Walikuwa ni wauaji wadogo wa Kishetani.........! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Walikuwa ni wauaji wadogo wa Kishetani.........!

Discussion in 'Mahusiano, mapenzi, urafiki' started by Mtambuzi, Feb 3, 2012.

 1. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #1
  Feb 3, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280

  front_page_six.jpg
  Natasha, kiongozi wa wauaji
  db_GirlsJail4.jpg
  Natasha na wenzake wakiwa Gerezani
  lillelidFamily.jpg
  Lillielid na Familia yake kabla ya kuuawa


  Ilikuwa ni jumapili majira ya saa 2:20 usiku, April 6, 1997, kitengo cha ulinzi wa jamii katika mji wa Greene County ulioko jimboni Tennessee nchini Marekani, kilipokea simu kupitia namba ya dharura ya kupokelea matuki ya uhalifu au hatari inayotumika nchini humo. Mpiga simu alitoa taarifa kuwa katika eneo lao imesikika milio ya bunduki. Iliwachukuwa dakika 10 askari wawili waliokuwa zamu katika kitengo hicho, Sajenti Frank Waddell na mkuu wa Kitengo hicho msaidizi Jeff Morgan kufika kwenye eneo la tukio.

  Walipofika tu kwenye eneo hilo walipokelewa na hali ya kutisha, kwani kulikuwa na miili ya watu wawili iliyokuwa imelala chini huku ikivuja damu na hivyo kufanya eneo lote la tukio kutapakaa damu. Miili hiyo ilikuwa imelala pembezoni mwa barabara na ilikuwa ni ya mwanaume na mwanamke. Kwa haraka haraka walionekana kama wanakaribia kufikisha umri wa miaka thelathini au ndio wanatimiza miaka thelathini. Wote wawili walikuwa wamepigwa risasi kadhaa mwilini na walikuwa wameshakufa.

  Katika mwili wa mwanamke kulikuwa na mtoto mchanga wa kiume ambaye alikuwa amemlalia mwanamke huyo huku akikoroma na pembeni kidogo kulikuwa na binti wa miaka mitano au sita ambaye naye alikuwa amepigwa risasi, lakini aligundulika kuwa bado yuko hai, ingawa alikuja kufariki saa kadhaa baadae akiwa anatibiwa hospitalini.

  Hata hivyo, yule mtoto mchanga ambaye alikuwa amepigwa risasi ya jicho na kwenye nyonga, kama miujiza, madaktari walifanikiwa kuokoa maisha yake, ingawa alibaki kuwa kipofu wa jicho moja na mlemavu wa kudumu. Akieleza hali aliyoikuta katika eneo la tukio mbele ya waandishi wa habari, mkuu wa kitengo cha usalama wa jamii katika eneo hilo Terry Jones, huku akitokwa na machozi alisema "Kwa jinsi tulivyokuta watoto wale ilionekana kama vile walikuwa wamekumbatiwa na wazazi wao kabla hawajakata roho, na ukweli ni kwamba hatufahamu majina yao au kama ni watu wa familia moja au la, hakuna Pochi, vitambulisho, fedha au kitu chcochote kilichopatikana kutoka katika eneo la tukio, ambacho kitaweza kurahisisha kuwatambua wahanga hawa" Aliendelea kufafanua mkuu huyo wa kitengo cha jamii Terry Jones.

  Mkuu huyo aliendele kuwaambia waandishi wa habari kuwa hata gari walilokuwa wakisafiria wanafamilia wale nalo halikuwepo katika eneo hilo la tukio. Akijibu mojawapo ya maswali ya waandishi wa habari, Jones alisema kwamba, hata mwonekano wa familia ile uliashiria kuwa ilikuwa ni familia ya watu wanaoheshimika, hivyo mpaka kufikia hapo wanalichukulia tukio lile kama la mauaji ya kihalifu.

  Hata hivyo polisi walikuta gari lingine aina ya Chevrolet likiwa limekwama kwenye mtaro umbali wa mita chache kutoka katika eneo la tukio na namba zake pamoja na vielelezo muhimu vinavyohitajika kuwepo kwenye gari vilikuwa vimeng'olewa, na hata taa ya za mbele za gari hilo zilikuwa bado zinawaka. Jones aliendelea kusema kuwa anaamini kuwa huenda gari lile aina ya Chevrolet lilikuwa likiendeshwa na wauaji, na analazimika kuamini kuwa wauaaji walikuwa ni zaidi ya mtu mmoja, ambapo waliwalazimisha wanafamilia wale kuendesha gari lao mpaka katika eneo la tukio na baada ya kuwauwa waliamua kutoroka na gari la wanafamilia ile.

