SoC02 Zanzibar Na uchumi wa buluu (Blue Economy)

Stories of Change - 2022 Competition

Chode kanju

Member
Sep 26, 2019
17
19
Zanzibar ianze na lipi kuelekea uchumi wa buluu wenye tija ?


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwenye Dira yake ya maendeleo ya mwaka 2050 miongoni mwa yaliyopewa kupaombele ni pamoja na sera ya uchumi wa buluu. Katika Dira ya maendeleo ya mwaka 2020 ambayo ilitekelezwa ndani ya miaka 20 kutokea mwaka 2000 hadi mwaka 2020, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kufikia hadhi ya uchumi wa kati wa kiwango cha chini (Lower-Middle Income status) ambapo imeshuhudiwa uchumi ukikua kwa kiwango cha 7% ambayo si mbali sana na lengo la ukuaji wa kati ya 9% na 10%. Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2020 ni wa kwanza tokea mapinduzi yaliyofanyika mwaka 1964, na kwa malengoya ujumla Dira hii ya maendeleo ya mwaka 2020 ilifanikiwakwa kiasi kikubwa kwani katika kipindi cha miaka 20, tumeshuhudia uboreshwaji wa huduma za jamii hasa katika Elimu kwa kufikia uandikishaji/usajili wa wanafunzi hasa wa elimu ya awali kwa kufikia uwiano wa 118.1 mwaka 2019 ; afya, majisafi na salama, pamoja na udhibiti wa machafuko ya kisiasa.

Dira ya maendeleo ya mwaka 2050 imelenga kufikia hadhi ya uchumi wa kati wa juu (Upper- middle income status), uchumi wa buluu ukiwepa kipaombele kama silaha muhimu ya kuchochea mafanikio hayo. Ukuaji wa uchumi wa nchi yoyote eidha uwe wa buluu ama wa kijani (Green or Blue economy) hutegemea kwenye mambo mengi.

Nchi ya Afrika ya kusini (South Africa), pamoja na visiwa vya Mauritius na Seychelles, ni nchi tatu za barani Afika za kupigiwa mfano katika mageuzi na maendeleo ya uchumi wa buluu ambayo ni ya kuigwa na nchi nyengine za barani Africa zilizo pembezoni mwa bahari kama Tanzania na Kenya, lakini pia bila kusahau visiwa vya Zanzibar, Madagascar, Comoros, na Cape Verde.

Maswali ya Kwanini Zanzibar ielekeze nguvu zake kwenye Uchumi wa buluu ? Ni kwa namna gani Zanzibar itayafikia malengo yaliyopo kwenye Dira yake ya maendeleo ya mwaka 2050 kwa kupitia uchumi wa buluu ? Ni maswali ya msingi sana yatakayo iwezesha serikali ya mapindunzi ya Zanzibar kuweka mikakati thabiti ya utekelezaji wa sera ya mageuzi ya kiuchumi.

Uchumi wa buluu ni aina ya uchumi ambao unalenga na kuelekeza nguvu katika matumizi endelevu yaliyo fanisi ya bahari pamoja na rasilimali zake. Aina hii ya uchumi hutegemea kwa kiasi kikubwa ufanisi wa sekta za utalii (tourism) kwani inaaminika kuwa zaidi ya 50% ya watalii duniani hutembelea nchi za fukwe ; Usafirishaji wa majini (maritime transportation) zaidi ya 80% ya biashara duniani husafirishwa kupitia maji ; Uzalishaji wa Gesi na mafuta (zaidi ya 30% ya uzalishaji wa mafuta na gesi duniani hufanyikia pamoja na sekta za Uvuvi na Kilimo cha baharini (Aquaculture). Uchumi kama mfumo, hutegemea ufanisi wa sekta za Elimu, Afya, Nishati, Tehama, Usafrishaji, Utalii, Viwanda na Uwekezaji, Huduma za kifedha, Maji, zote kwa ujumla wake ambazo nazo pia hutegemeana pamoja na ubora wa taasisi.

Jeografia ya Zanzibar haiipi Visiwa vya Zanzibar hiari ya kutegemea uchumi wa buluu wa kiushindani (Competitive Blue Economy) kama kipaombele na kichochezi (Engine) cha ukuaji na maendeleo ya kiuchumi pamoja na kijamii, bali ndio njia pekee ya kuikwamua Zanzibar kutoka kwenye kundi la Dola masikini duniani. Zanzibar yenye ukubwa wa eneo wa kilomita za mraba zisizopungua 2400, ambazo kutokana na ongezeko la idadi ya watu, eneo hili haliwezi kukidhi mahitaji ya makazi na wakati huohuo kuendesha shughuli za kiuchumi hasa kwa kukifanyakilimo cha mazao ya nafaka na biashara kuwa sekta yenye kuchangia kwa kiasi kikubwa kwenye pato la taifa kwa kutosheleza mahitaji ya ndani pamoja na kushiriki kikamilifu katika biashara ya kimataifa, hivyo basi kutokana na sababu za kijeografia, Zanzibar haiweza kufikia kiwango cha uchumi kilicho kwenye Dira yake ya maendeleo ya mwaka 2050 kwa kuifanya sekta ya kilimo kuwa tegemezi.

Lakini pia kutokanana udogo wa eneo wa visiwa vya Zanzibar, pia imechangiakuwa na ufinya wa rasilimali za nchi kavu (Inland resources). Ufinyu wa rasilimali za nchi kavu (Inland resources), sababu za kijeografia ambazo zinaifanya Zanzibar kuwa katika eneo la kimkakati (strategically located), lakini piakutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu kila siku zinavyozidi kwenda, Uchumi wa bluu ni aina pekee ya uchumi ambao utaifanya Zanzibar ndani ya miaka thelathini, hamsini, mia ijayo kuwa kama Singapore ya Afrika. Lakini itafikaje huko ? ndio swali la msingi ambao waandaaji wa sera za kimaendeleo (policy makers) pamoja na Viongozi wa serikali (admistrators) ambao ndio watekelezaji wa mipango yote wanayopaswa kujiuliza. Kujiuliza pekee haitoshi lakini ni kujiuliza kwa kujitathimini, kwa kuingalia Zanzibar ilipo na masafa ya hadhi ya uchumi inayoitamani kuifikia, je taasisi zinaubora utakaochochea na kuakisi ukuaji na maendeleo ya uchumi na jamii za wazanzibar inayotarajiwa? Ubora na wingi wa rasilimali watu inaweza hamasisha ukuaji na maendeleo ya kiwango cha ushindani ? vipi kuhusu teknolojiaya uzalishaji, mawasiliano na habari ? ni kwa namna gani itawavutia wawekezaji kutoka mataifa mengine kujakuwekeza kwenye miradi mikubwa ya kimkakati itakayo kuwa chachu ya mageuzi ya kiuchumi ya kuifanya zanzibar kuwa kama Singapore na nchi nyengine zilizopiga hatua.

Maswali haya wanapaswa wajiulize watu wakuaminika wenye maono, wazalendo na uchungu wanaotamani kuiona Zanzibar kuwa kama nchi nyengine zenye chumi kubwa duniani.

Kama ilivyo dhamira ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuifanya Zanzibar kupiga hatua yenye mashiko kiuchumi ambayo itaakisi maendeleo ya watu wake (significant economic movement), ni ndoto ya muda mrefu ambayo inatekelezeka lakini kwa kufanya uwekezaji wenye tija hasa kwenye miradi mikubwa ya kwenye sekta za usafirishaji kwa kupanua na kuifanya Bandari ya Malindi amabyo ndio bandari tegemezi inayoshughulikia zaidi ya 95% ya shughuli zote za forodha za Zanzibar, kutoa huduma hata mara mbili au tatu ya kiwango cha huduma inayotoa sasa, lakini pia kuja na mradi mkubwa wa kuendeleza bandani ya Pemba ; lakini pia uwekezaji wenye tija katika sekta ya Utalii ambayo huchangia karibia 30% kwenye pato la Zanzibar kila mwaka, Zanzibar bado ina mengi ya kufanya ili kuiwezesha kuwa kituo kikubwa cha utalii barani Afrika na duniani kwa ujumla, hasa katika maeneo ya ujenzi wa hoteli zenye hadhi ya nyota tano za kutosha, udhibiti na muendelezo wa vivutio hasa katika fukwe, lakini pia kitengo cha matangazo kupitia vyombo vikubwa vya habari vya dunia kama BBC, Aljazeera, CNN na CGTN, lakini pia pamoja na kumiliki vyombo vikubwa vya habari hasa matangazo ya Televisheni Redio na Magaazeti.

