Wadau wa Haki za Binadamu kuja na tafiti inayolenga kuwasaidia watetezi wa watu wenye ulemavu nchini

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Wakati wadau mbalimbali wakifanya jitihada tofauti za kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu nchini, Watetezi wa watu wenye ulemavu wamedaiwa kukabiliwa na changamoto zinazotajwa kuwa kikwazo kwa taasisi zao kukua pamoja na watetezi hao kutofikia malengo yao kwa wakati.

Changamoto hizo zimegusiwa na baadhi ya wadau Novemba 14, 2023 Jijini Dar es salaam wakati wa kikao cha kujadili masuala mbalimbali ambayo yaliyoibuliwa kwenye taarifa ya tafiti inayomulika mazingira yanayokabili wadau hao.

Akizungumzia baadhi ya Changamoto Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa haki za binadamu, Wakili Onesmo Olengurumwa amesema kuwa Watetezi wa watu wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto zaidi ikilinganishwa na Watetezi wengine katika maeneo tofauti, amesema kuwa Watetezi wengi wenye ulemavu miundombinu bado haiwawezeshi kufika kwenye ofisi mbalimbali, ambapo ametolea mfano Watetezi wenye ulemavu wa miguu.

Amesema kuwa pia bado jamii na wadau awajahamasika kuwaunga mkono zaidi watu wenye ulemavu, amedai kuwa changamoto hizo kwa ujumla wake zimepelekea taasisi za Watetezi wenye ulemavu na Watetezi wa kujitegemea kushindwa kupata rasilimali za kuwawezesha kufanikisha malengo ya utetezi.

Pia Mwenyekiti wa Shirikisho la Watu wenye ulemavu Tanzania, Ernest Kimaya amesema kuwa tafiti za aina hiyo wanazichukua kwa uzito kwa sababu inasaidia kuonesha umuhimu wa watetezi wa watu wenye ulemavu.

"Tafiti iliyofanywa imelenga kila sekta ambayo kila mmoja anatamani tuwe kwenye haki na itaenda kusaidia kuona umuhimu wetu katika Taifa" amesema.

Amesema kumekuwepo na changamoto ya kuzingatia miongozo ambayo hipo hasa kwa watendaji wa ngazi za chini, licha ya viongozi wa ngazi za juu Serikalini.

Ofisa Mkuu wa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Waziri Mkuu, Vijana na Watu Wenye ulemavu, Joy Maongezi, kwa niaba ya Mkurugenzi Watu wenye ulemavu kutoka ofisi hiyo, amesema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa tafiti za wadau katika jitihada za kuandaa sera, sheria na kanuni kanuni mbalimbali zinazolenga watu wenye ulemavu.

"Bila kufanya Tafiti hatuwezi kupata takwimu sahihi ili kufanya kazi, hivyo kupitia ripoti hiyo itasaidia kuona ni kwa namna gani tunaweza kufanya majukumu yetu kwa usahihi katika kukabiliana na changamoto za watu wenye ulemavu" amesema Ofisa huyo.

Aidha amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kwa kushirikiana na wadau katika kuboresha mazingira ya watu wenye ulemavu ikiwemo kuwawezesha kiuchumi na kuchua hatua kwa wahusika ambao wamekuwa wakidaiwa kuwatumia vibaya watu wenye ulemavu.

Tafiti hiyo imeelezwa kugusia changamoto mbalimbali za kisheria, changamoto za kitaasisi, wadau pamoja na jamii ambapo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni Zanzibar mara baada ya mchakato wa kuiandaa kukamilika.

Ambapo tafiti hiyo inatazamiwa mara baada ya kuzinduliwa itasaidia kupunguza kuonesha changamoto zilizopo na kuleta suluhu kwa baadhi ya changamoto baada ya uwajibikaji.
 
Back
Top Bottom