Ngeleja aibomoa CHADEMA
na Sitta Tumma na Stella Ibengwe, Sengerema
WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ameibomoa ngome ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya viongozi wa chama hicho Wilaya ya Sengerema, mkoani Mwanza kurudisha kadi na kuhamia Chama cha Mapinduzi
Viongozi hao wa CHADEMA waliohamia CCM, ni Mwenyekiti wa Wilaya ya Sengerema, Ayub Malima, Katibu wa wilaya, Kesi Misalaba, Katibu wa Baraza la Wanawake, Sarah Mathayo na Mwenyekiti wa Vijana, Stanslaus Pastory. Viongozi wengine ni Katibu wa Vijana, Frank Dotto, Lusia Mussa na Sayi Busumabu (wajumbe) pamoja na mwanachama mmoja wa Chama cha Wananchi (CUF), Peress Essau, ambaye mwaka 2005 aligombea ubunge katika Jimbo hilo la Sengerema.
Katika mkutano ulioandaliwa na Waziri huyo ambaye ni mbunge wa Sengerema, viongozi hao wa upinzani walieleza kuchoshwa na sera za vyama vyao kwa madai kwamba havina mwelekeo mzuri. "Nimeamua kuhamia CCM baada ya kugundua kwamba vyama vya upinzani havina shukurani. Kuna mambo mazuri yamefanywa na Serikali ya CCM kama barabara za lami lakini wao bado wanabeza mafanikio hayo. "Kwa hiyo nimeona ni bora nihamie CCM kwa chama ninachokiona kina mwelekeo na sera mzuri, nawaomba wanachama wengine wa CHADEMA muondoke huko mje CCM chama kikubwa," alisema Malima, aliyekuwa mwenyekiti wa CHADEMA katika wilaya hiyo ya Sengerema.
Kabla ya Malima kuhamia CCM kutoka CHADEMA, aliwahi kusimamishwa Machi, mwaka jana kwa barua yenye kumbukumbu Na. CDM/J/SENG/01/2011 iliyotumwa kwa Katibu wa CHADEMA wa Mkoa wa Mwanza, kwa madai ya kusababisha mgogoro ndani ya chama hicho, lakini baadaye Baraza la Uongozi wa mkoa wa CHADEMA lilitengua uamuzi huo.
Awali Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Sengerema, Jaji Tasinga Gabanyaga, aliwapongeza viongozi hao wa upinzani kwa kuhamia CCM, kwa maelezo kuwa, hali hiyo inaonesha dhahiri kwamba sera za chama tawala ni nzuri.
Kwa upande wake, Ngeleja alifurahia ujio huo wa wanachama hao wa upinzani, kwa maelezo kuwa hali hiyo inaonesha wazi kazi nzuri inayofanywa na Serikali ya Awamu ya Nne inaleta maendeleo.