Elias Msuya
Senior Member
- Dec 23, 2011
- 173
- 671
Jamii Forums inakuletea wasifu wa wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano kwa mwaka huu 2025. Tutaendelea kutoa nafasi kila wasifu unapopatikana kupitia uzi huu.
1. Mgombea urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan- Wasifu
Samia Suluhu Hassan aliyezaliwa Januari 27, 1960, Zanzibar sehemu ya, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo tangu mwaka 2021.
Alishika wadhifa huo kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Hayati Rais John Magufuli aliyefariki Machi 17, 2021.
Aliingia madarakani kwa matumaini makubwa ya Watanzania ya kujenga mfumo wa demokrasia uliokuwa ukilalamikiwa na mtangulizi wake, akibeba falsafa yake ya “4Rs” yaani, maridhiano, ustahimilivu, mageuzi, na ujenzi mpya.
Hata hivyo, kwa miaka mine aliyokaa madarakani, amekuwa akikosolewa kwa kufifisha matumaini hayo, ambapo utawala wake unalaumiwa kwa kukandamiza uhuru wa maoni, kukithiri kwa matukio ya watu kutekwa na kupotea na vyama vya upinzani kudhibitiwa.
Januari 2025, alipitishwa na Chama cha Mapinduzi kuwa mgombea urais katika uchaguzi mkuu na endapo atashinda, ataendelea kutawala hadi mwaka 2030.
Maisha ya awali
Samia alizaliwa Zanzibar mwaka 1960, miaka minne kabla ya visiwa vya Uguja na Pemba (Zanzibar) kuungana na Tanganyika kuunda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alipata elimu ya msingi katika shule mbalimbali, zikiwemo Shule ya Msingi Chwaka iliyoko Unguja kuanzia 1966 hadi 1968, Shule ya Msingi Ziwani mwaka 1970 na Shule ya Msingi Mahonda mwaka 1972. Baada ya hapo, alijiunga na Shule ya Sekondari ya Ng’ambo kwa ajili ya masomo ya Kidato cha Kwanza hadi cha tatu, na Shule ya Sekondari Lumumba kwa ajili ya Kidato cha Nne kati ya mwaka 1973 hadi 1976.
Mwaka 1983, alipata astashada katika mafunzo ya takwimu kutoka Chuo cha Uchumi, Zanzibar. Baada ya kufanya kazi kwa kipindi kifupi kwenye Wizara ya Mipango na Maendeleo, mwaka 1983 hadi 1986, alijiunga na Chuo cha Maendeleo ya Uongozi Mzumbe (IDM) kwa ajili ya masomo ya juu katika Utawala wa Umma.
Mwaka 1987 hadi 1988, alikuwa Afisa Mipango Rasilimali Watu na Mwaka 1977 hadi 1983, Karani Masijala.
Aidha, alipata mafunzo mbalimbali katika Taasisi ya Chuo cha Utawala wa Umma Lahore, Pakistan 1987, Taasisi ya Eastern and Southern African Management Institute (ESAMI) 1991, na Taasisi ya Uongozi ya Hyderabad India 1998 kwa ajili ya Astashahada ya Utawala.
Baada ya hapo, alijiunga na Chuo Kikuu cha Manchester kilichopo Uingereza kwa ajili ya masomo ya Juu ya Uchumi. Vilevile, alipata Shahada ya Uzamili ya Maendeleo ya Jamii kupitia programu ya pamoja kati ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania na Chuo Kikuu cha Southern New Hampshire, Marekani.
Aliolewa na Hafidh Ameir mwaka 1978, na wamejaliwa watoto wannne wakiwamo wa kiume watatu.
Kupanda Kisiasa
Hassan, ambaye ni mwanachama wa muda mrefu wa chama tawala cha Tanzania, Chama Cha Mapinduzi (CCM), alianza safari yake ya kisiasa aliposhinda kiti cha Baraza la Wawakilishi Zanzibar na kuteuliwa kuwa Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira, Maendeleo ya Wanawake, na Watoto (2000/2005).
Mwaka 2005 alichaguliwa tena na kuteuliwa kuwa Waziri wa Utalii, Biashara na Uwekezaji katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, akiwakilisha jimbo la Makunduchi na kisha akateuliwa kuwa Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia mambo ya Muungano (2010/2015).
Mwaka 2014, alihudumu kama Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kuandaa rasimu ya Katiba mpya ya Tanzania.
Uzoefu ndani ya CCM
Samia aliingia katika siasa kama mwanachama wa CCM, Juni 10, 1987. Aliingia katika siasa za uchaguzi mwaka 2000 katika nafasi ya Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Zanzibar kama Mwakilishi wa Viti Maalum vya Wanawake hadi mwaka 2010. Kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, aligombea na kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwakilisha jimbo la Makunduchi, Zanzibar.
Mwaka 2002, alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi, na vile vile, kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi; nyadhifa ambazo ameendelea kuzifanyia kazi hadi leo. Ndugu Samia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Kusini Unguja; na alikuwa Mjumbe wa Kamati za Siasa Mkoa na Wilaya ya Kusini Unguja.
Kwa upande wa Jumuiya za Chama cha Mapinduzi, Ndugu Samia ni mwanachama wa Jumuiya ya Wanawake wa Tanzania (UWT) kuanzia mwaka 1996 hadi leo. Aidha, ameshiriki katika kuandika Ilani ya Chama cha Mapinduzi mara nne mfululizo kuanzia 2005/2010, 2010/2015, 2015/2020 na 2020/2025.
Uhusiano na taasisi nyingine
Mwaka 2016, Mhe. Samia aliteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, kuwa Mjumbe wa Jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu Uwezeshaji wa Wanawake Kiuchumi, akiwakilisha Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kati ya mwaka 2016 na 2017.
Katika kipindi cha ujumbe wake, aliwasilisha mambo 27 kwenye Jopo hilo, ambayo Serikali ya Tanzania ilibainisha kama hatua za kimkakati kwa ajili ya kuweka mfumo endelevu wa kufikia usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi.
Miongoni mwa matokeo ya kazi zake ni kusimamia uanzishwaji wa majukwaa ya uchumi ya wanawake nchini kwa lengo la kuwaunganisha wanawake wafanyabiashara wadogo na wakati kwenye masoko, hasa wanawake wanaoishi mipakani, kuwaunganisha na mikopo nafuu na kuhimiza mafunzo ya ujasiriamali; na kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kuanzisha kampeni ya kuongeza uwajibikaji katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto, maarufu kama “Jiongeze Tuwavushe Salama”.
Samia wamewahi kufanya kazi na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (World Food Programme) mwaka 1988 hadi 1997.
Vilevile, amefanya kazi katika Kamati, Bodi na Taasisi mbalimbali kama vile; Mjumbe wa Kamati ya Msamaha wa Wafungwa (Parole Committee) ya Zanzibar (2001- 2010), Mlezi wa Jumuiya ya Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Zanzibar (1997-2000), Mjumbe wa Bodi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote – EOTF (1996-2000), Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Taasisi zisizo za Kiserikali Zanzibar (ANGOZA) 1995-2000, Mwanachama wa Lions Club Zanzibar (1991-1998), Mjumbe wa Kamati ya Uundaji wa Sera ya Elimu Zanzibar (1996) na Mwanachama Mwanzilishi wa Taasisi ya Kuchochea Maendeleo ya Wanawake Zanzibar (1991-1994).
Makamu wa Rais
Umaarufu wa Hassan uliongezeka baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais wa CCM pamoja na John Magufuli katika uchaguzi wa Oktoba 2015. Walishinda uchaguzi huo, na Samia akaapishwa kuwa Makamu wa Rais Novemba 5, 2025. Hii ilikuwa mara ya kwanza kwa mwanamke kushika wadhifa huo.
Yeye na Magufuli waligombea tena katika uchaguzi wa Oktoba 2020 na kupata muhula mwingine.
Akiwa msaidizi wa Hayati rais Magufuli wakati huo, walilalamikiwa kwa kuendesha utawala uliokandamiza demokrasia na uhuru wa maoni, huku pia wakikosolewa kwa kupuuza tahadhari za maambukizi ya UVIKO-19, ambapo Magufuli alipendekeza Zaidi njia za asili kukabiliana na maambukizi hayo tofauti na maelekezo yaliyokuwa yakitolewa na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO).
Machi 17, 2021 Rais Samia alitangaza kifo cha Hayati Magufuli akisema kimetokana na matatizo ya moyo, huku kukiwa na uvumi kuwa kiongozi huyo alifariki kutokana na maambikizi ya Uviko-19.
Samia alikula kiapo kuwa rais Machi 19 kukamilisha muhula wa awamu ya tano.
Katika demokrasia, Samia aliondoa katazo la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, kuondoa marufuku kwa vyombo vya habari vya magazeti na redio na televisheni, pamoja na kufuta sera iliyowazuia wasichana wajawazito kuhudhuria shule.
Akitumia falsafa yake ya 4Rs, yaani maridhiano, ustahimilivu, mageuzi, na ujenzi mpya.
Aliboresha mazingira ya siasa na kijamii kwa kukutana na makundi mbalimbali na aliunda kikosi kazi chini ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kilichovikutanisha vyama vya siasa kasiro CHADEMA.
Licha ya kumfungulia mashitaka ya ugaidi, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, aliifuta kesi hiyo na kuanza mazungumzo ya maridhiano kati ya viongozi wa chama hicho na CCM.
Pamoja na kwamba mazungumzo hayo hayakuleta matokeo yaliyotarajiwa, lakini yaliiwezesha CHADEMA kupata malimbikizo ya ruzuku iliyowawezesha kununua jingo la ofisi ya makao makuu jijini Dar es Salaam.
Kikanda, alifanya juhudi za kuboresha uhusiano na nchi nyingine za Afrika Mashariki na nje ya Afrika zikiwamo za Ulaya, Asia na Marekani.
Umaarufu umeshuka?
Kufuatia kuvunjika kwa mazungumzo ya maridhiano kati ya CHADEMA na CCM mwaka 2023, malalamiko kuhusu utawala wa Rais Samia yaliongezeka.
CHADEMA walidai zaidi ya asilimia 90 ya mambo waliyopeleka kwenye mazungumzo hayo hayakukubaliwa likiwamo la mchakato wa mabadiliko ya Katiba.
Badala yake Serikali ilipeleka bungeni muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani (2023), Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (2023) na Sheria ya Vyama vya Siasa (2023) zilizopitishwa na kuwa sheria.
