Ubaya haulipwi kwa ubaya, bali ubaya hulipwa kwa wema. Ikitokea umekutana naye, msalimie kiroho safi kabisa, na ikitokea kapata matatizo, au kakwama, hana msaada wowote, na kwamba amekata tamaa, wewe jitokeze na umpe msaada. Hakika hapo utakuwa kama umemuunguza na kaa la moto, lakini wakati huohuo wewe unapata thawabu kwa Mungu.
Habari ya kulipiza kisasi achana nayo na wala usiifikirie kabisa. Kulipiza kisasi sio suluhisho, unaweza ukaongeza tatizo juu ya tatizo. Labda utauliza kivipi? Binadamu yeyote ameumbwa na roho ya huruma (hata awe jambazi). Sasa ukiamua kumdhuru kwa namna yoyote ile huyo mbaya wako, unaweza kumuathiri kiasi cha kuharibu viongo vyake au hata kifo. Umesema unatamani umpe hata sumu, je akifa, na pengine familia yake (mke, watoto, nk) wanamtegemea yeye, watoto wakianza kutaabika kutokana na kukosa malezi, huoni kama hili litakuathiri kisaikolojia? Utakuwa umejiongezea tatizo badala ya kupunguza!