Wizi nyumba za ibada tishio

Oldmantz

JF-Expert Member
Jan 24, 2023
428
996
Matukio ya uhalifu katika nyumba za ibada yamewaibua viongozi wa dini na wanasaikolojia, huku lawama zikielekezwa kwa viongozi hao.

Kwa mujibu wa wanasaikolojia, mahubiri yao yamejikita katika masuala ya ndoa, kazi na utajiri badala ya tabia njema.

Licha ya utitiri wa nyumba za ibada zilizoota kama uyoga nchini, matukio ya uhalifu bado yanashuhudiwa, ikiwa ni ishara ya kutoweka kwa hofu ya Mungu.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo alisema kwa sasa watu wanapenda kujifurahisha wenyewe bila toba na kinachoonekana katika baadhi ya nyumba za ibada sio imani, bali ni uigizaji.

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Taasisi ya Mental Hygiene Institute ya Dar es Salaam, Ramadhan Masenga alisema mahubiri mengi yanajikita katika fedha, ndoa na kazi, lakini yale ya uaminifu na upendo, yamepewa kisogo.

Kauli za viongozi wa dini na wanasaikolojia zinatokana na matukio ya wiki iliyopita ya watu wasiojulikana kuingia katika Parokia ya Narumu ya Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi na kuiba kapu lililokuwa na sadaka.

Mbali na tukio hilo, mtu mmoja anadaiwa kuzidiwa na ulevi kisha kuingia katika Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Geita, kuvunja vioo vya mlango na kuharibu eneo la kuhifadhia sakramenti.

Kwa mujibu wa Askofu wa kanisa hilo Jimbo la Geita, Flavian Kasala, kijana huyo alimwaga ekarist takatifu na kuvunja vifaa vyote vya altare na kabla ya kutelekeza adhma yake hiyo alivunja kamera za ulinzi na usalama (CCTV).

Hata hivyo, Askofu Kasala ametangaza kulifunga kanisa hilo kwa siku 20 kuanzia Februari 27 mwaka huu akisema kilichofanyika ni unajisi wa kanisa.

Alisema waumini wataingia katika adhimisho la toba ya malipizi kuanzia Februari 27 hadi Machi 18.

Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za pole kwa Askofu Kasala, huku Serikali ikitangaza kuchangia ukarabati wa kanisa hilo.

Jeshi la Polisi mkoani Geita, lilitangaza kuendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa kijana huyo alikuwa amelewa wakati anavamia na kufanya uharibifu kanisani hapo kutokana uchunguzi wa kitabibu kubaini kiwango kikubwa cha kilevi mwilini mwake.

Matukio mengine

Miezi miwili iliyopita, huko mkoani Njombe polisi walikamata vitu mbalimbali vilivyokuwa vimeibwa baada ya wezi kuvunja katika nyumba mbalimbali za ibada,

Miongoni mwa vilivyoibwa kanisani mjini Njombe ni Biblia.

Mwaka mmoja uliopita, vijana 12 wanaotuhumiwa kuwa ni wezi waliwajeruhi watawa watatu wa Kanisa Katoliki mkoani Pwani na kuiba ekaristi takatifu na kikombe kiitwacho sivorium, katika matukio yanayoibua maswali.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Don Bosco, Padri Benno Kikudo alikaririwa akisema tukio hilo lililotokea Vikuge, Kata ya Kongowe wilayani Kibaha kwenye nyumba ya watawa, vijana hao walikuwa wakiongozwa na mwanamke.

Machi 9, 2021, watu wasiojulikana waliingia Kanisa la Parokia ya Mt. Augustino Wanging’ombe Jimbo Katoliki la Njombe kwa kupitia dirishani (kwa kulivunja) na kuiba vitu mbalimbali vinavyotumika kwa ajili ya maadhimisho ya misa takatifu.

Mbali na tukio hilo, Aprili 5, 2018, watu wanaodaiwa kuwa majambazi walivamia Kanisa Katoliki Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu-Mbezi Mwisho jijini Dar es Salaam na kupora fedha na baadhi ya vifaa vya kuendeshea misa kanisani hapo.

Juni 14, 2015 kundi la wezi lilivamia Kigango cha Bomambuzi cha Kanisa Katoliki Jimbo la Moshi na kuiba Sh350,000 za sadaka na vifaa mbalimbali vya muziki na tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi wakati huo, Fulgence Ngonyani.

Hali ilivyo msikitini

Kadhia kama hiyo imekuwa ikijitokeza misikitini, Aprili 4, 2018, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro lilitangaza kumshikilia mkazi mmoja mkoani humo kwa tuhuma za kuiba mikeka, mbao na baiskeli ambavyo vyote vilikuwa mali ya Msikiti wa Masjid Nuru Kichangani, Manispaa ya Morogoro.

Januari 4, mwaka jana, watu wanne walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakikabiliwa na shtaka la wizi wa Sh480. 5 milioni ambazo ni mali ya msikiti wa Shree Sanatan Dharma.