Sheria hizo zimekuwa zikilalamikiwa na vyama vya upinzani kutozingatia malalamiko yao, yakiwamo ya kuweka mfumo bora wa uchaguzi ili kuepusha madhila yaliyojitokeza katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Kuonyesha kuwa kuwa malalamiko ya wapinzani yana mashiko, uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024, madhila yale yale waliyokuwa wakiyalalamikika yalijitokeza; yakiwamo ya wagombea wao kuenguliwa, mawakala kuondolewa vituoni.
Katika uchaguzi huo, CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 99, huku vyama vya upinzani vikiambulia chini ya asilimia 1.
Kufuatia matokeo hayo, CHADEMA ilitangaza msimamo wake wa kutoshiriki uchaguzi na ikiwezekana kuuzuia mpaka yafanyike mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi, maarufu; No Reforms No Election.
Baada ya CHADEMA kupata uongozi mpya chini ya Mwenyekiti, Tundu Lissu na Makamu Mwenyekiti, John Heche, waliendeleza msimamo huo wakifanya mikutano ya hadhara ya kudai mabadiliko hayo.
Hata hivyo, Aprili 9, Lissu alikamatwa akiwa wilayani Mbinga Mkoa wa Ruvuma baada ya kuhutubia mkutano na kisha alisafirishwa hadi Dar es Salaam na kupandishwa kizimbani Aprili 10 na kusomewa mashitaka ya uhaini na kuchapisha taarifa za uongo mitandaoni. Kesi hizo zinaendelea mpaka sasa.
Kesi hiyo imeibua malalamiko ya ndani na kwa jumuiya za kimataifa ikiwamo Jumuiya ya Ulaya juu ya ukandamizwaji wa demokrasia nchini.
Apitishwa kugombea urais na CCM
Januari 19, 2025 Mkutano mkuu wa CCM ulimpitisha Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea urais kupitia chama hicho.
Pia ulimpitisha Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza na kwa upande wa Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi aliteuliwa kuwa kuwa mgombea urais wa chama hicho visiwani humo.
Hata hivyo, kupitishwa kwa Rais Samia kulizua minong’ono, huku ikielezwa kuwa taratibu hazikufuatwa.
Miongoni waliolalamika ni kada wa chama hicho chungaji Godfrey Malisa ambaye sasa amevuliwa uanachama, aliyedai kuwa katiba ya CCM imevunjwa katika uteuzi huo.
Vyanzo: Ikulu, Britannica.
2. Luhaga Mpina: Kutoka CCM, ana nafasi gani ya urais kupitia ACT Wazalendo
Wakati Luhaga Joelson Mpina alipokanyaga mara ya kwanza ndani ya Bunge la Tanzania mwaka 2005, wachache wangeweza kutabiri kuwa angebaki kuwa sehemu ya chombo hicho kwa kipindi cha miongo miwili, akishiriki katika kuunda baadhi ya sera muhimu za kiuchumi, mazingira na kilimo cha nchi.
Wasifu wake
Akiwa amezaliwa Mei 5, 1975 mkoani Simiyu, safari ya Mpina ilianza mbali na jukwaa la siasa za kitaifa. Alisoma Shule ya Msingi Mwandu-Itinje, kisha Meatu na Karatu kwa masomo ya sekondari. Hatua yake ya kitaaluma ilimfikisha Chuo Kikuu cha Mzumbe, ambako alipata shahada ya uhasibu msingi ulioujenga mtazamo wake wa kisera na usimamizi wa fedha.
Hatua za awali za kazi yake zilikuwa katika serikali za mitaa. Kati ya mwaka 2003 na 2005, alihudumu kama mhasibu wa wilaya, afisa manunuzi msaidizi na katibu wa bodi ya usimamizi katika Wilaya ya Meatu. Lakini hata akiwa kwenye kazi za utumishi wa umma, siasa zilianza kumuita.
Kupanda kwake ngazi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kulikuwa kwa kasi. Akianzia kama Kamanda wa Vijana wa Wilaya ya Meatu mwaka 2003, Mpina alijipatia nafasi muhimu katika kamati za siasa za wilaya na mkoa. Ukaribu wake na wananchi pamoja na uwezo wa kupanga mambo vilimpa tiketi ya ubunge mwaka 2005, akiwakilisha wananchi wa Kisesa — nafasi ambayo ameendelea kuishinda tena katika chaguzi za 2010, 2015 na 2020.
Bungeni, Mpina alijijengea sifa ya kuwa mbunge anayefanya kazi kwa karibu na kamati zenye ushawishi mkubwa. Kuanzia Kamati ya Masuala ya Uchumi, Viwanda na Biashara, hadi Kamati ya Bajeti, mchango wake umeonekana katika sera nyingi za biashara na fedha zilizounda mwelekeo wa uchumi wa Tanzania hivi karibuni. Ushawishi wake wa kimataifa ulipelekwa hadi Bunge la Panafrika kati ya 2010 na 2015, ambako alishiriki mijadala ya bara kuhusu masuala ya fedha na uchumi.
Apanda kisiasa
Mwaka 2015, nguvu yake ya kisiasa iliongezeka alipoteuliwa na hayati Rais John Magufuli kuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais akishughulikia Muungano na Mazingira. Miaka miwili baadaye, Rais Magufuli alimteua kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi. Katika kipindi chake cha uwaziri (2017–2020), Mpina alisukuma mageuzi yaliyolenga kurahisisha mfumo wa sekta hiyo, kuboresha usimamizi, na kuongeza tija kwa wafugaji na wavuvi wadogo.
Aigeukia Serikali
Hata hivyo, baada ya kuondoka serikalini, Mpina amekuwa mchungu kwa Serikali, akitumia mijadala yake bungeni kuwakosoa mawaziri tofauti na wabunge wenzake wa CCM waliokuwa Zaidi ya asilimia 98.
Miongoni mwa mawaziri walioonja hasira za Mpina ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe ambaye mara kadhaa walipishana kuhusu uendeshaji wa wizara hiyo.
Mvutano huo ulimsababishia asimamishwe kuhudhuria vikao 15 vya Bunge Julai 24, 2024, akidaiwa kutoa kauli za uongo dhidi ya Waziri wa Kilimo Hussein Bashe.
Bunge likiongozwa na Spika Dk Tulia Ackson lilipitisha azimio la kumsimamisha kuhudhuria bungeni vikao 15 mbunge huyo wa Kisesa kwa tuhuma za kusema uongo na ukiukwaji wa kanuni za Bunge.
Baada ya kufukuzwa bungeni, Mpina alikwenda kufungua kesi akiwashitaki Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Hata hivyo, kesi hiyo ilitupwa, baada ya Mahakama kusema haina mamlaka ya kuingilia kazi au majukumu yaliyofanywa na Bunge kwa mujibu wa kanuni na sheria labda itokee vinginevyo.
Alirudi bungeni Novemba 2024.
Baada ya hapo, Mpina alijikita kwenye siasa za wananchi wa chini, akikosoa viomngozi wa Serikali.
Kutokana na kusigana kwake na viongozi wa CCM na Serikali yake, haikushangaza kuona Mpina akitemwa kwenye kura za maoni za chama hicho.
Ana nafasi gani baada ya kuhamia ACT Wazalendo
Agosti 5, 2025 alijiunga na chama cha ACT Wazalendo na Agosti 66 alipitishwa kuwa mgombea urais. Wachambuzi wa masuala ya siasa wanaona hatua hiyo inaweza kumjenga kumjenga kama kiongozi wa kitaifa mwenye uthubutu, kwani kuhama kutoka CCM, chama kilichomlea kisiasa kwa zaidi ya miongo miwili, kutamfanya aonekane kama mwanasiasa jasiri anayeweza kupinga mfumo aliokuwa sehemu yake.
Pia anaweza kuvutia wapiga kura waliuokatishwa tamaa na CCM na wanaotafuta sura mpya na mawazo mapya, hasa miongoni mwa vijana na wasomi wanaoona vyama vikuu vya zamani havibadiliki haraka.
ACT tayari inajitambulisha kama chama kinachopigania uwazi wa rasilimali, utawala wa sheria na sera mbadala, hivyo kumruhusu Mpina kutumia ajenda hizo kujitofautisha na CCM.
Hata hivyo, Mpina ameingia kwenye chama ambacho bado hakina mtandao mkubwa nchini kulinganisha na mpinzani wao mkuu CCM. Pia kwa mfumo wa uchaguzi, kanuni za kampeni, na hali halisi ya ushindani vinaweza kuathiri nafasi yake, hasa kama hakutakuwa na umoja wa vyama vya upinzani.
Nafasi ya kushinda huenda ikawa ndogo kwa sasa kutokana na nguvu ya CCM na mgawanyiko wa kura za upinzani. Hata hivyo, anaweza kuongeza sana umaarufu wa ACT, kuleta kura nyingi zaidi bungeni na kwenye serikali za mitaa, na kumjengea msingi wa kisiasa wa baadaye.
Inawezekana ameamua kugombea urais kama mkakati wake wa muda mrefu ili kujiweka kwenye ramani ya kisiasa kama mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani, akijipanga kwa uchaguzi wa baadaye au kushika nafasi muhimu ndani ya ACT na siasa za taifa.
%%%%%
3. Salum Mwalimu
Ataibebaje CHAUMMA uchaguzi mkuu 2025
Salum Mwalimu Jumaa alipoteuliwa kuwania nafasi ya urais katika Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), kulikuwa na hisia tofauti kutokana na uzito wa nafasi hiyo na uzoefu katika chaguzi.
Hata hivyo, akisoma wasifu wake Agosti 6 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzo na Oganizesheni wa CHAUMMA, Edward Kinabo alisema Mwalimu anaaminika kuwania nafasihiyo, kwani hata mwaka 2020 aliaminiwa na CHADEMA na kuwa mgombea mwenza wa urais akiwa na Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Tundu Lissu aliyegombea urais.
“Hata nchi yetu leo hii inaongozwa na rais aliyekuwa Makamu wa Rais. Kwa hiyo yule aliyeonekana kuwa anafaa kuwa rais akiwa CHADEMA, Kamati ya Utafiti ya CHAUMMA imebaini kuwa anatosha kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Tayari Salum Mwalimu ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CHAUMMA pamoja na mgombea wake mwenza, Devotha Minja ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, wameshachukua fomu za kugombea urais zinazotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) tayari kuteuliwa kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza baada ya kuchukua fomu hiyo jijini Dodoma Agosti 12, Mwalimu ameahidi kwamba endapo atachaguliwa kuwa Rais, chama chake kitashriki kufumua upya sheria zote ambazo Watanzania wana kiu nazo na kuhakikisha kuwa Taifa linaenda kupata Katiba Mpya
Alisema kuwa yeye na mgombea Mwenza Devotha Minja wanatamani kuona Bunge lenye uhuru pamoja na kutengeneza Serikali ambayo inaangalia matakwa na maslahi ya wananchi.
Hata hivyo, kumekuwa na hisia tofauti kuhusu mfombea huyo, hasa kutokana na historia yake kisiasa na hasa za ushindani, kwani bado anaonekana hajakomaa kuwa tishio kwa wapinzani wao CCM, licha ya kushika nafasi kadhaa ndani ya CHADEMA kabla ya kuhamia CHAUMMA.
Uzoefu wa siasa
Mwalimu aliingia kwenye siasa kikamilifu mwaka 2014, ambapo aliteuliwa kuwa Naibu Katibu mkuu wa chama hicho upande wa Zanzibar, nafasi aliyoishika hadi mwaka 2024.
Amewahi kugombea ubunge mara kadhaa bila mafanikio. Mwaka 2015 aligombea ubunge katika jimbo la Kikwajuni Zanzibar, lakini hakushinda. Mwaka 2017 aligombea ubunge katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni na mwaka 2018 aligombea ubunge wa Bunge la Afrika, huko nako hakushida.
Mwaka 2020 alikuwa mgombea mwenza wa urais wa CHADEMA katika uchaguzi uliolalamikiwa kutokuwa huru na wa haki na hatimaye chama hicho kiliambulia mbunge mmoja tu.
Mei 2025, Mwalimu na baadhi ya makada wa CHADEMA walihamia CHAUMMA baada ya kutoa malalamiko kwa uongozi mpya wa chama hicho chini ya Tundu Lissu kwamba hawakusikilziwa maoni yao na kwamba walikuwa wakitukanwa wakiwa ndani ya chama hicho.
Baada ya kuingia kwenye chama hicho, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama hicho.
Maisha ya awali
Alizaliwa Novemba 24, 1979 kisiwani Zanzibar. Ni mtoto wa tatu wa familia ya Mzee Mwalimu Jumaa Mwalimu na mama Faudhia Ismail Abood. Alipata elimua yake ya msingi Mkunazini kisiwani Zanzibar, na kumalizia darasa la saba katika shule ya Msingi Mlimwa iliyopo jijini Dodoma mwaka 1995.
Mwaka 1999, Salum Mwalimu alihitimu kidato cha nne katika shule ya Sekondari Kibaha, lakini kabla ya hapo alisoma Dodoma sekondari na Umbwe iliyopo mkoani Kilimanjaro.
Mwaka 2002 alihitimu elimu ya juu ya sekondari katika Shule ya Sekondary ya Shycom iliyopo mkoani Shinyanga. Kati ya mwaka 2004 hadi 2007, Salum Mwalimu alisoma Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) akiwa amesomea fani ya Teknolojia ya Habari, na baada hapo alisoma Chuo Kikuu cha Dar es slaam alisomea shahada ya uzamili ya uandishi wa habari iliyotolewa kwa ushirikiano na Taasisi ya Kimataifa ya Biashara ya India.
Kati ya mwaka 2012 hadi 2014, Salum Mwalimu alisomea shahada ya uzamili katika utawala biashara akijikita katika biashara za kimataifa katika Taasisi ya Usimamizi wa Fedha (IFM).
Kazi
Salumu Mwalimu alifanya kazi kwa miaka minane akiwa mwandishi wa habari katika televisheni ya Chanel TEN kati ya mwaka 2003 hadi 2011. Kati ya mwaka 2011 hadi 2014 alifanya kazi katika kampuni ya Vodacom.
4. Gombo: Msomi wa Mipango Miji anayeusaka urais kupitia CUF
Japo jina lake halina umaarufu kwenye anga siasa nchini, Gombo Samandito Gombo amekuwa kwenye siasa tangu CCM na baadaye akahamia upinzani. Amejiunga na Chama cha Wananchi CUF Julai 5, 2025 na sasa anautaka urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia chama hicho.
Gombo alipendekezwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CUF kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
Gombo, ambaye amewahi kuwa mtumishi wa umma akishika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Mkurugenzi wa Wilaya ya Mbinga, aalipata kura 467 kati ya 545 zilizopigwa, akimshinda mshindani wake Siwale Mkungutila aliyepata kura 78.
Katika uchaguzi huo uliofanyika katika ukumbi wa Lekham, Buguruni Jijini Dar es Salaam Agosti 9, 2025, upande wa Zanzibar, Hamad Masoud Hamad amependekezwa kuwa mgombea ursi baada ya kujikusanyia kura 406 kati ya zilizopigwa.
Akizungumza wakati wa kuomba kura kwa wajumbe wa Mkutano mkuu wa CUF, Gombo alisema kiu yake ni kuona utoaji wa huduma za jamii hasa afya ikitolewa bure kwa kuwa wananchi wanalipa kodi.
“Utoaji mbovu wa huduma ya afya nchini ni jambo ambalo halikubaliki hasa kwa kuwa Serikali inakusanya kodi. Huduma hiyo inatakiwa kutolewa bure,” alisema.
Suala linguine linalomgusa ni ukosefu wa ajira kwa vijana, akisema rasilimali zilizopo nchini zinatosha kutoa ajira kwa vijana wote, tofauti na sasa ambapo kundi kubw ala vijana halina ajira.
Alikotokea
Gombo alizaliwa mwaka 1970 Ukiriguru wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza, alisoma shule ya msingi Isebya wilayani Mbogwe Mkoa wa Geita kisha akaenda shule ya sekondari Shinyanga na elimu ya juu ya sekondari ya Lake jijini Mwanza.
Baada ya hapo alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akichukua kozi ya Mipango miji na Vijiji aliyomaliza mwaka 2001. Pia ana shahada za uzamili ya Usimamizi wa miji na maendeleo aliyopiata katika Taasisi ya Nyumba na Maendeleo ya Miji (HIS) Uholanzi mwaka 2005.
Pia ana stashahada ya Usajili Mijini aliyoisomea Chuo Kikuu cha Lund Sweden mwaka 2008, ana cheti cha Njia za kupata fedha kwa nyumba za ngazi ya chini kwa nchi za Maendeleo Kuzini mwa Afrika (SADC).
Amewahi kuwa Salaam Ofisa Mipango Miji Manispaa ya Ilala Dar es Salaam (2001 hadi 2010, Ofisa Mipango Miji mkuu wa Manispaa ya Songea (2010- 2011).
Mwaka 2016 aliteuliwa na Hayati Rais John Magufuli kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbinga Mkoa wa Ruvuma na baada ya hapo alistaafu utumishi wa umma mwaka 2028 na kuendelea kusimamia kampuni yake ya Ardhi Plan Ltd Dar es Salaam ambako ni Mkurugenzi Mtendaji.
Awali alikuwa mwanachama wa CCM kabla ya kujiunga na chama cha UMD mwaka 2020. Msaidizi wake, Enock Mabonesho amesema kuwa Gombo alijitoa chama hicho kwa madai ya kuhumiwa kwa ndoyo zake katika chama hicho.
“Wanachama wengi wa CUF wanamfahamu ombo kwa sababu waliondoka naye UMD na hata alipotangza kugombea urais, wengi walimuunga mkono,” amesema.
5. Doyo: Nina akili kubwa kumudu urais
Jina la Doyo Hassan Doyo si geni katika siasa za Tanzania, kwani amewahi kupita katika Chama cha Wananchi (CUF), Alliance for Democracy na sasa yupo National League for Democracy (NLD) akiwa Katibu Mkuu.
Mwaka huu amejitokeza kuwa mgombea urais kupitia NLD, akidai kuwa ana uwezo wa kiakili kumudu nafasi hiyo.
“Nimejipima na kuona kuwa nina mawazo makubwa ya kisiasa ya kuwa rais. Nina mawazo makubwa ya kutatua kero ya ajira kwa vijana. Nilishangazwa na kauli ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliposema wale wahitimu wa shahada ya chuo kikuu waende tena vyuo vya Ufundi (VETA). Inakuwaje mhitimu wa chuo kikuu aende VETA? Huko ni kukosa maarifa ya kuleta ajira kwa Watanzania na ndipo yanapohitajika mawazo makubwa niliyonayo,” amesema.
Akiwa mwanasiasa kwa Zaidi ya miaka 25, Doyo alikuwa mwanachama na kiongozi wa CUF, ikiwemo nafasi ya CUF Mwenyekiti wa chama Wilaya ya Handeni mkoani Tanga kwa miaka 17 na mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa kuanzia mwaka 1996 hadi 2011.
Atimuliwa CUF
Mnamo mwaka 2011, Doyo na wanachama wengine wakiongozwa na Hamad Rashid walifukuzwa CUF na ndipo walipoanzisha chama kingine kilichoitwa Alliance for Democratic Change (ADC Dira ya Mabadiliko).
Akifafanua sababu za kufukuzwa, Doyo amesema, “nilidai kuwa katibu mkuu wa CUF (Wakati huo Maalim Seif Sharif Hamad) anakiua chama ajiuzuru ili abaki na nafasi ya umakamo wa kwanza wa Rais huko Zanzibar, nikaonekana muasi hivyo nikafukuzwa.”
Akiwa ADC alikuwa Mkurugenzi wa Habari na Uenezi 2013 hadi 2014 na kisha akawa Naibu Katibu Mkuu hadi mwaka 2016 ambapo alipanda cheoi na kuwa Katibu Mkuu mwaka 2017 hadi 2024. Alijitolea sana kukieneza chama hicho kipya nchini Tanzania, hususani katika mkoa wa Tanga ambako aliweka kambi kuu ya upinzani kwa upande wa Bara.
Mambo magumu ADC
Hata hivyo, ilipofika mwaka 2024 ndio ikawa hatima yake kuwepo ADC, kwani mwaka huo ndio chama kilifanya uchaguzi na yeye aligombea uenyekiti, lakini alishindwa kwa kupata kura 70, huku mpinzani wake, Shabani Itutu aliyekuwa Makamu Mwenyekiti akipata kura 121.
Hata hivyo, Doyo hakuridhika na matokeo yake, hivyo akakata rufaa katika Kamati ya Rufaa ya chama hicho, ambako huko pia alikwaa kisiki.
Baada ya kuona hivyo, Doyo alijitoa kwenye chama hicho na kukimbilia NLD. Alipoulizwa sababu za kukimbia ADC, Doyo amehusisha anguko lake katuika uchaguzi na tofauti zake na Hamad Rashid, akidai kuwa kiongozi huyo hakumtaka awe mwenyekiti.
Ahamia NLD
Baada ya hapo alihamia Chama cha National League for Democracy (NLD) alipo mpaka sasa akiwa ni Katibu Mkuu.
Nje ya siasa
Mbali na siasa, Doyo Hassan Doyo ni mfanyabiashara, na mkuregezi mkuu wa kampuni za Mzigwa Investment, Mtibwa Complex Company, na Hamod Tracking investment akijishughulisha na biashara za madini ya viwandani.
Doyo pia ni mchambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, mtafito wa masuala ya miamba, mtaalamu wa biashara.
Kielimu ana Ana stashahada ya uandishi wa habari aliyoipata katika Chuo cha Unadishi wa Habari cha Dar es Salaam (DSJ).
****************************************************************
6. Kadege:
Mtaalamu wa uzalishaji nguo aliyegeukia siasa, sasa autaka urais
Akiwa na miaka 73 sasa, Twalib Ibrahim Kadege anapambana na kupata nafasi ya juu kabisa ya Taifa yaani urais. Akihojiwa na kituo cha Radio East Africa Julai 29, 2025, Kadege amesema amejipima kutokana na uongozi wake aliouonyesha katika chama chake cha United People's De,ocratic Party (UPDP).
“Nimejipima kwenye uongozi wangu wa chama, kwa sababu uongozi unaanzia pale uliopo na kwenye chama nimeongoza vizuri, nimeangalia waliopita walipita vipi na wapi waliteleza ili nipanyooshe na kuongoza watu katika siasa bora na maisha bora,” amesema.
Alipoulizwa jinsi anavyojipima na wagombea wengine, Kadege ambaye ni Mwenyekiti wa UPDP amesema “Sioni mtu wa kushindana na mimi kwenye uchaguzi wa rais. Mwaka 2020 nilishiriki kwenye uchaguzi na bahati nzuri watu wengi wananfahamu na wanafahamu sera zangu. Mimi siwezi kuchukua sera za chama kingine au za mwu mwingine. Tunachukua sera za chama, tutawatetea wananchi na matatatizo yao tunasema tutayatatua vipi.”
Licha ya mfumo wa uchaguzi kulalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa, Kadege anaiona Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iko sawa kusimamia uchaguzi.
Wasifu wake
Kadege alizaliwa mwaka 1952 katika Kijiji cha Kiwawa Kingongo kilichopo Kilwa Masoko Mkoa wa Lindi na ni kitinda mimba katika familia ya watoto sita wa baba Ibrahim Kadege na mama Zalia Kikombe.
Mwaka 1963, akiwa na umri wa miaka 11, Kadege alianza darasa la kwanza Shule ya Msingi Lihimalyao iliyopo Tarafa ya Pande wilayani Kilwa na kutokana na uwezo wake, alisoma madarasa manne kwa miaka miwili hadi mwaka 1964.
Kadege, alifaulu mtihani wa darasa la nne, hivyo mwaka 1965, alichaguliwa kuendelea na darasa la tano, Shule ya ya kati ya Msingi Msanga iliyopo Kilwa Masoko.
Alisoma hapo mpaka darasa la sita mwaka 1966, kabla ya kuhamia shule ya msingi Pande Extended, alikomalizia darasa la sita na kuhitimu la nane mwaka 1968.
Mwaka 1970, Kadege aliajiriwa na kiwanda cha nguo cha Urafiki, Ubungo, Dar es salaam, kama mwendeshaji wa mitambo. Baada ya miaka 14 ya ufanyaji kazi katika sekta tofauti za uzalishaji wa nguo kiwandani, mwaka 1984, alipewa nafasi na uongozi wa kiwanda kuendelea na masomo ya juu.
Uongozi wa kiwanda cha Urafiki ulianzisha utaratibu wa kuwaendeleza kielimu wafanya kazi wake, hivyo wakateua baadhi ya vyumba kiwandani na kuvifanya madarasa, kisha wakawa wanawaalika walimu kutoka shule na vyuo mbalimbalii ili kufundisha wafanyakazi palepale kiwandani.
Kupitia utaratibu huo Kadege alipata nafasi ya kuanza masomo ya kidato cha kwanza mwaka 1984. Mwaka 1985 alifanya mitihani ya kidato cha pili na kupata namba, ambayo ilimuwezesha kufanya mtihani wa kidato cha nne kama mtahiniwa binafsi mwaka 1988.
Mwaka 1988, alifanyaj mtihani wa kuhitimu kidato cha nne, ambapo katika masomo matatu aliyofanya Kiingereza alipata ufaulu wa daraja C, Kiswahili B na Siasa D.
Mwaka 1989, Kadege alipewa fursa nyingine ya kusomea astashahada ya teknolojia ya utengenezaji nguo. Alihitimu na kukabidhiwa cheti daraja la tatu kama mtaalamu wa utengenezaji nguo.
Katika harakati zake za kujiendeleza kimasomo, mwaka 1998, alianza masomo ya kidato cha tano, lakini harakati hizo zikakatishwa mwakwa 1999 akiwa anaingia kidato cha sita, baada ya kiwanda cha Urafiki kubinafsishwa.
Uongozi mpya ulioingia kiwandani hapo haukuruhusu tena utaratibu wa kuwaendeleza kielimu wafanyakazi wake, kwa hiyo Kadege hakuweza kukamilisha masomo ya kidato cha sita na hakufanya mtihani.
Vilevile, Kadege anasema kuwa kipindi kiwanda cha Urafiki kinabinafsishwa, alikuwa pia anasoma uandishi wa habari, ngazi ya astashahada, lakini hakuweza kuendelea mpaka kukamilisha masomo yake, kwani alikuwa akisomea palepale kiwandsani kwa utaratibu uliokuwepo.
Ahamia kwenye kilimo
Mwaka 1999, Kadege aliacha kazi Urafiki, kwa kile anachoeleza kuwa hakuwa na maelewano na uongozi mpya na hiyo pia iliwakumba wafanyakazi wengine ambao nao waliamua kuacha kazi.
Tangu Kadege alipoondoka Urafiki, alianza kijishughulisha na kilimo, vilevile kuweka mkazo zaidi katika siasa. Kadege ni mkulima mwenye mashamba ya mpunga na ufuta wilayani Rufiji na kilimo cha minazi katika eneo la Lutando wilayani Mkuranga Mkoa wa Pwani na pia ana mashamba Turiani mkoani Morogoro.
Kuingia kwenye siasa
Kadege anasema alianza kushiriki siasa tangu mwaka 1992 alipokuwa mjumbe wa tawi la CCM la kiwanda cha Urafiki, Ubungo, Dar es salaam. Mwaka 1995 upepo wa siasa za mageuzi ulimng’oa CCM na kuhamia NCCR Mageuzi wakati huo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na baadaye Wizara ya Kazi na Vijana, Augustine Mrema alihamia chama hicho na kuwa mgombea urais.
Mwaka 1995, Kadege alichaguliwa kuwa katibu wa NCCR Mageuzi, tawi la Ubungo (urafiki na National Housing). Mwaka 1996 Kadege alichaguliwa kuwa Katibu wa NCCR Mageuzi Kata ya Ubungo Dar es salaam.
Hata hivyo, kutokana na mgogoro uliokikumba chama hicho uliohusisha kundi la Mrema (mwenyekiti) na Katibu Mkuu, Mabere Marando na uliodumu hadi mwaka 1999, Mrema alihamia TLP akifuatwa na kundi la wanachama akiwamo Kadege.
Akiwa TLP, Kadege alichaguliwa kuwa Katibu wa Kata ya Ubungo na mwaka 2000 akachaguliwa kuwa mwenyekiti wa TLP jimbo la Ubungo.
Safari ya siasa ikaendelea na mwaka 2006 alihama TLP na akajiunga na UPDP na alibaki kuwa mwanachama wa UPDP mpaka mwaka 2010, alipochaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya UPDP.
Mwaka huo pia aligombea Udiwani kata ya Manzese Ubungo, Dar es Salaam, lakini hakushinda. Mwaka 2015 Kadege alikuwa mmoja wa wanachama wa UPDP walioteuliwa na Kamati kuu ya Chama hicho, kuwa wajumbe wa Kamati ya uchaguzi.
Kwa vile alikuwa mjumbe Kamati ya Uchaguzi, alikosa sifa ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi. Hata hivyo, baada ya Uchaguzi, aliyeshinda uenyekiti Fahmi Dovutwa alimteua kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa.
Kuelekea uchaguzi Mkuu 2015, Kadege aliteuliwa kuwa meneja kampeni za mgombea urais wa UPDP, Fahmi Dovutwa. Agosti 9, 2018, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa UPDP Bara, Felix Makua alihamia Ada-Tadea, Kadege akateuliwa kuwa Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa UPDP-Tanzania Bara.
Desemba Mosi, 2019, Dovutwa alifutwa uanachama wa UPDP, hivyo kupoteza sifa ya kuwa mwenyekiti. Aliyekuwa Makamu wake Zanzibar, Abdallah Mohamed Hamis, akawa kaimu mwenyekiti.
Kaimu Mwenyekiti, Hamisi alimteua Kadege kuwa naibu Katibu Mkuu Bara na kuthibitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa UPDP.
Mwenyekiti mpya UPDP
Julai 26, mwaka 2020, katika ukumbi wa Equator Grill wilayani Temeke, Dar es Salaam, UPDP walifanya mkutano mkuu kuchagua viongozi, Kadege aligombea na kushinda uenyekiti wa chama hicho.
Machi 2025, Kadege alichaguliwa tena na Mkutano Mkuu kuwa Mwenyekiti wa UPDP na hapo hapo alichaguliwa kuwa mgombea wa urais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.
ITAENDELEA.....

Urais
Akiwa rais, Hassan alichukua hatua za haraka kurekebisha makosa ya Magufuli kuhusu Uviko-19 kwa kuruhusu chanjo na hata yeye mwenyewe alipokea chanjo hadharani, huku akiwataka wananchi kuzingatia masharti yaliyotolewa na wataalamu wa afya.Katika demokrasia, Samia aliondoa katazo la vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara na maandamano, kuondoa marufuku kwa vyombo vya habari vya magazeti na redio na televisheni, pamoja na kufuta sera iliyowazuia wasichana wajawazito kuhudhuria shule.