Kutokana na tukio la kinyama
lililotokea Arusha, sitaweza kusoma
hotuba ya Bajeti Kivuli Bungeni.
Wabunge wote wa CHADEMA
tunaenda Arusha kuomboleza,
kutafakari na kuwapa moyo
watanzania wenzetu. Kufuatia
matokeo ya mchezo wa leo dhidi ya
Ivory Coast, nimeona niwamegee
kile ningesema kuhusu Michezo.
Soma natafakari.
MAENDELEO YA MICHEZO
Mheshimiwa Spika, maendeleo
mazuri ya michezo katika taifa
lolote, ni utambulisho mzuri wa
taifa hilo katika mataifa mengine
kutokana na ushirikiano wa
kimichezo na mataifa hayo. Pamoja
na mambo mengine, michezo katika
nchi yetu inaweza kutumika
kutengeneza fursa za kiuchumi kwa
kuitangaza nchi yetu duniani katika
sekta za utalii na uwekezaji. Ukiacha
mbali suala la manufaa ya kiuchumi
yanayoweza kupatikana kupitia
michezo, michezo pia inawajengea
vijana wetu afya na hivyo kuwa na
taifa la watu wakakamavu. Kwa
upande mwingine, michezo pia ni
ajira. Inasikitisha kwamba katika
hotuba nzima ya Waziri wa Fedha,
hapakuwa na mpango wowote wa
kukuza michezo hapa nchini bila
hata kujali kwamba timu yetu ya
Taifa ya Mpira wa Miguu ipo katika
nafasi nzuri sana hivi sasa kuliko
wakati mwingine wowote katika
kuweza kufuzu kucheza fainali za
kombe la Dunia mwakani.
Mheshimiwa Spika, Kamati ya
Bunge ya Maendeleo ya Jamii katika
barua yake ya tarehe 5/4/2013
iliomba Kamati ya Bajeti kuangalia
namna ya kusaidia kupata fedha za
kujenga michezo na hasa kusaidia
Taifa Stars katika juhudi zake za
kuelekea kufuzu kwenye michuano
ya kombe la Dunia huko Brazil.
Hata hivyo Wizara ya Fedha
haikutoa hata senti tano kwa ajili
hiyo. Kamwe hatuwezi kufanikiwa
kwenye michezo bila kuwekeza na
kutegemea juhudi za dharura za
kamati za kusaidia ushindi. Tukitaka
tungae kwenye michezo ni lazima
tuwekeze sana na kuwekeza ni
gharama, gharama ambayo
thamani yake ni kubwa sana kwa
nchi.
Mheshimiwa Spika, licha ya
michezo kuliingizia taifa mapato
kupitia asilimia 18 ya Kodi ya
Ongezeko la Thamani (VAT)
inayotokana na viingilio katika
michezo mbalimbali, hakuna
uwekezaji wowote wa maana
uliofanyika kwenye michezo jambo
ambalo ni hatari kwa uhai na
maendeleo ya michezo hapa nchini.
Aidha hakuna mipango madhubuti
ya muda mrefu kuhusu maendeleo
ya michezo hapa nchini.
Kutowepo kwa mipango madhubuti
na ya muda mrefu,
kumeshababisha timu zetu kufanya
vibaya katika mashindano mengi ya
kimataifa na hivyo kulifanya taifa
letu lionekane kuwa ni taifa dhaifu
au kichwa cha mwendawazimu
kama alivyopata kusema Rais
Mstaafu was Awamu ya Pili, Alhaji
Ali Hassan Mwinyi. Kambi Rasmi ya
Upinzani, inatoa angalizo kwa
Serikali kwamba, kamwe hatuwezi
kufanikiwa katika michezo kwa
mipango ya kukurupuka. Aidha ni
aibu kwa Serikali kukusanya kodi
kutokana na michezo, halafu vijana
wetu wanakosa fedha ya nauli
kwenda nchi nyingine kwa
mashindano ya michezo mpaka
wafanye harambee ya kukusanya
fedha kwa wahisani. Hivyo, Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na CHADEMA
inapendekeza mambo yafuatayo
yafanyike ili kunusuru tasnia ya
michezo hapa nchini;
1. Timu yoyote itakayowakilisha
taifa katika mashindano yoyote ya
kimichezo igharamiwe na Serikali
kwa asilimia 100.
2. Viwanja vyote vya Michezo hapa
nchini viundiwe Wakala wa Serikali,
Wakala wa maendeleo ya michezo
(Sports Development Agency).
Wakala huo uwe na majukumu ya
kujenga viwanja vipya na
kusimamia viwanja hivyo kwa niaba
ya Serikali. Viwanja vyote vya
michezo vilivyoporwa na CCM kama
Lake Tanganyika Kigoma, Ali
Hasan Mwinyi - Tabora, Kirumba
Mwanza, Maji Maji Songea nk
virejeshwe Serikalini mara moja
chini ya Wakala wa Viwanja vya
Michezo. Wakala pia ujenge
academies za michezo maeneo
kama vile Mbeya, Tanga, Mtwara,
Mwanza, Manyara na Dar es
Salaam ili kukuza vipaji vya watoto
na vijana.
3. Mashirika yote ya Umma, hasa
mashirika makubwa yawe na timu
za michezo. Ushauri uliotolewa na
IMF na Benki ya Dunia dhidi ya
Mashirika ya Umma kuwa na timu
ulikuwa ushauri usio wa maana.
Wenzetu Uganda kwa mfano,
Mamlaka ya Mapato Uganda (URA)
wana timu katika ligi Kuu, ambayo
ni moja ya timu mahiri katika
ukanda huu wa bara la Afrika.
4. Serikali ianzishe Mfuko Maalum
wa Michezo (Sports Fund). Pia,
Serikali ianzishe Kodi ya Maendeleo
ya Michezo (Sports Development
Levy). Kodi hii ipatikane kama
ifuatavyo: Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) ya asilimia 18
iliyokuwa ikikatwa kwenye viingilio
katika michezo mbalimbali
iondolewe na badala yake kiasi
hichohicho kiingizwe kwenye Mfuko
wa Michezo (Sports Fund)
utakaoanzishwa.
5. Matumizi ya Mfuko wa michezo
yawe kama ifuatavyo:
i. Asilimia 50 ya fedha
zitakazokusanywa zitumike kujenga
miundombinu ya michezo (Sports
Infrastructure) kupitia kwa Wakala
wa Maendeleo ya Michezo na
Academies.
ii. Asilimia 50 inayosalia itumike
kuhudumia maandalizi ya timu za
Taifa.