LEGE
JF-Expert Member
- Oct 14, 2011
- 5,122
- 9,204
AYA: Wimbo wa Gaidi
MTUNZI: Hussein Tuwa
UTANGULIZI
Ni miaka mitatu tangu kuuawa kwa Osama bin Laden nchini Pakistan. Wanamgambo wa Al-Qaida wamesambaratika. Wengi miongoni mwao wameuawa, wengine wamekamatwa na majeshi ya marekani nchini Pakistani…na kikundi cha wachache wengine kimefanikiwa kutoroka na kukimbilia eneo la Waziristan lililo kaskazini mwa Pakistan, hususan kwenye kitongoji cha Miramshah kinachodhibitiwa na wapiganaji wa Taleban, ambao walikuwa ni washirika wao wakuu na huko wakapata hifadhi baada ya kifo kile kichungu cha kiongozi wao.
Na tangu wakati huo, hali ya wakaazi wa kijiji kilichokuwa kiasi cha kilomita saba kutoka kwenye ile ngome ya wa-Taleban iliyowahifadhi wale wanamgambo wachache wa Al-Qaida, imekuwa ni ya mashaka makubwa. Njaa ilikuwa imetawala, mahitaji yote muhimu yametoweka, maradhi hayakuwa na wa kuyatibu, ilhali magonjwa ya mlipuko na yatokanayo na lishe duni yakishamiri…na roho za wanakijiji kile zikiwa sio mikononi mwao tena, bali mikononi mwa wapiganaji wa taleban waliokidhibiti kijiji kile.
Kwa nini?
Kwa kuwa Osama Bin Laden alikuwa ameuawa na wamarekani…na taarifa ziliwafikia wa-Taleban kuwa tabibu aliyefika mahala ambapo Osama alikuwa amejificha kwa ajili ya kumtibu binti wa mpiganaji yule mwenye msimamo mkali ndiye aliyetoa siri ya mahala Osama alipokuwa, kwani wamarekani walivamia eneo lile siku mbili tu baada ya tabibu yule aliyeaminika kuwa alikuwa akiiunga mkono Al-Qaida kufika eneo lile. Kwa kuwa Al-Qaida ilisambaratika kwa muda baada ya kifo cha Osama, Taleban wakachukua jukumu la kulipiza kisasi kifo cha mshirika wao mkubwa kwa niaba ya Al-Qaida.
Hivyo basi, pale binti wa Osama aliyekuwa akishikiliwa na wanajeshi wa Pakistani kabla ya kukabidhiwa kwa wamarekani, alipofanikiwa kupenyeza taarifa kwa watalebani kupitia kwa mmoja wa watendaji wa jeshi la Pakistani aliyekuwa akiiunga mkono Al-Qaida kwa siri, kuwa tabibu huyo alikuwa akiongea kwa lugha ya ki-pashtuni, lakini kwa lafudhi ya watu watokao kwenye kijiji kile, ilitosha sana kuwajulisha watalebani kuwa dakitari aliyemchomea utambi Osama kwa wamarekani hadi akauawa, alikuwa ametokea kwenye kijiji kile kilichokuwa kiasi cha kilometa saba tu kutoka pale kwenye ngome yao.
Kilichofuatia kilikuwa ni kizazaa kikubwa pale kijijini.
Mauaji, mateso, na utekaji nyara viliwaandama wanakijiji, ikitafutwa familia ya tabibu aliyemchoma Osama kwa wamarekani. Msako wa nyumba hadi nyumba uliondeshwa ukazaa matunda. Familia ya tabibu aliyehusika kumchomea utambi Osama ilipowekwa kizuizini kwa wiki nzima na kuwekwa kwenye wakati wa mateso na vitisho visivyosemeka ikiwamo kubakwa, kupigwa mijeledi na baadhi yao wakiuawa huku wengine wote wakishuhudia, siri ikabidi itolewe. Tabibu wa Osama akatajwa na wanafamilia wake mwenyewe, wakati huo yeye akiwa jijini Islamabad.
