Lwakatare: Sikuhamia Chadema kutafuta cheo
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananci (CUF), Wilfred Lwakatare, amesema hakuhamia Chadema kusaka cheo, bali amegundua kuwa chama hicho kunawapambanaji wa kweli dhidi ya ufisadi.
Aliyasema hayo jana kwenye viwanja vya Tangamano wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Operesheni Sangara inayoendeshwa na Chadema.
Lwakatare alisema Chadema kuna watu makini ambao wana uchungu wa kweli na rasilimali za nchi. Nilimwambia hata Mbowe, mimi sikuja kufuata cheo maana kama kusoma nina elimu ya kutosha kufanya kazi popote, isipokuwa nataka kuendeleza mapambano dhidi ya wezi wa mali za umma. Septemba 2007 pale Mwembeyanga mlitangaza majina ya mafisadi waziwazi bila woga pale ndipo nilipobaini kuwa huku kuna wanaume wa shoka, alisema Lwakatare.
Alisema baadhi ya vyama vya upinzani vinafanya siasa za kujitafutia umaarufu binafsi, badala ya kutafutia wananchi ukombozi.
Alisema baadhi ya vyama hivyo vinaendeshwa kama asasi zisizo za serikali. Lwakatare alisema kazi ya kuiondoa CCM madarakani sio lelemama kama watu wanavyoweza kudhani, ni ngumu inayohitaji kukomaa.
Naye Joseph Selasini, ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi NCCR Mageuzi, alisema kuna vyama vya siasa ambavyo vimekuwa vikiibuka wakati wa uchaguzi.
Selasini alisema vyama hivyo viliandikishwa tangu kuingia mfumo wa vyama vingi, lakini vina hali mbaya kutokana na kuendeshwa kihuni.
Wakazi wa Tanga tuungane tutengeneze ngumi ya nguvu tuitandike CCM, mageuzi ni muhimu maana tuna tatizo la uongozi, nchi inaongozwa kisanii na CCM imefulia kisera, alisema.
Aliongeza kuwa badala ya kuwaletea wanachi maisha bora, CCM imekuwa wakati wa uchaguzi ikiwaletea wananchi fulana tena za bei rahisi ambazo huchanika muda mfupi.