Wimbo wa Gaidi

Jamani mbona hatuambiani kumbe kuna mambo mazuri huku...? Hii nayo inahusu ujasusi?
 
RIWAYA: Wimbo Wa Gaidi
MTUNZI: Hussein Tuwa
SEHEMU YA SABA
“Lazima tutoweke hapa…sasa hivi!” Benson alisema huku akiinuka. Akaganda kwenye hatua zake pale wote mle ndani waliposikia mlango wa kile chumba walichokuwamo ukabishwa hodi kutokea nje.
Wakatazamana, wakiwa kimya, macho yakiwatembea.
Hodi ikabishwa kwa mara ya pili, kwa nguvu zaidi.
“Wamefika.” Brey Jabba alisema kwa utulivu wa kuogopesha.
“Oh, Shit!” Benson Kanga alilaani huku akijibingirisha sakafuni, akaikwapua ile bastola yake iliyokuwa imetupwa pale sakafuni baada ya kupigwa teke kutoka mkononi mwake na Brey, na kujipanza ukutani huku akiwa ameielekezea ile bastola yake kule mlangoni kwa mikono yake yote miwili.
Muda huo huo Brey akamrushia yule dada mwenye umbo dogo ile bastola aliyompokonya hapo awali. Dada akaidaka kizoefu mikononi mwake, na hapo hapo akajitupa nyuma ya kitanda, akabaki akiwa ameinyooshea ile bastola kule kule mlangoni kwa mikono yake yote miwili kutokea chini ya tendegu la kitanda kile, mwenyewe akiwa katikati ya tendegu lile na ukuta wa chumba kile.
Mlango ukabishwa tena kwa nguvu zaidi pasina mtu aliyekuwa kule nje kusema lolote kutambulisha uwepo wake au nia ya kubisha kwake mlangoni pale.
Brey Jabba aliwaashiria wale washirika wawili aliokurupushana nao mle ndani dakika kadhaa tu zilizopita kuwa watulie, huku kwa mkupuo mmoja akiunyofoa waya wa pasi iliyokuwa mle chumbani kutoka kwenye kichwa cha pasi ile, akiiacha ile sehemu inayochomekwa kwenye soketi ukutani ikiwa kama itakiwavyo. Haraka mno alizisonga nyaya za umeme wa pasi ile kwenye kitasa cha chuma cha mlango ule huku bado ule waya ukiwa umechomekwa kwenye soketi iliyokuwa ukutani kando ya mlango.
Akaiwasha ile swichi ya umeme, kisha hapo hapo akaitumia ile pasi kupasua kitufe cha kengele ya dharura ya moto kilichokuwa mle chumbani, na hapo hapo ving’ora viikaanza kurindima kwa fujo mle hotelini, kama kwamba kulikuwa kuna moto, naye akajirusha upande wa pili wa mlango ule na kujibanza.
Kizaazaa!
Kutokea kule nje, mtu alikamata kitasa cha mlango ule na hapo hapo ukelele wa mshituko na maumivu vikasikika baada ya mtu yule kupigwa shoti kali za umeme huku akijibamiza pale mlangoni, mayowe na vishindo vya wapangaji wengine vikasikika huko nje kutokana na ving’ora vile vya tahadhari ya moto.
Mlango ulisukumika ndani kwa nguvu na mtu mmoja akabwagika kwa kishindo mle ndani na kubaki akitetemeka mithili ya mwenye kifafa. Kabla ya yeyote kati ya waliokuwa mle ndani hajatabahi, mtu wa pili alijitupa mle ndani kutokea kule nje huku akimimina risasi za mfululizo pasina milipuko yoyote kusikika. Benson Kanga alipiga ukelele, Brey Jabba akatupa teke kali lililokuwa likimuendea shingoni yule jamaa wa pili lakini ni muda huo huo ambapo yule mvamizi aliinama kwa lengo la kumchukua yule mwenzake pale chini huku kwa mkono mmoja akiendelea kumwaga marisasi pande zote mle ndani, ilhali kwa mkono mwingine akiikamata sehemu ya mkanda wa suruali ya yule mwenzake aliyebwagika kifudifudi pale sakafuni na kuanza kumvutia nje.
Teke la Brey likasalimiana na hewa.