  Uchunguzi wa awali ulionesha kuwa gari lile la aina ya Chevrolet lilikuwa likimilikiwa na na mama mmoja aitwae Mary Castle, karani wa duka anayeishi Paintsville katika jimbo la Kentucky nchini humo. Akihojiwa na askari wa upelelezi wa Paintsville aitwae Tom Haney alidai kwamba gari lake liliazimwa na mwanae wa kiume aitwae Joseph Risner (21) siku mbili nyuma na tangu alipochukua gari lake hajapata kumuona, si yeye wala gari. Mama huyo alitoa picha ya mwanae huyo na Haney aliituma kwa njia ya fax haraka kwenda Greene County katika kitengo cha ulinzi wa jamii.

  Wakati huo huo askari wa Tennessee waliitambua miili ya wanafamilia ile kuwa ni ya Vidar Lillelid aliyekuwa na umri wa miaka 34 mhamiaji kutoka nchini Sweden, mkewe Delfina aliyekuwa na miaka 28, binti yao aitwae Tabitha aliyekuwa na umri wa miaka 6 na mtoto wao mdogo wa kiume aitwae Peter aliyekuwa na umri wa miaka 2. Familia ile ilikuwa inasafiri ikitokea katika mji wa Johnson ulioko katika jimbo la Kentucky, walikokwenda kuhudhuria mkutano mkuu wa kidini wa dhehebu la mashahidi wa Jehova.

  Majira ya sa saba na robo za mchana ikiwa ni kabla ya kutimia masaa 24 tangu tukio lile kuripotiwa gari la Lillelid lilikamatwa na askari wa upande wa Mexico, kutokana na nyaraka za umiliki wa gari lile kutiliwa mashaka na askari wa upande huo. Watu wote sita waliokuwa wakisafiri na gari hilo wakiwa ni wavulana watatu na wasichana watatu walikamatwa kwa kutuhumiwa kuiba gari na kuhusika na mauaji ya familia ya Lillelid.

  Vijana hao walitambuliwa kwa majina ya Joseph L Risner, aliyekuwa na umri wa miaka 21, Dean Mullins na Karen Howel wote wakiwa na umri wa miaka 20, Natasha Cornet na Crystal Renea Sturgil wakiwa na umri wa miaka 18 na Jason Blake Bryant aliyekuwa na umri wa miaka 15, wote wakiwa ni wakazi wa Paintsville katika jimbo la Kentucky. Vijana hao walikuwana muonekanao wa kihuni kama walivyo watumiaji wa madawa ya kulevya, kwani walikuwa wamejichora katika miili yao picha za kutisha huku wakiwa wamejitoga masikioni puani, kwenye ulimi, kidevuni, midomoni, kwenye nyusi, na kujivika vipuri, pia walikuwa wamekata nywele zao katika mitindo ya ajabu.

  Wapelelezi wa Tennesee walipata shida kidogo katika kufuatilia nyendo za vijana wale kutokea Kentucky hadi katika mpaka wa Mexico. Kwa mujibu wa maelezo ya watuhumiwa ilionesha kwamba, watuhumiwa wote sita walikutana April 6, 1997 na walipanga kusafiri kwenda katika jimbo la New Orleans ambapo wangekutana na marafiki zao. Risner aliazima gari la mama yake aina ya Chevrolet na wote sita waliondoka na gari hilo hadi kwa afisa mmoja wa kitengo cha uthibiti wa silaha na kuvunja kisha wakaiba bastola aina ya Caliber namba 25 na makasha mawili ya risasi pamoja na fedha kiasi cha dola 500 za Kimarekani.

