Watoto maelfu wanaofaulu la saba hawafiki Sekondari

Watoto maelfu wanaofaulu la saba hawafiki Sekondari

UTPC

Journalists' Union
Joined
Apr 17, 2026
Posts
45
Reaction score
30
Katika eneo la soko lililochangamka la Kata ya Kazuramimba, Wilayani Uvinza mkoani Kigoma, sauti za vicheko na vishindo vya furaha vinavyotoka ndani ya skrini za runinga vinapotezea mwelekeo wa watoto wenye umri kati ya miaka 12 na 17.
2 (1).jpg
Wakati kengele za shule zikilia kuwaita wanafunzi madarasani, vijana hawa wadogo wao wanashinda kutwa nzima ndani ya vibanda 14 vya kurusha filamu, maeneo matatu ya michezo ya watoto (gaming stations) na ubashiri, au wakizurura mitaani wakiuza mayai ya kuchemsha na biashara ndogondogo.

Taswira hii ya kuhuzunisha, inafichua uwepo wa tatizo kubwa la wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi lakini wanashindwa kuendelea na elimu ya sekondari, hali inayotishia mustakabali wa nguvu kazi ya taifa na kuwaacha watoto hawa wakiangalia dunia kupitia matundu ya ukosefu wa maarifa, huku mamlaka zinazohusika zikiendelea kukaa nyuma ya makaratasi ya takwimu ofisini.

Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala hii unaonesha kuwa idadi kubwa ya wanafunzi wanaoshindwa kujiunga kidato cha kwanza katika wilaya ya Uvinza, wanashinda kwenye vibanda hivyo vya filamu na michezo ya kubashiri, na wengine wakifanya biashara ndogondogo kama uuzaji wa mayai, karanga na mifuko katika eneo la soko na wengine wakifanya kazi za majumbani ndani na nje ya mkoa wa Kigoma, na wapo wanaoishia kufanya mashambani.
Screenshot 2026-10-20 144324.png

Baadhi ya watoto wakiwa kwenye vibanda vya michezo ya kubashiri katika Kata ya Kazuramimba, Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, mkoani Kigoma hivi karibuni.
PICHA: ADELA MADYANE
​

Kifungu cha 41 cha Sheria ya Michezo ya Kubahatisha ya mwaka 2019 kinakataza watoto chini ya miaka 18 kushiriki katika michezo hiyo, huku kikiweka adhabu ya faini ya kati ya shilingi milioni moja hadi tano au kifungo cha hadi miezi sita kwa mhusika; hata hivyo, utekelezaji wake umekuwa ni kitendawili.

Richard Kimaro, meneja masoko kutoka bahati nasibu ya taifa anaeleza kuwa husimamia utekelezaji wa sheria hiyo kupitia leseni wanazozitoa kwa waendeshaji wa michezo hiyo ili kuhakikisha mtoto hashiriki kwa namna yoyote ile.

Vilevile ameeleza kuwa hutumia njia ya kutoa taarifa kupitia namba za simu wanazotoa katika jamii ili kuwapatia taarifa kuwa watoto wanaruhusiwa katika michezo ya kubahatisha na mwenye leseni katika eneo fulani, japo hajaeleza wazi hatua walizokwisha chukua kwa wamiliki wanaohusisha watoto katika michezo ili wajipatie pesa.

Kwa upande wake Sera ya Elimu ya mwaka 2024 toleo la mwaka 2023 ibara ya 3.1.1.5, inabainisha kuwa, elimu ya lazima inajumuisha elimu ya msingi na elimu ya sekondari kidato cha kwanza mpaka cha nne, ambapo itatolewa kwa jumla ya miaka 10.

Lengo namba nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), linaelekeza mataifa kuhakikisha kuwa watoto wote, wa kike na kiume, wanakamilisha elimu ya msingi na sekondari ambayo ni bure, yenye usawa, na ubora ifikapo mwaka 2030.

Hata hivyo, takwimu za Ofisi ya Elimu Idara ya Sekondari wilayani Uvinza zinaonesha kuwa kwa miaka mitano mfululizo, kuanzia 2021 hadi 2025, zaidi ya wanafunzi 5,000 sawa na asilimia 20 ya wanafunzi wanaofaulu kujiunga na kidato cha kwanza wamekuwa hawaripoti shuleni kabisa.

Takwimu hizo zinaonesha mwaka 2022, wanafunzi 7,702 walifaulu, lakini walioripoti shuleni walikuwa 5,745 pekee (asilimia 74.5), mwaka 2023, wanafunzi 6,353 walichaguliwa, walioripoti walikuwa 5,690 (asilimia 89.54), mwaka 2024, kati ya wanafunzi 6,268 waliopangiwa, walioripoti walikuwa 4,702 tu (asilimia 75.02) na mwaka 2025, wanafunzi 6,317 walichaguliwa kuanza kidato cha kwanza lakini wanafunzi 4,827 pekee ndio walioripoti (asilimia 76.41).

Hali ilizidi kuwa mbaya mwanzoni mwa mwaka huu, ambapo ripoti ya elimu ya mwaka 2025/2026 iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinna Mathamani, katika kikao cha wadau wa elimu mnamo Machi 2026, ilionyesha kuwa hadi mwanzoni mwa mwezi huo, zaidi ya asilimia 49 ya wanafunzi waliopaswa kuanza kidato cha kwanza walikuwa bado hawajaripoti shuleni.

