hasara, Sensa endelevu pia ina hasara zake ikiwemo kukosekana uwajibikaji kwa wote watakaohusika matokeo yake Sensa Endelevu itakwama na kukosekana kwa takwimu za idadi ya watu katika kipindi husika hatimaye suala la Serikali kupanga bajeti ya maendeleo kukwama au kufanyika pasipo kuwa na takwimu sahihi za idadi ya watu.

MWISHO:

NB: Tujiandae kuhesabiwa ili tuweze kuhamia kwenye Sensa Endelevu, kwani ukihesabiwa sasa watakaokuwa wanaendelea kuhesabiwa ni wale tu watakaokuwa wanazaliwa baada ya siku tarehe 23 Agosti 2022.
 

Attachments

  • Sensa_Kiswahili_logo.jpg
    1.1 MB · Views: 6
Back
Top Bottom