DOKEZO Watanzania tuliositishiwa ajira Sisalana Cordage Factory (Tanga) tunaendelea kuteseka, Rais Samia sikia kilio chetu

Hili ni dokezo maalum toka kwa mwananchi mtumiaji wa JF mwenye nia ya kuusaidia umma kuwa na taarifa 'maalum'
A

Anonymous

Guest
659d25a7-bc7a-421a-86df-03cd07d3b3ed.jpeg
Mimi ni Mkazi wa Muheza, Kijiji cha Ngomeni, Kambi ya Mikoroshini Mkoani Tanga, tunaomba Serikali Kuu na Mamlaka zenye nafasi ya kutusaidia kufikisha salamu kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie tupate haki zetu za kazini ambazo zinaminywa na zinapotea hivihivi.

Tunateseka sana na unyanyasaji unaoendelea kwetu tunaofanyiwa na Kampuni tanzu ya NSSF inaitwa Sisalana Cordage Factory, ambapo NSSF aliahidi kutulipa mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka juzi (2021) alipokuja hapa kiwandani Ngomeni.

Kampuni ya Sisalana Cordage Factory inatuamuru tuhame kwenye nyumba za kampuni wakati haijatulipa stahiki zetu kama tulivyokubaliana, pia wametusitishia Huduma ya Umeme tangu tarehe 27/01/2023, tupo gizani.

Maisha yetu yanaendelea zaidi kuwa hatarini wakati wa usiku na kuongeza ugumu, matokeo yake kumekuwa na matukio ya wizi, wadudu hatari kuvamia makazi zetu na vingine vingi.

Kampuni ya Sisalana inayojihusisha na Katani ilitaifishwa na Serikali Mwaka 2021 baada ya kushindwa kulipa mkopo.

Baada ya hapo baadhi ya Wafanyakazi wakabaki kwenye Kampuni wengine 100 tukaachishwa kazi, tukakubaliana kuwa watatulipa stahiki zetu za kusitishiwa ajira, mishahara ya miezi 8 ambayo tunadai pamoja na malipo yetu ya NSSF, kinachotuuma ni kuwa vyote hivyo hatujalipwa.

Jambo lingine ambalo linakera ni suala la Chama cha Wafanyakazi kutotupa ushirikiano wakati huu tukiwa kwenye mateso kwa madai kuwa hatupo kwenye ajira, lakini wanadai ikitokea tukalipwa fedha za Mishahara ya miezi 8 tunayofai etu watataka kutoa kiasi ili tuwalipe, hiyo ni haki kweli?

Nimeambatanisha na sehemu ya taarifa yetu ambayo tuliipeleka kwenye vyombo vya habari na hapa iliandikwa na Gazeti la Mtanzania (Mei 11, 2023) lakini mpaka leo hakuna hatua zilizochukuliwa kutusaidia.

Tunaandika kwa kuandika hapa Jamii Forums ujumbe wetu unaweza kufika kwa Rais Samia na ukafanyiwa kazi kwa haraka.
2a239688-098c-4d7e-aad4-961672e4b0cf.jpeg
***

Waliokuwa wafanyakazi Tancoard waiomba Serikali kuweka zuio wasiamishwe

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
WALIOKUWA wafanyakazi wa kampuni ya Tancoard ambayo kwa sasa inaitwa Sisalana Cordage Factory wameiomba Serikali kuingilia kati suala la notisi ya kuhama ili wasihamishwe kwenye nyumba za kampuni hadi watakapolipwa stahiki zao.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Mei 11, na waandishi wa habari kwa niaba ya wafanyakazi wenzake Moses Shekalaghe amesema walio kuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo wanaishi kambi ya mikoroshini, kata ya Ngomeni Wilaya ya Muheza mkoani Tanga hawajalipwa mishahara na malimbikizo yao tangu mwaka 2018.
a5b69632-d1ba-4880-b479-aa8b3112de1d-1024x624.jpg
“Kampuni hiyo ilikuwa na zaidi ya wafanyakazi 120 ambao wanadai haki zao za kazini ikiwemo mishahara na malimbikizo mengine, na kuna wafanyakazi 100 wamesimashiwa kazi mpaka sasa bila malipo,”amesema Shekalaghe.

Amesema Januari 26, mwaka huu walipewa notisi ya kuhama katika nyumba za kampuni kinyume cha sheria pamoja na makubaliano waliyoingia wakati wanaanza kazi katika kampuni hizo.

Aidha Shekalaghe amesema wanaiomba kampuni hiyo ifuate haki na taratibu na sheria ilivyoanishwa katika katiba ya nchi sheria ya ajira na mahusiano kazini, pamoja na mikataba ya kimataifa ya haki za Wafanyakazi.

Mtanzania Digital ilimtafuta kwa njia ya simu Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Sisalana Cordage Factory, Elizabeth Kalambo ambapo amesema kampuni hizo mbili ni tofauti na Sisalana haihusiki inayohusika ni Katani Limited na Tancoard.

Amesema ni kweli walipewa notisi na walitoa tangazo waachie nyumba hizo na sasa wamepewa notisi ya pili kisheria hawatakiwi kuwepo pale ni ubinadamu tuu.

“Kesi yao ipo Mahakamani na hairuhusiwi kuzungumzia kisheria vitu vikifika mahakamani tunachia Mahakama,” amesema Kalambo.
 
Back
Top Bottom