Wazo Langu Umasikini usitumike kutetea polisi wabambika kesi

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,318
33,125
UKITAKA kufahamu ugumu wa kazi ya Polisi, nenda kwenye matukio ya uhalifu kama vile ujambazi. Ingawa polisi ni binadamu kama wengine, lakini yanapojitokeza matukio kama hayo yanayohatarisha usalama wao, jamii huwatazamia wawe mstari wa mbele kupambana, wakiamini kwamba wao ndio wenye dhamana ya usalama wa raia na mali zao.

Kwa kuzingatia mazingira hayo ya kazi, ndiyo maana wabunge wiki hii waliyavalia njuga maslahi ya watumishi hao, wakiitaka Serikali ihakikishe inawawekea mazingira bora ya kazi. Katika kuchangia hotuba ya bajeti iliyowasilishwa wiki hii na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Lawrence Masha, wabunge wengi walionesha kuguswa na kazi nzito wanazokabiliana nazo polisi kila siku.

Naungana na wabunge hao kuichagiza Serikali kufanya juhudi kuhakikisha, kwamba polisi wanapewa posho na mishahara inayokwenda sambamba na hali ya maisha. Hata hivyo, katika kuwatetea polisi, baadhi ya watu wamekuwa wakijenga hoja kuwa mara nyingi vitendo vya polisi kujihusisha na rushwa vinachangiwa na mazingira mabovu ya kazi.

Binafsi, ingawa nasisitiza kwamba maslahi kwa polisi ni muhimu, lakini siungani na hoja kwamba malipo kidogo ya mishahara, makazi duni au ukosefu wa posho, ni sababu rasmi za wao kutozingatia maadili ya kazi. Haipaswi kuhalalisha kwamba unyanyasaji wa raia, kuwabambikia kesi au kunyanyasa watuhumiwa, unatokana na kulipwa kidogo.

Katika kuchangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani, Kambi ya Upinzani ilikariri Taarifa ya Maendeleo ya Hali ya Umasikini (PHDR) iliyotolewa mwaka juzi, ikionesha kwamba Polisi imekithiri kwa vitendo vya kunyanyasa raia, watuhumiwa na wasio watuhumiwa. Baadhi ya polisi wamekuwa wakijichukulia sheria mikononi kwa kuwapiga wananchi na kuwafanyia vitendo viovu ikiwa ni pamoja na kuwabambikia kesi.

Kwa mfano, si ajabu kusikia mtu amekwenda Polisi kumshtaki mwingine, lakini baada ya kufika Polisi, aliyekwenda kushtaki ndiye ‘anageuziwa kibao’ na kuitwa mhalifu kutokana na mtuhumiwa kuhonga askari. Imefikia hatua baadhi ya polisi wanatumia vituo kama sehemu ya kujadili malipo ya hongo bila woga wowote. Wapo wanaotuhumiwa kuingia ubia na watu wenye fedha wakiwamo majambazi na kutumia ubia huo kuwanyanyasa wanyonge wanaokwenda kusaka haki yao.

Kutokana na nafasi ya jeshi hili, hata baadhi ya raia wanaofahamu haki zao, wamekuwa wakikumbana na vizingiti wakati wakifuatilia haki zao kutokana na kutishiwa kuswekwa ndani au ‘kutengenezewa’ kesi. Hata wasomi ambao wanatarajiwa kuwa pengine wangekuwa mstari wa mbele kutambua haki zao na kuwanusuru wasio na elimu, pia wamekuwa wakijikuta wakinyanyaswa kwa namna mbalimbali na Polisi.

Niliwahi kushuhudia watu wawili waliokuwa wamekorofishana na suala lao likafikishwa Polisi, lakini baadaye mmoja wao alikwenda Polisi kufuta kesi hiyo ambayo haikuwa na jinai ndani yake. Hata hivyo polisi aliyekuwa anahusika, alikataa katakata kuifuta akishinikiza apewe fedha kwanza.

Alikuwa akihalalisha usemi wa ‘kuingia Polisi ni bure lakini kutoka ni kwa pesa.’ Ingawa upande mwingine wa sarafu, jamii pia inatakiwa kulaumiwa kwa kutofahamu au kuthamini haki zao, lakini bado hali hiyo pia haiwahalalishi askari hao wachache kutowajibika kulingana na maadili ya taaluma yao.

Izingatiwe, kwamba maslahi duni si kwa polisi pekee, bali pia watumishi wengine. Lakini isitoshe ndani ya Jeshi hilo hilo, wapo waadilifu wanaoishi kwa mshahara huo mdogo. Iweje baadhi watumie mwavuli wa mazingira duni kukiuka maadili?

Napongeza hatua za kuwafukuza kazi askari 46 waliobainika kwenda kinyume na kazi hiyo tangu Julai mwaka jana hadi Machi mwaka huu. Naishauri Serikali inapoangalia uwezekano wa kuboresha maslahi ya Polisi, vile vile iendelee na mkakati wake wa kuwaweka kando askari watovu wa nidhamu.

HabariLeo | Umasikini usitumike kutetea polisi wabambika kesi
 
Back
Top Bottom