Wasomali 90 na Wakenya wawili watimuliwa Marekani - BBC Swahili
Raia takriban 90 wa Somalia na wawili wa Kenya wametimuliwa kutoka Marekani saa chache baada ya taarifa kuibuka kwamba Rais Donald Trump atakabiliana na watu wanaoishi nchini humo kinyume cha sheria.
Wote waliwasili katika uwanja wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi, lakini baadaye raia wa Somalia wakaendelea na safari hadi uwanja wa ndege wa Aden Abdulle mjini Mogadishu.
Msemaji wa serikali ya Kenya Eric Kiraithe ameambia BBC kwamba ni kweli raia hao wamefukuzwa Marekani, ingawa hakusema iwapo hatua hiyo imetokana na msimamo wa Bw Trump..
"Ni watu 90 kulingana na habari ambazo tulipewa. Wakati unaondolewa nchi fulani kurejeshwa kwenu, huwa unarejeshwa hadi kwenu," ameambia BBC.
Kuhusu sababu iliyowafanya kufurushwa, Bw Kiraithe amesema: "Inategemea sheria za nchi ambayo walikuwa wamehamia (Marekani),"
Trump kuwazuia wahamiaji kuingia Marekani
Watakaoumia na watakaofaidi chini ya Trump Marekani
Bw Trump alisema Jumatano itakuwa siku muhimu kwa usalama wa Marekani.
Anatarajiwa kuweka masharti makali kwa raia wa mataifa saba ya Mashariki ya Kati na Afrika yenye idadi kubwa ya Waislamu wanaotafuta viza za kwenda Marekani.
Taarifa zinasema nchi hizo ni Syria, Iraq, Iran, Libya, Somalia, Sudan na Yemen.