mwanamwana
JF-Expert Member
- Aug 1, 2011
- 1,076
- 4,113
----
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja linawashikilia watu saba kwa tuhuma za mauaji ya Said Salum Suleiman (32) mkazi wa Mwembemakumbi mjini Unguja.
Wanaoshikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya Suleiman ambaye alikuwa katibu wa ACT-Wazalendo tawi la Mwembemakumbu ni askari wanne wa vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na maofisa watatu wa idara ya misitu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 12, 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Awadh Juma Haji amesema tukio hilo limetokea jana saa 8 mchana ikidaiwa kuwa alipigwa risasi na maofisa hao eneo la Mwembemakumbi.
Amesema askari hao wakiwa wameambatana na maofisa wa idara ya misitu walikuwa katika doria maalumu kuwabaini wanaojihusisha na uhalifu wa mazao ya misitu na uharibifu wa mazingira.
Amesema wakiwa wanatokea katikati ya mji wakiwa na gari lenye namba za usajili SMZ 451B aina ya Mitsubishi walimkuta Suleiman akiwa na mkokoteni uliopakiwa mchanga.
Amesema mkokoteni huo ulikuwa ukivutwa na punda na alikuwa akitokea eneo la bondeni kuingia barabarani lakini alipowaona alikimbia na kuacha mkokoteni huo.
Amebainisha kuwa askari hao walichukua mkokoteni huo kwa lengo la kuupeleka katika ofisi zao zilizopo Maruhubi lakini muda mfupi baadaye walivamiwa na kundi la vijana wakiwa na mapanga na silaha mbalimbali, akidai kuwa walitaka kuwazuia polisi na maofisa hao kutoondoka na gari walilokuwa wamepanda.
Amesema katika kile alichokiita mapambano watu hao walivunja kioo cha nyuma cha gari na kusababisha askari kufyatua risasi iliyompata Suleiman.
“Baada ya kutokea kwa tukio hilo maofisa hao waliondoka mara moja katika eneo hilo na kuwaachia wananchi wakitoa msaada kwa Suleiman ikiwa ni pamoja na kumpakia kwenye gari kwa lengo la kumpeleka hospitali,” amesema.
Chanzo: Mwananchi