Ni dhahiri kwamba kuufikia uchumi wa kati wa kiwango cha juu (Upper- middle income status) au hata uchumi wa juu kabisa, Zanzibar itahitaji msaada wa nje wa kifedha, kiteknolojia, na wa rasilimali watu (human capital) itakayowezesha utekelezeji wa miradi mikubwa hasa katika sekta za usafirishaji, utalii, Uvuvi pamoja na Nishati (Mafuta na Gesi).

Suala la Taasisi ni changamoto kubwa sana linalo zikabili nchi nyingi zinazoendelea. Nchi nyingi zinazo endelea hasa za barani Afrika licha ya kutunukiwa na rasilimali nyingi za madini, ardhi yenye rutuba, wingi wa watu, kuwa pembzoni au kuzungukwa na bahari, lakini bado zinashindwa kujikwamua kimaendeleo ya kiuchumi na kijamii ikichangiwa kwa kiasiki kubwa na utendaji kazi wa taasisi zilizopo katika nchi husika ambazo zinashindwa kuchochea ukuaji na maendeleo ya kiuchumi.

Ndoto ya kuifanya Zanzibar kama singapore ya Afrika haitatokea kimiujiza, ni lazima watu wawajibike, kila mmoja kwa nafasi yake, lakini Zanzibar itafikaje huko kama mfumo wake wa Elimu hauna mitaala mabayo haimfanyi mwanafunzi kuwa mvumbuzi mwenye uwezo wa kufikiria kwa kina masuala yenye kuakisi maendeleo ya taifa katika nyanja zote za kiuchumi, jamii, siasa na tamaduni ? vipi Zanzibar itafika huko inapo dhamiria kama huduma za kifedha hazishawishi ukuaji wa sekta nyengine lakini pia hazivutii wawekezaji wa nje ? mikataba ya miradi mikubwa ya kimaendeleo itajadiliwa vipi kama mfumo wa Elimu haiwaandai watu wenye uwezo wa kutetea masilahi ya Zanzibar katika kujadili mikataba ? kunahaja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuweka nguvu kiuwekezaji kwenye sekta ya Elimu, kwani hii ndio chachu ya maendeleo ya sekta nyengine zote, haiwezekani na hainogi ajili ni serikali iwe na mpango mkubwa kama huu alafu itarajie kufanyiwa kil akitu na wageni.

Huduma bora za afya, maji safi na salama, huduma za nishati ya umeme, huduma za kisheria na mahakama, usafirishaji, uongozi na utawala bora, teknolojia za uzalishaji katika sekta mbalimbali, masuala ya tehama, ubora wa taasisi za kifedha na mengine mengi, yote kwa ujumla wake ni matunda ya uwekezaji wenye tija katika mfumo wa elimu utakao zalisha wataalamu mbalimbali ambao kila mmoja kwa nafasi yake ataweza kuwa sehemu muhimu ya mageuzi ya kiuchumi kupitia uchumi wa buluu.

Kwa kuhitimisha, kwa kuitazama Zanzibar na rasilimali zake ina nafasi kubwa sana ya kuwa na uchumi mkubwa dunia kama ilivyo singapore na Afrika ya kusini. Bara la Afrika lina jumla ya nchi 54 katika hizo ni nchi 38 zilizo pembezoni mwa bahari zinazoifanya bara la Afrika kuwa una ukubwa wa eneo la fukwe wa kilomita 30,500, lakini bado shughuli zote zinazohusiana na bahari hasa usafirishaji (marinitime transportation) zinazofanyika katika nchi hizi ni za kiwango cha chini (small scale activities). Hivyo basi mageuzi makubwa ya kiuchumi kwa zanzibar yanawezekana hasa ukizingatia hakuna nchi inayofanya vizuri sana katika uchumi wa buluu, lakini yote inategemea utekelezaji wa sera na miradi yote ya kimaendeleo.

Kufanya yote kwa pamoja si vibaya lakini inaweza kuichelewesha Zanzibar kufikia malengo, na tukisema uwekezaji wa nguvu na wenye tija uelekezwe kwenye sekta fulani haimaanishi kama na maeneo mengine ya kimaendeleo yapuuzwe, lakini inamaana ya kwamba iangalie eneo gani ambalo litakuwa chachu ya maendeleo ya sekta nyengine ndio ianze nalo na ni vyema kulipangilia upya(structural reforms)

Mbwana Kanju Salim (Quantitative Economist)
kanjuchode@gmail.com

0655510642
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom