KERO Wakuguzi wa Mikopo ya Vijana wana changamoto

KERO Wakuguzi wa Mikopo ya Vijana wana changamoto

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Mikopo ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu imeanzishwa kwa lengo jema, hasa katika kipindi hiki ambacho changamoto ya ajira imekuwa kubwa nchini. Mfumo huu umekuwa msaada muhimu kwa wengi katika kujiajiri, kukuza biashara ndogo ndogo na kuinua uchumi wa wananchi. Hata hivyo, bado kuna changamoto kubwa katika mchakato wa utoaji wa mikopo hiyo kutokana na baadhi ya watendaji na wakaguzi wa miradi kutotekeleza majukumu yao kwa uadilifu na haki.

Baadhi ya wakaguzi wamekuwa wakitoa vitisho kwa vikundi vya waombaji wa mikopo, ikiwemo kutishia kutopitisha miradi au kutokutoa fedha kwa mfumo wa cash endapo vikundi hivyo havitafuata masharti wanayoyataka wao binafsi.

Aidha, kumekuwa na tabia ya kupunguza kiwango cha fedha kilichoombwa kwenye andiko la mradi bila kuzingatia mahitaji halisi ya mradi husika. Mfano, mradi unaoomba milioni 60 au 70 unaweza kuidhinishiwa milioni 20 au 30 pekee, jambo ambalo linaathiri moja kwa moja utekelezaji na mafanikio ya mradi wenyewe.

Mbaya zaidi, baadhi ya wakaguzi hao hao, pale ambapo mradi unahusisha ununuzi wa vifaa, hutaka wao wawe wasimamizi wa manunuzi hayo na kuvilazimisha vikundi kununua vifaa katika maeneo wanayoyapendekeza wao. Hali hii inaleta mashaka makubwa kuhusu uwazi, uaminifu na uwepo wa maslahi binafsi.

Vikundi vinapokataa kuelekezwa huko, hupewa vitisho vya kutopitishiwa miradi yao. Hili si jambo sahihi hata kidogo, kwani jukumu la mkaguzi linapaswa kuishia katika tathmini ya mradi, ushauri wa kitaalamu pamoja na ufuatiliaji wa matumizi sahihi ya fedha, na si kuwa dalali wa manunuzi.

Ni jambo lisilo la haki kwa mkopeshaji kutoa fedha halafu tena kuingilia matumizi yake kwa namna inayokwenda kinyume na andiko la mradi lililoandaliwa na kikundi husika. Endapo mfumo huu utaendelea, miradi mingi ya vijana itafeli mapema kutokana na kukosa mtaji wa kutosha pamoja na uhuru wa kutekeleza mipango yao kwa usahihi. Haiwezekani mradi wa milioni 70 utekelezwe kwa ufanisi ukipewa milioni 30 pekee bila kuathiri malengo yake.

Serikali inapaswa kulichukulia suala hili kwa uzito mkubwa. Kuna baadhi ya watendaji wasiokuwa waaminifu wanaojaribu kuvuruga juhudi za serikali pamoja na jitihada za vijana kujikwamua kiuchumi kutokana na tamaa binafsi na maslahi yao binafsi na ikiwa mazingira haya yataendelea, itakuwa vigumu kwa vijana wengi kufanikiwa katika safari yao ya kujiajiri na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Ni muhimu kuwepo kwa uwazi, uadilifu na heshima kwa waombaji wa mikopo ili kuhakikisha fedha hizi zinafikia malengo yaliyokusudiwa ya kuwawezesha wananchi kiuchumi badala ya kuwa chanzo cha vikwazo, kukatisha tamaa na kudhoofisha ndoto za vijana wengi wenye nia ya kujiletea maendeleo.
 
Sana kama kuna uku kwetu kuna mama anakiwnda cha kutengeneza batiki aliomba milion 25 lakini siku ya mwisho anapatiwa milion mbili!
 
Back
Top Bottom