Kwa msio jua, ni afadhali msiendelee kujua; ila mambo ni kama hivi,
Wakati Mobitel inaingia TTCL ilikuwa na share mle kama asilimia 40. Baadaye serikali ikazibeba. Walichofanya na hizo hisa hakijulikani, ila leo serikali haina hisa Tigo
Mwaka 1999 TTCL iliamua kuanzisha mradi wake wa simu za Mkononi (kwa fedha zake), wakati huo ilikuwepo Tigo na Tritel peke yake. Serikali kupitia TCRA wakauzuia mradi huo kwa madai kuwa kampuni iko kwenye mchakato wa ubinafsishaji - Mwaka 2000 Vodacom wakaingia.
Mwaka 2001 akaingia Mbia kwa madai ya kununua asilimia 35 kwa Dola million 120. Akaishia kupewa hizo hizo kwa dola million 65.
Mbia huyo akatumia leseni ya biashara za simu za mikononi ya TTCL (mradi ulisimamishwa haukufutwa) kuanzisha celtel Tanzania, TTCL ikawa imenyang'anywa rasmi uwezo wa kufanya biashara za simu za mikononi, si kwa sababu ya uwezo wa watendaji, sababu ya uamzi wa mezani (serikali)
Celtel international (aliyekuwa na hisa ndani ya TTCL) ndo akaanzisha Celtel Tanzania ikiwa kama subsidiary company ya TTCL
Baadaye TTCL ikanyang'anywa Hisa zote ndani ya Celtel, zikahamishiwa hazina, TTCL ikabaki haina hisa na haina biashara ya simu za mkononi na ikazuiwa kuanzisha ya kwake kwa sababu masharti ya leseni hayakuiruhusu kuanzisha
Mwaka 2005, serikali ikaondoa masharti ya leseni, ila mbia mwingine wa serikali; Celtel international (ambaye sasa ni mshindani wa TTCL - lakini akiwa na share ndani ya TTCL) akakataa TTCL isijiingize kwenye biashara ya simu za mikononi.
Wafanyakazi wazalendo ndani ya TTCL wakaamua kuingiza biashara hizo kwa mgongo wa nyuma, ndivyo ilivyoingia TTCL Mobile na Technolojia ya CDMA. Hawa wazalendo waliidanganya bodi kuwa wanaingiza CDMA kufanya fixed wireless (WLL) ila kwa siri wakanunua full mobile solution. Bodi ingejua isingiruhusu asilani.
Hata hivyo baadaye bodi iligundua kuwa kilichoingia ni Mobile si WLL. Ikaamua kuzuia uwekezaji zaidi katika mradi huo, hivyo TTCL mobile ikashindwa kujitanua kama ilivyotarajiwa.
Mwaka 2007, serikali ikaleta menejimenti nyingine ya wazungu, kutoka Canada. Hawa walivyokuja wakaiambia serikali tiba ya TTCL ni kuuendeleza ule mradi wa TTCL mobile ulioanzishwa na wazalendo. Serikali ikakubali, lakini ikishirikiana na Celtel international (wakati huo Zain) wakazuia TTCL kukopa kwa ajili ya kuuendeleza mradi wa TTCL Mobile - Kwa hiyo mradi ukabaki bila kuendelezwa.
Mwaka 2009, baada ya kusuguana sana na serikali kuhusu kuendeleza mradi huo (serikali na Zain wakikataa), wa Canada waliamua kujitoa rasmi wakaondoka mwezi July 2009.
Toka hapo ni dana dana tu. Serikali wanashangaa kwa nini TTCL haifi? Wao wanataka ife, wauze mbao! Menejimenti ya wazalendo na wafanyakazi wao, wanapambana kulinda ajira zao. Ila serikali kwa kushirikiana na Zain (sasa airtel) wanataka hiyo kampuni ife, waipeleke kwa mufilisi ili viongozi wa serikali wajichotee masalia (TTCL inazo mali nyingi sana - Ikiwemo majengo, viwanja katika maeneo muhimu katika miji yote ya Tanzania, n.k.)
Ni dharau kwa watanzania kuwasema vibaya wafanyakazi wa TTCL, ni kampuni ngapi zingeweza kuhimili hujuma kutoka kwa wamiliki wake? Ni wafanyakazi pekee wanojua kuwa wanaohujumiwa pale ni watanzania, si wafanyakazi wa TTCL!! Watanzania ndio wenye mali serikali ni msimamizi tu.
Serikali dhaifu inashirikiana na matapeli wa nje kuhakikisha hii kampuni itakufa. TTCL ikifa, atakayenufaika ni watendaji wa serikali waliokaa mkao wa kula, wakisubiri kujichotea ma properties yatakayotelekezwa. Atakayenufaika ni Makampuni ya nje yatakayojichukulia biashara kubwa ambazo bado TTCL inazo.
TTCL ikifa atakayeumia ni mtanzania atakayekosa kazi. Mapato ya serikali yatashuka kwani TTCL pamoja na hali yake bado ni mlipa kodi mkubwa (waulize TRA watakuambia). TTCL hawafanyi lolote kukwepa kodi. Kodi zote za serikali wanalipa bila matatizo (bado wanalipa kodi kubwa kuliko makampuni mengi ya simu yanayokwepa kulipa kodi). Kushuka kwa mapato ya serikali kutawaumiza watanzania, si wawekezaji kutoka nje.
Ni vizuri tuujue ukweli, kwani ukweli utatuweka huru!