Watu Wenye Ulemavu Wanastahili Kuwezeshwa Kutumia Fursa za Teknolojia ya Digitali

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
Ujumuishaji wa Kidigitali.PNG

Dunia inapitia mapinduzi ya kidigitali yenye uwezo wa kuharakisha utatuzi wa matatizo katika jamii, hivyo kuwezesha watu na jamii kwa ujumla kustawi.

Teknolojia na ufikiaji nafuu wa intaneti vinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuondoa utofauti mkubwa wa kijamii uliopo. Teknolojia na intaneti vinawawezesha watu kupata elimu, kazi, kufikia huduma za kifedha pamoja na huduma za afya.

Vitu hivi vinaweza kumsaidia mtu yeyote kupata ujuzi na fursa zinazohitajika ili kustawi, na uwezekano wa kupata nafasi ya kuwa mtatuzi wa changamoto katika jamii. Hata hivyo, kundi moja lipo katika hatari ya kuachwa nyuma katika mapinduzi ya kidigitali; kundi hilo ni watu wenye ulemavu.

Takriban 15% ya idadi ya watu duniani, zaidi ya watu bilioni 1, wanaishi na aina fulani ya ulemavu. Watu wenye ulemavu wana changamoto za kuwa na afya duni, mafanikio ya chini ya elimu, ushiriki mdogo wa kiuchumi na viwango vya juu vya umaskini kuliko watu wasio na ulemavu.

Umoja wa Mataifa unasema ukosefu wa ajira miongoni mwa watu wenye ulemavu umefikia asilimia 80 katika baadhi ya nchi. Lakini pia, watu wengi wenye ulemavu ambao wameajiriwa hufanya kazi katika nafasi za muda au kazi zisizo za kawaida, za malipo ya chini na usalama duni wa kazi.

Hata hivyo, tunaamini teknolojia na upatikanaji wa ujuzi wa kidigitali unaweza kusawazisha uwanja kwa watu wenye ulemavu. Kusaidia watu wenye ulemavu kukuza ujuzi wa kidigitali ambao ni muhimu sana katika dunia ya leo kunaweza kuwatengenezea fursa mpya na kuwafanya wajihisi kuwa sehemu muhimu ya jamii yao.

Watu wengi wenye ulemavu hasa katika nchi za kipato cha chini hawana ufahamu wa zana zinazopatikana mtandaoni na jinsi zinavyoweza kutumika, na hata kama wanafahamu basi wanaweza kuwa na changamoto ya kutozifikia (access) au kutoweza kuzitumia. Hivyo basi, kuhakikisha kwamba watu wenye ulemavu wanaweza kuzitumia ipasavyo ni muhimu ili kuhakikisha ushiriki wao mtandaoni, jambo litakalowawezesha kupaza sauti zao na kuchangamana na dunia.

Ili kuhakikisha ushirikishwaji mzuri wa taarifa kwa ya watu wenye ulemavu, maudhui yanapaswa kutayarishwa na kuwasilishwa kupitia njia zilizo rafiki kwa watu wa kundi hili. Kufanya ushiriki kuwa rahisi kwa walemavu katika ulimwengu wa kidigitali ni mojawapo ya namna za kuwatimizia haki yao muhimu ya kibinadamu.

Watu wenye ulemavu wataendelea kukandamizwa na kuachwa nyuma ya wakati endapo wataendelea kukosa uwezo wao wa kujihusisha na huduma za kidigitali, hivyo kuna umuhimu wa serikali na asasi za kiraia kubuni na kutoa huduma kwa njia tofauti ili kujumuisha zaidi watu wenye ulemavu.

Ujumuishaji wa Kidigitali (digital inclusion) unapaswa kutomwacha mtu yeyote nyuma. Hii itasaidia kukuza maendeleo jumuishi bila kuacha mtu yeyote nyuma.
 
Back
Top Bottom