  Baada ya wizi ule, vijana hao wote sita walisafiri kupitia barabara kuu ya kusini kuelekea jimboni Virginia. Majira ya saa 12:20 za jioni wakiwa wanakatisha viunga vya maeneo ya Virginia walisimamishwa na askari wa usalama barabarani na kutozwa faini kwa kuendesha gari kwa mwendo wa kasi. Risiti waliyopewa baada ya kulipa faini ilikutwa kwenye eneo la tukio. Kwa kujibu wa askari wa usalama barabarani wa Virginia walikiri kwamba vijana wale hawakuwa wamelewa wala kuonekana kama walikuwa wametumia dawa za kulevya. Saa moja baadae gari hilo lilionekana likiwa limeegeshwa kando ya barabara kuu iendayo katika mji wa Greene County Tennesee. Kwa mujibu wa shuhuda aliyeliona gari hilo lililokuwa na vijana hao sita, waliokuwa na muonekano wa kihuni alidai kwamba gari hilo lilikaa katika eneo hilo kwa takribani dakika 45.

  Wakati huo huo familia ya Lillelid ilikuwa ikisafiri kurejea nyumbani kwao matika mji wa Powell jimboni Tennessee wakiwa katika msafara wa mgari kadhaa yaliyokuwa yakiendeshwa na marafiki zao ambao wote walikuwa wakitokea katika mkutano mkuu wa kidini wa mashahidi wa Jehova. Inasemekana, Lillelid alikuwa amechoka hivyo akaamua kuegesha gari lake pembeni ya barabara ili apate kupumzika, na kuwaacha rafiki zake wakiendelea na safari. Kumbe wakati Lillelid anaegesha gari lake hakujua kama jirani kulikuwa na gari lingine aina ya Chevrolet limeegeshwa likiwa na vijana sita ambao wangekuja kumdhuru.

  Mmoja wa mashuhuda alidai kwamba waliwaona watuhumiwa wakiongea na Lillelid na kisha waliyaona magari yote mawili yakiondoka kutoka katika eneo lile. Polisi wanaamini kwamba huenda gari la Lillelid lilitekwa na watuhumiwa na kundeshwa na mmoja na watuhumiwa hadi katika eneo la tukio ambapo waliwapiga risasi wote na kuwauwa lakini wakimuacha mtoto Peter akiwa amejeruhiwa vibaya.

  Huku wakiamini kwamba wamewauwa wote, watuhumiwa waliamua kuondoka na magari yote mawili yaani lile la kwao aina ya Chevrolet pamoja na lile la Lillelid, lakini kutokana na wembamba wa barabara waliyoingia, gari lao lilikwama kwenye mtaro. Ili kuepuka kupoteza muda waliamua kutelekeza gari lao, lakini kabla ya kulitelekeza gari hilo, waling'oa namba za gari pamoja na nyaraka muhimu ambazo zingefanya gari lile kufahamika mmiliki wake kirahisi. Walichukua fedha, vitu vya thamani na vitambulisho vyote walivyokuwa navyofamilia ya Lillelid ili kuchelewesha kutambuliwa kwao.

  Baada ya kukamatwa watuhumiwa wote sita walirejeshwa katika mji wa Greene County Tennessee wakitokea katika jimbo la Arizona na kuwekwa katika gereza kuu la mji huo kwa mahojiano zaidi. Siku chache baada ya watuhumiwa wote kuwekwa rumande, walikiri kwamba Natasha Cornett ndiye aliyekuwa mkuu wa kikundi na pia msemaji mkuu.

  Natasha aliwashangaza askari wa upelelezi pale aliposema kwamba yeye ni mtumishi wa shetani na alifafanua kwamba amekuwa akiwasiliana na shetani tangu akiwa na umri mdogo. Akihojiwa na polisi kuhusiana na maelezo yake hayo, kwa maneno yake mwenyewe Natasha alisema , "Nadhani nilikuwa naitwa na mtu nisiyemwona, na kulikuwa na roho nisiyoiona ambayo ilikuwa ikizungumza na mimi tangu nikiwa na umri wa miaka miwili. Nimekuwa kwa umri na kimo huku nikiandaliwa kuwa mtumishi wa shetani"

  Akjibu mojawapo ya maswali ya askari wa upelelezi, Natasha alikiri kuwa yeye ni mpinzani wa Masihi Yesu Kristo na binti wa shetani. Natasha alizidi kusisitiza kuwa maisha yake yalitawaliwa na nadharia za ajabu kiasi cha kuasi imani ya kikristo aliyokuwa nayo mama yake. Maelezo ya Natasha yalitoka katika vyombo vya habari nchini Marekani na hivyo kutomfurahisha wakili aliyekuwa akimtetea aitwae Eric Conn. Hata hivyo wakili huyo alimuonya Natasha kutoongea na waandishi wa habari au mtu yeyote kuhusiana na kesi hiyo.