Wataleban wakamfuata huko huko kwa lengo la kumuua. Lakini sio kabla ya kumtesa na kumhoji kikatili. Tabibu akakiri kuwa hakuwa peke yake…alikuwa na mwenzake kutokea kwenye kijiji kile kile ambaye alikuwa ni miongoni mwa wapiganaji wa Al-Qaida waliokimbilia kule kwa Wataleban na kuhifadhiwa.
Hah!
Wateleban wakahamanika. Ni nani huyo?
Tabibu akafa na siri yake kwa kujitia kumpora silaha mmoja wa watesaji wake ili awateketekeze.Wakamuwahi na kummiminia risasi. Kifo cha Osama kikalipizwa… miezi mitatu tu baada ya kifo chake. Lakini sasa wataleban wakabakiwa na kitendawili kikubwa. Ni nani miongoni mwa wale maswahiba wao wa Al-Qaida waliowahifadhi kule kwenye ngome yao jirani na kile kijiji walichokibatiza jina “kijiji cha wasaliti”, aliyekuwa akishirikiana na yule tabibu msaliti?
Sasa huyu ndiye alikuwa anasakwa na kijiji kile kikawekwa chini ya karantini kabambe na watalebani.
Na mpaka msaliti huyo na wengine kama yeye watakapobainishwa na kuuawa, hakuna atakayetoka wala kuingia kwenye kijiji kile.
Kijiji kikawa kimetengwa na dunia.
Jitihada za majeshi ya Pakistani kukiokoa kijiji kile hazikufua dafu asilani, kwani Waziristan ilikuwa ni ngome kuu ya wataleban, na hakukuwa na namna ya kuiangusha isipokuwa kwa kuipenya kijasusi kama jinsi alivyopenyezwa yule tabibu mzaliwa wa kijiji kile ndani ya kundi la Al-Qaida.
Na hilo lilikuwa haliwezekanin tena sasa. Watalebani wlaikuwa wkimshuku kila aliyewaendea na kila waliyemuona kuwa si miongoni mwao.
Na sasa hali ilikuwa imefikia pabaya.
Wapiganaji wote wa Al-Qaida waliokuwa wamehifadhiwa kwenye nyumba salama ya uongozi wa wa-Taleban. Miongoni mwao alikuwamo msaliti. Talebani walidhamiria kumtia mikononi na kumuangamiza. Ilikuwa ni mahojiano ya mara kwa mara, mitihani ya hapa na pale kwa wale Al-Qaida waliokimbilia mikononi mwa washirika wao wa ki-Taleban.
Amani ikapotea. Ndani nan je ya nghome ile kubwa ya watalebani.
Jumuia ya kimataifa ilifanya bidii za kila namna kuwaokoa wakaazia wa kijiji kile bila mafanikio yoyote. Serikali ya Pakistani pamoja na kulaani kwake kuuawa kwa Osama ndani ya nchi yake bila ya wao wenyewe kushirikishwa, haikufua dafu, kwani Taleban siku zote wamekuwa wakiamini kuwa serikali ya Pakistani ilikuwa ni kibaraka wa wamarekani.
Marekani ikatoa tamko. Talebani iwaachie huru wana kijiji wale waondoke kijijini pale na kwenda kwenye kambi za wakimbizi nje ya kitongoji kile cha Waziristan, na iwasalimishe wapiganaji wote wa Al-Qaida iliowahifadhi, ama si hivyo ndege za maangamizi zinazoruka bila ya rubani, yaani “drones”, zitatumwa kuisambaratisha ngome yao.
Taleban wakagoma.
Na wao wakatoa tamko.
Wamarekani wakituma hizo ndege ijue pia itaua raia wa kijiji wasio na hatia…na watalebani watakuwa wanaua kila mmarekana watakayemuona, popote pale duniani.
Ngoma nzito…
______________
SEHEMU YA KWANZA
Kijiji cha Dargah Mandi, kilomita saba magharibi mwa kitongoji cha Miramshah, Waziristan ya Kaskazini, Pakistan.
Ni saa saba za usiku. Baridi kali ilikuwa ikipambana na mashuka mazito yaliyokuwa yakijaribu kuihifadhi miili ya wanakijiji waliorundikana upande mmoja wa eneo pana la tambarare lililokuwa mpakani kabisa mwa kijiji kile kilichojaa madhila makubwa na mashaka mazito.
Ni kijiji cha Dargah Mandi kilichokuwa ndani ya kitongoji cha Waziristan ya Kaskazini, ambayo ilikuwa ni ngome kuu ya wapiganaji wa Taleban, nchini Pakistani.
Wanakijiji walikuwa wamejikunyata wakisubiri msaada waliokuwa wameutarajia kwa muda mrefu bila matumaini ya kuupata. Wapiganaji wa Taleban wenye silaha walikuwa wamewazingira wanakijiji wale kutoka pande zote za eneo lile, nao wakiusubiri msaada ule ambao kwa hakika na wao walikuwa wakiuhitaji, maana hali kijini Dargah Mandi ilikuwa tete kila upande.
Mbele yao, kiasi cha kama mita mia tatu hivi kutoka pale ambapo wale wanakijiji walikuwa wamejikunyata huku wakiwa wamewekewa mitutu ya bunduki za wapiganaji wale wenye roho zisizosita kutekeleza mauaji, kulikuwa kuna uwanja mpana wa wazi wenye majani mafupi, na kwenye maeneo sita tofauti ya uwanja ule, kulikuwa kuna mioto iliyokuwa ikiwaka kutokana na marundo ya kuni zilizowashwa kwa kusudio maalum, ikitupa miale yake hewani na kuleta mwanaga kiasi eneo lile na wakati huo huo ikiacha baadhi ya maeneo ya uwanja ule kuwa na kiza kizito.
Dakika zilisonga na baada ya muda ulioonekana kuwa ni mrefu kuliko uhalisia wa muda wenyewe, miungurumo ya ndege ilisikika ikitokea angani upande wa mwisho kabisa wa eneo lile la wazi lililowekewe mioto, eneo ambalo liliiishia kwenye korongo refu sana lililoanguka umbali wa mita zipatazo mia nne kwenda chini, ambako kulikuwa kuna mto mkubwa sana uliokuwa ukipeleka maji kwa ghadhabu isiyosemekana hadi kwenye bahari ya Arabia (Arabian Sea), kilometa nyingi kusini mwa Pakistani.
Dargah Mandi haikuweza kabisa kuingilika kutokea upande ule hatari, ambapo hakuna binadamu ambaye angeweza kukiingia kijiji kile kwa kulikwea korongo lile kutokea kule chini kwenye mto ule mkali.
Na ni kutokana na uhatari wa eneo lile ndipo watalebani waliojaa hila na shuku zisizo ukomo, walipoelekeza kuwa ndege zile za misaada ziangushie marobota makubwa ya chakula na madawa kwenye eneo lile, kisha ndege zitakazoangusha misaada ile zigeuzie huko huko angani na kwenda zake. Hakukuwa na ruhusa kabisa kutua pale kijijini wala sehemu yoyote ya eneo walilolidhibiti vilivyo, la Waziristan ya Kaskazini.
Ndege ya kwanza ikatokeza kutokea nyuma ya milima mingi iliyolizunguka eneo lile, na mining’ono ya viherehere ikazagaa miongoni mwa wanakijiji. Ndege ikazidi kukurubia na ikazidi kushuka. Watalebani wengi wa shuku wakajiweka makini kwa bunduki na makombora yao…
***MNH! Tuwa ndo kaanza hivi?? Haya NJOO TUSOME zaidi hapo kesho muda kama wa leo.