Bastola ya Benson Kanga ililipuka mara moja, na ya mara pili.
Brey aliruka kutoka pale kando ya mlago na kuipiga teke ile bastola kutoka mkononi kwa yule mvamizi, nayo ikatupwa pembeni.
Jamaa alimgeukia kwa kiwiko kikali lakini Brey alijizungusha kama anayecheza dansi aina ya “waltz”, kiwiko cha mvamizi nachi kikasalimiana na hewa, na Brey akaikamata sehemu ya mbele ya koti la yule jamaa na kumvuta mbele kwa nguvu huku akimuinulia goti lake kwa lengo la kuubabatiza uso wa yule mvamizi kwenye goti lake, lakini jamaa akawahi kuweka mikono yake kuukinga uso wake. Brey akamshushia kiwiko kwa nguvu nyuma ya shingo na jamaa akasukumwa chini kama mlevi, lakini hapo hapo akaibinukia bastola yake iliyokuwa pale chini, akaikwapua na mlipuko wa tatu bastola ukasikika mle ndani.
Jamaa akaachia yowe la maumivu huku akiitupa ile bastola aliyoinyakua na kujishika upande wa kichwa chake, damu ikimchuruzika kutoka sikioni, na hapo yule dada mweye umbo dogo alijiinua mzima mzima kutoka kule nyuma ya kitanda na kumtupia risasi ya pili yule mvamizi. Lakini yule mwenzake naye akawa amezinduka na kumsukumia kile kitanda kwa miguu yake, akambabatiza nacho ukutani, na risari ya yule binti ikaenda hewani na kuchimba dari sanjari na mlipuko wa nne wa bastola mle ndani.
Mvamizi wa pili alimrukia Brey mzima mzima, lakini kwa mara nyingine Brey akijigeuza mithili ya wale “El Matador”, wanaocheza mchezo wa ng’ombe wa kule Hispania, na kumpisha kistadi yule mvamizi ambaye alipitiliza kama ng’ombe kweli, na kujipigiza vibaya ukutani kando ya mlango na kusambaratika sakafuni.
Brey aliunguruma kama simba na kumgeukia yule mtu wa kwanza aliyepigwa shoti ya umeme hapo mwanzo, lakini jamaa naye alikuwa ameshajiinua na akaruka kwa hatua moja hadi kitandani, akadunda na kurudi tena sakafuni, akitua nyuma ya Brey. Brey alijigeuza kwa wepesi wa ajabu huku akichanganya miguu, lakini yule jamaa hakuwa tena na kasi, ari wala nguvu ya kuendelea na mapambano. Alimkumba mwenzake kutoka pale kando ya mlango na kutoka naye mbio nje ya chumba kile, wakijichanganya na watu wengine waliokuwa wakiishia pale kwenye korido wakikimbilia ghorofa za chini za hoteli ile.
Brey akawatukania mama zao wale wavamizi kwa hasira na kuwageukia wale wenzake mle ndani huku akiufunga mlango wa chumba chao kwa kisigino cha mguu wake.
Akabaki ameduwaa.
__________________
Kwenye eneo la mapokezi la hoteli ile taharuki ilikuwa imetawala. Meneja na watendaji wake walikuwa wakijitahidi kuwatuliza wateja wao waliopanga kwenye hoteli ile, ilhali wafanyakazi wanaohusika na maswala ya umeme kwenye lile jengo wakijaribu kutafuta hitilafu ilikuwa imetokea wapi, Imani ikiwa ni kwamba ni hitilafu ya umeme ndio iliyosababisha vingo’ora vile vya tahadhari ya moto.
Katikati ya sintofahamu iliyoshamiri katika eneo lile, watu wawili wenye asili ya kiajemi walichomoza kutokea kwenye ngazi za kuteremka kwa miguu na kufika pale mapokezi, kila mmoja akiwa na begi la wastani mkononi. Waliangaza huku na huko, kisha, huku nyuso zao wakiwa wamezifunika kwa miwani za jua ingawa muda ulikuwa ni usiku, walitoka nje ya hoteli ile huku wakiwa wamenuna, mmoja kati yao akichechemea kwa taabu sana. Waliingia kwenye gari lao aina ya Range Rover na kuondoka eneo lile kwa kasi.
