Tanzanians need to understand very well inside out of those who think they can be presidents of this country. Ni muhimu kuwachambua kinagaubaga watu wote wanaoutamani urais ili tuwalinganishe na Tanzania tunatoitaka- yaani nchi ya usawa wa hali na mali.
Hatutaki kupata marais ambao wanapitia mgongo wa nyumba- wanajificha ficha na kutotaka kujadiliwa. Wanataka wengine wajadiliwe lakini wao hawataki kujadiliwa. Kati ya watu ambao wameshajitangaza wenyewe kuutaka urais ni Zitto. Hivyo ni haki na ni wajibu wa wanachi wa Tanzania kumuelewa vizuri Zitto.
Ili tumuelewe tutajadili hoja zake, matangazo yake na matendo yake. Tunataka kila anayegombea urais apitie kwenye tanuru la kusafisha uchafu. Hatutaki tena kuwa na mgombea urais tusiyemjua. Tulishaumwa na nyoka mwaka 2005. Hatutaki tena kuuziwa mbuzi kwenye gunia. Jambo hili, tunataka lieleweke vizuri kwa wote wanaoutaka urais kuwa lazima wajadiliwe kwa uwazi.
Kila mmoja wao, awe Membe, Sitta, Lowasa, Zitto, n.k. Lazima wote wajadiliwe. Mtu kama Slaa ambaye wala hajajitapa kutaka kugombea urais mwaka 2015, amejadiliwa sana, na wananchi wanamfahamu vilivyo. Na huu ni ukurasa wa Zitto Kabwe, kurasa za wengine zitafunguliwa pia kwenye folder hii ya Tuwachambue wanaoutaka urais. Tunawataka hawa wanaoutamani urais wasiingilie kazi hii ya wananchi ya kuwachambua na kutaka kuwafahamu vilivyo.
Waache maongezi ya wazi ya wananchi juu yao yaendelee. Kama wanaufafauzi wanaweza kuutoa, lakini mwisho wa siku wananchi watachambua pumba na mchele. Katika ukurasa huu wa Zitto, ninaanza kuchambua machapisho yake kwenye gazeti moja la kila siku la Kiswahili. Anatoa hoja kwamba wananchi wafuate misingi wasifuate watu. Na sidhani kuwa Zitto anatarajia watu waseme, Amin au Amen au Amina. Hapana, Tutachambua hoja zinazotolewa. Hoja hii ya Zitto imekosa grounding.
Usahihi ni kuwa huwezi kutenganisha misingi ya Taifa au taasisi na watu. Watu ndio huandaa misingi. Kwa mfano waasisi wa Taifa letu la Tanzania walianzisha misingi ya usawa wa binadamu, ujamaa na kujitegemea, n.k. Wananchi walipoikubali misingi hii wakawa wafuasi wa watu hawa. Kwa hiyo wananchi wataendelea kuwafuata watu kwa kuwa ndio wanaotengeneza misingi.
Huwezi kutenganisha watu na misingi. Jambo lingine la kujadili kuhusu Zitto ni hoja yake ya kulinda umoja wa kitaifa. Amenukuliwa pia na gazeti la Kiswahili la Tanzania kuwa Kikwete na Serikali yake wanahatarisha umoja wa kitaifa kwa kushindwa kutoa nguvu ya hoja katika suala la gesi. Bali wanatoa vitisho na kutoa hoja za nguvu.
Tumjadili Zitto kama mtu anayeutamani urais juu ya uwezo wake wa kulinda umoja wa kitaifa. Je ni kweli Zitto ni aina ya watu wanaoweza kulinda umoja wa Tanzania? Mimi nadhani Zitto hana uwezo wala hana nia ya kuulinda umoja wa Tanzania.
Migogoro ndani ya chama chake cha siasa imemhusisha Zitto kwa njia moja ama nyingine. Mgogoro wa mwanzo ulimhusu yeye na Mbowe. Na hapa hoja za kibaguzi za kikabila zilitumika ili Zitto aonewe huruma na kukubaliwa kugombea uenyekiti wa chama chake. Pia gazeti la Mwanahalisi lililofungiwa na serikali ya Kiwete liliwahi kuripoti kuwa Zitto alikuwa na mahusiano ya karibu na watu wa usalama wa Taifa.
Bahati mbaya sana ukaribu huu wa Zitto na TISS haukusaidia hoja za udini kutumika dhidi ya Slaa katika mchakato wa kumpata rais wa awamu ya nne. Zitto anashirikiana kwa karibu na usalama wa taifa ambao wamechochea au wanaacha hoja ya udini dhidi ya Slaa na chama chake cha siasa itumike kuwapatia CCM urais huku umoja wa kitaifa ukiwekwa hatarini.
Hapa, Zitto hana uhalali wa kufikiriwa kuwa rais kwa kigezo cha umoja wa kitaifa. Hivi karibuni, Zitto amenukuliwa na mmoja wa walioasi kundi la masalia kuwa alikuwa akiwapatia msaada katika harakati za kumtukana Slaa kwa njia ya vyombo mbalimbali vya habari. Ingawa Zitto aliruka na kusema hamjui mtu huyo. Mhusika alisisitiza kuwa anamfahamu na anawapatia msaada katika mradi wao wa kumtukana Slaa.
Kitabu kimoja cha imani kinaeleza kuwa mfuasi mmoja alimkana Bwana wake mara tatu japo alikuwa anamfahamu. Kwenye mradi huu wa masalia ya Zitto hoja za ukabila, udini na ukanda zimetumika kumtukana Slaa kama njia ya kumwonyesha kuwa hafai kufikiriwa kugombea urais mwaka 2015.
Tunataka kuanza ukarasa mpya, na tunaomba wapambe wa hawa wanaoutaka urais waache watu wao wajadiliwe. Na tunawataka hao wanaoutaka urais wasifanye juhudi za kufunika habari za upande wa pili zinazowahusu. Hatutaki kuuziwa mbuzi kwenye gunia. Urais siyo mzaha, tumeshapata funzo mwaka 2005. Tuwajadili wanaoutaka urais na huu ni ukurasa wa Zitto.