Winda maisha yako

Robert Heriel Mtibeli

JF-Expert Member
Mar 24, 2018
21,341
51,907
WINDA MAISHA YAKO; MBINU KABAMBE.

Na, Robert Heriel
Maandishi ya Robert Heriel, Kwa Lugha ya Kiswahili.
Haki zote zimehifadhiwa.

Moja ya mambo niliyokuwa nikiyafanya kwa ufanisi mkubwa enzi nikiwa mdogo, na hapa ni chini ya miaka 13 ni pamoja na uwindaji wa ndege. Nilikuwa moja ya watoto wenye shabaha sana, hakuna ndege ambaye hakuonja joto langu, njiwa weupe, njiwa wa kijani, njiwa wa kufuga, wote nilishawashusha. Chokori bati, chokori bwenzi, mbanja, pugi, kwelea kwelea, na kitorinto( majina hayo ni kwa mujibu wa maeneo niliyokulia huko upareni).

Rafiki zangu wa utoto akiwepo Rashidi Bakari alimaarufu kama Rashidi Bichwa, pia alikuwepo Rafiki yangu aitwaye Omary Mweta ambaye sasa hivi ni Wakili msomi. Hawa ndio walikuwa mbele kwa uwindaji wa ndege kwa wakati huo na kwa umri wetu.

Uwindaji unahitaji akili, shabaha, utulivu, timing, na mbinu kabambe ili kuweza kulipata windo. Wawindaji wote wataungana na mimi kuwa uwindaji hauhitaji pupa, hauhitaji mihemuko, uwindaji ni sanaa kama zilivyo sanaa zingine, tena ni sayansi kama sayansi nyingine. Uwindaji unahitaji mahesabu yenye makadirio ya uhakika.

Leo tutatumia dhana ya uwindaji kama somo litakalo tusaidia kwenye mada yetu isemayo; WINDA MAISHA YAKO; MBINU KABAMBE.

Kwenye maisha kuna makundi mawili, ambayo ni;
1. Muwindaji
2. Muwindwaji/ windo.

1. MUWINDAJI.
Kundi hili ni lile linalohangaika kutafuta windo, Kundi hili hutumia silaha kuhakikisha linajipatia windo lake naam kitoweo. Kuna silaha za aina mbili;
1.1. Silaha huru
1.2. Silaha tegemezi

1.1 SILAHA HURU
Silaha huru ni silaha mpachiko, silaha mshikamano ambazo muwindaji huwa nazo wakati wote. Nimeziita silaha huru kwa sababu zinajitemegea na zipo ndani ya muwindaji. Silaha huru ni kama vile meno, kucha, mapembe, ngumi, kichwa, mate(yenye sumu) miongoni mwa silaha zingine zilizomo kwenye mwili wa mwindaji.

1.2. SILAHA TEGEMEZI
Hizi ni silaha tengano kwani zimetengana na mwili wa muwindaji. Nimeziita silaha tegemezi kwani zinatemea silaha huru ili zifanye kazi. Silaha tegemezi ni matokeo ya akili, ubunifu, na utashi wa muwindaji. Silaha Tegemezi ni kama vile mawe, mti, mshale, bunduki, miongoni mwa silaha zingine za kubuni au zilizopo kwenye mazingira.

Matumizi ya silaha huzingatia zaidi aina ya windo. Wawindaji hutumia silaha kwa sababu mbalimbali lakini kubwa zaidi ni kurahisisha shughuli ya uwindaji.

Kwa habari za silaha tuishie hapa, mbeleni nitaendelea.

2. MUWINDWAJI/ WINDO
Hili ni kundi la pili ambapo hugeuka kitoweo pale litakapotiwa mikononi mwa muwindaji.
Kundi hili huishi kimachale machale. Huwa na wasiwasi mara zote kwani linajua linawindwa.

