Taarifa za Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi Zasaidia Zoezi la Uhakiki wa Waathirika wa Maafa Hanang

Stephano Mgendanyi

JF-Expert Member
May 16, 2020
1,898
942

Taarifa za Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi Zasaidia Zoezi la Uhakiki wa Waathirika wa Maafa Hanang

SERIKALI imetumia taarifa za matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika mwaka 2022 kuthibitisha taarifa za makazi na kaya katika maeneo yaliyoathirika na maafa ya Maporomoko ya tope na mawe wilayani Hanang Mkoani Manyara.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera Bunge na Uratibu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 kwa Viongozi na Watendaji wa Mkoa wa Ruvuma, iliyohusisha Kamati za Sensa na Wawakilishi wa Makundi Mbalimbali katika jamii tarehe 23 Disemba, 2023 katika ukumbi wa Njunde social hall – Halmashauri ya wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma.

Waziri alisema, moja ya jukumu muhimu walilonalo ni kupata taarifa ya hali ya kaya, makazi na mali katika maeneo yaliyoathirika kabla ya maafa hayo.

“Hitaji hili lilipelekea timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Taifa ya TAKWIMU kuja na taarifa ya kitaalamu iliyoambatana na picha za satellite ambazo zilionesha kwa uhakika hali ya kaya, makazi na mali zilizokuwepo katika maeneo hayo kwa idadi yake na maeneo zilizokuwepo,” alibainisha Mhe. Mhagama.

Aliongezea kuwa,licha ya kwamba wametumia vyanzo vingine pia kuthibitisha baadhi ya masuala katika maeneo hayo, lakini chanzo cha kwanza cha kuaminika kimekuwa ni matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwakumbusha kuhusu maandalizi ya Dira ya Taifa ya Mwaka 2050 ambapo serikali imetoa fursa kwa wananchi kutoa maoni na mapendekezo.

”Niwasihi sana viongozi, watendaji na wananchi wote mshiriki katika zoezi hili ambalo ni muhimu kwa mustakabali mwema wa maendeleo ya nchi yetu, moja ya nyenzo muhimu zinazoweza kutuongoza kutoa maoni yetu ipasavyo historia ya taifa letu katika nyanja zote za siasa, uchumi, jamii pamoja na kuzingatia takwimu zinazozalishwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikiwemo ya matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022,”alifafanua.

Kwa upande wake Mwantumu Athumani Meneja Takwimu Mkoa wa Ruvuma akizungumza kwa niaba ya Mtwakwimu Mkuu wa serikali, alisema utoaji wa matokeo ya sensa ni tofauti na matukio mengine ya kitakwimu kwa kuwa wigo wa sensa ni mpana zaidi.

”Matokeo ya sensa hutolewa kwa awamu kulingana na ratiba ya utoaji na usambazaji wa matoke hayo ,” alisema

Ameongeza kusema kama kuna mdau anahitaji matokeo ya sensa, ambayo hayapo kwenye ripoti zetu kwa sasa anakaribishwa kuleta maombi yake kwenye ofisi Takwimu za mikoa.

Naye Mkazi wa Peramiho Bw. Tito Sowela alisema elimu ya sensa ya watu na makazi imeongeza uelewa mpana wa wananchi hasa juu ya taarifa zinazokusanywa na namna zinavyoweza kusaidia serikali katika kupanga miradi ya maendeleo kwa wananchi.

=MWISHO=
 

Attachments

  • c96e22b6a81b62b36608afb0042031da.jpg
    c96e22b6a81b62b36608afb0042031da.jpg
    182.5 KB · Views: 2
Back
Top Bottom