Helloo
Asante kwa majibu ya bashasha.
Hata hivyo niruhusu niweke kumbukumbu sawa.
1. Mchepuko/Michepuko sio habari mpya hapa duniani. Mahusiano haya yapo toka dahari. Ni sawa kwa vijana wa leo kuona kwamba kizazi chao hiki kimezongwa na michepuko. Maana ndio wakati wao huu kupambana na kadhia hii. Hivyo basi, usahihi ni kwamba michepuko sio jambo (phenomenon) mpya kwenye jamii yetu.
2. Kumjali sana mwenza wako (mume ama mke) sio kinga ya mwenza wako huyo kuwa na mahusiano ya nje. Haijawahi kuwa, sio kinga wala haitokuja kuwa kinga. Wapo waliojaribu kuwachunga wenza wao, wengine walithubutu kuwawekea mitego ya kiasili. Haikusaidia. Ukweli ni kwamba, kuepuka usaliti kwenye mahusiano hakuna kanuni. Ushauri mkuu ni kujikana nafsi na kuridhika na uliye naye, pia kutii sheria za Mwenyezi mungu kuhusu mahusiano ya kimapenzi. Ingawa ushauri huu unaonekana kama ni nadharia zaidi, lakini ndio ukweli.
3. Ni kweli madhara ya fumanizi ni makubwa sana. Lakini sio sahihi kuhitimisha kwamba michepuko inasababishwa na wanaume kutowajali wenza wao. Vilevile mwanaume/wanaume wanapoanzisha mahusiano ya ziada mbali na mwenza wake, sio sahihi kuhitimisha eti chanzo ni mwanaume pekee ama chanzo ni mwanamke pekee. Ndiposa awali niliandika raha ya kuimba ni kupokezana. Maana mahusiano ya mapenzi ni zao la jitihada za mume na mke kuboresha ahadi yao ya 'nakupenda' ama "i love you'. Ahadi hii haiwezi kuboreshwa na mume pekee ama na mke pekee.
Mwisho, itoshe kusema kwamba upo ushahidi wa kimaandiko kwenye vitabu vitakatifu kwamba kosa la Adamu lilikuwa kumwacha Hawa arande rande peke yake bustanini Edeni. Huko akakutana na nyota aliyeleta ushawihi mbaya ukapelekea madhara makubwa kwa kizazi cha Adamu na Hawa. Hivyo ni kweli kwamba mwanaume anayo nafasi kubwa kumlinda mwenza wake asipotoke. Hata hivyo, pamoja na maandiko kusimama, zama za maisha zimebadilika sana. Mtazamo wa maisha kwa wake na waume umebadilika sana. Nafasi na wajibu wa wanaume na wanawake kwenye familia nao umebadilika sana. Muhimu sana ni kudhoofika kwa imani na ujasiri wa mwanadamu kuzishinda tamaa za mema ya ulimwengu. Mema yanayopatikana kwa vipande vya fedha. Fedha imekuwa fedheha. Inatuletea fadhaa. Ndio maana haiwezekani kuhitimisha moja kwa moja kwamba mwanaume afanye yafuatayo na mwanamke afanye haya ili kulinda mahusiano yao ya kimapenzi. Ndiposa napendekeza kuzingatia sheria za mwenyezi Mungu zinazoongoza maisha ya mwanadamu.
Wakatabahu.