Jambo moja nitalizingatia; Kwenye maisha yeyote anaweza kuwa muwindaji au muwindwaji. Ni suala la maamuzi. ukiamua kuwa muwindaji ni maamuzi yako, halikadhalika na ukitaka kuwa windo au kitoweo ni wewe mwenyewe. Hii ni tofauti na mbugani katika mazingira ya wanyama pori ambapo kila kitu kinabaki costant, yaani Simba atabaki kuwinda swala, na kamwe swala hatokuja kumuwinda simba. Japo simba anawezwa kuwindwa na wanyama wenzake wala nyama kama chatu au mamba.

TUENDELEE...

Kila mtu anataka kufanikiwa katika maisha. Maisha usipoyawinda basi yatakuwinda. Usipowinda basi jua unawindwa. Usipotafuta mafanikio basi jua wewe ndio mafanikio ya wengine.

Kama unataka kufanikiwa kuyawinda maisha yako, na unajiuliza utayapataje au utafanikiwaje. Nakupa ushauri, wiki hii chukua manati na mawe kadhaa, kisha ingia porini ukawinde ndege, kisha winda kwa masaa sita kwa siku sita. Kisha siku ya saba njoo uniambie umegundua nini katika uwindaji?

Kama umefuata nilichokuambia basi utanipigia simu au kunitumia ujumbe kwenye email yangu, au whatsapp au messenger.

Lakini kama utaona uvivu, usikonde. Nitaeleza kwa ufupi.

Jinsi unavyowinda ndege ndio mfano halisi wa kuwinda maisha yako. Ndio mfano wa kuyatafuta mafanikio.

Katika mchakato wa uwindaji kuna mambo yafuatayo;
1. Muwindaji
2. Windo
3. Silaha
4. Mazingira
5. Vishtushaji

Muwindaji ni wewe
Windo ni kile unachokitafuta maishani, tunaita dili
Silaha; Silaha huru ulizonazo ni akili, utashi, mikono, miguu,. Silaha tegemezi ni elimu, pesa, dhana za kilimo, teknolojia miongoni mwa silaha zingine.
Mazingira ni mahali ulipo
Vishtushaji, ni adui, wambea, wazandiki, wafitinishaji, wachawi, wasaliti miongoni wa wengine.

Aina za Wawindaji
1. Mwindaji tuli
2. Mwindaji dhahiri

1. MWINDAJI TULI
Mwindaji Tuli ni mwindaji anayewinda akitumia mbinu ya kuvizia, kunyemelea kisha kuvamia. Wawindaji wa aina hii huwa hawana nguvu ila wanaakili sana, pia hawana pumzi yaani hawawezi kukifuata kitu kwa umbali mrefu. Huchoka haraka. Ndio maana huvizia mpaka hatua ya mwisho ndipo huvamia kwa mshtuko mkubwa hapo windo linaweweseka na kujikuta limeishiwa ujanja. Mbinu hii hutumiwa na chui, chita. Sababu nyingine ya uwindaji wa aina hii ni athari za kijiografia alizonazo muwindaji. Mfano Mnyama Mamba huvizia sana kutokana na kuwa endapo windo likishtuka linaweza kukimbilia nchi kavu, na hivyo mamba kushindwa kumkamata kwani hawezi kuwinda nchi kavu.

2. MWINDAJI DHAHIRI
Hawa ni wawindaji ambao pia hutumia mbinu ya kuvizia lakini hawaitegemei sana kwa sababu wanapumzi, wanauwezo wa kukimbia umbali mrefu bila ya kuchoka. Mara nyingi mwindaji shahiri hupendelea teamwork yaani ushirikiano na wenzake. Mfano ni kama mnyama simba. Huyu hutumia uwindaji dhahiri. Wawindaji wengine ni kama tai wa miambani awindapo paa.

Watu wengi hupenda kuwinda kwa wepesi, kupata mafanikio kwa haraka. Yaani hupenda mbinu ya uwindaji tuli. Lakini kinachowashinda ni kuwa uwindaji wa aina hiyo unahitaji akili, mbinu, na shabaha takatifu kwani unalishika windo bado likiwa na nguvu. Inashauriwa unapowinda kwa uwindaji tuli sharti unadake sehemu nyeti ya windo yaani kushika koo kwa nguvu ili windo lisifurukute kwa muda mrefu.

