Wamachinga na Haki-Jiji Nchini Tanzania

Teknocrat

JF-Expert Member
Oct 20, 2018
3,816
8,470
Ungemuona kijana Kulwa Makasi kwa mbali ungeweza kudhani ni kijana mwenye furaha.

Hujitahidi kumkaribisha mteja kwa bashasha japokuwa, tofauti na wenzake, angekuwa amekaa ndani ya kijibanda chake anamouzia viatu.

Kijibanda hicho kilikuwa kimepangiliwa vizuri na kwa unadhifu mkubwa,kama vilivyokuwa vijibanda vingine vya wamachingakatika eneo la Makoroboi jijini Mwanza, ungeweza kudhani amepumzika tu kwenye kiti akisubiri wateja.
Ni hadi pale ambapo ungekikaribia kibanda hicho ndipo ungeona kuwa Makasi alikuwa amekaa juu ya kiti chenye matairi cha walemavu.

Na hapo ndipo ungegundua kuwa mmachinga huyo mlemavu ndiye pia mwenye baiskeli ya kunyonga kwa mkono, yenye matairi matatu, iliyoegeshwa nje ya kibanda hicho.

Ukianza kuzungumza nae ndipo utaelewa kuwa ni mtu aliyepitia mateso makubwa na kwamba ulemavu wake ni kielelezo cha historia ya uonevu, dhuluma na uporaji wa bidhaa na maeneo ya kufanyia biashara unaofanywa na dola dhidi ya wafanyabiashara wadogo, maarufu kama wamachinga.

Mpaka kufikia Julai 5, 2011, Makasi alikuwa mzima wa afya, akitembea na kukimbia kwa miguu yake.

Rafiki yake mmoja waliekuwa wakiishi pamoja anamsimulia kama kijana aliyekuwa na ndoto kubwa, mtanashati na mwenye bidii ya kazi.

Julai 6, 2011 ndiyo siku ambayo Makasi alidhulumiwa uzima wa mwili wake na kuachiwa ulemavu wa kudumu.

Kosa lake lilikuwa kuzaliwa katika familia maskini, hali iliyomlazimu kwenda jijini Mwanza kwa ajili ya kujitafutia maisha.

Kama walivyo vijana wengi, baada ya kuhangaika huku na kule, hakuwa na chaguo zaidi ya kufanya biashara ya uchuuzi wa bidhaa na kuzipanga katika maeneo ya wazi kwa ajili ya kutafuta wateja.

Hata hivyo, kipindi hicho cha awamu ya nne (2005–2015), kilikuwa ni zama za giza kwa wamachinga nchi nzima.

Kama ambavyo imefafanuliwa katika sura yapili ya kitabu hiki, awamu ya nne ilianza mamlaka yake kwa barua iliyoandikwa na Waziri Mkuu kwa viongozi wa wa mamlaka wa majiji na miji mikubwa nchini ikiwaamuru kuwaondoa wamachinga kutoka maeneo ya katikati ya majiji.
Jijini Dar es Salaam pekee inakadiriwa kuwa wamachinga zaidi yamilioni 1 walitimuliwa kwa nguvu, na kusababisha hasara kubwa, ikiwemo majeraha na upotevu wa bidhaa.

Timua timua ziliendelea katika kipindi chote cha awamu ya nne na kuzua mapigano kati ya wamachinga, waliokuwa wakipigania haki yao ya kubaki katikati ya jiji, na mgambo waliotumwa kuwaondoa wamachinga kwa nguvu.

Mapigano hayo yalipelekea wakati mwingine askari kutoka Jeshi la Polisi kutumwa ili kuongezea nguvu kwa upande wa mgambo.

Endelea kwenye kitabu kilicho ambatanishwa hapa.

Angalizo:
Mchapishaji wa kitabu hiki anatoa ruhusa kwa mtu au taasisi yoyote kurudufisha, kunukuu na kuchapisha kitabu hiki kwa matumizi ya kielimu.


Kimehaririwa na Sabatho Nyamsenda

Dar es Salaam
2023
 

Attachments

  • Wamachinga-na-Haki-jiji-ebook.pdf
    1.6 MB · Views: 1
Back
Top Bottom