  Na ili kujenga mazingira mazuri ya kumtetea mteja wake, wakili huyo aliitisha mkutano wa vyombo vya habari na kukanusha madai yaliyokuwa yakitolewa na mamlaka ya kisheria jimboni Tennessee kwamba mauaji yaliyofanywa na watuhumiwa yalikuwa ni utekelezaji wa imani ya dini ya kishetani na badala yake wakili huyo alisisitiza kwamba watuhumiwa walikuwa na matatizo ya kiakili, ambapo wanalindwa kisheria na kifungu kinachowalinda watu wenye matatizo ya kiakili dhidi ya makosa waliyoyafanya.

  "Kila mtu anayeizungumzia kesi hii anaihusisha na dini ya kishetani, hiyo si sahihi hata kidogo," alikanusha wakili Eric Conn, na hakusita kusema hadharani kuwa atatumia kifungu cha sheria kinachowatetea watu wenye matatizo ya kiakili dhidi ya makosa waliyoyafanya. "Huwezi kuyatenganisha makosa haya na matatizo ya kiakili kwa sababu kulikuwa na nguvu isiyo ya kawaida iliyokuwa ikiwaendesha vijana hawa kufanya yale waliyoyafanya," alisema wakili huyo. Hata hivyo pamoja na Natasha kukatazwa kuongea na vyombo vya habari au mtu yeyote kuhusiana na kesi ile, hakuacha kuzungumza na vyombo hivyo kuhusiana na imani yao ya kishetani yeye na watuhumiwa wenzake.

  "Kuna wakati najihisi kama nimerukwa na akili, lakini hapana, nadhani mimi sio mwendawazimu" alinukuliwa akisema Natasha. Kwa mujibu wa rafiki zake, Natasha alijulikana kama binti aliyekuwa na tabia ya kuongoza wanaume na tabia hiyo amekuwa nayo hata katika kikundi chao. Natasha alikanusha kwamba alikuwa ni kiongozi wa kundi lao.

  "Mimi sikuwa na wafuasi na sisi sio wafuasi wa dini ya kishetani bali ni kikundi cha marafiki tulio na utashi wa aina moja" alisema Natasha. Akizungumzia juu ya minong'ono iliyoanza kuenea kwamba, yeye Natasha alikuwa na uhusiano maalum wa kusagana (Lesibian) na mtuhumiwa mwenzie Karen Howell, Natasha alikanusha tuhuma hizo pia. Akizungumza juu ya minong'ono hiyo, Natasha alisema, "Karen ni rafiki yangu wa karibu na sio urafiki wa kusagana. Kwa kawaida huwa tunabusiana lakini sio kama mnavyofikiria"

  Natasha aliongeza kuwa alikuwa na mpango unaoratibiwa na shetani wa kuwaandaa vijana wote duniani ili waasi. Alidai kwamba vita ya mwisho ya Armageddon iko karibu kuanza lakini baba yao shetani hajawaambia tarehe maalum vita hiyo itakapoanza, na aliwaomba waandishi wa habari wawatangazie watoto wote ulimwenguni kusimamia haki na imani zao kwa kuzipigania kwa jinsi watakavyoweza. (Armageddon ni vita takatifu vilivyozungumziwa katika Biblia agano jipya itakavyopiganwa mwiso wa dunia kati ya wafuasi wa shetani na watakatifu kwa mujibu wa maandiko ndani ya Biblia)

  Natasha aliongeza kusema kuwa anamwamini wakili wake Eric Conn na nguvu za shetani, "naamini baba yangu shetani atanisaidia na kunilinda" alisema Natasha. Mnamo Novemba 1997 watuhumiwa wote walifikishwa katika mahakama ya Greene County na kusomewa mashitaka 29 wote kwa pamoja. Jaji aliyekuwa akiendesha kesi hiyo James Backner alikataa mapendekezo yaliyotolewa na jopo la mawakili waliokuwa wakiwatetea watuhumiwa kuwa kila mmoja ashitakiwe na kosa lake.