Hii ni tofauti na uwindaji dhahiri ambao unalikimbiza windo kwa muda mrefu kiasi kwamba ukilikamata litakuwa hoi taaban likiwa limechoka. Huna haja ya kulishika sehemu nyeti, na ukilishika kamwe halitafurukuta.

Ili kuwinda maisha yako lazima uchague aina ya uwindaji na ujue mbinu za aina uliyoichagua. Lakini haukatazwi kuchanganya mbinu kutoka pande mbili.

Bahati njema ni kuwa, mambo mengi kwenye maisha yanahitaji utumie uwindaji dhahiri. Yaani uwe na pumzi kulifuatilia jambo unaloliwinda kwa muda mrefu hata siku ukilikamata haliwezi kufurukuta. Litakuwa limechoka, nawe utakuwa unalijua vizuri.

Ukianza biashara, itakuhitaji muda ili biashara hiyo ufanikiwe. Lakini kama utataka ufanikiwe kwa usiku mmoja unaweza shindwa kumudu gharama zake kwani sharti ushike sehemu nyeti pale biashara inapofurukuta, itahitaji mtaji wa kutosha, location nzuri yenye wateja ambapo kimsingi ni gharama.

MBINU KABAMBE ZA KUWINDA MAISHA YAKO.;

1. Chagua windo lako kabla hujaenda porini kuwinda
Unapoenda kuwinda, hakikisha unajua unaenda kuwinda nini, sio unaenda porini bila kujua unachowenda kukiwinda, yaani chochote kitakacho jitokeza ndio hicho hicho, hilo ni kosa. Hakikisha unajua kile unachoenda kukiwinda. Hii itakusaidia kujiandaa, kuandaa silaha gani itakayotumika, mbinu na mahali windo lilipo.

2. Chagua aina ya uwindaji, kama ni uwindaji tuli, au uwindaji dhahiri. Ukishajua windo, sasa unatakiwa uchagua utakuwa mwindaji tuli au mwindaji dhahiri. Hii itakufanya utumie mbinu kulingana na aina uliyochagua ya uwindaji na aina ya windo.

3. Andaa silaha maalumu
Silaha ndio hatua ya tatu, andaa silaha zako vizuri. Kumbuka kuna silaha huru na silaha tegemezi. Hakikisha akili yako, mikono na miguu, macho unaviandaa vizuri kwani hizo ndio silaha za kwanza kabla ya silaha tegemezi ambazo ni elimu, maarifa na ujuzi, bunduki, pesa, na silaha zingine. Silaha ziendane na aina ya windo.

4. MUDA na MAJIRA
Kwenye uwindaji muda na majira ni muhimu sana. Lazima upange muda na majira ya kuwinda windo lako, na hii inategemea na aina ya windo. Kuna mawindo yanapaswa kuwindwa usiku, yapo yapaswayo kuwindwa alfajiri na mapema, mengine mchana kweupe. Mawindo mengine ni rahisi kuwindwa wakati wa baridi, mvua na manyunyu, wakati wa kiangazi na kipupwe.
Muda na majira itakusaidia kupata mawindo kwa urahisi.

5. ELEWA RAMANI NA JIOGRAFIA YA WINDO LAKO
Lazima uelewe mazingira, jiografia ya mahali lilipowindo lako, je kuna miti au vichaka, kuna bonde au tambarare, kuna mito au maziwa. Kuwinda haimaanishi kuwa na shabaha pekeake bali pamoja na kuelewa ramani na jiografia ya eneo husika. Unaweza kumpiga ndege lakini asianguke akabakia juu kwenye mti wa miiba, au akakimbilia kwenye vichaka vizito, hivyo ni lazima ujue mazingira litakapodondokea windo lako.

Hii pia inatumika katika maisha halisi, huwezi winda maisha yako kwa kuwekeza sehemu usiyoijua ramani na jiografia yake. Utapoteza mtaji wako bure.