Mle garini, yule aliyekuwa kwenye kiti cha abiria alikuwa ameshikilia kiganja chake kilichobabuka baada ya kunyanyaswa na shoti ya umeme mkali pale alipojaribu kushika kitasa cha mlango wa chumba namba mia tatu na saba kwenye ile hoteli.
“Who the hell was that guy?” Alifoka kwa hasira huku akiupapasa mkono wake uliobabuka, akimaanisha kuwa anataka kujua kuwa yule mtu waliyekabiliana naye mle ndani alikuwa nani.
“Nadhani ndiye hasa tuliyemkusudia…ila ametuzidi mahesabu kidogo tu, mjukuu wa ibilisi yule!” Mwenzake alimjibu kwa hasira huku akiendesha gari lile kwa kasi, kuelekea maeneo ya katikati ya jiji.
“Ulipata kumuona sura yake vizuri…ndiye yeye kweli?” Mwenzake alihoji.
“Taarifa zetu zimetuongoza moja kwa moja mpaka pale alipokuwa…tatizo ni wale watu aliokuwa nao mle ndani…ni kina nani wale?” Mwenzake alisema na kuuliza kwa utulivu wa ghadhabu.
“Wale sio ishu Mukri…kazi yetu ni yule jamaa…na tumeshapoteza nafasi moja…”
“Shaka ondoa patna…” Mukri alimjibu mwenzake huku akiendesha gari kwa utulivu, na kuendelea, “…leo kanusurika, lakini kila siku sio leo…tutakapokutana naye tena ndio utakuwa mwisho wake…”
Yule mwenzake alisonya kwa hasira.
“Lazima tumzime huyu mtu tutoweke hapa…viza yetu ni ya miezi mitatu tu hapa Tanzania…sina nia ya kumalizia miezi yote mitatu kwenye nchi hii aisee!” Jamaa aliyebabuka mkono alisema.
Mwenzake aliuma midomo kwa ghadhabu, lakini hakujibu kitu.
_________________
Benson Kanga alikuwa ametawanyika sakafuni akiwa amekodoa macho kwa mshangao wa kudumu, damu ikimchuruzika kutoka sehemu ya kifua chake ilhali ile bastola yake ikiwa bado mkononi mwake.
“Nooo, Benson, NOOOH!” Dada mwenye umbo dogo alipiga ukelele huku akimkimbilia yule mwenzake kutokea ubavuni kwa kile kitanda alichokuwa amebabatizwa nacho hapo awali.
Brey Jabba aliitazama ile hali, na mara moja akajua kuwa hakukuwa na la kufanya kuhusu yule mtu aliyejitambulisha kwake kwa jina la Benson Kanga.
Yule dada alimtikisa Benson kwa nguvu huku akilia, lakini uhai ulikuwa umeshamtoka yule bwana.
“Amekufa huyo…tuondoke hapa haraka sana…” Brey alimwambia kwa kuhimiza.
“No! Hatuwezi kumuacha hapa! Haiwezekani…” Dada alikuja juu.
“Okay, endelea kumsubiri tu hapo hapo…mimi sikutwi na wanausalama nikiwa na maiti humu ndani bi mdogo…kwa heri!” Brey alimjibu huku akigeuka. Alifungua mlango na kuchungulia nje. Korido ilikuwa tupu.
“Huwezi kuniacha humu namna hii wewe!” Dada alimaka. Brey akamgeukia na kurudi ndani, akiufunga tena mlango.
“Look, bibie…sikujui…hunijui…nilikuwa naelekea kujuana nawe zaidi lakini naona hujui tunapambana na watu wa aina gani…naondoka!” Alimkoromea.
“Una uhakika sikujui mimi wewe?” Binti alimkoromea.
“Sio ishu…wako wengi wanaonijua zaidi ya wewe…na nimejuana na wengi kabla ya wewe…nijuali ni kwamba nahitaji kuendelea kuishi, na kukaa hapa hadi kukutwa na wanausalama au wambea wengine wa kawaida hakutanihakikishia uhai wangu…tuondoke hapa mwanamama…hatun
a tunaloweza kulifanya kuhusu Kanga kwa sasa!” Brey alimwambia.
***Makubwa!
NJOO TUSOME zaidi hapa hapa...muda

“Sio ishu…wako wengi wanaonijua zaidi ya wewe…na nimejuana na wengi kabla ya wewe…nijualo ni kwamba nahitaji kuendelea kuishi, na kukaa hapa hadi kukutwa na wanausalama au wambea wengine wa kawaida hakutanihakikishia uhai wangu…tuondoke hapa mwanamama…hatun
a tunaloweza kulifanya kuhusu Kanga kwa sasa!” Brey alimwambia.
Mwanadada aliinuka na kujifuta machozi.
“Okay…tunaenda wapi sasa?” Alimuuliza.
Badala ya kumjibu, Brey aliuendea ule mwili na kuusachi haraka haraka. Akatoa pochi ya yule mtu iliyokuwa na vitambulisho kadhaa pamoja na kisu kilichokuwa kimefutikwa kiunoni kwa yule marehemu. Aliinuka na kuvishindilia mfukoni mwake vile vitu.
“Tutajua mbele ya safari….twen’zetu!” Alimjibu huku akiongoza na kufungua mlango. Baada ya kuchungulia nje kidogo, alitoka nje bila ya kugeuka. Binti akamfuata nyuma kwa mwendo wa haraka.
Brey aliongoza usawa wa sehemu ya kujisaidia, akijipenyeza miongoni mwa wananchi waliorundikana pale mapokezi.Mwanadada akamfuata kule kule na walipofika sehemu ambapo ilibidi wagawane njia kila mmoja aelekee kwenye maliwato ya jinsia inayomhusu, Brey alimgeukia.
"Una sehemu ya kwenda kutoka hapa?" Alimuuliza.
"Nyu...nyumbani kwangu tu sasa..."
"No...usiende nyumbani...tafuta nyumba ya wageni leo...kama una mume utajua namna ya kujieleza....mi ntakufuata nyuma kwa pikipiki..." Alimjibu haraka na kugeuza kurudi kule mapokezi, ambako alikuta watu wakielekezwa kutoka nje ya hoteli ile. Bila kujali kuwa yule dada alikuwa akimfuata au la, alitoka moja kwa moja nje ya geti la hoteli ile, na dakika tano baadaye aliliona gari la yule dada nalo likitoka nje ya geti lile. Akaanza kulifuata kwa nyuma akiwa kwenye pikipiki yake.Mwendo wa kama saa moja baadaye dada aliingiza gari kwenye maegesho ya magari ya kulipia yaliyokuwa kwenye ofisi ya chama tawala maeneo ya Kigogo. Brey naye akaifunga kwa mnyororo pikipiki yake kwenye moja ya nguzo za zege kwenye jengo la ofisi ile, wakamlipa mlinzi ipaswavyo kisha wakatoka kwa miguu nje ya uzio wa eneo lile la kulazia magari.
"Nini kinaendelea...?" Brey alihoji huku akimfuata yule dada aliyekuwa akitembea kwa mwendo wa haraka.
"Tunaenda gesti...si ndivyo ulivyotaka?" Alijibiwa.
"Vipi kuhusu mumeo...?"
"Si kazi yako!" Alijibiwa tena.
Akapiga kimya na kuendelea kumfuata huku akiwa makini sana na kila waliyekuwa wanapishana naye humo njiani.
______________________
Dakika chache baada ya watu wote kutolewa nje ya hoteli ile, gari la kikosi maalum cha usalama lilifika pale hotelini kwa makeke na askari sita waliteremka na kuingia ndani ya hoteli ile. Meneja alihamanika. Hakuwa amepiga simu kuita wana usalama wowote hadi kufikia muda ule na alikuwa akiuliza kwa wahka ni nini ilikuwa azma ya ujio wa wale askari pale.
"Watu wote wabaki nje...tunahitaji kufanya uchunguzi ndani ya jengo hili!" Kiongozi wa wale askari waliovalia nguo maalum za makabiliano zilizotisha alisema kwa mamlaka.
"Kwa...kwa vipi? Hapa palilia king'ora tu kilichoashiria kulikuwa kuna moto jengoni...lakini sasa tunaamini kuwa ilikuwa ni bahati mbaya tu...hakuna moto wowote...na..." Meneja alitoa maelezo.
"Mnataka kusema kuwa hamkusikia milipuko ya bastola humu ndani?" Yule askari alihoji zaidi, na meneja akahamanika.
"Ah..kuna mipuko ilisikika wakati na ving'ora vinaendelea kulia...lakini...tulidhani ni sehemu ya hitilafu iliyosababisha moto...kumbe ni bastola? Mungu wangu! Sasa...?" Meneja alibwabwaja kwa woga.
"Okay...kwa hiyo hamna mlilogundua mpaka sasa..?"
"Hakuna...ndio tulikuwa tunaendelea..."
"Basi wote subirini nje...!" Yule askari aliamuru, na meneja kwa woga mkubwa akatii...akiwaona wale askari wakipanda lifti ilhali wengine wakipanda kwa miguu...mmoja wao akiwa na fuko kubwa sana jeusi la plastiki ngumu.
Hakuelewa.
Na alizidi kutoelewa pale wale askari walipotoka kule ndani, nusu saa baadaye, wakiwa wamebeba furushi kubwa na refu kwenye lile fuko ambalo awali lilionekana tupu. Ilikuwa ni kama kwamba kulikuwa kuna mwili wa binadamu kwenye like fuko.
"Heh! Ni...ni nini hicho...?" Meneja alihoji kwa wahka.
