Zanzibar kuzuia uvutaji sigara hadharani

mdau wetu

JF-Expert Member
Apr 20, 2011
548
58
SHERIA ya Afya ya Jamii ya mwaka 1936, itafanyiwa marekebisho makubwa na kuongezwa baadhi ya vipengele kikiwemo cha kupiga marufuku uvutaji wa sigara katika mikusanyiko ya watu.

Waziri wa Afya, Juma Duni Haji alisema hayo jana wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Chake Chake, Omar Ali Shehe (CUF).

Omar alitaka Serikali ieleze athari za sigara kwa jamii na mikakati iliyopo ya kupiga marufuku uvutaji wa sigara hadharani.

Duni alikiri kuwepo kwa madhara makubwa ya sigara kwa binaadamu kwa zaidi ya watu wanaovuta ambao huathirika mapafu na sehemu nyengine za mwili wa binadamu.

Alisema kazi kubwa inayofanywa na wizara kwa sasa ni kuipitia Sheria ya Afya ya Jamii ya Mwaka 1936 na kuifanyia marekebisho ambayo suala zima la uvutaji wa sigara hadharani litashughulikiwa.

“Wizara ya Afya ya Jamii inafahamu athari za sigara kwa wavutaji na tumekuwa tukitoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu madhara ya sigara,” alisema Duni.

Alisema Wizara ya Afya ya Jamii itashawishi Wizara ya Fedha ili iweke masharti makali ya kutoza kodi kwa bidhaa zote za sigara zinazoingia nchini ikiwemo kudhibiti matumizi ya sigara.

“Mheshimiwa Naibu Spika tutafanya ushawishi kwa Wizara ya Fedha ili ushuru sigara na bidhaa zake upande kwa lengo la kudhibiti matumizi ya sigara,” alisema. Hata hivyo, Duni alisema Serikali itaendelea kutoa elimu kuhusu madhara yanayotokana na uvutaji wa sigara na hatari zake kwa binadamu.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom