'Nyau' Kariakoo wanavyowaliza Wamachinga, nani yupo nyuma yao?

Nyakijooga

Senior Member
Dec 9, 2018
123
202
Ni uchunguzi wa Kundi la 'Wazalendo' uliofanyika kwa zaidi ya miezi mitatu katika eneo maarufu la Kariakoo Jijini Dar es Salaam.

Wazalendo hao wanabisha hodi kwenye eneo hilo ambalo lina mikusanyiko wa Watu wengi na hekaheka za kutosha katika pitapita Wazalendo wanakutana na wakina Mama vijana na watu wenye ulemavu wakifuta machozi na kulalamika.

Wazalendo walitaka kujua nini changamoto inayopelekea wahusika kutoa machozi na kunung’unika mithili ya watu waliotapeliwa na kisha kukosa msaada, jibu ni moja tu ambalo linatoka kwenye vinywa vyao "Tumechoshwa na Mgambo wa Jiji".

Wazalendo wanafanya Uchunguzi baada ya kutonywa

Ni Uchunguzi uliolenga kubaini tatizo, ambapo baadhi ya Wafanyabiashara wadogo maarufu kama 'Machinga' wanaotembeza biashara zao Mitaa ya Kariakoo wanadai mali zao kukamatwa na mgambo wa Jiji, ambao wamepewa jina la utani 'Nyau'.

Baadhi ya madai ambayo Wazalendo wanakumbana nayo ni kuwa mgambo hao wamekuwa wakiwakamata baadhi ya Wamachinga kwa kuwapiga na virungu kisha kuchukua mali zao kuzipeleka kwenye ofisi ya Machinga iliyoko Mtaa wa Pemba karibia na linapojengwa soko, huku mali nyingine zikipelekwa kwenye ofisi za Jiji.

'Waathirika hao' wanadai katika mchakato wa ukamataji Machinga hao wamekuwa wakipoteza au kuibiwa mali zao hali ambayo wengi wao imewafanya washindwe kupiga hatua.

Mmoja kati ya waliokumbwa na mkasa huo ni Juma Salim marufu kwa jina la 'vipensi', anadai amekumbana na changamoto ya aina hiyo kwa mara kadhaa.

"Ni kama mwaka sasa tunaharibiwa biashara walisema tusiweke maeneo yasiyo rasmi tutembeze biashara zetu wengi tukafuata utaratibu, mimi nauza soksi za wanafunzi na vitu vya urembo na Watoto kuchezea, kila wakija nyau lazima nipate hasara, wao wenyewe wanaweza kukuibia au katika kukusanya vitu vingine vikadondoka wao hawajali kama nimejinyima nimewekeza pale, tumeumizwa sana kiukweli" anaeleza Kipensi

Kauli ya Kijana huyo (26) mkazi wa Kigogo Jijini Dar es Salaam inaenda sambamba na Machinga wengine wanaodai kukumbana na mazingira hayo ambayo kwao wanaona kama kizungumkuti kwa kuwa wanadai kukosa mtetezi.

Pia Mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina Mama baraka ambaye anakabiliwa na changamoto ya ulemavu wa mguu, anaeleza juu ya kizungumkuti alichowai kukutana nao kwa mgambo wa Jiji.

"Kwa sasa unaniona nipo hapa naomba barabarani lakini sipendi kubakia kwenye hali hii, miaka ya nyuma nilikuwa hivi lakini kupitia pesa nilizopata kwa kuomba nikaamua kuwa nauza uza vitu mfano vitambaa vya kufutia jasho na nilikuwa nikipata hela lakini kutokana na changamoto ya miguu yangu nilikuwa siwezi kuzunguka huku na kule kama mnavyoona wengine wanafanya kwahiyo nilikuwa nakaa pale napanga chini nauza" anaeleza Mama huyo

Anaendelea kueleza "Lakini siku moja walikuja migambo wakachukua vitu vyangu wakasema nitawafuata kwenye Ofisi za machinga nikiwa na pesa ya faini elfu 30. Kiukweli mtaji wangu kama ulikuwa mkubwa elfu 45 sasa niliamua niwaachie mpaka leo sijawai kwenda nimerejea kwenye hali yangu ya zamani ya kuombaomba"

Nini kinabainika katika uchunguzi?
Kufuatia madai hayo Wazalendo waliamua kupiga kambi eneo hilo kubaini uhalisia wa madai hayo, ambapo kwa mara kadhaa walishuhudia mgambo wa Jiji sambamba na mgambo wanaojitambulisha kuwa wanatokea kwenye uongozi wa machinga Kariakoo wakikamata baadhi ya mali za machinga kwenye mitaa mbalimbali ya Kariakoo.

Wazalendo wanashuhudia ukamataji huo ukifanyika kwenye mazingira yenye utata, ambapo Watu hao wanaojiita migambo wamekuwa wakikamata mali na kwenda nazo kwenye zoezi lao endelevu la kuwakamata wengine, huku wakiwataka wahusika kuzifuata mali hizo kwenye ofisi za Machinga bila kuambatana nao wala kufanya utaratibu wowote wa kuhakiki mali hizo.