Kiongozi wa wale askari alimkamata bega na kumvutia pembeni wakati wale wenzake wakiuingiza kwenye lile gari lao aina ya Land Rover lililokuwa mwenye muundo wa pick-up bila kumjali.
"Hakuna tatizo lolote...rudisha wateja wako hotelini wakalale..." Alimwambia.
"Aaah! Inawezekanaje hii? Na vipi kuhusu hiyo milipuko ya bastola mliyosema? Mmegundua nini bwana?" Meneja alisaili.
"Inaelekea ilitokea nje ya jengo hili...lakini kuna chumba kimoja kimeathiriwa kwa risasi...ila hakuna tatizo lolote..." Jamaa lilimjibu.
"Na...ule...ule mwili vipi?" Meneja alihoji huku akioneshea kule kwenye gari. Jamaa lilimuacha na kuingia kwenye gari sehemu ya mbele, kando ya dereva.
"Mwili gani?" Alimuuliza huku gari liking'oa taratibu na kuchanganganya kasi kutoka eneo lile.
Meneja alibaki "gaa".
________________________
“Okay, sasa hebu tuwekane sawa…pale hotelini ulisajili chumba wewe…? Au Benson? Maana nimekuona ukijinadi kwa herufi kubwa sana pale kuwa upewe ufunguo wa chumba chako, namba mia tatu na saba…ina maana wale wahudumu wa hoteli wote wamekuona sura yako na yumkini ya Benson…” Brey alianza mara baada ya kuwa wamejifungia chumbani.
Walikuwa wamepanga chumba kwenye nyumba ya wageni ya hadhi ya wastani iliyojificha maeneo ya kule kule Kigogo.
“Una wasiwasi kuwa wakiukuta mwili wa Benson mle chumbani maaskari wataanza kunisaka sio?” Mwanadada alimuuliza huku akiwa amekunja sura kwa tafakuri, maswala ya kumlilia Benson yalikuwa yameisha, ingawa macho bado yalikuwa yamemuwiva na yamemvimba.
“Ndio maana yake…tatizo linalotuandama peke yake ni kubwa, sasa ikija kuingiliana na swala la maaskari tena, itakuwa…”
“Hakuna askari atakayefuatilia swala hili.” Dada alimkatisha. Brey akamuinulia nyusi kwa kuuliza.
“Ukimaanisha nini? Yaani wale wahudumu wa hoteli wakute maiti mle chumbani, halafu wasiitarifu polisi?”
“Kama kila kitu kitaenda sawa hawatakuta mwili wala damu mle chumbani…” Mwanadada alijibu, na Brey aliyejijengea tabia ya kutoshitushwa na mambo kirahisi akatumbua macho kwa mshangao.
“Ongea zaidi mwanadada…sijaelewa hapo!” Alimwambia.
Mwanadada akaguna, na kutazama pembeni, kisha akamgeukia.
“Nilipokuwa kwenye gari nilipiga simu moja…na nikawaeleza watu tunaofanya nao kazi juu ya kilichotokea…wataendea kumchukua Benson bila tamasha yoyote pale…na hakuna maswali yatakayoulizwa…sitasakwa mimi wala wewe kuhusika na kifo kile…”
Ikawa zamu ya Brey kuguna sasa. Akabaki akitikisa kichwa huku akimung’unya midomo, akiieneza akilini mwake taarifa ile.
“Kwa hiyo nyie ni akina nani…yaani ni taasisi gani ya dola, au usalama, au ujasusi, au chochote kinachofana na hivyo?” Hatimaye alimuuliza.
Kwa mara ya kwanza mwanadada akatabasamu.
“Kuna kichekesho chochote hapo?” Brey alimuuliza.
Tabasamu likazidi kuwa pana.
“Hapana…ni namna tu ulivyouliza hilo swali ndio iliyonifanya nitabasamu…”
“Na sasa kwa kuwa swali limeshakuchekesha, naomba jibu…”
“Sisi ni akina nani sio muhimu…muhimu ni wewe kuondoka hapa jijini haraka sana…ili wengine tuendelee na maisha yetu.” Dada alimjibu kwa kiburi.
Brey akamkata jicho.
“Okay, tutalipatia ufumbuzi tu hilo naamini…haya, wewe ni nani?”
“Hilo ndo uloliacha…”
“Enh?”
“Naitwa Sandra…na niko upande wako…”
“Sawa Sandra nimefurahi kukufahamu…tupange mikakati sasa. Natakiwa niondoke vipi hapa jijini?”
“Kila kitu kilikuwa kimeandaliwa na Benson…itanibidi nikafuatilie kesho kwa wenzangu, na kisha nije nikupe maelekezo…na mpaka hiyo kesho, hutatoka nje ya chumba hiki…”
“Unawasahau wale wahindi koko waliotuibukia kule hotelini? Tunajipanga vipi kuhakikisha kuwa hawatuibukii tena?”
“Sina namna ya kuhakikisha hilo, lakini nadhani ukiwa umejificha huku haitakuwa rahisi wao kukuona…yumkini pale walitubahatisha kutoka makaburini…na baada ya kuwakurupusha namna ile kule hotelini, itawachukua muda kuja kutushitukia tena mahala tulipo…ndio maana wewe inabidi utoweke haraka kabla hawajakushitukia tena…”
“Okay, na iwe hivyo basi!” Brey alisema, ilhali bado akiwa ana kiu ya kujua zaidi.
Haikuwa…
**** DUH!
 
RIWAYA: Wimbo wa Gaidi

MTUNZI: Hussein Tuwa

SEHEMU YA PILI

Na ni kutokana na uhatari wa eneo lile ndipo watalebani waliojaa hila na shuku zisizo ukomo, walipoelekeza kuwa ndege zile za misaada ziangushie marobota makubwa ya chakula na madawa kwenye eneo lile, kisha ndege zitakazoangusha misaada ile zigeuzie huko huko angani na kwenda zake. Hakukuwa na ruhusa kabisa kutua pale kijijini wala sehemu yoyote ya eneo lile walilolidhibiti vilivyo, la Waziristan ya Kaskazini.
Ndege ya kwanza ilitokeza kutokea nyuma ya milima mingi iliyolizunguka eneo lile, na minong’ono ya viherehere ikazagaa miongoni mwa wanakijiji. Ndege ikazidi kukurubia huku ikizidi kushuka. Watalebani wengi wa shuku wakajizatiti kwa silaha makini wakiwa miongoni mwa wanakijiji ambao sasa waliwakusanya kuwafanya kama ngao zao dhidi ya shambulizi lolote kutoka kwenye ndege ile. Na hata pale walipoanza kujizatiti namna ile, ndege nyingine tatu zilioneka kutokeza juu ya vilele vya milima iliyolizunguka eneo lile, na dakika kumi baadaye marobota makubwa yalionekana kuanguka kutoka angani. Mayowe yalizagaa, wanakijiji wakazidi kujirudisha nyuma ili kuwa mbali na eneo lile la wazi lililokuwa likimulikwa kwa ile mioto kutoka pembe sita tofauti. Lakini muda si muda, maparashuti yakafunuka kutoka kwenye marobota yale makubwa, nayo yakaanza kushuka taratibu huku yakinesanesa hewani kwenye anga ile ya usiku. Wanakijiji na watalebani walijitahidi kwa kadiri walivyoweza kufuatilia ushukaji wake kwenye kiza cha usiku ule wenye mbalamwezi hafifu, lakini haikuwa rahisi. Marobota yalizidi kushuka, kila moja kwa uelekeo wake…kila moja likiwa na shehena muhimu kwa wanakijiji wa Dargar Mandi ndani yake…lakini pia juu ya kila mgongo wa robota la vyakula vile, kulikuwa kuna siri kubwa….