  Jaji huyo alisema, watuhumiwa wote watashitakiwa kama kundi. Wakati kesi hiyo ikiendeshwa, siri nyingi za watuhumiwa zilianikwa pale mahakamani. Akitoa ushahidi wake mama yake Natasha aitwae Madona Wallen aliiambia mahakama kuwa mwanaye alikuwa ni mfuasi wa shetani na alikuwa ni muumini wa Ouija Board, ambayo ni imani kuwa watu walio hai wanaweza kuwasiliana na watu waliokufa. Mama huyo alikiri kuwa, kuna wakati aliwahi kumuona mwanae, midomo yake ikiwa imetapakaa damu baada ya kunywa damu. Naye rafiki wa karibu wa Natasha aitwae John Slayer aliyekuwa na umri wa miaka 19 akitoa ushahidi wake mahakamani alikiri kwamba, siku moja Natasha na mwenzie Karen walimuomba wamkate kifuani ili wapate kunyonya damu, naye akawaruhusu, ndipo wakamfunga kitambaa usoni kisha wakamkata na kuanza kumnyonya damu. John alikiri pia kuwa zoezi hilo la kunyonya damu liliendelea kwa mtuhumiwa mwenzao John Risner na rafiki yao mwingine aitwae Jason Cecil.

  Jambo lililowashangaza watu wengi wakati wa kusikilizwa kwa kesi hii ni kitendo cha Crystal Sturgil kumtaja mtuhumiwa mwenzake mwenye umri mdogo kabisa kuliko wote Jason Bryant kuwa ndiye aliyefyatua risasi na kuwauwa Lillelid na familia yake. Wakati huo Jason alikuwa amehifadhiwa kwenye jela ya watoto ya Arizona akisubiri kusikilizwa kwa shauri lake tofauti na wenzie kutokana na umri wake.

  Hata hivyo, kuna wakati alinukuliwa na mfungwa mwenzie aitwae Richard Arvizo akijisifu kwa kuuwa. Kwa mujibu wa maelezo aliyoandikisha polisi chini ya kiapo, Richard alidai kuwa, alipomuuliza Jason kama anajisikiaje kuuwa ? Jason alijibu kwamba, kuuwa huwa kunampa furaha na nguvu za ajabu. Ushahidi mwingine uliotolewa pale mahakamani ni ule wa mwalimu aliyekuwa akimfundisha mmoja wa watuhumiwa Dean Mullins. Akizungumzia tabia ya mwanafunzi wake wa zamani, mwalimu huyo alikiri kwamba, kuna wakati aliwahi kutoa zoezi la kuandika insha.

  Mwalimu huyo anakumbuka maelezo yaliyoandikwa na Dean Mullins kuhusiana na namna ya kutoa macho kwenye mwili wa mtu aliyekufa. Katka maelezo yake juu ya nadharia hiyo, Dean aliandika, "Imesemwa kuwa macho ni ufunguo wa rohoni, kwa hiyo kama nikiyachukua macho ya watu waliokufa nitakuwa nimechukua na roho zao pia, napenda sana nadharia hiyo"

  Mtuhumiwa mwingine Crystal Sturgil maelezo yake yalikuwa ni yakusikitisha. Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa mahakamani, ilibainika kwamba binti huyo alilazimika kukimbia nyumbani kwao na kuishia kuhama hama kutoka kwa ndugu huyu hadi mwingine kutokana na kunyanyaswa kijinsia na baba yake wa kambo.

  Karibu watuhumiwa wote walikuwa wanatokea katika familia zilizosambaratika na zilizowapuuza. Lakini hiyo haikumfanya mwanasheria Berckley Bell kuyafumba macho yake dhidi ya yale yaliyofanywa na watuhumiwa hao. Akizungumzia juu ya adhabu wanayostahili watuhumiwa pindi wakipatikana na hatia, mwanasheria huyo aliitaka mahakama itoe adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa watuhumiwa wanne waliokuwa na umri zaidi ya miaka 18, ambao ni Joseph Risner, Dean Mullins, Crystal Sturgill pamoja na Natasha, na adhabu ya kifungo cha maisha bila uwezekano wa kupewa msamaha kwa watuhumiwa wawili waliokuwa na umri wa miaka 18 ambao ni Jason Bryant na Karen Howell.

