Walimu: Hatukubali tumepunjwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
Walimu: Hatukubali tumepunjwa
Mwandishi Wetu
Daily News; Sunday,November 23, 2008 @20:05

Chama cha Walimu (CWT) kimesema madai ya walimu bado ni mabichi kutokana na walimu wengi wanaodai kupunjwa fedha zao, licha ya serikali kuahidi kufanya malipo yote. Rais wa CWT Gratian Mukoba aliliambia gazeti hili jana kuwa taarifa alizozipata kutoka ofisi nyingi za wilaya zinaonyesha kuwa licha ya majina kubandikwa, lakini malipo ni tofauti na madai yao halali.

Kiongozi huyo wa walimu alisema licha ya serikali kutangaza kufanya malipo yote; ameshangazwa na hatua ya baadhi ya walimu kukatwa malipo yao. Alisema kutokana na malalamiko hayo, chama chake kitaitisha baraza kuu la chama hicho kuona watafanya nini kutokana na malalamiko kuongezeka.

“Tutaitisha wakati wowote baraza kuu kufanya tathmini ya malipo ya walimu,” alisema Mukoba. Aliongeza kuwa bado walimu wa sekondari hawajaanza kulipwa kiasi chochote cha fedha. “Hata mimi naidai serikali na hakuna mwalimu wa sekondari aliyelipwa.”

Alisema hesabu za chama hicho zinaonyesha kuwa walimu wanadai zaidi ya Sh bilioni 16, lakini kiasi hicho kinaweza kuwa kimeongezeka kwa vile madai ya walimu yanazidi kuongezeka. Kiongozi huyo wa walimu, alisema anaamini kuwa baada ya nchi wahisani kuisamehe deni Tanzania, ilitangazwa kuwa fedha hizo zingepelekwa katika sekta ya elimu, lakini walimu wamebaki watu wa kuonewa.

“Kule kwenye halmashauri imeenda orodha ya walimu, lakini fedha hazijaenda, huu ni uonevu mkubwa,” alisema Mukoba. Alisisitiza kuwa kile ambacho kitaamriwa na Baraza Kuu itakuwa ni uamuzi mzito kwani yeye kama kiongozi wa walimu alishaapa wataendelea kugoma hadi mwalimu wa mwisho alipwe haki zake.

Madai ya Mukoba yaliungwa mkono na baadhi ya walimu waliozungumza na gazeti hili, wakiwamo wa Dar es Salaam ambao walidai malipo ambayo wamelipwa ni ya nauli tu. “Tumelipwa nauli, malimbikizo mengine bado, wametupooza, eti tutalipwa pamoja na mishahara yetu,” alisema Mwalimu aliyejitambulisha kwa jina la Beatrice Mwerinde.

Mmoja wa walimu wa wilayani Bagamoyo, Bether Kalyege alisema hawajalipwa malipo yoyote yale. “Hatujajua tutalipwa lini malimbikizo yetu, tunasuburi tuone mwisho wa mwezi maana hata mshahara wenyewe hatujalipwa.” Mwalimu mwingine wa Halmashauri ya Rufiji aliyejitambulisha kwa jina la Mwinyimkuu, alisema yeye anadai fedha za uhamisho na malimbikizo kadhaa, lakini jina lake halimo.

“Ndugu yangu sijui cha kufanya, jina langu halimo, nataka nikamwone mkurugenzi aniambie sababu ya mimi kutokuwapo kwenye orodha wakati nilishawasilisha madai yangu,” alisema mwalimu huyo. Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Profesa Khamis Dihenga alisema wizara yake kwa kushirikiana na Tamisemi watafanya ukaguzi katika shule mbalimbali juu ya malalamiko hayo ya walimu.

Alisema walimu wa shule za msingi na sekondari wataelezwa taratibu za malipo zilivyofanywa na kama kuna walimu wenye malalamiko pia watayasikiliza. Alisema baada ya malipo hayo kufanywa na halmashauri zote, ofisi yake kwa kushirikiana na Tamisemi wameandaa timu ambayo itazunguka kila shule kuzungumza na walimu kusikiliza malalamiko ya walimu ambao watakuwa hawajalipwa au wamelipwa pungufu.

“Kama mtu amelipwa pungufu tutamweleza sababu ya yeye kulipwa pungufu ya kiasi alichoomba, lakini kama kuna mapungufu ya stakabadhi alizowasilisha pia tutamweleza,” alisema Profesa Dihenga. Alisema malengo ya utaratibu huo ni kutaka suala la madai ya walimu limalizike na kila mwalimu awe ameridhika kuhusu madai yake aliyokuwa anadai.

Kuhusu walimu wa Sekondari kutokuanza kulipwa, alisema walishawasilisha orodha Hazina na utaratibu wa kuwalipa bado unaendelea kufanywa na wizara hiyo. Hivi karibuni serikali ilitangaza kupeleka zaidi ya Sh bilioni 12 katika halmashauri mbalimbali kwa ajili ya kuwalipa walimu madai yao mbalimbali.
 
Serikali yetu ni ya kisanii kweli. Wanasubiri mpaka walimu wagome na watoto wetu waandamane kwa kukosa kufundishwa?
Hapa utasikia wanatumia visingizio kwamba madai mengine si halali ili kutumia delaying tactic wakati wanajua mwisho wa yote lazima walipe. Hapa ndipo mimi nachoka kabisa. Tukiendelea kwa kamtindo haka ka kutosema ukweli basi tumekwisha.
Hivi hivi ndivyo walivyowafanya wale wastaafu wa jumuiya ya afrika mashariki. Walikula pesa yao tangu 1977 na sasa wanatumia kila kisingizio ili wasilipe. Hata wengine wamekufa bila kulipwa mafao yao, lakini wao viongozi wetu wanapostaafu check huwa ziko mezani. Kwa ujinga wetu tunawataka wapumzike kwa amani. Amani gani? kuna amani katika wizi wa wazi wazi huu?
 
Back
Top Bottom