________________

Makomando wanne walishuka kwa maparashuti wakiwa wamelala juu ya migongo ya yale marobota makubwa ya chakula cha msaada yaliyokuwa yakiangushwa na ndege za msalaba mwekundu kwenye kile kijiji cha Dargar Mandi. Wote wanne walikuwa wamevaa nguo maalum za kuzamia mbizi majini bila ya kulowa.
Lengo lao lilikuwa ni moja tu. Kumkomboa mtanzania aliyenaswa ndani ya kijiji kile, akiwa ni mmoja wa wapiganaji wa Al-Qaeda aliyetajwa kutafutwa na FBI baada ya shambulizi la kutisha kwenye ubalozi wa Marekani jijini Dar mnamo mwaka 1998. Sasa ngome iliyosalia ya Taleban ilikuwa inawahifadhi baadhi ya wapiganaji wa Al-Qaeda waliobakia, yeye akiwemo, ilikuwa imezingirwa na majeshi ya ushirika wa Marekani na Pakistani. Upinzani wa Taleban ulikuwa unaelekea kushindwa, na wamarekani wakiingia ndani ya ngome ile hakutakuwa na garantii ya mtanzania yule kunusurika.
Isipokuwa kama atatolewa mle ngomeni kabla majeshi ya washirika hayajavamia.
Lakini kivipi?
Ndipo nafasi ilipojitokeza pale Taleban walipokubali wanakijiji waletewe vyakula vya msaada kwa njia ile.
Marobota yanatua kwa vishindo ardhini na kuviringika shaghala baghala, kila moja upande wake. Makomando wanagaragazwa vibaya na yale marobota makubwa, lakini kwa kuwa walikuwa mahiri kwenye kazi zao na kwa kuwa walishalifanyia mazoezi mara kadhaa tukio lile kabla ya siku ile, kila mmoja alifanikiwa kujirusha pembeni na kubaki akiwa amejilaza kimya kwenye majani mafupi ya eneo lile, macho yao yakitafuta uelekeo ambao kila mmoja aliamini kuwa ni kusini ya pale walipoangukia, wakiyaacha yale marobota makubwa kabisa yakiendelea kubingirika huku yakijizonga na yale maparashuti yaliyoyashusha.
Kule kwa wanakijiji wenye njaa, watalebani walikuwa wakiyafuatilia yale marobota kwa umakini kwa kadiri walivyoweza. Kwa namna fulani ambayo sio bahati mbaya, marubani waliokuwa wakiyadondosha yale marobota waliyaangusha mbali na ile mioto mikubwa iliyowashwa kuwaelekeza ni wapi yale marobota yaangushwe, na hii iliwapa nafasi makomando walioshuka na marobota yale kuweza kutumia kiza kilichopo, mbali na ile mioto, ili kijiweka mbali na marobota yale na kwenda kwenye jukumu lililokuwa mbele yao. Jukumu kubwa na la hatari sana…wenyewe waliliita ni jukumu la kujitoa muhanga…suicide mission. Kwa ajili ya mtu mmoja ambaye hata hivyo hawakuwa wakimjua kiukaribu wowote zaidi ya kuwa alikuwa akihitajika sana na nchi kubwa duniani, na kwamba malipo yao kwa kujitoa kwao kwenye kulitekeleza jukumu lile, yalikuwa ni makubwa sana kiasi cha kuhalalisha lolote ambalo wangekutana nalo ndani ya eneo lile lililoshindikana kabisa hata kwa mataifa makubwa yenye uwezo mkubwa wa kivita…
Kila mmoja alibaki akiwa amelala mahala pake, akitafuta ishara aliyoandaliwa kuitafuta mara baada ya kutua ndani ya eneo lile kusudiwa. Wakaiona. Kutokea kwenye kona moja ya eneo lile, hatua kadhaa kutoka kwenye moja ya marundo ya mioto iliyokuwa ikiwaka eneo lile, taa nyekundu ilikuwa ikiwashwa na kuzimwa kwa kufuata utaratibu maalum. Iliwaka mara nne kwa kuacha kiasi cha kama sekunde moja baina ya muwako mmoja na mwingine, kisha ikafuatiwa na miwako mingine mitatu ya haraka haraka. Ilikuwa ni mbinu maridhawa kwani kwa pale ile toch maalum yenye mwanga mwekundu ilipokuwa ikiwakia, haikuwa rahisi hata kwa mtalebani mwenye macho makali kiasi gani, kuweza kuutofautisha mwanga ule kutoka kwenye mwanga wa moto uliokuwa ukiwaka hatua chachekutokea pale.
“Mmeona?” Mmoja alisaili kwa mnong’ono mkali.
“Yah!” Mwingine alijibu, na wengine wawili nao walituma majibu yao kuwa wameiona ile ishara. Lakini hakuna aliyetoka pale alipokuwa amelalia tumbo, akiwa na silaha yake mgongoni.