Kulingana na takwimu hizo jumla ya wanafunzi 5,696 katika wilaya ya Uvinza wameshindwa kujiunga kidato cha kwanza katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Idadi hiyo ingeweza kutosha kujaza shule za msingi 126 zenye darasa moja moja la kwanza hadi la saba, huku kila darasa likiwa na wanafunzi 45.

Wilaya ya Uvinza ina jumla ya sekondari 29, kati ya shule hizo mbili za watu binafsi na 27 za serikali.

Wakazi wa wilaya ya Uvinza wanasema wimbi la wanafunzi wanaofaulu darasa la saba na kushindwa kujiunga na kidato cha kwanza limekuwa ni tatizo kubwa. Mmoja wa wakazi hao, Thomas Roman, mkazi wa Kazuramimba na ambaye amewahi kuwa kiongozi wa kijiwe cha bodaboda, anaeleza kuwa wimbi la watoto katika vibanda vya filamu na kuzurula katika maeneo ya masoko limehamia huko baada ya kuondolewa kwenye vijiwe vya bodaboda kutokana na kuwa na umri chini ya miaka 17.

“Hivi sasa wapo watoto zaidi ya 40 wanaouza mayai na kuzurura mitaani, ambao tuliwaondoa katika bodaboda, maana walikuwa hawawezi kumudu pilikapilika za barabarani kutokana na umri wao,” alisema Roman.

Ripoti ya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma ya Machi 2025 inaonesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya watoto mkoani humo wanakosa malezi sahihi, hali inayochochea utoro, mimba na ndoa za utotoni. Katika Kata ya Kazuramimba, athari hizi zimeanza kujionesha kwa vitendo vya kikatili dhidi ya watoto wa kiume.

Mwananchi mmoja wa Kazuramimba ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu za kiusalama anafichua kuwa kuna mtu anayewarubuni vijana wadogo kuwa atawabadilishia maisha kisha kuwafanyia vitendo vya ukatili wa kijinsia baada ya kuwahadaa kwa nguvu za kifedha. Mtu huyo anadaiwa kuhamia eneo hilo akitokea Nguruka baada ya kufukuzwa kutokana na tabia hizo.

Kauli hiyo inathibitishwa na kijana Ernest Daudi (si jina lake halisi), muathirika wa vitendo vya ukatili mwenye umri wa chini ya miaka 18 kwa sasa, anayeeleza namna alivyokaribishwa kwenye mtego huo kwa ahadi ya kununuliwa pikipiki kabla ya kupata maumivu na makovu ya kisaikolojia yaliyomfanya ajichukie. Licha ya mkasa huo, alijinasua na kujiunga na masomo ya ufundi katika Chuo cha VETA ili kujitegemea.

Akizungumzia hali hiyo, Mchungaji Elias Joshua wa Kanisa la Free Pentecost Church of Tanzania (FPCT) kata ya Kazuramimba anatahadharisha kuwa jamii inatengeneza kizazi kisichothamini elimu ambacho kitaishia kwenye uhalifu, unywaji pombe, uvutaji bangi na kucheza kamari.

Mtazamo huo unasisitizwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha Kazuramimba, Moshi Kamlonga, anayebainisha kuwa ukosefu wa elimu utaiacha jamii katika lindi la umaskini wa kutupwa.

Kwa upande wake, Ofisa wa Idara ya Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kigoma, Msafiri Nzunuri, anakiri uwepo wa changamoto hiyo ya uchelewaji wa wanafunzi kuanza kidato cha kwanza, huku akisisitiza kuwa umasikini wa wazazi haupaswi kuwa kisingizio cha kuwanyima watoto haki yao ya msingi ya kupata elimu.

Kwa upande wa Adrian John mmoja wa waajiriwa katika vibanda vya kurusha filamu anadai yeye hajui kama watoto hawaruhusiwi katika maeneo yao, na kwamba yeye huwapokea kwakuwa yupo katika kazi hiyo kufanya biashara na lazima kila siku akabidhi kiasi cha shilingi elfu 10,000 kwa mwajiri wake.

Wimbi hili la wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza kushindwa kuripoti shuleni wilayani Uvinza ni donda ndugu linalotishia mustakabali wa taifa. Wakati viongozi na jamii wakiendelea kulalamikia ugumu wa maisha na jiografia, vizazi vya kesho vinaangamia kupitia utoro, ajira hatarishi, na ukatili wa kinyama. Kama hatua za dharura hazitachukuliwa kulinda nguvu kazi hii, Uvinza itaendelea kuzalisha jamii ya wajinga, maskini, na inayotawaliwa na lindi la kukosa maarifa.

Sehemu ya pili ~ Miundombinu inavyochochea maelfu ya watoto Uvinza kukosa kidato cha kwanza

Makala hii ni mfululizo wa makala tatu za uchunguzi juu ya changamoto ya mdondoko wa wanafunzi kutoka shule ya msingi kuelekea sekondari wilayani Uvinza, mkoani Kigoma, makala ya hii imeeleza ukubwa wa tatizo, makala ya pili itajikita kujua sababu za tatizo na makala ya tatu itatoa suluhisho la kudumu la kumaliza chagamoto hiyo.

ANDIKO LA: Adela Madyane – Kigoma
Makala imeandaliwa na Mwandishi anayeshiriki katika programu maalum ya kukuza uandishi wa maslahi kwa umma (Public Interest Journalism Fellowship) inayoratibiwa na UTPC kwa kushirikiana na IMS.
 
Kwa hio huko kigoma tiiiviiii ndio kila kitu mpaka mtoto anakacha shule? Tuna safari ndefu sana
 
Back
Top Bottom