  Mnamo February 20, 1998 watuhumiwa wote walifikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka na Jaji James Backner. Jaji Backner alipomaliza kuwasomea mashitaka aliwauliza kama watuhumiwa wote kwa pamoja wanakubaliana na mashitaka yote yaliyosomwa mbele yao au la. Jibu lililotoka kwa watuhumiwa wote lilikuwa ni "ndiyo tunakubaliana na mashitaka yote tuliyosomewa"

  Siku ya hukumu, Jaji wa mahakama hiyo alisoma hukumu ambapo aliwahukumu watuhumiwa wote kifungo cha maiasha jela bila uwezekano wa msamaha wa parole. Mara baada ya kumalizika kusomwa kwa hukumu hiyo, dada wa Delfina Lillelid aitwaye Ivette Zelaya alimpongeza jaji kwa kutoa hukumu hiyo, ambayo aliieleza kama adhabu nzuri inayowastahili watuhumiwa zaidi ya kunyongwa.

  Akiongea na waandishi wa habari Zelaya alisema , "Ninayo furaha kubwa kwamba vijana hawa hawatapata fursa ya kuishi maisha wanayoyataka kwa kitendo chao cha kudhulumu roho ya dada yangu na familia yake na kuziacha familia zao zikiwa salama"
   
 2. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #2
  Feb 3, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Kama kawaida, nimeweka habari hii siku ya leo Ijumaa kwa sababu najua ni ndefu, na kwa kuwa tunaanza weekend nimeona wasomaji wengi watakuwa na muda mzuri wa kusoma na kujifunza kupitia habari hii ambayo imesheheni mambo mengi ya kujifunza hususan kwa wazazi, walezi na wazazi watarajiwa kuhusiana na swala zima la malezi kwa watoto wetu.

  Kwa wale wanaume wenzangu na wanawake ambao wametelekeza watoto wao, huu ni wakati muafaka wa kuangalia kizazi tunachokitengeneza, kwani watoto bila malezi mazuri inawezekana wakawa ni janga si la kitaifa tu bali kwa dunia yetu hii ambayo haikuwa ni mpango wa Mungu kuwa kama ilivyo leo hii.

  Nawatakia mapumziko mema............................................
   
 3. Fidel80

  Fidel80 JF-Expert Member

  #3
  Feb 3, 2012
  Joined: May 3, 2008
  Messages: 21,976
  Likes Received: 104
  Trophy Points: 145
  Mwishoni uwe unasamalaizi wengine wavivu kusoma mwanzo mwisho.
   
 4. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #4
  Feb 3, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  @Fidel80-Nimeweka wazi kwamba ni vyema ukaisoma habari hii ukiwa umejipumzisha nyumbani na familia yako au ni vyema ukawasomea hata watoto wako maana watajifunza mengi kupitia habari hii.......................... Nakutakia mapumziko mema wya mwishoni mwa Juma

   
 5. arabianfalcon

  arabianfalcon JF-Expert Member

  #5
  Feb 3, 2012
  Joined: Oct 19, 2010
  Messages: 2,292
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 135
  Unkooo, nzuri lakini ndefuu!
   
 6. fazaa

  fazaa JF-Expert Member

  #6
  Feb 3, 2012
  Joined: May 20, 2009
  Messages: 2,986
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
 7. Lokissa

  Lokissa JF-Expert Member

  #7
  Feb 4, 2012
  Joined: Nov 20, 2010
  Messages: 7,079
  Likes Received: 155
  Trophy Points: 160
  ahsante baba kwa hadithi yao nzuri nimeisoma hadi mwisho.
  ,kweli ukitaka kumkamata mtanzania mwandikie kitu hatasoma
  uvivu ni mwingi mno wa kusoma ndio maana tunadhulumiwa haki zetu bila kujua
  igeni kwa wenzetu hapo kenya, nako umangani kibibi na kibabu kimezeeka lkn unakutana nacho kwneye train au basi kumeshika kitabu kinasoma sisi vijana wa bongo tunapenda kitafuniwa lol.
  sheria zipo kwenye mtandao wa bunge lkn unakuta mtu anakuuliza haki zake ktk kazi nk kumbe angejisomea angeelewa kuliko kuangalia tv mda mwingi na pia kupekuwa pekua habari ktk mtandao na magazeti kunakuongezea upeo.kwa wenzetu Uk kuna tax fulani inapita mtaani watu wanaikodi bila kujijua wanaulizwa maswali mbalimbali na wakishinda wanapata miji euro kibao na ni maswali ya kawaida tu wanaulizwa,kama husomi magazeti au vitabu au kufuatilia matukio mbali mbali duniani we ni binadamu gani????
  wekend njema
   
 8. Hagga

  Hagga Member

  #8
  Feb 4, 2012
  Joined: Jan 24, 2012
  Messages: 36
  Likes Received: 0
  Trophy Points: 0
  Hadithi ni nzuri sana, urefu si hoja maana inavutia sana hata ingekuwa kurasa mia bado kama unavutia ntaendelea kusoma bila kuchoka.
   