Kule kwa wanakijiji, watalebani waliendelea kujificha huku wakiyatazama yale marobota yakiendelea kubiringika huku wakiwa wamewaamuru wanakijiji wote kutulia mahala walipokuwa. Marobota yalipotulia kila moja upande wake, bado watalebani waliojaa shuku na wasiyemuamini yeyote isipokuwa wao wenyewe, wanawazuia wanakijiji kuyasogelea. Wanayatazama kwa umakini mkubwa yale marobota kutokea kule walipokuwa, wakitaraji jambo baya kutokea. Lakini halitokei. Hatimaye wanatoa amri kwa wanakijiji kuyaendea yale marobota. Kelele za shangwe zasikika pale wanakijiji wanapokurupuka na kuyakimbilia marobota yale, na ndipo kule walipokuwa, wale makomando wanatambaa kwa kasi sana kuelekea kule ile ishara ilipotokea. Wakati watalebani wako makini kufuatilia harakati za wanakijiji kule kwenye yale marobota ya vyakula, hawatakuwa makini kufuatilia kitu kingine na hawataweza kuona wakati wale makomando wakitambaa kwa uficho namna ile kuelekea sehemu tofauti na kule yale marobota yalipokuwa.
Makomando wanafika pale ishara ilipotokea, na hapo wanakutana na mshirika wao, mwenyeji wao, raia wa Pakistani aitwaye Imraan Gopang. Naye akiwa amevaa nguo kama walizovaa wao, ila akiwa amebeba begi mgongoni na akiwa amening’iniza bunduki mbili mgongoni kwake, Imraan anawaongoza kwa usiri bila ya kuongea lolote hadi kwenye shimo la wastani mithili ya yale mashimo ya vyoo yatumikayo kwenye jamii nyingi.
Haraka haraka wanaufunua mfuniko mzito wa zege wa shimo lile, na tochi zilizounganishwa kwenye bunduki zao zinawaonesha ngazi za chuma zilizojengewa kwenye ukingo wa shimo lile, ambazo zingewateremsha hadi kwenye kichanja kikubwa cha chuma kizito ambacho kilikuwa kinakatisha kutoka upande mmoja wa mtaro mkubwa kabisa wa chini ya ardhi, hadi mwingine, na kuwa kama daraja la aina fulani..
Wale makomando wanne na yule mwenyeji wao wanaingia ndani ya shimo lile na kuufunika ule mfuniko wake kwa ndani. Wateremka hadi pale kwenye kile kichanja kirefu cha chuma kizito, sasa wakiwa ndani ya mtaro mkubwa wa chini ya ardhi. Kiasi cha kama mita tatu hivi chini ya daraja lile, maji machafu ya kitongoji kile cha Waziristan yalikuwa yakitiririka kuelekea kwenye mdomo mpana wa mtaro ule, ambao ulichomoza kutokea kwenye uso wa jabali refu sana, kiasi cha kama kilomita moja zaidi kutokea pale walipokuwa. Njia nyingi kutoka pande mbali mbali za nchi ile zilikuwa zikimimina vinyesi na majitaka kwenye mtaro ule mkubwa kabisa, ambao nao ulisafirisha shehena ile ya uchafu kwa hiyo kilometa moja zaidi kutokea pale wale makomando walipokuwa na hatimaye kwenda kuitiririsha kwenye mto mkubwa kabisa uliokuwa umbali wa mita zipatazo mia saba kwenda chini kutokea kwenye uso wa jabali refu ambalo juu yake ndipo kijiji kile cha Dargah Mandi kilikuwepo.

***Watu wakazi mtaroni! Lengo lao litatimia kweli? NJOO KESHO muda uleule...
Kumbe ni hadithi za kutungwa napata tabu kusoma
 
nasubiri nikiona neno end ndo nianze kuisoma. Plz siku ikiisha mniite
Hutakaa uone hilo neno mkuu, maana mtunzi wa hadithi Hussein Tuwa ameacha kuiendeleza kwenye page yake ya facebook kwa sababu watu wanacopy na ku-share bila idhini yake. kwa hiyo ameamua kuandika kitabu..

sisi wenyewe tuko kwenye foleni ya kusubiri hicho kitabu
 
Hutakaa uone hilo neno mkuu, maana mtunzi wa hadithi Hussein Tuwa ameacha kuiendeleza kwenye page yake ya facebook kwa sababu watu wanacopy na ku-share bila idhini yake. kwa hiyo ameamua kuandika kitabu..

sisi wenyewe tuko kwenye foleni ya kusubiri hicho kitabu
shukrani mkuu kwa maelezo murua maana ningeisoma ningejitia genye tu halafu nisingefika kileleni hata
 
Back
Top Bottom