Hata hivyo kundi la Wazalendo linashuhudia mubashara baada ya mali hizo kufikishwa kwenye ofisi za machinga wahusika wakitakiwa kutoa elfu 30 ili wawarejeshee mali zao.

Ambapo wengi wao wamekuwa wakitoa pesa hiyo sambamba na wale ambao vitu vyao vimekuwa vikipelekwa kwenye ofisi za Jiji baadhi wamekuwa wakitakiwa kutoa hela bila risiti wala utaratibu rasmi wa kimaandishi ili mali zao ziweze kuachiliwa waweze kudelea na biashara kama kawaida.

Hata hivyo licha ya wahusika wengi kutoa pesa hizo lakini Wazalendo wameshuhudia manunguniko ya mara kwa mara juu ya baadhi ya mali za wahusika kutoonekana, ambapo baadhi ya wahusika wakiulizwa wamekuwa wakiwatisha kuwakamata na kuwaweka ndani, jambo hilo wengi wanadai kuwa wamekuwa wakibakia na manunguniko tu kutokana na kuhofia kukamatwa.

‘Kuna Ubaguzi kwenye ukamataji’
Uchunguzi unabaini mbinu mpya ambayo inatia mashaka ambayo imekuwa ikitumiwa na migambo hao. Mbinu hiyo ni kuwa kwa sasa wamekuwa na utaratibu wa kukusanya kiasi cha Sh.500 hadi 2,000 kila siku kwa Wamachinga ambao wamekuwa wakipanga au kuzungusha bidhaa eneo la Kariakoo, ambapo pesa hiyo inatolewa bila utaratibu rasmi mfano kutoa risiti.

Baadhi ya wahusika ambao wamekuwa wakigoma au kukwepa kutoa pesa hizo wamekuwa wakiangukia kwenye mikono ya migambo hao. Ambapo Wazalendo wanaelezwa na kushuhudia utaratibu huo kama umehalalishwa, hali ambayo inaacha maswali kwamba pesa hizo zinaenda wapi.

Sanjali na hayo baadhi ya viongozi wa machinga kwa kushirikiana na viongozi wa Jiji wamekuwa wakikodisha maeneo mbalimbali bila utaratibu rasmi ambapo uchunguzi unabaini yapo maeneo ambayo yanatozwa kuanzia elfu 30 mpaka laki mbili na wahusika wa baadhi ya maeneo wanakili wazi kuwa utaratibu wa malipo ambao umekuwa ukitumika sio wa kiofisi ni baina ya muhusika na waratibu wa maeneo hayo Jiji au Uongozi wa Machinga.

Jambo lingine linalobainika katika uchunguzi huo ni kutozingatiwa kwa haki za binadamu hususani katika zoezi la ukamataji ambapo baadhi ya Wanawake wamekuwa wakivamiwa na kunyanganywa bidhaa zao na maafisa wa kiume jambo ambalo wakati mwingine linafanya baadhi ya Wanawake kudhalilika mbele ya umati wa watu.

Katika mazingira hayo uchunguzi pia unabaini baadhi ya mgambo kuendesha oparesheni hizo wakiwa wamelewa hali ambayo wakati mwingine inachangia kuwepo kwa ugomvi baina ya anayekamatwa na mgambo hao kutokana na kutaka kutumia nguvu katika zoezi la kukamata mali sambamba kutumia lugha za matusi.

Uchunguzi unabaini kuwa hali hiyo ilianza baada ya Serikali kutangaza kuwaondoa wamachinga kwenye maeneo yasiyo rasmi, ambapo kwa Kariakoo zilifanyika oparesheni mbalimbali za kuwaondoa wahusika, ambapo baada ya zoezi hilo kuzoeleka baadhi waratibu wamekuwa wakilitumia kama fursa ya kujinufaisha kupitia 'kauli ya zuio'.

Nini kifanyike?

Wazalendo hao wanashauri Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI na vyombo vingine vya kiusalama kufanya uchunguzi wa utaratibu wa ukamataji unaoendelea Kariakoo tokea oparesheni ilipoanza, pia kufanya uchunguzi wa utaratibu unaotumika kukodisha maeneo ya wafanyabiashara wadogo wadogo ili kupata uhalisia wa masuala yanayoibuliwa kwenye makala hii.

Kuweka utaratibu rafiki kisha kuwachukulia hatua watakaobainika kwenda kinyume na taratibu hususani kujipatia pesa kinyume na taratibu kwa kutumia vibaya ofisi za umma.
 
Hao wazelendo hawajatimiza wajibu wao 100%

Ilitakiwa wachukue graphic evidence either picha au video za hao mgambo zipo namna nyingi za kuchukua hizo evidence bila kujulikana.
 
Back
Top Bottom