6. Dhibiti washtushaji
Kwenye mawindo kunawashtushaji, wakati unanyata au kunyemelea windo majani au vichaka vinaweza kutoa sauti na kufanya windo kusikia na kukimbia, pia wapo viumbe wengine wakikuona watapiga kelele na kulishtua windo lako. Namna bora ya kudhibiti washtushaji ni kunyata kwa umakini mkubwa ukiwa umebana pumzi, macho yako hakikisha yamelitazama windo lako muda wote.

Usiangalie pembeni pale unapowinda, angalia windo lako pumzi ukiwa umezibana na kuziachia taratibu.

7. Tuliza macho na mapigo ya moyo,
Ushafika eneo unaloona sasa unaweza kupiga windo lako na kulinasa. Tuliza macho yalinganane, au kama utashindwa basi punguza kipenyo cha jicho moja, kisha bana mapigo ya moyo kwa kushika pumzi kwa muda. Hapo ulishajua windo lako litadondokea wapi, na mazingira ni salama.

Hatua hii hutufundisha jambo moja kwenye kuwinda maisha, unapofikia windo fulani, elekeza macho yako kwenye windo hilo hilo, usiwe na tamaa kuangalia mawindo mengine, usitake kupiga mawindo mengi kwa wakati mmoja. Watu wengi huwa na tamaa ya mafanikio kwa wakati mmoja,. Hawana focus, hawana msimamo na jambo moja. leo utakuta anawinda dili la kilimo hajamaliza vizuri utashangaa anaanzisha biashara ya nguo, hajakaa sawa anaendelea na biashara ya ufugaji wa kuku.

Kanuni ya uwindaji ipo hivi, unawinda windo moja, sio mawindo mengi. Ukishapata windo moja ndio unatafuta windo la pili.

Ni kawaida kwa muwindaji akifika kwenye target akaona windo jingine lililo karibu yake kuliko lile alilo likusudia, kama ni muwindaji mahiri, hatahadaiwa na windo jipya liliokaribu yake, yeye ataendelea na lile lile alilokusudia. Hili ambalo lipo karibu yake ambalo hakuliona awali hawezi kulipata kwani wakati anavizia windo la kwanza hili jipya lilikuwa likimtazama, hivyo lilishamuona muda mrefu.

Hivyo akisema alipige litakimbia na kuwakimbiza wale wengine.
Kwa wawindaji wanajua jambo hili, hata wawindaji wa ndege.

Pia hata kwa wanyama kama simba, huwinda kwa kanuni hii. Yule aliyemchagua ndiye huyo huyo atadili naye mpaka amkamate, hata kama windo jingine lipite mbele yake hata lishika, hata kama windo lake liko mbali kabisa yeye atalifuata hilo hilo. Hiyo inaitwa Focus.

8. Hakikisha hauathiri mazingira uliyoyakuta, Kuwinda ni Siri.
Unapowinda hakikisha mazingira yaliyopo yasijue kama kuna kinachoendelea. Mazingira yajue kuna usalama, mazingira yakijua kuna usalama hata windo nalo litajua kunausalama. Kuyafanya mazingira yahisi tofauti ni kulishtua windo.

Kwa mfano ikiwa msitu upo kimya hakikisha unapoingia kuwinda eneo liendelee kuwa kimya vile vile. Au Ikiwa msitu ulikuwa una kelele za sauti za ndege hakikisha kelele zinaendelea vile vile. Kwani kitendo cha ndege kunyamaza kwa ghafla kutafanya windo lishtuke kulikoni kuna nini.

Unapofukuzia dili fulani kwenye maisha, usiwaambie watu, usiseme kwa majira au ndugu au mtu yeyote yule. Fanya mambo yako kimya kimya. Tambua upo kwenye mawindo. Unaposema sema unaleta disturbance kwenye uwindaji. Ni rahisi sana kukosa dili hilo.

Moja ya kanuni za kuwinda ni ukimya, lakini kama itahitaji ambush basi kelele ni muhimu ili kulipagawisha windo.

Kwa leo niishie hapa, ikiwa kuna sehemu sijaeleweka waweza kuandika hapo chini kwenye maoni, na ikiwa utaona kuna mapungufu pia waweza toa mawazo yako.

Ulikuwa nami;

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
robertheriel99@gmail.com
 
Back
Top Bottom