 9. Horseshoe Arch

  Horseshoe Arch JF-Expert Member

  #9
  Feb 4, 2012
  Joined: Aug 10, 2009
  Messages: 11,230
  Likes Received: 4,951
  Trophy Points: 280
  Mkuu nimeiprint...nitaipitia nikiwa kwenye ujenzi wa Taifa
   
 10. p

  punainen-red JF-Expert Member

  #10
  Feb 4, 2012
  Joined: Nov 18, 2010
  Messages: 1,735
  Likes Received: 11
  Trophy Points: 0
  Watu wanaoona kuwa simulizi hii ni ndefu ni wa kuhurumiwa tu... Big up mkuu Mtambuzi!
   
 11. Mgombezi

  Mgombezi JF-Expert Member

  #11
  Feb 4, 2012
  Joined: Mar 23, 2009
  Messages: 630
  Likes Received: 16
  Trophy Points: 0
  Mara nyingi nasoma story zako, BIG UP Bro!, kuna jambo la kujifunza katika suala la malezi.
   
 12. bucho

  bucho JF-Expert Member

  #12
  Feb 4, 2012
  Joined: Jul 13, 2010
  Messages: 4,547
  Likes Received: 427
  Trophy Points: 180
  Duh sio mchezo kabisa .
   
 13. The Mockingjay

  The Mockingjay JF-Expert Member

  #13
  Feb 4, 2012
  Joined: Jan 11, 2011
  Messages: 380
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 35
  Nimeisoma yote non stop. Very sad. Thank you for sharing
   
 14. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #14
  Feb 5, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280
  Thanks Mtambuzi siku nyingine ukiwek hizi habari zako uwe unanishitua maana huwa ni nzuri ,tunapata mambo ambayo wengine tulikuwa hatuyajui.
   
 15. King'asti

  King'asti JF-Expert Member

  #15
  Feb 5, 2012
  Joined: Nov 26, 2009
  Messages: 27,508
  Likes Received: 2,249
  Trophy Points: 280
  Dah! Mungu atusaidie manake unadhani litoto linasoma na wenzie kumbe yananyonyana damu!
  Dingi, hapo ndo nakumbuka wimbo wa zamani!
  Ee Mungu uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia
  Usinipe utajiri wala umaskini!
   
 16. BADILI TABIA

  BADILI TABIA JF-Expert Member

  #16
  Feb 5, 2012
  Joined: Jun 13, 2011
  Messages: 30,873
  Likes Received: 6,226
  Trophy Points: 280
  thanx
  kuha funzo hapa, malezi ya watoto muhimu sana
   
 17. FirstLady1

  FirstLady1 JF-Expert Member

  #17
  Feb 5, 2012
  Joined: Jul 29, 2009
  Messages: 16,575
  Likes Received: 541
  Trophy Points: 280

  Fidel80 acha uvivu
   
 18. K

  Konya JF-Expert Member

  #18
  Feb 5, 2012
  Joined: Jun 4, 2011
  Messages: 920
  Likes Received: 10
  Trophy Points: 35
  ni story ya kusisimua,yenye mvuto,majonzi na mafundisho pia
   
 19. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #19
  Feb 6, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Nitakuwa naku-PM kilanikiweka kitu kipya................Nafikiria kuanzisha utaratibu wa kuweka mada za namna hii kila Ijumaa kwa ajili ya kusomwa mwishoni mwa Juma pale wanafamilia wanapokuwa wamejumuika pamoja.................mie huwa simulizi hizi nawasomea wanangu mida ya jioni tukiwa tunasubiri mlo wa usiku. Ngina anapenda kweli simulizi za aina hii.
   
 20. Mtambuzi

  Mtambuzi Platinum Member

  #20
  Feb 6, 2012
  Joined: Oct 29, 2008
  Messages: 8,795
  Likes Received: 1,247
  Trophy Points: 280
  Mwanangu Mwenye-enzi Mungu atuepushe na hili balaa...........................
   
Loading...