Washtakiwa hao ni Kshary Motichand (22), mkazi wa Kisutu, Vasant Solanki (73) mkazi wa Jamatin, Ramesh Shash (62) mkazi wa Zanaki na Shailesh Chauda (48) mkazi wa Ilala.

Mahakama ilielezwa, kati ya Januari na Novemba 2016 maeneo ya Jiji la Dar es Salaam wote kwa pamoja walikula njama kwa nia ya kutenda kosa na kuiba kiasi hicho cha fedha mali ya msikiti huo, huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Matukio mengine ya wizi msikitini ni ya kandambili, viatu, bodaboda, simu, ama vitu vya thamani vya waumini wanapokuwa wamekwenda kuswali kuibiwa.

Juni 2018, watu wasiofahamika, walivunja mlango mdogo wa mimbari katika Msikiti Mkuu wa Igunga, Mkoa wa Tabora na kuiba Sh720,000 za sadaka.

Aprili 18, 2022, kamera za ulinzi ‘CCTV’ zilimnasa kijana mmoja akimwibia simu mmoja wa waumini aliyekuwa akiswali katika Masjid Mindhir (msikiti wa Baghani, visiwani Zanzibar) kisha akaondoka pasina kukamatwa.

Baadhi ya misikiti imekuwa ikilazimika kuwataka wanaofika kuswali kuweka vitu vyao mbele ama kuwa navyo makini, huku mmoja wa wakazi wa Tabata, Dar es Salaam, Abadllah Juma akisema, “mimi nimeibiwa sana viatu, ukiingia ukitoka huvikuti, imekuwa kawaida.”

Naye Said Juma, alisimulia mkasa uliompata katika msikiti uliopo Tabata Relini, Dar es Salaam akisema, “mimi siku moja nilikwenda kuswali, nilipofika nikaenda kutia udhu, nikaweka begi ndani, nikaenda moja kwa moja kwenye safu, kwa kuwa swala ilikuwa imekwisha anza.

“Kuja kumaliza, sikuliona begi, kulikuwa na vitabu, vitambulisho vya kazi na modem mbili,” alisema Juma na kuongeza, “hii ni dalili ya kukosa hofu ya Mungu, kwa kuwa huwezi kwenda kuiba katika nyumba za ibada.”

Alichokisema Askofu Shoo, TEC

Akizungumza na gazeti hili jana, Askofu Shoo alikiri sasa hofu ya Mungu imetoweka kwa watu wengi na kwamba imani ya kweli huendana pamoja na kumcha Mungu na ni pamoja na kuukataa uovu wa kila namna.

“Watu wa sasa wanapenda kuabudu kwa mazoea, au kwa kujifurahisha tu wenyewe bila toba na kurarua mioyo kuliruhusu neno la Mungu liwabadilishe tabia na mienendo yao sio kwa kulisikia tu, bali kulitii neno hilo,” alisema.

“Tunachokiona leo (siku hizi) katika makusanyiko mengi ya kinachoitwa ibada ni uigizaji tu. Imani ya kweli, mafundisho ya kweli sio kuhusu utajirisho, mafanikio, bali kuacha na kuchukia dhambi na uovu.

“Sasa walio wengi hawataki kuhubiriwa kuhusu kuacha dhambi, na wahubiri wasio waaminifu wanatafuta tu kuwafurahisha watu kwa manufaa yao kuliko kukemea dhambi na uovu. Viongozi wa dini watimize wajibu wao,” alisema Askofu Shoo.

Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu wa Katoliki Tanzania (TEC), Dk Charles Kitima alisema matukio hayo ni ya kusikitisha na kudhalilisha dini, akiitaka Serikali kwa kutumia vyombo vyake vya dola kuhakikisha matukio hayo yanakomeshwa.

Dk Kitima, ambaye kitaalamu ni mtafiti, alisema matukio hayo yanaonyesha kwenye jamii maadili yameshuka na watu hawaheshimu imani za watu wengine, akitaka jamii ijenge tabia ya kuheshimiana kwani matendo yanaidhalilisha nchi.

“Ibara ya 19 ya Katiba ya Tanzania imeeleza kila mtu ana uhuru kwenye dini anayoitaka na kuwa na mawazo ya kidini ya kile anachokiamini na atakuwa na jukumu la kueneza dini yake kwa namna anavyoona inafaa.

“Tunachokiona waliofanya matukio haya wamekiuka Katiba ya Tanzania juu ya uhuru wa watu kuabudu, kwani matukio haya tumeyaona ni ya kusikitisha na kudhalilisha dini. Serikali na vyombo vyake ikomeshe mambo haya,” alisema Dk Kitima.

Alichokisema mwanasaikolojia

Matukio hayo mawili yanatafsiriwa na Mtaalamu wa Saikolojia, Ramadhani Masenga akisema, matukio hayo yanatokea sasa kutokana na viongozi wa dini kuacha majukumu ya msingi ya kuzungumzia mambo ya kiroho na kujikita kwenye utajiri pekee.

