Hii ameandika Prof. Joseph Mbele ...
Warsha Zangu Hazina Posho
Tangu mwaka juzi, nimeendesha warsha Tanzania, kuhusu masuala ya utamaduni, utandawazi, na maendeleo. Nina malengo kadhaa katika kufanya hivyo.
Lengo moja ni kuwapa wa-Tanzania ujuzi ambao ninaendelea kuupata huku ughaibuni, kutokana na kusoma vitabu, kuongea na watu, na kuendesha warsha kuhusu masuala niliyotaja hapo juu. Natambua umuhimu wa kutoa fursa kwa wa-Tanzania kuyaelewa masuala hayo, waweze kujizatiti kwa ushindani wa dunia ya leo. Hakuna msingi bora na imara kuliko elimu.
Lengo la pili la kuendesha warsha hizi Tanzania ni kuleta mwamko mpya katika mfumo na uendeshaji wa warsha. Kwanza, kuna mtindo wa kutegemea wafadhili. Watu wamezoea kuona warsha zikifanyika kwa kutegemea fedha kutoka kwa wafadhili au taasisi fulani. Wahudhuriaji wa warsha wanategemea kulipiwa gharama za ushiriki, pamoja na posho. Vibahasha vya posho ni sehemu ya utamaduni wa warsha katika Tanzania.
Ninapinga utamaduni huu. Sitafuti wafadhili wa kulipia warsha zangu, na warsha zangu hazina posho. Badala yake, wanaohudhuria wanalipia.
Kwa mtazamo wangu, warsha ni fursa ya kujielimisha. Elimu ni mtaji mkubwa, pengine muhimu kuliko mitaji yote. Kama mtu analipia trekta limzalishie mazao shambani, kwa nini asilipie mtaji huu mkubwa kuliko yote, yaani elimu?
Huku Marekani, ninaona utaratibu huu wa kulipia warsha. Mimi mwenyewe nimeshalipia hela nyingi kuhudhuria warsha hizi. Ninajua umuhimu wake. Niligusia kidogo jambo hili katika blogu hii, nilipoongelea suala la
kununua vitabu.
Ninanunua pia vitabu na kuvisoma. Kati ya vitabu nilivyonunua hivi karibuni ni
Global Literacies. Kwa kusoma vitabu na kuhudhuria warsha, ninajiongezea mtaji wa elimu. Ufanisi wangu kama mtoa mada na mwendesha warsha unaendelea kuongezeka.
Katika kuendesha warsha zangu Tanzania, nataka kujenga utamaduni wa kuthamini elimu. Msimamo huu unanipa wajibu mkubwa. Nawajibika kujielimisha kwa uwezo wangu wote, ili niweze kuwa mwelimishaji bora. Ndio maana ninafanya bidii kuhudhuria warsha, kununua vitabu na kuvisoma, na pia kuendesha warsha. Ninaelimika hata ninapoendesha warsha.
Nawakaribisheni kwenye warsha zangu za mwaka huu: