Asha Abdala,
Dr Slaa kasema hivi:- Je ni Serikali 100% Kama sivyo Serikali inahusika vipi na Trust hii...
Hapa akiwa na maana hata yeye hafahamu undani wa shirika hili..sioni mahala amesema siii la serikali.
Hakuna propaganda ikiwa hujaulizwa mbele ya sheria. Huyu ni mwanasheria wa shirika iweje amwage vitu tuu kwa sababu Dr. Slaa kasema.. Utaratibu upo na rahisi kabisa mnashindwa kitu gani kusimamaisha sheria!
Dr Slaa alishaweka wazi msimamo wake toka mwaka 2007, msome hapa chini
Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Karatu, Dk. Wilbroad Slaa (Chadema) ametamba kuwa ana ushahidi na vielelezo kuthibitisha madai aliyokuwa ayawasilishe bungeni kuhusu ufisadi wa mabilioni ya shilingi unaodaiwa kufanyika ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Ametishia pia kutaja hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kuhusika na ufisadi huo ifikapo Septemba 15.
Dk Slaa, ambaye wiki iliyopita aliondoa hoja kuhusu madai hayo aliyokuwa aiwasilishe katika kikao kijacho cha Bunge akidai kwamba ilikuwa inapigwa danadana kupangiwa tarehe ya kusikilizwa ili kuiwezesha Serikali kujipanga upya, aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba vielelezo alivyonavyo si vya kughushi na amevipata kutoka ndani ya taasisi za umma, ikiwamo BoT yenyewe.
Hata hivyo wakati akizungumzia madai hayo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), Dk Batilda Burian alisema kitendo cha Dk Slaa kuondoa hoja yake hakikutokana na mbinu zo zote za Serikali, bali hoja yake ilikuwa ya kishabiki yenye lengo la kuonyesha mbele ya jamii kwamba wapinzani wanaonewa bungeni.
Alisema baadhi ya vielelezo vilivyopelekwa na mbunge huyo kwa Spika vilithibitika kuwa havitoshelezi hivyo alichokuwa anamtaka Spika ni kuwasilisha ushahidi zaidi na siyo kuondoa hoja. Alisema yawezekana mbunge huyo alitambua kwamba hana ushahidi wa kutosha ndiyo maana akaiondoa hoja yake.
Hata hivyo alisema Dk Slaa bado ana nafasi ya kuwasilisha hoja hiyo katika kikao kijacho cha Bunge. Madai ya Dk Slaa yanahusu tuhuma kwamba BoT ililipa deni la kampuni ya Meremeta linalodaiwa kufikia Sh bilioni 155 kinyume cha utaratibu, ililipa fedha kwa kampuni binafsi ya Mwananchi Gold na Sh bilioni 38 kwa kampuni hewa.
Alisema vielelezo alivyo navyo kuhusiana na tuhuma hizo ni vya kweli na akamshangaa Spika wa Bunge, Samuel Sitta kudai baadhi ya vielelezo vyake ni vya uongo wakati si mtaalamu wa maandishi ya kughushi. Wakati akizungumza katika kipindi kimoja cha televisheni wiki iliyopita, Sitta alisema kwamba atapeleka Polisi suala la kughushiwa kwa baadhi ya nyaraka alizowasilishiwa na Dk Slaa.
Dk Slaa aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba alipoomba kuwasilisha hoja yake aliamini ushahidi wake kwa vile umetoka ndani ya taasisi muhimu. Kuna Watanzania ndani ya taasisi hizi ambao wanashuhudia baadhi ya watu wanavyojineemesha kwa ufisadi, wamechoka na hawa ndiyo wanaotusaidia.
Alitumia mkutano wa jana kuwaonyesha waandishi namna ambavyo alikuwa anaandika barua kwa Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela) kuomba nyaraka mbalimbali na akapewa. Akichambua tuhuma hizo kuhusu madai kwamba kampuni ya Tangold iliandikishwa kijanja kuwa ni mali ya Serikali, Dk Slaa alisema kampuni hiyo ni ya kigeni ambayo iliandikishwa kwa mara ya kwanza Mauritius mwaka juzi na baadaye ikasajiliwa nchini Februari mwaka jana. Dk Slaa alisema licha ya Serikali kudai kuwa kampuni hiyo ni ya serikali lakini hakuna hati zilizoko Brela zinazoonyesha kuwa wakurugenzi wake wanafanya kazi kwa niaba ya serikali. Pia anahoji kama ilianzishwa kwa biashara na kama imelipa kodi.
Kampuni hii wiki nane tu baada ya kupata usajili ilipewa mkopo wa Sh bilioni 30.8 na BoT wakati hata wakurugenzi wake hawafahamiki, alisema Dk Slaa. Kuhusu tuhuma za BoT kulipa fedha kwa kampuni binafsi ya Mwananchi Gold Co. Ltd, Dk Slaa alisema kuna utata juu ya kuandikishwa kwa kampuni hiyo, jinsi ilivyolipwa na BoT dola milioni 5.5 na jinsi BoT ilivyolipa deni la Kampuni ya Meremeta wakati mmiliki wake hajulikani.
Alisema BoT ambaye ni msimamizi wa taasisi zote za fedha na uchumi wa nchi, mwenendo wake haupaswi kutiliwa shaka. Alisema kuna malipo mengi yamefanywa na benki hiyo ambayo yanatia wasiwasi na akadai kuwa kwa sasa ana ushahidi kuonyesha namna fedha hizo zilivyohamishwa na wajanja.
HabariLeo; Thursday,August 23, 2007