“Baadhi ya wahubiri hawazungumzii tena maadili wala makuzi ya vijana na watoto. Yale makuzi na heshima ambayo watu walikuwa nayo kwenye nyumba za ibada yamepotea,” alisema mwanasaikolojia huyo katika mahojiano na gazeti hili.

“Mahubiri ambayo sasa tunayasikia kwenye nyumba za ibada ni rahisi kuyasikia yakizungumzwa na wahamasishaji kwenye nyumba za starehe au kwengineko. Kuna mahali baadhi ya viongozi wetu wameteleza kiimani.”

Masenga alisema, kuna namna ambavyo viongozi wa kiroho wameyaunganisha majukwaaa yao na watu duniani, jambo ambalo limechangia matukio yaliyozoeleka nje ya nyumba za ibada sasa kutokea kwenye nyumba hizo.

Kwa mujibu wa Masenga, kwenye nyumba za ibada, maneno ya baraka yamekuwa yakizungumzwa kwenye eneo la fedha, ndoa na kazi pekee, huku matukio ya uhai, kauli nzuri, upendo na uaminifu yakipewa kisogo.

“Kwa hiyo matukio haya kwenye nyumba za ibada ni kushindwa kwa viongozi wetu wa dini ambao wengine wanaenda kulingana na mitandao ya kijamii inavyotaka, wanasahau suala la maadili na imani kwa ujumla wake,” alieleza Masenga.

Pia, alisema ili kuondoa matukio haya yanayoivua nguo jamii, inapaswa viongozi wa dini kutambua kuwa wana nafasi kubwa ya kutengeneza leo na kesho ya watu kwenye jamii na kuwataka viongozi wa dini kuwalisha waumini neno la Mungu.

Sheikh, mchungaji

Kwa upande wake Mchungaji Mkuu wa Jimbo la Kati Dayosisi ya Mashariki na Pwani ya KKKT, Frank Kimambo akizungumzia matukio hayo alisema yanaonyesha watu kukosa hofu ya Mungu katika nyumba za ibada, jambo ambalo ni la hatari.

“Tunashuhudia majambazi wanavunja na kuiba kwenye nyumba za ibada, lakini majambazi hao wakikamatwa utashangaa ni kutoka jimbo hilo hilo na si kwenye madhehebu mengine. Hii inatokana na watu kukosa hofu ya Mungu,” alisema.

Mchungaji Kimambo wa Tabata Shule na Buguruni, alifafanua kuwa hofu ya Mungu haianzii ukubwani, bali kuanzia kwenye makuzi ya watoto, ndiyo maana wanasisitiza elimu ya dini kwa watoto.

“Hofu ya Mungu inapaswa kuanza kujengwa kwa watu kuanzia utotoni, kwa kuwa matukio ya udokozi unaofanywa na watoto matunda yake ni kuja kupokonya kapu la sadaka kanisani au kulichoma kanisa.

“Viongozi wa dini tunapaswa kuhakikisha watoto wanakuwa na maadili tangu wakiwa wadogo ili jamii ikue ikiwa na hofu ya Mungu, kwa matukio yanayotokea kwenye nyumba za ibada inaonyesha hali ni mbaya kwa baadhi ya vizazi.

“Sasa viongozi wa dini, wazazi na walimu mashuleni tushirikiane kuhakikisha watoto hawa wanakaa katika misingi ya kumpenda Mungu,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Kiislamu (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka alisema matukio yaliyojitokeza siku za karibuni, yanaonyesha jamii kuzama kwenye mmomonyoko mkubwa wa maadili.

“Watu wakipungukiwa hofu ya Mungu wanaweza kufanya jambo lolote kukidhi matamanio yao. Kwa hiyo mtu anaweza akaua au kudhuru kwa ajili ya fedha. Leo sehemu za ibada zinazoheshimika watu wanakwenda kutenda uhalifu,” alisema.

Sheikh Mataka alipendekeza njia inayopaswa kuchukuliwa ni kwa viongozi wa dini kuwarudisha watu na kuhuisha imani zao ili wawe na hofu ya Mungu.

“Tusiwasubiri katika nyumba za ibada, viongozi wa dini watengeneze mfumo mbadala wa kuwafuata watu kama wanapatikana kwenye facebook, twitter, michezo basi viongozi wawafuate huko huko,” alisisitiza Sheikh Mataka.

“Jamii yetu imeharibikiwa kwa kiwango kikubwa. Ni lazima tubadilike kuchukua hatua madhubuti za kulinda nyumba za ibada. Tusidhani wote wanaokuja ibada wanakuja kumuomba Mungu, hapana wapo pia wahalifu.”

Kwa upande wake, muumini Greyson Mgonja alisema watu waliofanya wizi kwenye nyumba za ibada wanafahamika kwenye jamii na matukio hayo yamechangiwa na watu kuona maeneo ya ibada kama sehemu za kawaida.

Chanzo: Mwananchi
 
Yetu macho,mapadri na masheikh wanalawiti na kubaka huku wahuni wakivunja makanisa na kuiba
 
Back
Top Bottom